03-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Ikiwa Yeye Amesema Hivyo Basi Mimi Namsadiki

 

Siku zikapita kwa haraka sana, na safari ya kurudi Makkah ikawadia, na usiku kabla ya safari yake, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliota ndoto ya ajabu sana. Aliota kuwa mwezi umepasuka na vipande vya nuru yake vimeanguka, vikapukutika na kuingia ndani ya kila nyumba ya Makkah.

Asubuhi yake akawaendea wale wacha Mungu aliokuwa akihudhuria darsi zao na kuwauliza juu ya tafsiri ya ndoto yake hiyo, na wote wakamwambia kuwa inaleta bishara njema.

Safari ikaiva. Ngamia wakaanza kuondoka kuelekea Makkah, na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akiielezea safari hiyo alisema:

"Ngamia siku hiyo walikuwa wakitoa sauti za furaha kama kwamba  wanasherehekea sikukuu."

Mara baada ya kuwasili Makkah, wafanya biashara na wanunuzi wa kawaida wakawa wanausogelea msafara huo kwa ajili ya kununua bidhaa zitokazo nchi ya Sham. Wengine walikuwa wakipatana na wengine wakizungumza, wote walikuwa wakipaza sauti zao, na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwasikia baadhi yao wakizungumza juu ya Mtume mpya aliyedhihiri hapo Makka na namna anavyodai kuwa anapata habari za mbinguni.

Alipounyanyua uso wake akamuona Abu Jahl (Amr ibn Hisham) akimsogelea na kumvamia kwa masuali:

"Umesikia juu ya rafiki yako Muhammad ewe Atiq?" (Atiq lilikuwa jina la kubandikwa la Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Abu Bakr  :      "Amepatwa na jambo gani?"

Abu Jahl :       "Muhammad anadai kwamba eti yeye ni Mtume na kwamba eti anapata habari kutoka mbinguni" .

Abu Bakr :       "Nani anayemletea habari hizo?"

Abu Jahl :       "Anasema eti Malaika aitwaye Jibril."

Abu Bakr :       "Yeye mwenyewe amesema hivyo?"

Abu Jahl :       "Ndiyo! nimemsikia kwa sikio langu."

Abu Bakr :       "Ikiwa yeye mwenyewe ametamka hivyo basi mimi namsadiki."

Abu Jahl hakuweza kustahamili msituko huo na miguu yake ikaaanza kutetemeka, akakaa chini.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akaona bora kwanza aende nyumbani akawaone watu wake na kuitua mizigo yake, kisha ende nyumbani kwa sahibu yake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa  aalihi wasallam) na kumsikiliza.

 

Share