14-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Imani ya hali ya juu

 

Imani ya hali ya juu kabisa ya Abu Bakr ilionekana pale alipofariki Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)alipokuwa akiumwa maradhi yake ya mwisho, alimtaka Abu Bakr awe anasalisha watu. Siku moja baada ya kuwasalisha Waislam,  Abu Bakr, aliingia chumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)na baada ya kuzungumza naye muda mrefu akamtaka ruhusa arudi nyumbani kwa ajili ya kukidhi haja zake.

Baada ya kumaliza haja zake na alipokuwa akijitayarisha kurudi msikitini, akasikia sauti za watu wanalizana, akazipokea habari za kufariki kwa Mtume wa Allaah huku anakimbia kuelekea msikitini na huku machozi yakimtoka huku akisema;

"Innaa liLLaahi wa innaa ilayhi raaji'uun".

Ndani ya nyumba ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)watu walikuwa mfano wa waliorukwa na akili.

Hata 'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhum), mwenye nguvu, shujaa, alisimama mbele ya watu panga mkononi huku akisema:

"Wanafiki wanadai kuwa eti Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekufa, Mtume hajafa, bali amekwenda kwa Mola wake kama alivyokwenda Musa mwana wa Imran na atarudi. Sitaki kumsikia mtu akitamka kuwa Mtume amekufa., nikimsikia mtu anasema hivyo nitamkata kichwa chake kwa upanga wangu huu."

Ikiwa hii ni hali ya 'Umar, ilikuwaje basi hali ya walio chini yake? Waislam hawakutegemea kuwa Mtume wao, kipenzi chao, (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)siku moja atakuja kuwatoka, msituko ulikuwa mkubwa sana.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliingia moja kwa moja chumbani alipolazwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akamfunua uso wake na kuubusu huku akisema;

"Uso wako unapendeza ukiwa uhai au umekufa. Ama kile kifo alichokuandikia Mola wako kimekwishakufikia".

Akaufunika uso wake na kutoka nje na kumkuta 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) angali anawasemesha watu. Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamtaka anyamaze lakini 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakunyamaza, na alipomuona hanyamazi akawaelekea watu na kuwaambia;

"Aliyekuwa akimuabudu Muhammad, basi Muhammad kesha kufa, ama aliyekuwa akimuabudu Allaah, basi Allah yu hai na wala hafi."

Kisha akaisoma kauli ya Allaah isemayo:

"Na hakuwa Muhammad ila ni Mtume tu. Wamepita kabla yake Mitume (wengi kabisa). Akifa au akiuawa ndiyo mtarudi nyuma (kwa Visigino vyenu), muwe makafiri kama zamani? Na atakayerudi nyuma kwa visigino vyake hatamdhuru Allaah chochote. Na Allaah atawalipa wanaomshukuru."

Aali Imran- 144

Alipoisikia tu aya hiyo 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuweza kusimama, akakaa kitako mfano wa simba aliyenyeshewa mvua. Siku zilizofuata alisema:

"Ilikuwa kama kwamba ninaisikia aya hiyo kwa mara ya mwanzo, miguu haikuweza kunichukua nikajitupa chini na kukaa".

Bukhari.

Ama Ibn 'Abbaas alisema;

"Wallahi ilikuwa kama hawaijui aya hii, na mara walipomsikia Abu Bakr akiisoma, watu wote waliipokea na kila aliyeisikia alikuwa akiisoma na kuirudiarudia".

Bukhari.

Huu ndio ushujaa wa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), wakati kama huu, umma wote ulipobabaika na kutetereka, akiwemo 'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu), Abu Bakr Asw-Swiddiyq alikuwa thabiti mfano wa jabali mbele ya kimbunga kilichouvamia umma siku hiyo, na aya aliyoisoma siku ile ikawa inarudiwarudiwa na kila mtu;

"Aliyekuwa akimuabudu Muhammad, basi Muhammad keshakufa, ama aliyekuwa akimuabudu Allah, basi Allah yu hai na wala hafi."

Neno la Tawhiyd, neno la kuuamsha Umma, 'Ikiwa mnamuabudu Allah basi amkeni na muifanye bendera ya Laa ilaaha Illa Allaah ipepee kila mahali. Aamkeni muyaendeleze mapambano yaliyoanzishwa na Mtume wenu huyu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)'.

Neno hilo liliwaamsha na kuwatanabahisha Waislamu, wakaanza kutimiza wajibu wao, wakamuosha, wakumshughulikia na kumswalia na kumuaga Mtume wao mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

"Je, kusingekuwepo na Abu Bakr, hali ingekuwaje siku hiyo?"

 

 

Share