55-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Je, husomewa Qur’an na Al-Faatiha?

 
Je, husomewa Qur’an na Al-Faatiha?
 
Ni jambo ambalo limezoeleka kwa watu wengi kusema, ‘Al-Faatiha kwa roho ya fulani, au kusoma surat Yaasin katika kaburi la maiti, au kusoma baadhi ya aya au sura katika Qur’an na huleta nakala za misahafu kuwagawia watu wengine watumie katika kusoma pale kaburini, wengine hujenga hema kubwa baada ya kifo na baada ya hapo linakuwepo kila alhamisi ya mwanzo na ya pili ya kifo chake na arbaini na kumbukumbu ya mwaka ya kifo chake bali haiishii hapo na katika misimu mbali mbali kumbukumbu yake inaendelea na katika hali hizo hukodiwa mtu maalum ambaye atasoma Qur’an na watu hukusanyika. Kila inapokuwa jamaa wafiwa wana mali nyingi na watu wenye hadhi katika jamii basi yule msomaji wa Qur’an anayekodishwa huwa ni maarufu zaidi na mahema yenye kufungwa au kumbi zenye kukodishwa huwa ni kubwa na ghali zaidi. Mali nyingi hutumiwa katika shughuli hizi na malipo atakayelipwa huyo msomaji wa Qur’an ili kuzihuisha siku hizo za kumbukumbu itakuwa ni kubwa sana kwa kusoma robo ya Qur’an mbali na gharama nyingine ambazo wanatakiwa walipe wafiwa. La shaka kuwa mambo haya ni kinyume kabisa na sheria ya dini ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika nyanja mbali mbali mfano:
·         Kinyume na Sunna katika kuacha kufanya Istighfaar iliyokokotezwa kisheria na dua zilizothibiti hadi kuzua matendo na maneno ambayo Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) hakuteremsha.
·         Katika kufanya mambo kama haya mtu anakuwa anajiingiza katika israfu, na haya yamekatazwa na Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) pamoja na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), kwa mfano tunasoma katika Qur’an: “…na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanao fanya israfu. (7:31) hali kadhalika katika sura nyingine tunajifunza, “ Hakika wabadhirifu ni ndugu wa Mashetani…” (17:27) mambo haya ni katika mambo ya bid’a na haramu iweje mtu akadhani mambo kama haya yatamfaa maiti?! Huku ni kukuza mambo na kukumbusha huzuni kila mara na kujeruhi donda linalokaribia kupona. Huenda ikapelekea kila Alhamisi hizo za kumbukumbu na kila vikao hivi vinapofanyika watu wakawa wanalia kila wanapokutana. Haya si katika mambo yenye kufaa kufanywa.
 
Share