12-Adabu Za Ndoa Katika Sunnah Iliyotakasika: Kufanya Wudhuu Baada Ya Jimai Na Kabla Ya Kulala

Ni bora kabisa mume na mke wasilale baada ya kujimai mpaka wafanye wudhuu kwanza.  Kuna Hadiyth mbali mbali kuhusu mas-alah haya kama zifuatazo:

 

Kwanza:

عن عائشةَ قالت: كان النبيُّ صلى الله عليه وسلم إِذا أرادَ أن [يأكل أو]  يَنامَ وهوَ جُنُبٌ غَسلَ فَرجَهُ وتَوضَّأَ وضوءه للصلاة  

Imetoka kwa mama wa waumini ‘Aaishah رضي الله عنها ambaye amesema: "Kila alipotaka (kula) au kulala akiwa katika hali ya janaba, (yaani baada ya kujimai na kabla ya kukoga) Mtume alikuwa akiosha sehemu zake za siri na kufanya wudhuu kama wa Swalah"[1]

 

Pili:

عن أبن عمر  رضي الله عنهما أن عُمرُ  قال: يا رسول الله :  أَيَنامُ أحدُنا وهوَ جُنبٌ؟ قال: ((نَعمْ، إِذا تَوضَّأَ))  وفي رواية ((توَضَّأْ واغْسِلْ ذَكَرَكَ ثمَّ نَمْ))  وفي رواية ((نَعَمْ. لِيَتَوَضَّأْ ثُمَّ لْيَنَمْ، حَتَّى يَغْتَسِلَ إِذَا شَاءَ))  وفي أخرى: ((نَعَمْ، وَيَتَوَضَّأُ إِنْ شاءَ))

 

Imetoka kwa Ibn 'Umar رضي الله عنهما kwamba 'Umar رضي الله عنه alisema: "Ee Mjumbe wa Allaah, tunaweza kulala tukiwa katika hali ya janaba?" Mtume akajibu: "Ndio baada ya kufanya wudhuu"[2]

 

Katika riwaya nyingine "Fanya wudhuu na osha sehemu zako za siri kisha ndio ulale"[3]

 

Na katika riwaya nyingine "Ndio, unaweza kufanya wudhuu, kulala na kuoga unapopenda"[4]

 

Na katika riwaya nyingine pia: "Ndio na fanya wudhuu ukipenda"[5]

 
Riwaya ya mwisho inaonyesha kuwa wudhuu huu sio fardh.

 
 

Tatu:

عنْ عَمَّارِ بنِ يَاسِرٍ ، أنَّ رَسُولَ الله صلى الله عليه وسلم قالَ: ((ثَلاَثَةٌ لاَ تَقْرَبُهُمْ المَلاَئِكَةٌ: جِيْفَةُ الْكَافِرِ، وَالمُتَضَمِّخُ بِالخُلُوقِ، وَالْجُنُبُ إلاَّ أنْ يَتَوَضَّأَ))

Imetoka kwa 'Ammaar ibn Yaasir kwamba "Mtume amesema: "Watu watatu Malaika hawawakaribii; maiti ya kafiri, mwanamume anayejitia manukato ya kike, na mwenye janaba (aliyefanya jimai) hadi afanye wudhuu"[6]

  
 

 

[1] Al-Bukhaariy na Muslim

[2] Al-Bukhaariy na Muslim

[3] Al-Bukhaariy na Muslim

[4] Muslim, Al-Bayhaaqiy na Abu Daawuud

[5] Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan: Swahiyh

[6] Abu Daawuud, Ahmad na wengineo: Hasan

Share