24-Adabu Za Ndoa Katika Sunnah Iliyotakasika: Nyumba Lazima Iwe Na Sehemu Ya Kuogea

Wanaofunga ndoa lazima wawe na sehemu ya kuogea nyumbani mwao. Na mume asimruhusu mkewe kwenda kuoga katika vyoo vya nje.  Hii imekatazwa na kuna Hadiyth mbali mbali zinazokataza jambo hili miongoni mwa hizo ni:

 
Kwanza:

 

عن جابر أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((مَنْ كانَ يُؤْمِنُ بالله واليومِ الآخِرِ فلا يُدْخِلْ حَلِيلَتَهُ الحَمَّامَ  وَمَنْ كَانَ يُؤْمِنُ بالله وَاليَوْمِ الآخِرِ فلا يُدْخِلْ الحَمَّامَ إلا بِمئزَرٍ، وَمَنْ كَانَ يُؤْمِنُ بالله وَاليَوْمِ الآخِرِ فلا يَقْعُدْ على مائِدَةٍ يُشْرَبُ عَلَيْها الخَمْرُ))

 
Imetoka kwa Jaabir ambaye amesema: Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alisema, ((Yeyote anayemuamini Allaah na siku ya mwisho, basi asimuache mke wake kwenda vyoo vya nje (vitumiwavyo na watu wote, Mwenye kuamini Allaah na Siku ya mwisho, asiende bafuni isipokuwa na (awe amevaa) nguo ya kiunoni. Na yeyote anayemuamini Allaah na siku ya mwisho asikae katika meza inayonywewa ulevi)) [1]

Pili:

Imetoka kwa Ummu Ad-Dardaa ambaye amesema:

 

خرجت من الحمام فلقيني رسول الله صلى الله عليه وسلم فقال: ((مِنْ أَيْنَ يا أُمَّ الدَّرْدَاءِ؟)) قالت: من الحمام، فقال: ((وَالَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ مَا مِنْ امْرَأَةٍ تَضَعُ ثِيَابِها فِي غَيْرِ بَيْتِ أَحَدٍ مِنْ أُمَّهاتِها الإِ وَهِيَ هاتِكَةٌ كُلَّ سِتْرِ بَيْنَها وَبَيْنَ الرَّحْمٰنِ))

 

"Nilitoka kutoka vyoo vya nje nikakutana na Mtumeصلى الله عليه وآله وسلم ambaye aliniambia: ((Umetoka wapi ewe Ummu Ad-Dardaa?)) Nikasema: Kutoka vyooni. Kisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema: ((Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake. Kila mwanamke anayevua nguo zake popote isipokuwa nyumba ya mmoja wa mama yake, atakuwa ameondosha stara yake mbele ya Ar-Rahmaan))[2]

 

Tatu:

Imetoka kwa Abu Al-Maliyh ambaye amesema:

 

دخل نسوة من أهل الشام على عائشة رضي الله عنها فقالت: لعلكن من الكورة التي تدخل نساؤها الحمام، سمعت رسول الله يقول: ((أَيُّما امْرَأَة وَضَعَتْ ثيابَها في غَيْرِ بَيْتِ زَوْجِها فَقَدْ هَتَكَتْ سِتْرَها فيما بَيْنَها وَبَيْنَ الله عَزَّ وَجَلَّ))

 

"Baadhi ya wanawake kutoka Ash-Shaam waliingia kwa mama wa waumini ‘Aaishah رضي الله عنها na akasema: 'Mnatoka wapi?'  Wanawake wakajibu: 'Sisi ni watu wa Ash-Shaam' (ambayo sasa ni Syria). Bibi ‘Aaishah akasema: 'Labda nyinyi mnatoka katika wilaya (kitongoji) ambayo inawaruhusu wanawake kuingia katika vyoo vya nje?' Wakasema: 'Ndio'. Akasema: 'Ama mimi nimemsikia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akisema: ((Mwanamke yeyote atakayevua nguo zake nje ya nyumba ya mumewe, amechana shela (ameondosha stara) ya hayaa baina yake na Allaah))[3]

 

[1] Al-Haakim, At-Tirmidhiy na wengineo: Swahiyh

[2] Ahmad: Swahiyh

[3] At-Tirmidhiy, Abu Daawuud na wengineo: Swahiyh

Share