Kadi Za Michango Na Kadi Za Mialiko Katika Ndoa Za Kiislam

 
 
SWALI:
 
Assalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh.
ndugu mpendwa katika imani naomba nipatiwe ufumbuzi wa kina wa kisheria juu ya suala la kutoa kadi kwa ajili ya michango au mualiko katikandoa za kiiislam. Je suala hili lina nafasi gani kwa mujibu wa kitabu na sunnah
 

 
JIBU:
 
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
 
Shukrani zetu kwa swali lako hili zuri kuhusu mambo hayo mawili. Hili ni suala ambalo limezua tatizo kwa sababu limekosa ule msingi kuwa jambo hilo halikuwepo wakati wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake baada yake.
 
Huenda wengine wakapinga mambo ya kuchapisha kadi za michango au harusi kwa kutoa dalili ifuatayo. Imepokewa kwa Mama wa Waumini, Ummu 'Abdillaah 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
 
"Mwenye kuzua katika hili jambo (Dini) letu lisikuwamo humo litakataliwa" (al-Bukhaariy na Muslim). Katika riwaya nyengine ya Muslim: "Mwenye kufanya amali isiyokuwa na hukumu yetu, itakataliwa".
 
Hivyo, hizi riwaya mbili zinaonyesha kuwa kuzua amali au kuzua maneno katika Dini, ni mambo yasiyokubalika.
 
Hadiyth hii ieleweke inabidi tueleze baadhi ya ibara ili ifahamike vyema. ‘Kuzua ni kuanzisha kitu kwa mtu kupenda mwenyewe na kufuata hawaa yake tu. ‘Katika jambo hili letu ina maana katika Dini na Shari 'ah yetu aliyotuchagulia Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). ‘Lisilokuwamo humo ina maana lenye kupingana na kutokubaliana na Shari'ah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na jambo ambalo halina ushahidi wala dalili yoyote ya kuafikiana na misingi ya Dini. Mwenye kufanya hivyo jambo hilo litakataliwa na halitakubaliwa kabisa. Haya ni mambo ambayo yanafungamana moja kwa moja na Dini na Shari'ah.
 
Ama mambo ambayo yanahusiana na dunia yetu hayo ni mambo yanayopendeza katika Dini yakiwa mazuri na kuweka nidhamu muruwa na barabara. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipofika Madiynah aliwakuta watu wake wakichavusha mitende yao kwa kutumia chembe za chavua. Akawauliza kwanini wanafanya hivyo? Mwaka huo mazao yakawa kidogo sana, naye (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza sababu ya hilo. Wao wakamjibu kwa kumwambia: "Sisi tulikuwa tunachavusha mitende nawe ukatukataza, na hii ndio natija". Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia: "Nyinyi mnajua vyema mambo ya dunia yenu".
 
Tukiyapigia darubini mas-ala haya ya kadi utaona kwamba yana uzuri wake na ubaya wake:
 
Kuhusu Kadi za Michango
 
Ni kupatikana maslahi kwa jamii yetu baada ya kuvurugika katika ufisadi na ulaji wa pesa kwa njia za haramu. Maslahi kwa jamii ni jambo muhimu sana ikiwa haitakwenda kinyume na Shari’ah na Dini. Mara nyingi watu wanaokusanya pesa kwa njia isiyokuwa ya kadi labda wawe waaminifu sana lakini huwa hawapeleki pesa zote kwa mradi wanaoukusanyia pesa. Nyingine wanakula na nyingine wanapeleka, lakini kwa sababu ya kutoa kadi imeondoa ufisadi mwingi sana hivyo kuwa ni maslahi kwa miradi na jamii.
 
Kuhusu kadi za Mwaliko wa Ndoa
 
Kadi katika harusi zimekuja kwa kutokea vurugu kwa watu ambao hawakualikwa au kuleta aibu kwa chakula kutotosha kwa sababu ya watu ambao wamekwenda bila kualikwa. Kwa hiyo, wenye harusi wanatoa kadi ili kudhibiti wasioalikwa kuingia katika Waliymah (Karamu ya Ndoa).
Imepokewa na Ibn ‘Umar kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yeyote asiyekubali mwaliko amemuasi Allaah na Mtume Wake, na mwenye kuingia bila kualikwa anaingia kama mwizi na kutoka katika sehemu hiyo kama mvamizi” (Abu Daawuud).
Pia waalikwa wengi wanakiuka agizo la Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambalo ni mtu akialikwa basi ajibu mwito kama tunavyozinukuu hapa dalili kutoka katika Sunnah:  
 

Kwanza:
 
  ((فُكُّوا الْعَانِيَ، وَأَجِيبُوا الدَّاعِيَ، وَعُودُوا الْمَرِيضَ))
 
((Acheni huru wafungwa, itikieni (kubalini) mwaliko na tembeleeni wagonjwa)) [AL-Bukhaariy]
 
Pili:
 
((إِذَا دُعِيَ أَحَدُكُمْ إِلَى الْوَلِيمَةِ فَلْيَأْتِهَا  عَرْساً كَان أَوْ نَحْوه  وَمَنْ لَمْ يُجِبِ الدَّعْوَةَ، فَقَدْ عَصَى اللّهَ وَرَسُولَهُ))
 
((Anapoalikwa mmoja wenu katika karamu, basi ahudhurie, ikiwa ni karamu ya harusi au nyingineyo. Na yeyote asiyeitikia (asiyekubali) mwaliko basi atakuwa amemuasi Allaah na Mtume Wake)) [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]
lakini kwa sababu ya vurugu au maasi yanayokuwemo katika baadhi ya sherehe za Ndoa ndizo zinasababisha mtu asiitikie mwaliko, na anapofanya hivyo mtu katika hali hiyo, huwa hatumbukii katika hukumu za Hadiyth hizo hapo juu kwa sababu Muislam haruhusiwi kushiriki shughuli zozote zenye maasi.
 
Ubaya wake:
 
Baadhi ya watu hufanya israaf katika kutengeneza hizo kadi. Wengine huwa ni kutaka kushindana kutengeneza kadi iliyokuwa nzuri kabisa na yenye gharama ya juu, wakati hiyo gharama ya hizo kadi angeliweza mwenye Waliymah kuwaalika watu wengine ambao ni masikini. Aghlabu wanaoalika kwa kadi hupendelea kualika matajiri na kuwasahau masikini jambo ambalo linakwenda kinyume na maagizo ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokataza kualika matajiri pekee na kupendelea masikini pia waalikwe:
 
 ((شَرُّ الطَّعَامِ طَعَامُ الْوَلِيمَةِ يُدْعَىٰ لَهَا الأَغْنِيَاءُ وَيُتْرَكُ الْمَسَاكِينُ، وَمَنْ لَمْ يَجِبْ الدَّعْوَةَ فَقَدْ عَصَىٰ اللَّهَ وَرَسُولَهُ)).
 
((Chakula kiovu kibaya kabisa ni chakula cha karamu ya harusi ambayo wamealikwa matajiri na kutengwa kando masikini. Yeyote atakayekataa mualiko atakuwa amemuasi Allaah na  Mtume Wake))[Muslim na Al-Bayhaqiy]
 
Ubaya mwingine ni kuwa hizo kadi nyingine huwa za kuchorwa picha za viumbe mfano bwana harusi na bibi harusi. Dini yetu imetukataza kuchora picha za viumbe wenye roho.
 
Pamoja na kuwa kuwepo na nidhamu ya kualika watu kwa kadi kumekuwa na maslahi pamoja na nidhamu kwa karamu hizo, lakini wengi hawatumii njia hizo vizuri na huchukua fursa hiyo ya kualika watu kwa kadi ili waweze kualika tu wale wanaowataka wao ima kwa ujamaa, ukabila, uhali wa kijamii kama ni wafanyabiashara wenzake, au wafanyakazi wenzake tu, au wanaofanana naye kihali ya kijamii n.k. na kuacha kualika maskini na mafakiri kama alivyohimiza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Wanaofanya hivyo wanapaswa wamche Allaah na waache tabia hizo ambazo haziendani na uzuri wa Uislam.
Kwa hivyo, kisheria, hakuna tatizo lolote kwa watu kutoa kadi kwa ajili ya michango au Waliymah (karamu) maadam kutafuatwa taratibu za kisheria na hakutakiukwa ndani yake mafunzo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
 
Na Allaah Anajua zaidi
 
 
 

Share