Naswali Na Kuacha, Nisaidieni Kuokoka Na Madhambi Haya

  

 

 

 

SWALI

 

salamaaleikum

mimi naitwa  ……...swali langu ni naomba msaada ninania kubwa sana ya kuwa mcha mungu lakini kila napoaanza kuswali na swali wiki 1 au 2 kisha nawacha je unanisdhauri nini? na mimi sijui mambo mengi kuhusu dini nashkuru kuipata hii web inanifundisha mambo mengi nawashkuru sana.

 

 


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tunashukuru kuona kwamba dada yetu ushatambua makosa yako na unataka kurudi kwa Mola wako. Pia tunakushukuru kutukabili sisi kutafuta nasaha kwetu upate kujiweka katika hali ya kumridhisha Mola wako. Utambue kwamba wewe ni miongoni mwa wale ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anataka kuwahidi kwani wangapi wasioswali kabisa au huswali na kuacha lakini wakaona ni jambo la kawaida na wakawa wanaendelea kufanya hivyo bila ya kutafuta ufumbuzi wa kujirekebisha. Basi inakupasa kwanza umshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Kukuongoza hadi umetanabahi dhambi hiyo kubwa.

Vile vile utambue kuwa Shaytwaan hamuachi Muislamu anayetaka kumtii Mola Wake kwa kufuata amri Zake khaswa za fardhi kama hizo za Swalah. Hivyo atakufanyia kila hila akutie uvivu na uzito wa kuzitekeleza Swalah, kwani Swalah ndio ibada kuu inayomkurubisha Mja na Mola Wake na kumuepusha maasi, maovu na kuasi amri. Naye Shaytwaan ndio kazi yake kubwa kukupambia kwa uzito wote huo uonao ili akutoe katika njia iliyonyooka ubakie katika njia panda hadi mwisho aweze kukupotosha kabisa ushindwe hata kuswali moja kwa moja.

Shaytwaan huyo alipofanya kibri yake ya kukataa amri ya Mola wake kuwasujudia Malaika Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Alimtoa Peponi na kumdhalilisha. Naye ndipo alipotamani kuwapotosha binaadamu kama alivyopotoka yeye, yanaelezewa hayo katika Aaya zifuatazo:

((قَالَ فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ))

(( ثُمَّ لآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَآئِلِهِمْ وَلاَ تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ))

((Akasema: Kwa kuwa umenihukumia upotofu, basi nitawavizia katika Njia yako Iliyonyooka))

 

((Kisha nitawazukia mbele yao na nyuma yao na kuliani kwao na kushotoni kwao. Wala hutawakuta wengi wao wenye shukrani)) [Al-A'raaf: 16-17]

 

Kisha baada ya kukupotosha atakugeuka na kukukana na kudai kuwa hakukuamrisha hayo yote bali yalikuwa ni matanio yako mwenyewe na kisha wote wawili muwe pamoja motoni! Allaah Akuhifadhi na hilo.

 

((كَمَثَلِ الشَّيْطَانِ إِذْ قَالَ لِلْإِنسَانِ اكْفُرْ فَلَمَّا كَفَرَ قَالَ إِنِّي بَرِيءٌ مِّنكَ إِنِّي أَخَافُ اللَّهَ رَبَّ الْعَالَمِينَ))   ((فَكَانَ عَاقِبَتَهُمَا أَنَّهُمَا فِي النَّارِ خَالِدَيْنِ فِيهَا وَذَلِكَ جَزَاء الظَّالِمِينَ))   

 

((Ni kama mfano wa shaytwaan anapomwambia mtu: Kufuru. Na akikufuru humwambia: Mimi si pamoja nawe. Hakika mimi namwogopa Allaah, Mola  wa walimwengu wote)) 

 

((Basi ikawa mwisho wa wote wawili hao ni kuingia Motoni, wadumu humo daima; na hiyo ndiyo jaza ya madhaalimu)) [Al-Hashr: 16 -17]

 

Kwa hiyo usimuendekeze Shaytwaan akakufanya ufanye mchezo na Swalah zako kwani hatari yake ni kama hivyo ulivyoona katika hizo Aayah na pia usije kuwa miongoni mwa wale Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anaowataja:

 

((فَوَيْلٌ لِّلْمُصَلِّينَ))

 

((الَّذِينَ هُمْ عَن صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ))

((Basi, ole wao wanaoswali))

((Ambao wanapuuza Swalah zao)) [Al-Maa'uun: 4-5]

 

Swalah ni fardhi ambayo lazima Muislamu aitimize kwani asipoitimiza yeyote anayejiita Muislamu basi ajue kwamba hakuutimiza Uislamu wake, kwani Swalah ni nguzo ya Dini. Ni mfano wa nguzo za nyumba au nguzo za meza, ikivunjika moja huporomoka. Vile vile asiyeswali ni sawa tu na kafiri kutokana na kauli nyingi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

عن جابر بن عبد الله، عن النبي ((إن بين الرجل وبين الشرك، والكفر، ترك الصلاة))  رواه مسلم  

Kutoka kwa Jaabir bin 'Abdillahi kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika Baina ya mtu na shirki na kufru, ni kuacha Swalah)) [Muslim]

عن بريدة بن الحصيب رضي الله عنه، قال: سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول: ((العهد الذي بيننا وبينهم الصلاة، فمن تركها فقد كفر)) [رواه أحمد وأبو داود والترمذي والنسائي وابن ماجه  

Kutoka kwa Buraydah bin Al-Haswiyb (Radhiya Allaahu 'anhu ambaye amesema: "Nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Ahadi (mafungamano) baina yetu na baina yao (wasio Waislam) ni Swalah, atakayeiacha atakuwa amekufuru)) [Ahmad, Abu Daawuud, An-Nasaaiy na Ibn Maajah]

 

Ujue pia kuwa jambo la kwanza atakaloulizwa mja siku ya Qiyaamah ni Swalah, ikiwa imetimia basi mengine yote yatakuwa

عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم (( إن أول ما يحاسب به العبد يوم القيامة من عمله صلاته ، فإن صلحت فقد أفلح وأنجح ، وإن فسدت فقد خاب وخسر ، فإن انتقص من فريضته شيئا قال الرب  عز وجل : انظروا هل لعبدي من تطوع فيكمل بها ما انتقص من الفريضة ، ثم يكون سائر عمله على ذلك )) رواه الترمذي  و قال حديث حسن

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kitu cha kwanza atakachohesabiwa nacho mja siku ya Qiyaamah katika amali zake ni Swalah yake. Ikitengenea atakuwa amefuzu na amefanikiwa, na ikiharibika, atakuwa ameambulia patupu na amekhasirkia. Kikipunguka kitu katika faradhi yake, Allaah ('Azza wa Jalla) Atasema: Tazameni kama mja Wangu ana ziada (Swalah za Sunnah) ili akamilishiwe kilichopungua katika faradhi zake. Halafu matendo yake yote yatakuwa ni kwa namna hii)) [At-Tirmidhiy ni amesema Hadiyth hii ni Hasan Swahiyh]   

Umuhimu wa kutimiza Swalah tano, makatazo ya kuzipuuza, adhabu zake, fadhila zake na mengi yote tumeyaelezea katika Nasiha za Ijumaa ambazo tunakuwekea viungo vyake tayari hapa. Ni LAZIMA uzisome mada zote hizo ikiwa kweli unataka ufumbuzi wa matatizo yako.

SWALAH - 1 - Maana Ya Swalah Na Kuwajibika Kwake

SWALAH - 2 - Kusisitizwa Kwake na Malipo yake

SWALAH - 3 - Amri za Mwanzo kwa Mitume iliyopita

SWALAH - 4 - Maamrisho Ya Swalah Kwetu

SWALAH - 5 - Ni Ibada Muhimu Kabisa

SWALAH - 6 - Adhabu Za Mwenye Kuacha Swalah

SWALAH - 7 - Hukmu Ya Taarikus-Swalah (Asiyeswali)

SWALAH - 8 - Fadhila Za Swalah

 

Kisha fuata yafuatayo ili upate kumkimbiza Shaytwaan asikutie wasiwasi wa kuacha Swalah na nasaha hizi pia zitazidi kukukurubisha kwa Mola wako, zitakupa ridhaa ya nafsi, utasikia raha sana katika moyo wako, utaonja ladha ya Iymaan, na wala hutojali lolote ila tu kufanya ibada na mema upate ridhaa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

  1. Hakikisha kwanza kusoma mada zote hizo za Swalah

  2. Sikiliza Mawaidha kila siku japo mawaidha moja. Anza kusikiliza hizi zifuatazo kuhusu Swalah:

Hukmu Ya Mtu Mwenye Kuacha Swalah part I

Hukmu Ya Mtu Mwenye Kuacha Swalah part II

Swalah Inapotuelekeza

  1. Soma Qur-aan kila siku japo ukurasa mmoja.

  2. Soma nyiradi za asubuhi na jioni kila siku ufululize usiache japo kwa muda hadi uwe thabiti katika Swalah zako. Adkhaar zote zinapatikana hapa:

          28 Nyiradi za asubuhi na jioni

Anza kwanza na hayo kisha tutafurahi kama utarudi kutujulisha maendeleo yako ili tukupe nasaha zaidi uzidi kubakia katika usalama na ridhaa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

 

 

 

 

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Share