Zingatio: Kitabu Kitukufu

 

Zingatio: Kitabu Kitukufu

 

Imetayarishwa Na: Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Yareti kama Vitabu vyote Duniani vitabaki na uasili wa Kitabu cha Rabb Mtukufu! Yareti kama wangelipata angalau Aayah moja tu yenye kufanana na Kitabu cha Rabb Mtukufu! Wangelitakabari na katu Waislamu wasingelikuwa na nafasi tena ya kujinasibu kwa uzuri wa Kitabu hichi. Juu ya hali zote, twamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kukihifadhi Kitabu hichi, kwani sisi hatuna nguvu wala uwezo wa kuhifadhi japo aya moja.

 

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿٩﴾

Hakika Sisi Tumeteremsha Adh-Dhikra (Qur-aan) na hakika Sisi bila shaka ndio Wenye kuihifadhi. [Al-Hijr: 9]

 

Ndugu zangu Waislamu, hatukai kukiangalia kwa makini Kitabu hichi cha Qur-aan? Namna kilivyo kitukufu. Kilichojaa miujiza, Subhaana-Allaah! Kitabu ambacho ndani yake kina kila aina ya raha na utulivu. Wa-Allaahi naapa kwa Rabb wa Mbingu na Ardhi, hakuna Kitabu chenye utamu na mazingatio kama Qur-aan. Mpangilio wa Aayah zake hakika ni maridhawa, wamepita washairi na washairi lakini ushairi uliomo ndani ya Qur-aan hakuna mfano wake.

 

أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ ۖ قُلْ فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِّثْلِهِ وَادْعُوا مَنِ اسْتَطَعْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴿٣٨﴾

Je, wanasema (Qur-aan) ameitunga (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم)?  Sema: Hebu basi leteni Suwrah ya mfano wake, na waiteni mnaoweza pasi na Allaah mkiwa ni wakweli. [Yuwnus: 38]

 

Hakikupata kuwepo wala hakitatokea Kitabu chengine. Kwa nini hatukipi heshima Kitabu hichi namna ambayo inastahiki? Ni furaha iliyoje kuwa na Kitabu namna hichi kwetu sisi Waislamu.

 

Yatosha kwetu kuwa na heshima kwa kuamini kuwa Kitabu hichi kimeshushwa kwa asiyejua kusoma wala kuandika. Huo ni miujiza tosha. Binaadamu tumejaaliwa na akili ya kufahamu, inakuwaje hadi milima ikawa bora kuliko binaadamu? Kwani yareti hii Qur-aan ingelishushwa kwa milima, ingelinyenyekea na kupasuka. Yote kwa sababu ya sisi binaadamu kukosa khofu kwa Rabb wetu. Anasema Rabb Mtukufu:

 

لَوْ أَنزَلْنَا هَـٰذَا الْقُرْآنَ عَلَىٰ جَبَلٍ لَّرَأَيْتَهُ خَاشِعًا مُّتَصَدِّعًا مِّنْ خَشْيَةِ اللَّـهِ ۚ وَتِلْكَ الْأَمْثَالُ نَضْرِبُهَا لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ﴿٢١﴾

Lau Tungeliiteremsha hii Qur-aan juu ya jabali, ungeliliona linanyenyekea likipasukapasuka kutokana na khofu ya Allaah. Na hiyo ni mifano Tunawapigia watu ili wapate kutafakari. [Al-Hashr: 21]

 

Utukufu wa Qur-aan ni wa kwake pekee, katu kalamu haiwezi kuiandika Qur-aan. Thamani yake ni kubwa kuliko vyote duniani. Tunachofanya sisi wanaadamu ni kukopia tu kutoa nakala zake. Lakini uasili wake katu hatuupati.

 

قُل لَّوْ كَانَ الْبَحْرُ مِدَادًا لِّكَلِمَاتِ رَبِّي لَنَفِدَ الْبَحْرُ قَبْلَ أَن تَنفَدَ كَلِمَاتُ رَبِّي وَلَوْ جِئْنَا بِمِثْلِهِ مَدَدًا ﴿١٠٩﴾

Sema: Kama bahari ingelikuwa ni wino wa (kuandika) maneno ya Rabb wangu, basi ingelimalizika bahari kabla ya kumalizika maneno ya Rabb wangu, japokuwa Tungelileta mfano wake kujaza tena. [Al-Kahf: 109]

 

Basi kwa hakika hichi si kitabu cha kukifanyia mzaha wala masikhara, Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَحْذَرُ الْمُنَافِقُونَ أَن تُنَزَّلَ عَلَيْهِمْ سُورَةٌ تُنَبِّئُهُم بِمَا فِي قُلُوبِهِمْ ۚ قُلِ اسْتَهْزِئُوا إِنَّ اللَّـهَ مُخْرِجٌ مَّا تَحْذَرُونَ﴿٦٤﴾ وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ ۚ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ﴿٦٥﴾

Wanafiki wanatahadhari isije kuteremshwa Suwrah itakayowajulisha yaliyomo nyoyoni mwao. Sema: Fanyeni istihzai; hakika Allaah Atayatoa yale mnayotahadhari nayo. Na ukiwauliza, bila shaka watasema: Hakika tulikuwa tunaporoja na tunacheza. Sema: Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayaat Zake na Rasuli Wake? [ At-Tawbah: 64-65]

 

Kitabu ambacho ndani yake kimejaa mawaidha juu ya mawaidha. Allaah Anatuuliza Hatufahamu?

لَقَدْ أَنزَلْنَا إِلَيْكُمْ كِتَابًا فِيهِ ذِكْرُكُمْ ۖ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿١٠﴾

Kwa yakini Tumekuteremshieni Kitabu (Qur-aan) ndani yake mna makumbusho yenu, je, basi hamtii akilini? [Al-Anbiyaa: 10]

 

Nawausia ndugu zangu kukisoma kwa mazingatio.

Share