Kusomea Maji Surah Za Ruqyah Kisha Kumwagia Kwenye Ukuta

 

Kusomea Maji Suwrah Za Ruqyah Kisha Kumwagia Kwenye Ukuta

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalamu Aleykum, namshuku ALLAAH alie wapa fahamu ndugu zetu wa alhidaaya kutuelimisha. pia salamu nyingi zimfikie Nabiy wetu (s.a.w.) pia nawashukuru sana ndugu zangu kwa iman alhidaaya naomba mutuvumilie na malipo yenu kwa Allaah na Allaah Awazidishie Elimu zaidi na zaidi na sasa namshukuru Allaah elmu yangu naipata kwa alhidaaya na ninawaamini sana.

 

Bismillah swali yangu.

 

Kuna mwalimu m1 aliniambia nisome Suwrah anam kwenye maji alafu ni mwagie katika ukuta bala itatoka kwa uwezo wa Allaah nikamuuliza sio vibaya? Akasema kama qu an inatundikwa na kumwagia itakuwa sio vibaya. Sijafanya ndio nawauliza nyie, nakusomea tiba ya ruqya katika maji ukamwagia katika ukuta pia itakua vibaya? na kitabu ya fadhila ya suratul fatiha ukiifata nivibaya na kitabu ya fadhila ya ikhlas ni nzuri kuisoma na kufuata. Samahani kwa usumbufu ya maswali yangu m.mungu atawazidishia kila la kher na mafanikio mema Amin.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’aalaa) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Nabiy. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu.

 

Mwanzo tungependa kukufahamisha kuwa Suwrah Al-An'aam si miongoni mwa Suwrah au Aayah za Ruqyah. Pia ifahamike Qur-aan haijateremshwa ili itundikwe ukutani bali lengo lake kubwa ni kubadili waliyonayo watu katika tabia, maadili, mas-ala ya kijamii, kiuchumi, kisiasa, kwani huo ni mfumo kamili wa maisha. Qur-aan imeteremshwa kuwaongoza watu katika njia ya sawa. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:

ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ ۛ فِيهِ ۛ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ ﴿٢﴾ 

Hiki ni Kitabu kisicho na shaka ndani yake, ni mwongozo kwa wenye taqwa. [Al-Baqarah: 2].

 

Pia,

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ

Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo (la haki na batili). [Al-Baqarah: 185].

 

Vile vile kuhusu kumwagwa kwa maji yaliyosomewa Aayah zozote au Suwrah zozote za Qur-aan ni jambo ambalo halina ushahidi kutoka mafunzo ya Quraan wala ya Sunnah, hivyo ni vizuri kuepukana nalo. Hatujui sababu gani au nia ya kutaka kufanya hivyo. Kama ni kwa ajili ya kuikinga nyumba, basi tayari tunayo mafunzo yenye dalili ya kinga za nyumba. Nazo utazipata katika Swali lifautalo ambalo limeelezewa kwa kirefu aina zote za kinga za nyumba:

 

Unapohamia Katika Nyumba, Unatakiwa Usome Au Kufanya Chochote

 

Ama kuhusu kitabu cha fadhila cha Suratul Faatihah hatufahamu ni kipi. Lakini fadhila za Surah hiyo zinafahamika kupitia kwa Qur-aan na Hadiyth sahihi. Qur-aan inasema:

 

وَلَقَدْ آتَيْنَاكَ سَبْعًا مِّنَ الْمَثَانِي وَالْقُرْآنَ الْعَظِيمَ﴿٨٧﴾

Na kwa yakini Tumekupa (Aayaat) Saba zinazokaririwa (kusomwa) na Qur-aan Adhimu. [Al-Hijr: 87].

 

Pia kupona kwa kiongozi wa kabila moja la Kiarabu ambaye kabila lake lilikataa kuwapatia ugeni Swahaba (Radhwiya Allaahu‘anhum). Kiongozi huyo aliumwa na nge akakosa dawa ya kupunguza machungu, hivyo kuwafanya watu wake waende tena kwa Swahaba kuona kama wana usaidizi wowote. Mmoja kati ya Swahaba alimsomea Suwrah hii naye (kongozi) huyo akawa ni mwenye kupona [al-Bukhaariy na Muslim].

 

Swaalah pia haisihi bila kuisoma Suwrah hii. Hivyo, kusoma fadhila zilizonukuliwa kutoka kwa Hadiyth sahihi hapana tatizo bali ni jambo lililohimizwa lakini ikiwa ni za kubuniwa itakuwa haifai.

 

Ama Suwrah Al-Ikhlaasw ina fadhila kubwa sana. Suwrah hiyo ni sawa na thuluthi ya Qur-aan. Inafaa tuisome asubuhi na jioni mara tatu tatu na pia wakati wa kulala na baada ya Swaalah. Suwrah hii pamoja na Mu‘awidhatayn ina kinga dhidi ya shetani.

 

Hakika ni kuwa sisi huwa hatupati usumbufu wowote kwa nyinyi kutuuliza mas-ala ili tuweze kuielewa Dini yetu. Tuzidi kuombeana ili tuweze kukidhi haja za watu kwa kujibu maswali yao. Na Allaah Aliyetukuka Atuzidishie mema hapa duniani na kesho Aakhirah  In shaa Allaah.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share