Afanye Nini Kwa Aliyemdhulumu? Ni Bora Kumlipa Kisasi Au Kumwachia Allaah?

 

Afanye Nini Kwa Aliyemdhulumu? Ni Bora Kumlipa Kisasi Au Kumwachia Allaah?

 

Alhidaaya.com

 

Swali:

 

Swali langu ni hili, ikiwa mtu amekudhulumu kwa aina yoyote wewe haki yako nikumfanya nini au muachiye Allaah.

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Mwanzo inahitajika ieleweke kuwa Muislamu hafai kukubali kudhulumiwa kwa njia yoyote ile na pia haifai kwake kudhulumu.

 

Hivyo, ikiwa mtu amekudhulumu inafaa uitafute haki yako kwa njia zote zile za kishariy'ah ili urudishiwe haki yako. Wala usichoke kufanya hivyo kwani kuachilia haki yako itamfanya mtu huyo awe na ujasiri wa kukudhulumu kwa mara nyingine tena.

 

Katika Hadiyth al-Qudsiy Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: Allaah Aliyetukuka Amesema: "Enyi waja Wangu! Mimi Nimejiharamishia dhuluma juu ya Nafsi Yangu na Nikaifanya ni haramu baina yenu basi msidhulumiane" (Muslim).

 

Unapodhuliwa kwa namna yoyote ile Uislamu umekupatia njia tatu ya kuliendea suala hilo: Kulipiza kisasi au kumsamehe na kufanya subra au kumuachia Allaah. Hakika ni kuwa kusamehe ni bora, kwani kufanya hivyo kuna faida nyingi tunazitaja chache zifuatazo:

 

1- Kuwa pamoja na Allaah, na kulipwa ujira wa kusubiri.

 

وَإِنْ عَاقَبْتُمْ فَعَاقِبُوا بِمِثْلِ مَا عُوقِبْتُم بِهِ ۖ وَلَئِن صَبَرْتُمْ لَهُوَ خَيْرٌ لِّلصَّابِرِينَ﴿١٢٦﴾وَاصْبِرْ وَمَا صَبْرُكَ إِلَّا بِاللَّـهِ ۚ وَلَا تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَلَا تَكُ فِي ضَيْقٍ مِّمَّا يَمْكُرُونَ﴿١٢٧﴾إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الَّذِينَ اتَّقَوا وَّالَّذِينَ هُم مُّحْسِنُونَ﴿١٢٨﴾

Na mkilipiza, basi lipizeni kulingana na vile mlivyoadhibiwa. Na mkisubiri, basi bila shaka hivyo ni bora kwa wenye kusubiri. Na subiri (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), na haiwi subira yako isipokuwa kupitia kwa Allaah. Na wala usiwahuzunukie, na wala usiwe katika dhiki kutokana na njama wanazozifanya. Hakika Allaah Yu Pamoja na wenye taqwa, na wale ambao wao ni wenye kufanya ihsaan. [An-Nahl: 126 – 128]

 

2- Kusamehewa madhambi ya mja

 

Vile vile kumsamehe aliyekudhulumu au aliyekukosea ni kupata maghfirah kutoka kwa Mola wako ambayo hakuna mmoja wetu asiyetaka kusamehewa madhambi yake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَلْيَعْفُوا وَلْيَصْفَحُوا ۗ أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٢﴾

Na wasamehe na waachilie mbali. Je, hampendi Allaah Akughufurieni? Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [An-Nuwr: 22]

 

3- Kupandishwa daraja na kuwa miongoni mwa Muhsiniyn

 

Pia ni kupandishwa daraja ya kuwa Muhsiniyn kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

الَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاء وَالضَّرَّاء وَالْكَاظِمِينَالْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ وَاللّهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ 

Ambao hutoa wanapokuwa na wasaa na wanapokuwa na dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Allaah Huwapenda wafanyao wema. [Al-'Imraan: 133]

 

4- Kulipwa ujira kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَجَزَاءُ سَيِّئَةٍ سَيِّئَةٌ مِّثْلُهَا ۖ فَمَنْ عَفَا وَأَصْلَحَ فَأَجْرُهُ عَلَى اللَّـهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ﴿٤٠﴾

Na jazaa ya uovu ni uovu mfano wake. Lakini atakayesamehe na akasuluhisha, basi ujira wake uko kwa Allaah, hakika Yeye Hapendi madhalimu. [Ash-Shuwraa: 40]

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share