Mume Hajulikani Kama Kazama Baharini Au Yuhai, Je Mke Akae Eda?

 

SWALI:

ASSALAM ALAYKUM WARAHMATULLAH WABARAKATUH.

SINA BUDU KUMSHUKURU ALLAAH KUFIKA HAPA NILIPO NA NYIE WANA ALHIDAAYA M/MUNGU AWAJAZE KHERI ZAKE. AMIN

SUALA; KUNA UTATANISHI HAPA KUNA MELI IMEPOTEA HAIJULIKANI IMEZAMA AU VIPI(NA HATA KAMA IMEZAMA HATUNA UHAKIKA KAMA HUYO KIJANA KAOKOKA AU VIPI). SASA TUNAOMBA MSAADA WENU SASA JE KIDINI TUSUBIRI KWA MUDA GANI ILI TUMUWEKE KIZUKA MKE WAKE? NA PIA TUDHIHIRISHE MSIBA?

WABILLAHI TAWFIK. TUNAOMBA HILI SUALA MLIPE KIPA UMBELE KWANI NDIO TUMEKAA HATUJUI TUFANYE NINI.

MAASALAM.


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa swali lako zuri na tunamuomba Mola Muweza awe ni mwenye kumrudisha mume salama salimini na Amnusuru na kumhifadhi.

Anapoghibu mume kama ilivyotokea kwa mume huyo katika swali lako, kughibu kwa njia ambayo habari yake imekatika na maisha yake hayajulikani, wanazuoni wametoa hukumu zao tofauti. Huyu mtu anaitwa 'Mafquud' – aliyepotea.

Katika mas-alah haya Wanachuoni wametofautiana, katika rai na kauli zao walizozitoa ni kama zifuatazo:

 

  • Mwanamke hawezi kuolewa wala hana haki ya kutaka kutenganishwa hata muda ukawa mrefu namna gani mpaka itakapobainika kuwa mume amekufa au mke kupewa talaka.

 

  • Mke anatakiwa kusubiri kwa miaka minne kutoka alipoghibu mumewe, kisha ndio atahukumiwa kuwa amefariki. Hapo mke ataanza eda yake ya miezi 4 na siku 10, na baada ya hapo ataweza kuolewa.

 

  • Hakuna njia ya kumzuilia, na ana haki kutaka hakimu (Qaadhi) kuivunja ndoa hiyo: Hiyo ni kuwa lau mke atahofia kuingia katika fitna na maasi basi ni juu yake kuomba kutenganishwa na mumewe asiyejulikana alipo. Kauli hii inachukuliwa kutoka kwa kauli ya jumla ya kuondoa dhara, kama kauli Yake Aliyetukuka: “Wala msiwaweke kwa kuwapa dhara mkaruka mipaka” (2: 231). Na pia kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Haifai kudhuru wala kulipana madhara” (Ibn Maajah, Maalik na ad-Daraqutwniy, nayo ni Hadiyth Hasan).

 

Shari'ah inakubali kutenganishwa huko ili kuondoa madhara kama ilivyo katika mas-alah mengine yaliyomo katika ndoa na mfano wake, na hapa madhara ni makubwa zaidi. Ama kuhusu muda wa kungojea hakuna chochote kilichopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hivyo sio lazima kuwe na muda maalum.

Ama kujuzu kwa mwanamke kuomba kutenganishwa na mume aliyeghibu, hapana shaka kuwa kanuni za shari'ah na misingi yake inatilia nguvu hilo. Hivyo hivyo, Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) walikuwa na rai hiyo hiyo ili mwanamke asiwe ni mwenye kudhurika.

Hivyo ni suala la mwanamke mwenyewe kuangalia uwezo wake wa kungojea na kuvumilia kwa kupotelewa na mume. Kwa hivyo pindi anapohofia fitna atalipeleka suala lake hilo kwa Qaadhi ambaye kwa maslahi ya mwanamke ataivunja ndoa hiyo.

Kwa ufupi, tukichukua mfano ikiwa mume kapotea kwa muda wa miezi minne, sita na kuendelea, na mke akaohisi kuwa baada ya muda huo ameona kuwa hawezi tena kuvumilia, basi atakwenda kwa Qaadhi au Shaykh mwenye kuaminika na kupeleka malalamiko yake. Hapo Qaadhi kwa kuangalia maslahi na madhara yaliyopo, anaweza kuamua kumwachisha mke, naye (mke) ataanza eda yake ya miezi 4 na siku 10.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share