Tofauti Baina Ya Wanawake Na Wanaume Kukimbia Katika Twawaaf Na Sa’y

 

Tofauti Baina Ya Wanawake Na Wanaume Kukimbia Katika Twawaaf Na Sa’y

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Je kuna tofuati baina ya wanaume na wanawake katika kutekeleza tawafu na saiy? Katika kuharakiza mwendo?

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Ipo tofauti baina ya wanawake na wanaume katika kutekeleza Twawaaf na Sa’y. Katika Twawaaf inajulikana kuna kitu kinaitwa ‘Ar-Raml’ nayo maana yake ni kuchepuka (kukimbia kidogo kidogo) katika mizunguko mitatu ya mwanzo.  Ar-Raml ina maana kwamba kuzunguka kwa mwendo wa haraka kwa hatua ndogo ndogo. Kisha anatakiwa atembee mwendo wa kawaida katika Twawwaaf zake nne za mwisho.

 

 

Katika Sa’y ambayo ni baina ya Asw-Swafaa na kuelekea Al-Marwaa mwanamume anatakiwa atembee kwa mwendo wa kawaida mpaka anapofika katika alama ya kijani, hapo atakimbia mpaka alama ya kijani nyingine.  Ataendelea kuelekea Al-Marwaa kwa mwendo wa kawaida. Atakapofikia ataupanda (mlima) na kuelekea Qiblah, atanyanyua mikono na kurudia kusema kama alivyosema alipokuwa Asw-Swafaa. Atateremka Al-Marwah kuelekea As-Swafaa, akihakikisha anatembea sehemu zinazohusika na kukimbia katika sehemu zinazohusika.

 

 

Hikma hiyo ya kuwataka wanaume watembee kwa mwendo wa kukimbia ni kuonyesha nguvu zao na ukakamavu na wanawake hawakujumuika katika kitendo hiki kwani ni maumbile yao kuwa tofauti na wanaume katika nguvu. Hivyo, wanawake watatembea kawaida bila kuwa na haja ya kukimbia mchaka mchaka kama wanaume.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share