Skip navigation.
Home kabah

Elimu Ni Wajibu Kwa Mwanamke Wa Kiislamu

 

Mfumo Na Muelekeo Wa Nyaraka Hizi Umechukuliwa Kutoka Kwa Kijitabu Kinachoitwa

 

“Al-Mar’at Al-Muslimah Fiy Twalabil ‘Ilm”  

(Mwanamke Muislamu Katika Kutafuta Elimu)

 

Kilichochapishwa Na Daarul Arqam,

Chapa Ya Pili,

Mwaka Wa 1411 H/ 1991 M.






 1.0    UTANGULIZI

Sifa zote njema anastahiki Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala), ambaye Ameumba wanadamu, Akawaongoza na Kuwafundisha kwa kutumia kalamu. Akawaongoza pia kwa yale wasio yajua. Swalah na salamu zimshukie yule Aliyetumwa kuwa rehema kwa walimwengu Nabii wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na juu ya ahli zake na swahaba zake na waliomfuata miongoni mwa watu.

Hakika Ummah wa Kiislamu leo unahitaji waliotakasa amali na nyoyo zao kwa kutengeneza yaliyo haribiwa na kurudisha safu pamoja. Hilo halipatikani kwa kuandika vitabu vingi, lakini kwa juhudi, amali na matendo. Bila shaka! Uchapishaji wa vitabu umekithiri na makabati yamejaa kwa mijalada, umekuja wakati ambao tunatamani kuona matendo yenye kuzaa matunda kwa kizazi kitakacho jenga utukufu wa mababu zetu. Hili litapatikana kwa kuchapisha vitabu vya msingi katika elimu ya ufasiri ili kunyanyua bendera ya Uislamu na kutekeleza amana ambayo ametukalifisha Mola Mwenye nguvu na Utukufu pale Aliposema,

Kisha Tukakufanyeni nyinyi ndio wenye kushika mahala pao baada ya (kuangamizwa) hao katika ardhi ili Tuone jinsi mutakavyotenda.

Huku kupatiwa Ukhalifa (uongozi) ni kwa Waislamu sio wengineo, kwani viongozi wa upotevu miongoni mwa makafiri na mushrikina wataupeleka ulimwengu kuvunjika na kuharibika, haya tunayaona leo. Mpaka wajue Waislamu wajibu wao na kuwa ni wenye kuchukua madaraka hawana budi kuwa na elimu na muamko, waondoshe ujinga na kutowachukulia wasiokuwa wao.

Kwa hakika elimu aliyotunukia Muumba wetu Aliyetukuka inatutajirisha kuliko yale yaliyoko katika mikono mwa maadui zetu kwa kanuni na hukumu. Bali ni nuru ambayo kwamba huyafunua yaliyo chini yake katika elimu. Nao ni msingi ambao kwamba ni lazima tujenge juu yake ustaarabu wa mataifa kwani Uislamu ni dini ya ulimwengu. Ni juu ya Waislamu kufanya kazi ili kurudi katika uongozi wa mataifa na kutumia njia zifaazo katika kurudi kwao. Ummah ni mkusanyiko wa familia, nguzo yake ni vijana na wasichana, kina baba na kina mama, watoto kwa wazee na wanaume kwa wanawake. Na juu yao ni wajibu kuamka na kujizatiti katika huo Ummah ili yasiachwe hayo kwa wanaume peke yao. Uislamu umekuja kubainisha hayo katika aya zilizo wazi na Hadithi swahihi. Katika nyaraka hizi hataki kutoa bayana kuhusu haki za mwanamke katika Uislamu kwani huo ni mlango mwengine. Lakini hapa hatuna budi kuonyesha umuhimu wa majukumu ya mwanamke ubavuni mwa mwanamume katika kujenga Ummah na kujizatiti kwayo. Tunaona Qur-aan Tukufu inamkirimu mwanamume na mwanamke sawa sawa, kwa maneno ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala),

 Na hakika Tumewatukuza wanadamu na Tumewapa vya kupanda barini na baharini, na Tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na Tumewatukuza kuliko wengi katika wale Tuliowaumba, kwa utukufu ulio mkubwa (kabisa).

Haya yanachanganya waume na wake barabara na bila ubaguzi wowote. Kama vile jazaa na thawabu kwa amali ni sawa baina ya mwanamume na mwanamke. Hii ni kwa sababu ya kuwa ‘Ibadah zote zinatakikana zifanywe bila ubaguzi wa kijinsia. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) amesema,

 Mola wao Akawakubalia (maombi yao kwa kusema): ‘Hakika Mimi sitapoteza juhudi (amali) ya mfanya juhudi miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke; kwani nyinyi ni nyinyi kwa nyinyi”.

Pia, “Na watakaofanya vitendo vizuri, wakiwa wanaume au wanawake, hali wao ni wenye kuamini, basi hao wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa hata tundu ya kokwa ya tende”.

Pia, “Wafanyaji mema, wanaume au wanawake, Tutawahuisha Maisha mema, na Tutawapa ujira wao (Akhera) mkubwa kabisa kwa sababu ya yale mema waliokuwa wakiyatenda.

Majukumu ni ya wote katika kila jambo wala sivyo kama wanavyodai Mayahudi na Manasara katika Vitabu vyao vilivyobadilishwa kuwa mwanamke ndio sababu ya kutolewa kwa baba yetu Nabii Aadam ('Alayhis Salaam) Peponi na yeye ni mchafu. Bali Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema,

Lakini shaytwaan aliwatelezesha wote wawili (wakakhalifu amri ile, wakala katika mti huo waliokatazwa) na akawatoa katika ile hali ya waliokuya nayo. Tukawaambia: ‘Nendeni, hali ya kuwa maadui nyinyi kwa nyinyi.

Bali katika aya nyengine, Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) anamfanya mwanamume, Nabii Adam ('Alayhis Salaam) kuwa ndiye mkosa. Amesema (Subhaanahu Wa Ta’ala),

Basi wakaula wote wawili, na uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibadika majani ya Peponi. Na Aadam akamkosea Mola wake na akapotea kidogo njia. Kisha Mola Wake Akamchagua na akamkubalia toba yake na Akamuongoa.

 Lakini kitu muhimu ni kuwa baada ya kukosa, walitubia na Mola wao akawasamehe. Imepokewa na ‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Kwa hakika wanawake ni ndugu za wanaume”.

Mwanamke ana jukumu la kutengeneza uchumi kwa kufanya kazi au biashara. Kwa Uislamu ulimpatia haki ya kumiliki mali, haki ambayo haibadiliki hata anapoolewa. Haki hii anaipata kupitia kwa kurithi, zawadi kutoka kwa wazazi, mume, watoto, jamaa zake wengine, kufanya kazi au biashara. Kitu kinajulikana kabisa katika Shari‘ah. Kuhusu haki zao za kurithi, Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema,

Wanaume wana sehemu katika mali wanayoyaacha wazazi na jamaa wakaribu. Na wanawake pia wanayo sehemu katika yale wanayoyaacha wazazi na jamaa wakaribu. Yakiwa kidogo au mengi. Hii ni sehemu zilizofaridhiwa (na Allaah).

 Hata baada ya kuolewa, anachopata mke kwa kufanya kazi au njia nyengine ya halali ni chake na hawezi kupokonywa kwa njia yeyote ile. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema,

 Wanaume wanayo sehemu (kamili) ya vile walivyovichuma na wanawake nao wanayo sehemu (kamili) ya vile walivyovichuma.

Khalifa wa pili muongofu, ‘Umar bin al-Khattab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuachia idara ya kuangalia masoko Shaf‘aa bint ‘AbdAllaah bin ‘Abd Shams (Radhiya Allaahu ‘anhu). ‘Umar alikuwa akitaka ushauri wake, akimheshimu na kumueka katika daraja na cheo cha juu. Zaynab ath-Thaqafiyyah (Radhiya Allaahu ‘anha) mke wa ‘AbdAllaah bin Mas‘ud (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kupitia kwa Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) kama inafaa kuwapatia sadaka na Zakah waume zao. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Watapata ujira (thawabu) mara mbili, moja ya kuunga kizazi na ya pili ni sadaka”.

Katika zama zetu hizi, mbali na tuhma zote walizokuwa wakirushiwa serikali ya Taliban huko Afghanistan, bado wanawake walikuwa wakifanya kazi. Sayyid Rahmatullah Hashemi, katika hotuba yake kama Balozi wa Mambo ya nje, mnamo tarehe 10 Machi 2001 katika Chuo Kikuu cha Southern California, Los Angeles huko Marekani alisema, “Wanawake wanafanya kazi katika Wizara za Elimu, Afya, Mambo ya ndani, Mambo ya jamii, n.k.”

Wanawake wanacheza duru muhimu sana katika kuboresha maadili na malezi bora ya watoto. Ndipo mshairi mmoja wa Kiarabu aliposema, “Mama ni madrasa, ukimuandaa vyema basi umeandaa jamii mzima”.

Jukumu la Jihadi katika aina zake zote, wanawake hawakuachwa nyuma kabisa. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema,

 Allaah Amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali yao (watoe nafsi na mali yao katika kupigania dini) ili na Yeye awape Pepo. Wanapigana katika njia ya Allaah; wanaua na wanauawa.

Historia ya Uislamu ina mifano mingi ya ushujaa wa wanawake ambao walicheza duru muhimu katika vita. Kawaida wao walibaki nyuma ya safu za mapambano kwa kuwatibu na kuwatizama majeruhi, kuwaangalia farasi, kuwatia moyo na hima Waumini wa kiume na mujahidina, kuchukua silaha za makafiri waliokufa, kuwalinda mateka, kupika chakula na kupigana hasa inapo bidi.

‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alichukua kiriba cha maji kuwanywesha majeruhi. Alisaidiwa katika kazi hiyo na Ummu Sulaym (Rumaysaa bint Milhaan) na Ummu Salit (Radhiya Allaahu ‘anha). Ummu ‘Ammarah Nusaybah bint Ka‘b (Radhiya Allaahu ‘anha) alimlinda Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) vilivyo katika Vita vya Uhud. Alipigana katika vita vya Yamamah na kupata majeraha kumi na mbili. Mwana-historia Waqidi alisema kuwa wanawake walikuwa nguzo muhimu katika kutekwa nchi za Shaam, hasa Ummu Hakim, Hind Asmaa, Ummu Katheer, Ummu Abban, Ummu ‘Ammarah, Khawlah, Lubna na Afira. Katika karne ya ishirini, wanawake wamekuwa msitari wa mbele kwa kupinga serikali za kidhalimu. Wengi wao walifungwa na kuadhibiwa vikali kwa mfano Zaynab al-Ghazali, Hamida Qutb, Aminah Qutb, n.k. wakati wa Gamal ‘Abdun-Naasir. Leo Palestina, wanawake wanacheza duru muhimu  na ya msingi katika kupinga udhalimu wa Israili. Mfano mzuri ni wa Ummu Muhammad ambaye watoto wake watatu wa kiume walifungwa katika magereza tofauti na serikali haramu ya Israili na wengine wawili kupelekwa Marj al-Zuhuur nje ya Palestina mwaka 1992 - 3. Yeye mwenyewe aliumizwa kichwani na afisa wa polisi wa Israili mwaka 1981 walipotaka kumshika mtoto wake Muhammad. Mama huyu alisema, “Natamani matumbo yangu yazae watoto ambao wataendelea na jihadi”.

Jukumu jengine ni siasa na kutoa maoni. Kiini cha siasa ni mambo ya watu katika jamii na mambo kwa ujumla wake yanayo husu jamii. Pia ni serikali na idara. Maumbile ya muundo wa Uislamu katika jamii ni muhimu na inawavuta watu wake kujihusisha katika elimu ya kisiasa na kutoa maoni. Shura (kushauriana), Istihsan (ubora/ kipao mbele) na Ijma‘ (kukubaliana) ni mabo ambayo yanawafanya watu kutoa maoni katika mambo yote ya upangaji na masuala muhimu na nyeti.

Waislamu, wanaume na wanawake ni lazima washirikiane kutoa maoni katika mambo ya kuamrisha mema na kukataza mabaya. Kuhusu shura, Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema,

na ushauriane nao katika mambo”. Na pia,Na wale waliomuitikia Mola wao na wakasimamisha Swalah na wanashauriana katika mambo yao…

kushiriki huku si kwa wanaume pekee. Baada ya sulhu ya Hudaybiyah, Waislamu waliona kuwa masharti ya mkataba huo yanawabana wao sana. Walikasirika sana, hata baada ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwaamuru wachinje wanyama na wanyoe nywele na kukariri hayo mara tatu hakuna hata mmoja aliyeinuka kutekeleza wakifikiriya kuwa masharti hayo huenda yakafutwa. Walipomuona yeye  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametekeleza hayo baada ya kufuata ushauri wa mkewe Umm Salamah Hind binti Abi Umayyah Hudhayfah al-Makhzumy (Radhiya Allaahu ‘anha) wote waliinuka kutekeleza maagizo hayo. Mfano mwengine ni uchaguzi wa Khalifah wa tatu, ‘Uthman bin ‘Affan (Radhiya Allaahu ‘anhu), kamati ya watu sita iliyochaguliwa na Khalifah wa pili, ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) ilichukua maoni kutoka kwa wanaume na wanawake kuhusu wanayemtaka awe khalifah. Wanawake wa Uswizi walipata haki hii miaka ya 1950.

Jukumu jengine muhimu na kubwa ni kutafuta elimu, nalo ndio maudhui ya nyaraka hizi. Haya ni baadhi ya majukumu ya wanawake ambayo yanaonyesha umuhimu wake. Huenda haya yakachosha masikio kwa kuwa maudhui ya wanawake na pande zake zote yamechukua nafasi kubwa. Lakini hakika ya maneno juu ya wajibu wa mwanawake kuelekeza kwa nafsi yake, dini yake na jamii yake inatufanya tuyakumbuke kwa kuyarudia kwa ukumbusho unawafaa Waumini. Kisha pia tunasikia makelele yakiita katika kumwacha huru, kumsomesha na kutaka usawa na mwanamume bado yana wafuasi. Inatakikana sisi tupumue kidogo na kutizama: Je, yuko wapi mwanamke wa Kiislamu leo? Vipi tutayafahamu kila yaliyopitika ubavuni mwake? Je, wajibu wake ni upi na yale makelele ya nguvu na mikusanyiko ya wanawake yanayoita katika kumtumikia mwanamke na jamii kwa elimu na amali ya kuieneza elimu?

 

2.0    ELIMU NA UMUHIMU WAKE KATIKA UISLAMU

2.1     SEHEMU YA ELIMU:

Elimu katika Uislamu ina sehemu na daraja ambayo haijapatiwa na dini nyengine yeyote. Hii tunaiona wazi katika aya tukufu inayosema, “Soma kwa jina la Mola wako Aliyeumba”. Kama alivyosema tena Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala),

Sema: ‘Je, wanaweza kuwa sawa wale wanaojua na wale wasiojua?

Dini ambayo maagizo yake ya kwanza ni kusoma na elimu ni dini ambayo inataka wafuasi wake wawe msitari wa mbele katika kusambaza elimu. Huu kwa hakika ni mfumo wa Mola, Ambaye ameifanya elimu kuwa faradhi (lazima) kama ilivyokuja katika Hadithi. Imepokewa na Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Kutafuta elimu ni faradhi kwa kila Muislamu”. Lafdhi ya Muslim (Muislamu) ina makusudio ya wanaume na wanawake kwani imewachang’anya wote bila kubagua.

 

2.2     FADHILA ZA ELIMU:

Uislamu unahimiza elimu na kubainisha ajra kubwa na thawabu kwa mwenye kuitafuta au kusimama katika kuifikisha. Hivi ndivyo alivyofahamu Abu Dardaa (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliposema, “Mwalimu msomi na mwenye kusoma (mwanafunzi) ni sawa katika ajra na wala hakuna kheri kwa watu wote baada yao”. Bila shaka hakuna kheri kwa mujibu wa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwani imepokewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), “Dunia yote imelaaniwa na zimelaaniwa zilizoko ndani yake ila kumtaja Allaah Aliyetukuka na Twaa ya Allaah au msomi au mwenye kusoma”.

Qur’ani imetilia mkazo sana elimu na imetumia maneno mengi yenye kuhimiza shughuli hiyo. Kwa mfano ‘Ilm (yenye maana ya sayansi, elimu na kujifundisha) imetajwa mara 80 na maneno yanayotokana na neon hilo zaidi ya mara mia tatu. Al-Albaab (ufahamu) mara 16, an-Nuha (ufahamu) mara mbili, ‘Aql (akili, ubongo na hisia) mara 49, Fikr (fikiri na tafakari) mara 18, Fiqh (fikihi, ufahamu, elimu) mara 21 na Hikmah (hekima na uoni) mara 20.

Wahyi wa kwanza alioteremshiwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa ni kumuhimiza kusoma japokuwa alikuwa ni Ummy katika pango la Hira. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema,

 Soma kwa jina la Mola wako Aliyeumba. Amemuumba mwanadamu kwa pande la damu. Soma, na Mola wako ni Karimu sana. Ambaye Amemfundisha (binadamu) kwa wasita (msaada) wa kalamu. Amemfundisha mwanadamu (chungu ya) mambo aliyokuwa hayajui

Sayyid Qutb anatueleza kuwa katika wahyi huu wa mwanzo tunapata mafundisho yafuatayo: Allaah ndiye chimbuko la elimu na neema nyingi. Alalah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Amemtukuza mwanadamu kwa kumteremshia wahyi. Hii inatupatia umuhimu kwani elimu imefaradhishwa kabla ya Swalah, Zakah, Swaum, Hajj na Jihaad. Nne, ni kuwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) hakuweka mgawanyo wa elimu - ya dini na dunia. ya mwisho ni kuwa unachosoma chochote usome kwa ikhlasi na kutaka radhi za Allaah”.

Katika aya ya kwanza na ya tatu Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Ametumia neno la Iqraa kwa tensi ya lazima. Kwa hivyo shughuli hiyo ya kusoma ni faradhi kwa wanaume na wanawake. Umuhimu wa jambo hilo la ziada ni kuwa katika hizo aya tano za mwanzo Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) ametumia maneno sita kati ya ishirini kuhimiza na kutilia mkazo elimu (yaani 30%).

Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema tena,

Na wale waliozama katika elimu husema: ‘Tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu’. Na hawakumbuki isipokuwa wenye akili.

 Anasema tena (Subhaanahu Wa Ta’ala),

 Allaah Atawainua wale walioamini miongoni mwenu. Na waliopewa elimu watapata daraja zaidi.

 Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Ametufundisha Du’aa ambayo inatakikana tuiombe kila wakati, “Rabbi zidni ‘ilman - Na (uombe) useme: ‘Mola wangu, nizidishe elimu”.

Ni lazima tufahamu kuwa elimu kwa Muislamu haijagawanywa, ya dini na ya dunia. Bali Uislamu unawahimiza wanawake washindane na wanaume katika kutafuta elimu kwa sababu elimu ni jambo jema na zuri. Kwa hivyo, kushindana na mwenzako katika hasanati (mambo mema) ndio lengo na mulekeo wa shari‘ah ya Kiisalamu. Tunapotafuta elimu ni lazima tuzingatie maneno ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala),

Kwa hakika wanaomuogopa Allaah ni miongoni mwa waja Wake ni wale wataalamu (wanavyuoni).

Ubora wa elimu ya Misingi sio tu inamleta msomi karibu na ukweli, bali humyanyua hadhi yake katika jamii ya Kiislamu na utamaduni wake. Pia tizama aya ya 9 ya sura ya 39 tuliyoitaja kabla.

Kuna Haduthi nyingi zinazotilia mkazo suala la elimu. Elimu ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliipata kupitia kwa wahyi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikihuzunika sana wahyi ulipokuwa unasangaa na alikuwa na pupa ya kutaka kuhifadhi maneno ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) pindi Jibriyl ('Alayhis Salaam) anapomaliza kisomo. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anatuelezea,

Usiutikise ulimi wako kwa (kuufanyia haraka wahyi) Kwa hakika ni juu yetu kuukusanya na kuusomesha. Wakati Tunapokusomea, basi fuata kusomwa kwake. Kisha ni juu yetu kukubainishia.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahimiza watu kusoma kwa dhati, kwa maneno na kuonyesha mfano. Imepokewa na Ibn Mas‘ud (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Hakuna hasadi ila kwa mambo mawili: Mtu aliyepatiwa mali na Allaah na akayatumia katika haki na mtu aliyepatiwa na Allaah hekima naye akaitumia na kuifundisha”.

Imepokewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Mwenye kufuata njia ya kutafuta elimu, Allaah atamsahilishia njia ya Peponi”. Amesema tena (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Yeyote anayeita katika njia ya uongofu atakuwa na ujira mfano wa wale wenye kufuata bila kupunguzwa kitu chochote katika ujira wao”. Amesema tena (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Pindi anapofariki mwanadamu amali yake yote hukatika isipokuwa mambo matatu: sadaka yenye kuendelea, au elimu yenye manufaa au mtoto mwema atakaye kuombea”.

Imepokewa na Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yeyote anayetoka kwa ajili ya kutafuta elimu, yupo katika njia ya Allaah mpaka atakapo rudi”.

Imepokewa na Abi Umamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Fadhila za mwanachuoni juuu ya mwenye kuabudu ni kama ubora yangu juu ya aliye chini miongoni mwenu”. Kisha akasema: “Kwa hakika Allaah, Malaikah zake na viumbe vya mbinguni na ardhini hata chungu katika shimo lake na nyanguni humsalia mwenye kufundisha watu kheri”. Imepokewa na

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yeyote anayeulizwa kuhusu elimu na akaficha, atazuiliwa Siku ya Kiyama ndani ya Moto”.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimuomba Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) amlinde kutokana na elimu isiyo na manufaa. Imepokewa na Zayd bin al-Arqam (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ee, Mola wangu! Najilinda Kwako kutokana na elimu isiyo na manufaa, na moyo usio ogopa na nafsi isiyo shiba na du‘aa isiyo jibiwa”.

Qatadah alisema Ibn Shahir amesema: “Fadhila ya elimu ni bora kuliko fadhila ya ibadah (Sunnah katika ibadah) na ubora wa dini yenu ni kumwogopa Allaah”. Maneno haya hakuyazua bali yametoka kwa maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum). Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema: “Kukaa kwangu saa moja ili kupata ufahamu wa dini ni bora kwangu kuliko kukesha usiku mzima katika ibadah”. Yote haya ni kuwa amali bila ya elimu inaharibika. Haya aliyaweka wazi ‘Umar bin ‘Abdul-‘Aziz aliposema: “Yeyote atakaye tenda pasi na elimu anakuwa ni mwenye kuharibu zaidi kuliko kutengeneza”.

Neema ya elimu ni tunu na zawadi kutoka kwa Allaah aliyetukuka. Kwa kupita wakati inaonekana kuwa mwanadamu amesahau na Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anamkumbusha:

Amemuumba binadamu. Akamfundisha kunena.

Baada ya kuumbwa kwake tunamuona mwanadamu anazungumza, anaweka mambo wazi, anafahamiana na kujibiana na wengine. Haya yote ni utukufu ambao binadamu ameusahau kwa kupitiwa na karne nyingi na Qur-aan ikaturudisha ili kutuamsha katika maudhui kadhaa”.

Elimu ni fadhila kutoka kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) aliyowapatia waja wake. Hapa haifai kukataa mmoja wetu kufadhilisha watu wema waliotangulia elimu juu ya amali za Sunnah. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika hadithi tuliyo itaja mbeleni kuwa: “Fadhila za mwanachuoni juu ya mwenye kuabudu ni kama ubora wangu juu ya aliye chini miongoni mwenu”. Angalia jinsi alivyolinganisha elimu na Utume na vipi alivyoiweka chini daraja ya bila matendo. Hata hivyo mwenye kuabudu anaabudu kila wakati na hangefanya hiyo ibadah kama hangekuwa na elimu. Wasomi wanastahiki daraja hii. Ni rehema kwa Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuliko baba na mama zao. Ikasemwa vipi? Akasema kuwa baba na mama zao wanawahifadhi na moto wa dunia na wao wanawahifadhi na moto wa Akhera.

Ali bin Abi Talib (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimpatia wasia Kumayl bin ziyad akimwambia: “Ewe Kumayl! Hii mioyo inahifadhi basi bora kati yao ni yenye elimu. Hifadhi kutoka kwangu ninayo kwambia: Watu ni aina tatu, Msomi kwa ajili ya Mola wake, mwanafunzi katika njia ya kufaulu na wasio na elimu wenye kufuata mkumbo wa mwenye kuwika. Ewe Kumayl elimu ni bora kuliko mali. Elimu inakulinda lakini wewe unailinda mali. Elimu inatoa uadilifu lakini mali inahitaji uadilifu. Mali yanapungua unapoyatumia lakini elimu inaongezeka. Maarifa ya elimu ni dini inayotegemewa na kwayo anapata mwanadamu twaa katika uhai wake na matokeo mazuri baada ya kufa kwake. Elimu ni hakimu na mali ni yenye kuhukumiwa”. ‘Ali alitoa mashairi kuonyesha ubora wa elimu na wasomi aliposema:

Fakhari ya wasomi pekee                                             Wameongoka na ni dalilikwa wanaotaka uongofu.

Kila mmoja anatukuzwa kwa kadiri ya elimu           Lakini wajinga kwa wasomi ni maadui.

Tafuta elimu nawe utaishi milele                                 Watu wote wamekufa isipokuwa wanavyuoni.

 

3.0    MSIMAMO WA UISLAMU KATIKA KUSOMESHA WANAWAKE

3.1     WAJIBU WA KUSOMESHWA WANAWAKE:

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kutafuta elimu ni faradhi (lazima) kwa kila Muislamu”. Tunaona kuwa mwanamke yumo ndani katika ujumla wa Hadithi kwani Muislamu anakuwa mume au mke na wote ni sawa. Yeyote atakaye ingia katika hukumu za kisheria ataona kuwa kwa hakika wanawake ni ndugu za wanaume wala hawana hukumu hasa kwao wao ila baadhi ya hukumu zinazotofautisha baina ya maumbile ya wanaume na wanawake.

Asili ni kuunganisha sheria na ujumla wa maneno wala haijathubutu utofauti ila kwa dalili. Mwanamke ni sawa na mwanamume katika majukumu ya ibadah za kinafsi (Dhikri, Swalah, Swaumu, Zakah, Hajj, n.k.) na katika maadili na mahusiano (ukweli, uadilifu, wema, taqwa na adabu) na Maisha kwa ujumla (subira, hijrah, kinyume cha ukafiri, twaa, kuwa pamoja na kikundi cha Waumini, urafiki na usaidizi).

Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema:

Bila shaka wanaume wenye kufuata vizuri nguzo za Uislamu na wanawake wanaozifuata vizuri nguzo za Uislamu, na wanaume wanaoamini vizuri nguzo za Imani na wanawake wanaoamini vizuri nguzo za Imani, na wanaume wanaotii na wanawake wanaotii, na wanaume wasemao kweli na wanawake wasemao kweli, na wanaume wanaosubiri na wanawake wanaosubiri, na wanaume wanaonyenyekea na wanawake wanaonyenyekea, na wanaume wanaotoa sadaka (na Zakah), na wanawake wanaotoa sadaka (na Zakah), na wanaume wanaofunga na wanawake wanaofunga, na wanaume wanaojihifadhi tupu zao na wanawake wanaojihifadhi tupu zao, na wanaume wanaomtaja Allaah kwa wingi na wanawake wanaomtaja Allaah kwa wingi. Allaah Amewaandalia msamaha na ujira mkubwa.

Na kwa haya ni bayana kabisa kuwa mwanamke ana haki ya kupata elimu kama ilivyo haki ya kakake. Kama tunavyoona haki yake ya kufundisha. Tunaona kwa uwazi kabisa ile sheria ya taklifu iliyompatia uwezo haijapungua ya mwanamume hasa yanayohusu upande wa jamii na uchumi katika maisha yake. Haya yote hayatimu bila elimu hata lau kwa kadiri ya mambo ya sahali, anaweza kuendesha mambo yake kwa kushirikiana na mwanamume.

Dalili nyengine iliyoonekana kuwa Uislamu unaita katika kumuelimisha mwanamke ni kuwepo wanawake wakati wa Utume, vikao vya elimu. ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa akisikika kwa fatwa  zake na wanawake walikuwa wakijadili rai zake na huku Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yupo pamoja na Makhalifa zake. Mwanamume anahitaji kulingania katika njia ya Allaah (Da‘wah) na wanawake wanalazimika kufanya hivyo. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema:

Na ni nani asemaye kauli bora zaidi kuliko aitaye (viumbe) kwa Allaah na akafanya vitendo vizuri na husema: ‘hakika mimi ni miongoni mwa Waislamu”. Anasema tena Allaah, “Sema: Hii ndio njia yangu ninaita kwa Allaah kwa ujuzi na uoni wa ukweli, mimi na kila wanaonifuata”.

Haya yanakusanya wanaume na wanawake sawa sawa.

Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) katika aya nyengine amelifanya jukumu la Da‘wah kwa wanaume na wanawake kwa kuwataja hasa. Anasema (Subhaanahu Wa Ta’ala):

 Na waumini wanaume na wanawake, ni marafiki na wasaidizi wao kwa wao. Huyaamrisha yaliyo mema na huyakataza yaliyo mabaya…

Uislamu ni dini ya Da‘wah na utangazaji na Da‘wah ni faradhi kwa kila Muislamu mwanamume na mwanamke. Kila mmoja kwa uwezo wa nguvu zake na kwa kadiri ya amali yake na katika mipaka ya sheria iliyo sawa sawa.

Je, inawezekana kwa mjinga kutekeleza faradhi hii? Elimu ni sharuti katika kutekeleza na kufanya Da‘wah. Tunaporudia makaratasi ya Historia ya Kiislamu, tutaona nuru ya watukufu wa kike ambao walitekeleza amana ya Da‘wah katika njia ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) na Mtume Wake na kazi ya kuueneza Uislamu na kuulinda… kuanzia wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na karne zilizofuata mpaka leo.

3.2     FADHILA ZA KUMSOMESHA MWANAMKE:

Mkazo wa kuwapatia elimu watoto umechanganya wavulana na wasichana. Lakini Uislamu umeupatia fadhila kubwa zaidi kuwalea wasichana kinyume na ufahamu wa wajinga wa kale na wajinga mambo leo (wa sasa) ambao walichukia kupata watoto wasichana. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliipandisha hadhi ya tunu hii inayotoka kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala), kwa kuwakaribisha wasichana na kunyanyua umuhimu wa kuwalea kwa maneno yanayowapatia wazazi moyo mkunjufu na bashasha.

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), “Yeyote anayewaangalia vizuri wasichana wawili mpaka wafike utu uzima - yeye na mimi tutakua pamoja Siku ya kufufuliwa, Na hapo alizishikanisha vidole vyake (akimaanisha Peponi)”.

Amesema tena, “Yeyote atakayekuwa na mabinti wa tatu au madada watatu au mabinti wawili au madada wawili, akaishi nao vizuri na kwa wema, akamuogopa Allaah kwa ajili yao - katika riwaya nyengine akawafanyia wema na akawaoza, basi Pepo ni yake”.

Amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Yeyote atakaye walea watoto wa kike watatu, akawafundisha tabia njema na maadili mazuri, akawaoza na kuwafanyia wema, Pepo ni yake”. Katika Hadithi nyengine inasema: “Wao (wasichana) watakuwa ngao kwake na Moto”.

Hii ihsani (wema) ambayo imetajwa katika Hadithi ni uzuri katika malezi na adabu na kukua. Hayapatikani hayo ila kwa elimu ambayo kwamba itahakikisha utamaduni wa kiakili na kuitohirisha nafsi.

3.3     ATHARI YA KUMSOMESHA MWANAMKE:

Aya tuliyoitaja hapo awali ya Surah Fussillat (41: 33 inatuonyesha duru ya mwanamke katika Da‘wah kwani ‘man’ inayopatikana katika aya hiyo

wa man ahsanu qawlan mimman da‘aa inachang’anya wanawake na wanaume. Na mwanamke katika kutekeleza Da‘wah ya kutengeneza jamii yoyote haikosi watu wema. Hawa wema kwa maumbile si wanaume pekee bali na wanawake wamo katika kuleta islahi. Jamii ni kama jengo sehemu moja inasaidia sehemu nyengine. Hapa tutaonyesha wajibu wa kumsomesha mwanamke. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema,

Basi waandalieni nguvu mziwezao (silaha), na mafarasi yaliyofungwa tayari tayari, ili kwazo muogopeshe maadui wa Allaah na maadui zenu…

Nguvu hapa zinachanganya idadi na kutayarisha watu, pesa na maadili. Nguvu zote zitakazo tumika dhidi ya maadui, miongoni mwazo ni kumtayarisha mwanamke Muislamu vizuri ili atekeleze wajibu wake. Miongoni mwa nguvu ni silaha, kwani maadui wa Allaah wanawatumia wanawake katika mipango yao yote ikiwa ni kama askari au kwa njama. Kwa hivyo ni wajibu kwa Waislamu kuwaandaa wanawake matayarisho sahihi. Matayarisho hayo yalipokuwa katika njia hiyo Da‘wah yake ilikuwa ni wajibu na ya sawa na sahihi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewahimiza wanawake kutoa sadaka inapotokea haja hiyo. Nao walitekeleza Da‘wah kwani hizo njia mbili (sadaka na Da‘wah) zinawasaidia madhaifu na masikini na kuitangaza dini ya Uislamu.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtaka Ummu Sulaymaan Shafaa (Radhiya Allaahu ‘anha) amfundishe mkewe, Hafsah bint ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anha) kuandika kama alivyomtaka amfundishe Ruqyah khasa ya kutibu ugonjwa unaoitwa Daan Namlah.

 

4.0    ELIMU ANAZOPASWA KUSOMA MWANAMKE

4.1     KUSAHIHISHA UFAHAMU MBAYA:

Huenda wakaona baadhi ya watu kuwa mwanamke wa Kiislamu hana uwezo wa kusoma na kusomesha. Na kuwa kuna vikwazo vya kisheria ya dini ya Kiislamu vinavyozuia harakati zake katika jambo hili. Muono huu ni wa makosa unaotokana na ufahamu mbaya wa Uislamu, kwani Uislamu ni nidhamu kamili ya Maisha. Yule anayeangalia kwa kina hali ya mwanamke na harakati zake katika chimbuko la Uislamu na duru yake katika historia kuanzia hasa wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Makhalifa Waongofu (Radhiya Allaahu ‘anhum) ataona hayo. Kinachotakikana leo kutoka kwa mwanamke Muislamu ni kujinyanyua kwa kila njia ili atekeleze majukumu yake ya kihistoria na kuutengeneza Ummah.

4.2     MASHARUTI YA MUAMKO:

Uislamu umempatia mwanamke na mwanamume amana ya Dini ambayo ni amana muhimu katika Maisha, bali ndio nguzo na msingi. Uislamu ulimjaalia kila mmoja ni mchungaji hasa katika kusahihisha na kuweka sawa ‘Aqiydah yake, ibadah zake, maadili yake na amali zake. Yule ambaye hatasoma hukumu za ‘ibadah na mafungamano na mahusiano na Allaah na mfumo wa utamaduni … na yule asiyesoma Misingi ya ‘aqiydah na asiye dhamini falsafa ya kweli na muelekeo wa jamii na ubora wa maadili na malengo ya maisha na misingi ya adabu, asiyesoma au kufundishwa haya na yote ni katika milango ya elimu na yenye kuondosha mateso ya ujinga na giza la hisia na maaddah ameingia katika dhambi la kupunguza. Na hapo ameitia nafsi yake katika kazi ya kubaki myuma katika ulimwengu na Akhera.

Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anasema:

 Enyi Mulioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu wenu, na moto ambao kuni zake ni watu na mawe.

Na neno ‘Mulioamini’ linajumlisha Waumini wanaume na wanawake kwa sifa ya mwisho. Hataweza mmoja wao (mume au mke) kujiepusha yeye na watu wake na Moto ila anapojifundisha au kusoma haki ya Mola wake na haki katika maisha yake.

Katika ulazima wa muamko kwa mwanamke wa Kiislamu leo ni kufundishwa mambo ya dini yake. Imepokewa na Mu‘awiyah bin Abi Sufyan (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yeyote ambaye ametakiwa kheri na Allaah, Humfahamisha dini”.

Inabidi mwanamke afundishwe ‘ibadah na maamrisho ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) kama yalivyo katika Suratun Nuur na Ahzaab. Aya za hukumu ni wajibu kwa kila Muislamu mwanamke kuzifahamu wala sio kuzisoma tu, kwani maarifa ya mazingatio na ufahamu na utekelezaji unamfanya yeye ajiamini wakati wa fitna ambao tumeonjwa nao leo na wasiokuwa na dini na wenye kutia shaka na maadui na wanafiki. Hawa wote wanajitahidi kuwaingiza Waislamu katika ujinga usiokuwa na huja wala muongozo kutoka katika Kitabu na Sunnah. Wanajaribu kuukashifu na kuutia aibu na dosari Uislamu na sheria inayomhusu mwanamke. Kwa hivyo ni wajibu kwa wanawake wa Kiislamu kutafuta elimu ya mambo ya dini yake na sheria inayo wahusu wao katika Maisha yao na adabu zao na umbile lao.

Jukumu la mwanamke katika myumba na watoto sio sahali. Imepokewa na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Kila mmoja ni mchunga na kila mchunga ataulizwa kwa alicho kichunga … na mwanamke ni mchungaji katika nyumba ya mumewe naye ataulizwa kwa alicho kichunga…” kazi hii ina pande nyingi, miongoni mwao ikiwa ni ya uchumi, siha na afya, ya jamii, ya malezi na ya idara.

Iliyo muhimu kabisa ni sehemu anayochukuwa ya kulea watoto nayo ni duru ya kunyonyesha kimawazo na adabu, fikra na maadili na huo ni msimamo hatari anaoutoa mwanadamu kwa mwanadamu mwenziwe. Inatakikana asome masomo ya kumuandaa na majukumu ya kukamilisha maarifa na ufahamu wake wa Uislamu mpaka awe kiigizo na uwezo kamili. Mwanamke anachukuliwa mwenye majukumu ambayo yan athari katika Maisha yake ya kifikra na ya kinafsi.

Mfumo huu wa Uislamu unamsaidia mwanamke, bali unamlazimisha kuwa na utamaduni na elimu ambayo hatuioni katika sheria na tamaduni nyenginezo na tunahesabu haya kuwa si maudhui ya khilafu. Kutafuta elimu sio tu haki ya mwanamke bali ni faradhi kwake na ni wajibu wake, ni juu yake au jamii kuchukua nafasi ya dola kumrahisishia hilo. Elimu inatakikana, nayo ni elimu ya dini yake na kila maarifa yanayofungua masikio yake na kuzindua dhamira yake. Kutengeneza maisha yake kwa ujumla na kuyaona kwa Misingi ya umuhimu wake na malengo ya ndoa na umama wa kiroho na kijamii. Na kutekeleza wajibu wake katika kutengeneza hali za hisia na za nafsi ili kutekeleza amali kwa mujibu wa kanuni za kindoa na za mama na hakika ya utu wake na kutekeleza risala ambayo amewajibika kuifikisha katika Maisha yake.

4.3     AINA ZA ELIMU:

Mambo yanayompatia Faida mwanamke Muislamu katika kutafuta elimu ni Hadithi inayofuata. Imepokewa na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Elimu ni aina tatu, mbali na hizo ni fadhila: Ayah muhkamah, au Sunnah qaimah au faridhah ‘adilah”.

Hadithi hiyo juu inatufahamisha kwa uhakika elimu zilizo faradhi. Nazo ni kama zinazofuata:

·   Ayah Muhakamah ni elimu ambazo zinazo bainisha halali na haramu katika Uislamu.

·   As-Sunnah al-Qaimah ni ambazo zinaelezea Kitabu cha Allaah na kuzielezea kwa kina.

·   Al-Faridhah al-‘Adilah ni elimu ambayo inampatia kila mwenye haki, haki yake. Inaingia faradhi hii kwa Muislamu yale mambo ambayo wanazuoni wameita Faradhi Kifaya. Nayo ni kusoma masomo yatakayokuwa na maslahi kwa Waislamu na Uislamu. Imaam al-Ghazali anatueleza yafuatayo: Ama Faradhi Kifaya katika elimu ni masomo yote yanayosimamisha mambo ya kidunia, kama utabibu (udaktari) kwani ni dharura kuiweka miili katika siha mzuri na hesabu ambayo ni dharura katika mahusiano na kugawanya mirathi na wasia na nyenginezo. Na masomo haya lau yakiachwa na watu katika nchi basi watu wake watakuwa katika makosa. Lakini anaposimama mtu mmoja ambaye atatosheleza katika kutekeleza wajibu basi wengine watakuwa hawana makosa. Wala usione ajabu kwa maneno yetu kuwa udaktari na hesabu ni katika Faradhi Kifaya. Pia Misingi ya utengenezaji wa vitu (sinaa) na siyasa, ushonaji na kuumika (hajjamah), ukulima na kufuma ni miongoni mwa Faradhi Kifaya”.

Masomo aliyoyataja Imaam al-Ghazali ni kwa njia ya mfano wala sio yote. Kusoma kwa wanawake katika elimu hizi na nyenginezo ni miongoni mwa Faradhi Kifaya na zipo ndani ya fani muhimu. Msingi wa Fikihi unasema, “Isipotimia wajibu ila kwa jambo Fulani basi jambo hilo pia linakuwa ni wajibu”. Kwa hivyo, elimu ya Lugha ya Kiarabu inaingia katika kuufahamu Ayah Muhkamah na Sunnah Qaimah. Elimu ya hesabu inaingia katika kuufahamu Faradhi ‘Adilah.

Tukizungumzia ufahamu wa fani na mgawanyo wa Faradhi Kifaya tutaona masomo kadhaa yaliyotajwa na Imaam al-Ghazali yanaingia katika fani za kike. Nazo ni udaktari, ushonaji, kuumika na tunaweza kuongezea nyenginezo kama ualimu, biashara, ukunga, n.k. Tunatakikana tusisahau msingi wa pili unaosema: “Dharura inakadiriwa kwa kiasi chake”. Inayozidi kile kipimo cha dharura, ndio Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekiita fadhila au ziada, na hukumu yake katika Fikihi ni kuruhusiwa.

Ni vizuri zaidi awe daktari anayetibu wanawake, mwanamke mfano wao. Mwalimu wa wanawake na watoto wadogo awe mwanamke. Kusimama kwa mwanamke katika mambo haya muhimu kama kusomea udaktari, ualimu, malezi ya watoto na kufanya Da‘wah kwa wengineo. Pia wanatakiwa wajitahidi waingie katika nyanja za elimu za vitu hai (Zoology), utaalamu wa madawa (Pharmacy), saikolojia na elimu ya jamii, malezi ya kujenga utu wa watoto na elimu ya kutumia njia za kisasa na mawasiliano kuandaa magazeti, majarida, vipindi vya idhaa katika redio na runinga na kutumia kompyuta katika Da‘wah na kufundishia.

Uhandisi mekaniki haujaharimishiwa mwanamke katika Uislamu lakini si maslahi ukilinganisha na maumbile yake. Sisi hatutakikani tubadilike kwa kasi kubwa kama ilivyobadilika Bara Ulaya kitu kilichopelekea kuzorota kwa maadili. Tusibadilike kufuata mila na desturi za Wazungu zinazoenda kinyume na akhlaqi za Kiislamu.

5.0 DURU YA WANAWAKE WA MWANZO KATIKA KUSOMA NA KUENEZA ELIMU

Hakika duru ya mwanamke Muislamu katika historia ya Uislamu, historia ya Da‘wah na historia ya mataifa na watu imesajili upeo wa ubora, utukufu na utakaso katika nyaraka. Sote tunajua na kuelewa yale aliyoyafanya Mama wa Waumini Bibi ‘Aishah bint Abubakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) katika kuhifadhi Hadithi nyingi pamoja na kuzisomesha. Huyu bibi mtukufu alikuwa anaulizwa maswali mengi na wakubwa miongoni mwa Masahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) katika mambo mengi ya dini.

Historia ya Kiislamu imesajili kwa herufi za nuru na dhahabu majina ya Sahabiyat watukufu (Radhiya Allaahu ‘anhum) mfano wa Asmaa bint Abubakr, Umm ‘Atiyyah al-Ansariyah, Umm Kabshah Qadha‘iyah, Asmaa bint ‘Umays, Umm Sulaym bint Milhan, Umm Dardaa na fatimah bint Qays (Radhiya Allaahu ‘anha), wote walikuwa wapokezi na waalimu wa Hadithi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kulikuwa na mwanamke amabaye alikusanya  Qur-aan. ’Allamah Sh. Dkt. Yusuf al-Qaradhawi anatuelezea: “Al-Hafidh Jamalud Deen as-Suyuty amemtaja mwanamke aliyekusanya Qur’ani lakini hajahadithia hayo mtu yeyote. Naye ni Umm Waraqah bint ‘AbdAllaah bin al-Harith (Radhiya Allaahu ‘anhu). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikumwa akimzuru na kumuita Shaheedah. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuamuru asalishe watu wa nyumbani kwake na alikuwa na muadhini. Aliuliwa na kijana aliyekuwa mtumwa wake wakati wa Ukhalifa wa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu). hapo ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema, ‘Amesema kweli Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alikuwa akisema: Twende pamoja tumzuru (tumtembelee) Shaheedah”.

Tunaporudia majina ya wanawake Muhaddithaat wa kipindi cha Tabi‘in tutaona majina mengi. Miongoni mwao ni Fatimah bint Siirin, Zaynab bint al-Muhajir, Safiyyah bint Shaybah, ‘Aishah bint Sa‘d bin Abi Waqqas na wengineo. Imaam Ahmad bin Hanbal katika Musnad yake pekee ametoa idadi inayafikia wanawake hamsini. Na huko Cordoba, Spain (wakati wa utawala wa Waioslamu baina ya 711 - 1492) kulikuwa na takriban Mafakihi wa kike sitini miongoni mwa Mafakihi wa Kiislamu ambao walishughulika kutoa Fatwa. Katika nyumba zao waliekewa taa. Taa hizo zilikuwa haziwekwi ila katika nyumba za watu wa Fatwa na Fikihi.

Alikuwa Fatimah bint Muhammad bin Ahmad as-Samarqandi mwandishi wa “Tuhfatul Fuqahaa” ambaye alipata elimu na ufahamu mikononi mwa babake. Alihifadhi Tuhfah na akaolewa na ‘Alaad Deen bin Abubakr mwandishi wa “Al-Badai‘”. Mumewe alikuwa akikosea naye akimrekebisha. Fatwa zilikuwa zikija na zinapotolewa nje zilikuwa na hati yake na ya babake. Alipoolewa Fatwa zikawa zinatoka na hati yake kwenye karatasi, hati ya babake na mumewe.

Wakati wa Sa‘eed bin al-Musayyab, Tabi‘i mkubwa na mtukufu aliyeteswa kwa misimamo yake katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah. ‘Abdul-Maalik bin Marwan, Khalifa wa tano wa dola hiyo alikwenda kumposea mwanane binti ya Sa‘eed ambaye alikataa. Baadae Sa‘eed alimuoza bintiye mwanafunzi wake aliyekuwa masikini lakini mchaji Allaah. Baada ya harusi, mume alikuwa anataka kila wakati kwenda kusoma kwa mwalimu na baba mkwe lakini mkewe alikuwa anamwambia kaa hapa nami nitakufundisha elimu ya Sa‘eed.

Aliandika Abu Muslim al-Farahiidi mtaalamu wa Hadithi juu ya wanawake sabiini waliokuwa huru na watumwa ambao walishindana katika nyanja ya Tarbiyah (malezi). Mwandishi wa msabaka huo alikuwa mwanamke ambaye alihadithia katika karne ya sita Hijri na sauti ikawa inasikika kwa mbali na halaiki ya watu.

Ni mambo gani ambayo yamefanya wanawake Waislamu wasifikie mifano ya mabibi hawa watukufu? Hasa tukiangalia kuwa sisi tunaishi katika vita vigumu na mapambano yasiyomalizika. Mapambano dhidi ya vita vya kifikra za Msalaba (Manasara) na hujumu kali na ya kukinaisha kutoka kwa Uzeyuni wa Kimataifa na Ujamaa (Ukomunisti) wa kilimwengu juu ya Uislamu na Waislamu katika kila sehemu na Pembe zote za dunia. Maadui wote hawa wanawafanyia Waislamu ubaya na kuonyesha kuwa Uislamu na wafuasi wake ni mdudu adui wa wanawake na elimu. Kuongezea yale wanayo yachapisha kwa kutoa Maelezo mabaya dhidi ya Uislamu na kueneza Misingi yenye kuua na kuvunja.

6.0    HAJA YETU YA MWANAMKE MUISLAMU MWENYE MUAMKO

Bila ya shaka, Ummah wa Kiislamu unahitaji wanawake wasomi wenye kufanya kazi ambao watasimama katikakujenga watoto watakaoshiriki katika muelekeo uliobarikiwa na muamko na kuelewa majukumu yao. Hamu yao ni kuzitakasa nafsi zao na za waume wao, watoto wao na kila kitakachorudisha katika Ummah wa Kiislamu nguvu na utukufu. Jambo hili ni wajibu liwe katika akili yake anapolala na kuamka na wala asiwe ni mwenye kushughulishwa na mambo mengi ya Maisha ambayo yamewasahaulisha kuhusu ndugu zao Waislamu na dini yao. Ni vizuri sana muamko wao uzinduliwe katika kutekeleza na kuwasaidia Waislamu wenziwao na Uislamu kwa nia mzuri, ikhlasi na kutaka ridhaa ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala).

6.4     DHARURA YA MUAMKO:

Kwa hivyo, hapana budi kumpatia ujuzi Muislamu mwanamke ambaye anaipendelea mazuri jamii kwa kuyabeba majukumu pamoja na mwanamume. Muamko unamfungulia msichana njia ya utekelezaji mwingi ambao atafahamu katika hicho kipindi ukweli wa Maisha bila kuyakuza au kuyafanya madogo. Muamko unafungua mlango wa mbele kwa msichana kuweza kuwa na uoni wa mbali na kuona njia za matendo, kazi na changa moto. Kwa njia hii atakuwa na uwezo zaidi wa kuwa na msimamo wa imara katika nyanja ya mapambano.

Muamko, kabla ya yote hayo inamjaalia msichana awe na ufahamu wa Imani na ukweli wa Uislamu. Hivyo anayafunga matendo yake kwa kutafuta radhi za Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala). Maadili yake yanaimarika kwa uwongofu wa sheria na mapendeleo yake yanakuwa na hofu ili asije akaipenda fitna na ufisadi. Muamko ni kipimo muhimu ambacho mwanamke na mwanamume wako sawa. Lakini sisi tutafuata njia itakayo saidia hilo.

Kipimi kinakua kwa kuongezeka Imani na kujikita ndani ya nafsi ya mwanamke na mwanamume. Itazidi kuongezeka kwa kuamsha hisia ambazo ni za kufuatilia maamrisho ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) na atabaki kuangalia Siku yahesabu na kudumu kufukiria Akhera. Hivyo hivyo, hiyo inapanuka kwa kupanuka maarifa na majaribio. Maarifa ya uhakika ya jamii ambayo imetuzunguka na ufahamu wa majaribio ambayo yameelezwa na wanavyuoni na wale walio wakweli kabla yetu na pia mitihani yaliyotukia.

Pindi atakapoweza mwanamke kutizama mambo kwa macho ya ukamilifu na kwa njia inayowafikiana na uoni wa Kiislamu wa Maisha, atazidi kuwa na muamko kwa Maisha haya na ufahamu wa mambo. Na atakapoweza kujua majukumu yake ya hakika katika kujenga jamii ya Kiislamu na kuyapanga mambo yanayotakiwa kupawa kipao mbele na yaliyo muhimu katika Maisha yake, bila shaka muamko utavama ndani na uoni wake utafunguka.

Muamko unapatikana kwa kuwa mbali na ujinga, ufahamu mdogo, uoni wa sehemu na kujikalifisha kwa mambo ya nje.

6.5     NJIA YA KUPATA MUAMKO:

Maadamu muamko umekusanya yote hayo, hatokuwa tayari mwanamke Muislamu kwa uharaka unaohitajika na hakuna budi kwa malezi ya pole pole na kuazima mfumo wa masomo ya yaliyopita na ya sasa ili juhudi hizi kuzaa matunda na kutoa natija mzuri kwa kufungua masikio na kuuwekea umuhimu.

Hapana budi kabla ya hayo kurudisha mazingatio katika urithi wetu wa zamani wa Uislamu na ufahamu wetu ambao tumeupata kutoka hapa na pale. Kurudi katika Kitabu cha Allaah, Aliyetukuka (yaani Qur’ani) mwanzo kabisa kwa kuisoma kikweli na kwa ikhlasi. Hivyo kuhakikisha kuwa mmoja amepata darasa ya kina na ufahamu wa uoni na mazingatio, inafungua njia kubwa kwa kuweka wazi muamko katika nafsi. Pindi nafsi itakapokuwa wazi kwa kupata maana ya Qur’ani Tukufu ina fanana na ardhi yenye rutuba inayongoja kupandwa mbegu na miche ili yatoe miti yaliyo imara na matunda yaliyo mazuri kabisa.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni Qur’ani inayotembea katika ardhi na aliwatayarisha Masahaba - wanaume kwa wanawake wawe katika hali hiyo. Maamrisho yote yaliyomo ndani ya Qur-aan yalikuwa yanatekelezwa barabara bila herufi moja kuanguka.

6. ATHARI YA MUAMKO KATIKA SHAKHSITA YA MWANAMKE:

Muamko utakapopatikana kwa mwanamke Muislamu ataweza kuutoa na kuzalisha matokeo mazuri.

·   Wakati huo atafahamu Uislamu wake kwa njia iliyo wazi na kamili, bila kuichukua kuwa ni sehemu ndogo wala kuchukua Pembe moja na kuacha nyengine.

·   Atafahamu Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), atafanya juhudi kupata maarifa hayo na kuyafanyia kazi katika aina zote za adabu na rangi tofauti za maisha.

·   Atafahamu kuwa na istiqaamah (kuwa na msimamo) katika dini na hasa katika zama hizi za sasa. Japokuwa hali zimekuwa ngumu lakini ataishi kwa kumtegemea na kumuamini Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala). Hivyo anapata utulivu kwa kuridhiwa Naye (Subhaanahu Wa Ta’ala) hata balaa na shida ikizidi namna gani.

·   Anaweza kuondoa shaka na kuitoa katika nafsi yake. Pia anamaliza unyonge na kuogopa na anajua kuwa atafuzu mbele ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) maadamu anashikilia hii dini. Kwa hivyo hatamuogopa yeyote isipokuwa Allaah pekee.

·   Atahakikisha na kupata katika nafsi yake aina ya ulinzi wa kibinafsi katika uso na umbele wa mashambulizi. Utamaduni wa kisasa ambao umenyanyua bendera ya kijinsi na kuchukua njia ya kueneza ufisadi wa kizazi na kupiga vita maadili na kutoa hukumu juu ya ‘aqeedah.

·   Muamko huu unamlinda na kumfanya afuate Maisha ya Kiislamu yaliyotakasika. Hivyo atajitokeza mbele ya wasichana wa jinsi yake kwa sura iliyo ya juu na mzuri, hapigi vita maumbile ya kibinadamu alioumbiwa nayo na Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) wala haumii na dhiki za moyo ambazo zimeanzishwa na utamaduni wa mijini.

·   Naye anafanya kazi ya jamii kwa njia yenye kuleta natija mzuri, anaita kwa maadili na matendo yake na kuwa yeye ni kiigizo na mfano mzuri wa wakati huo. Ataweza kulingania kwa njia mzuri kila mtu na kwa usawa na kuweka wazi ukweli wa Maisha kama laivyosoma katika Qur’ani na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

·   Naye atatoka katika duara ya taqleed (kufuata kama kipofu) mbovu ambayo imezuliwa na mashetani wa sasa kwa kupotosha katika jina la kukaa uchi na kubadilisha mambo kwa kufuata mambo ya kisasa yanayokwenda kinyume na Dini. Yeye anamiliki uhuru wake wa uhakika kuweza kuishi kama mwanamke anayetukuzwa mbali na macho ya kumdhalilisha na kumtweza na misimamo ya kumkandamiza.

·   Hivyo hivyo ameleta athari njema katika jamii kwa njia ya adabu na fikra na kutekeleza amali na mawaidha mazuri na yaliyo wazi.

Miongoni mwa muamko wa mwanamke Muislamu ni kuyachukulia umuhimu yanayotendeka katika Maisha ya Ummah na yanayo wafikia Waislamu katika mambo maovu ambayo anatakikana ayakataze. Pia katika mambo ya upotevu na kutoka katika mipaka ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mfano wa Waumini katika kupendana kwao na kurehemeana kwao na kuoneana huruma kwao ni kama mfano wa mwili. Pindi kinaposhtakia kiungo ndani yake, mwili wote unakosa usingizi na kuwa na homa”. Dkt. Abdul-Kareem Zaydan amesema yafuatayo alipokuwa akiielezea Hadithi hiyo  juu katika kitabu chake, Ama kuchukulia umuhimu wa mambo ya Waislamu kwa ujumla ni katika haki yake (mwanamke) bali ni wajibu wake. Miongoni mwa mambo ya Waislamu ni haja zao kwa ujumla ambazo wanazirekebisha au kulalamika. Katika umuhimu wa nje ni kufikiria haja zao na kueneza ufahamu wa Uislamu ambao utamleta mwanamke karibu na mumewe, watoto wake, jamaa na majirani. Yeye ana haki ya kutoa rai yake katika mambo ya kawaida na ya jumla na kutoa nasiha kwa njia anayoweza  na kufuatana na maumbile yake kama kuandika vitabu, kuandaa mikutano ya wanawake na kuwafundisha na kueneza maadili na adabu tukufu ndani yao na kuwahimiza katika kutekeleza wajibu wao na mfano wa hayo na kuwaepusha maovu na uchafu.

Na katika jambo hili amesema al-Bahi al-Khouli, Hivyo ni kuwa mwanamke Muislamu wa mwanzo hakudang’anya nyanja kwa upofu au kupoteza au kujiachilia bali alijifunika kwa matayarisho na mipango ya wazi. Jamii ilikuwa inamuita kwake ili achukue sehemu yake katika safu iliyo imara, kusaidiana juu ya kipimo na maslahi na muelekeo wate wenye kupimika na wa kiroho. Hakutoa mkono wake wala hakuwa peke yake … Na kwa mipango hii na maandalizi hakutoweka kwa fikra zake na kuwepo kwake katika kuona umuhimu kwa mambo ya jamii. Huenda akawa mwanamke wa pekee katika historia ya dunia ambaye kwamba umuhimu alioweka katika mambo kwa jumla hayapungui wala hayazidi ukilinganisha na umuhimu wa mambo yake hasa”.

Hakuna ajabu kwa hayo kwani sheria ya Kiislamu imempatia wizani na uhuru katika nyanja zote za maisha hata akawa anashiriki mashauri ya jamii na kutoa nasaha zake. Haya yalionekana katika kisa cha shura baada ya kuuliwa kwa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kushiriki wanawake. Amesema Ibn Katheer katika Al-Bidayah wan-Nihayah, Kisha akaanza ‘Abdur-Rahman bin ‘Auf (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuchukua rai za watu kuhusu wao (yaani ‘Athman bin ‘Affan na ‘Ali bin Abi Talib). Akajumlisha rai za Waislamu kwa rai za viongozi wa watu kwa pamoja na mmoja mmoja, wawili wawili na walio peke yao, aliojumuika kwa siri na Dhahiri mpaka akamalizia kwa wanawake waliokuwa wamekaa nyumbani”.

Mwanamke katika sheria amepatiwa uwezo wa kumiliki na kutumia mali na kufanya biashara. Qaylah bint Umm Bani Atmar amesema, “Mimi ni mawanamke ninaye uza na kununua”.

Kwa haya tunamalizia kuwa mwanamke Muislamu mwenye muamko na uoni na mwenye kushindana na kuwa na juhudi anahitajika. Jamii leo ina haja kubwa sana ya wao kwani kujenga jamii ya Kiislamu inahitaji wenye silaha ya imani na muamko na kujua malengo na kuyaendea kwa kujiamini na uoni.

7.0    MIFANO YA WANAWAKE WATUKUFU

7.1     UMMUL MU’MININA ‘AISHAH BINT ABUBAKR AS-SIDDIQ:

Alizaliwa mwaka wa 4 Baada ya Utume (614 BI). Babake alikuwa ni ‘AbdAllaah bin ‘Uthman bin ‘Aamir at-Taymi au Abu Bakr as-Siddiq bin Abi Quhafah. Mamake alikuwa Umm Ruman bint ‘Aamir bin ‘Uwaymir al-Kananiyah. ‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa ni msomi, mwenye akili, uoni wa hali ya juu na uwezo wa kutatua mambo nyeti na mazito ya Dini. Alikuwa msitari wa mbele katika upokeaji wa Hadithi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), nambari sita miongoni mwa Masahaba wote (Radhiya Allaahu ‘anhum). Amepokea Hadithi 2,220, miongoni mwa hizo 174 zikiwa ni Muttafaqun ‘alayhi, 54 katika al-Bukhari, 67 katika Muslim, na 2,017 katika vitabu vyengine vya Hadithi. Alikuwa mjuzi sana katika elimu za Qur’ani, Hadithi, Fikihi, Mashairi, Historia na Nasaba. Anahesabiwa miongoni mwa Mujtahid na jina lake linatajwabila ya shaka pamoja na yale ya Abu bakr, ‘Umar, ‘Athman, ‘Ali, Ibn Mas‘ud, Ibn ‘Abbas na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhum). Alikuwa akitoa fatwa wakati wa Abu Bakr, ‘Umar na ‘Athman.

‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa na fadhila kubwa kuliko wanawake wote. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ubora wa ‘Aishah kulinganisha na wanawake wengine ni kama ubora wa tharid kwa aina nyengine ya vyakula”.

Alikuwa mwalimu mzuri na mkubwa na alifundisha elimu kutoka kizazi kimoja mpaka chengine. Aliwafundisha wasichana, wavulana na watu wazima. Alitumia njia tofauti ya kufundisha kama kutoa muhadhara na baadae wanafunzi kuuliza maswali, mchanag’anyiko wa mazungumzo na mjadala au wakati mwengine wanafunzi walikuwa wakiuliza maswali na yeye akatoa majibu ya kina au wanafunzi na mwalimu walikuwa wakijadili bila vikwazo au pingamizi yeyote. Mayatima wa Madinah walipata uanagalizi maalumu na matumizi yao yalishughulikiwa na ‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha). Baadhi ya wanafunzi walikuwa wanatizamwa na kulelewa naye.

Idadi ya watu waliofaidi kutoka kwake walikuwa ni wengi. Walionawiri zaidi ni:

·   ‘AbdAllaah bin Zubayr, mtoto wa dadake ‘Aishah aliyekuwa akiitwa Asmaa.

·   Aswad.

·   ‘Urwah bin Zubayr, aliyekuwa mtoto wa Asmaa na mdogo wa ‘AbdAllaah bin Zubayr. Huyu aliinukia kuwa mwanachuoni mkubwa Madinah.

·   Qaasim bin Muhammad, mtoto wa kakake, ambaye alikuwa mwanachuoni mkubwa wa sheria.

·   Abu Salamah bin ‘Abdur-Rahman, ambaye alikuwa mwanachuoni maarufu wa Hadithi.

·   Masruq, kijana kutoka Iraq, ambaye baadae alikuwa mwanachuoni wa juu kabisa katika sheria huko Iraq.

·   Imam Nakhai, kutoka Iraq.

·   ‘Amrah bint ‘Abdur-Rahman, msichana wa Ki-Ansaar. Alikuwa msichana hodari sana, hivyo kupendwa sana na ‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha). Hadithi zilizokusanywa wakati wa utawala wa Khalifa ‘Umar bin ‘Abdul-‘Aziz zilikaguliwa na yeye.

‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alisema: “Nimepatiwa vitu ambavyo hakupatiwa mwanamke mwengine yeyote. Niliposwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nikiwa miaka saba. Malaikah alimletea sura yangu mkononi mwake ili aniangalie na nilianza kukaa naye nikiwa miaka tisa. Nilimuona Jibril ('Alayhis Salaam) na nilikuwa mke niliyependwa zaidi kuliko wote. Alipokuwa mgonjwa (Mtume) na baadae kufariki, hakushuhudiwa na mwengine isipokuwa na mimi na Malaikah. Katika riwaya nyengine alisema: Hakuowa bikra ila mimi wala mwanamke wazazi wake waliohama isipokuwa mimi. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) aliteremsha kutoka mbinguni aya za kujulisha kuwa sina makosa. Wahyi ulikuwa ukiteremka nami niko naye (Mtume). Tulikuwa tunaoga kutoka chombo kimoja na alifariki katika nyumba yangu na siku yangu na akazikwa katika chumba changu”.

Kuhusu elimu yake Masruq amesema, “Nimewaona Masahaba wazee miongoni mwa wale waliokuwa wakubwa wakimuuliza kuhusu mirathi”. Naye ‘Ataa bin Abi Rabah amesema, “‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha) ni Fakihi mkubwa na mwenye elimu miongoni mwa watu”. Amesema Hisham bin ‘Urwah kutoka kwa babake kuwa, “Sijamuona yeyote mjuzi wa Fikihi wala utabibu wala mashairimfano wa ‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha)”. Amesema Abu Burdah bin Abi Musa kutoka kwa babake kuwa, “Hatukuwa na tatizo lolote la jambo tukamuuliza ‘Aishah isipokuwa tulimpata anayo elimu kuhusu jambo hilo”.

‘Aishah aliaga dunia tarehe 17th Ramadhan 58 BH (13th Julai 678 BI) usiku wa Jumanne. Salah yake ya Jeneza iliongozwa na Abu Hurayrah.

Wake wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa ni wataalamu wa mambo ya Dini na walikuwa wakifundisha elimu hizo na kuzisambaza. Hafsah bint ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa anajua kuandika na kusoma. Ummu Salamah Hind bint Abi Umayyah (Radhiya Allaahu ‘anha) alipokea Hadithi nyingi na ni wa pili miongoni mwa wakeze Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

7.2     UMMU SULAYM BINT MILHAN:

Alikuwa anaitwa Rumaysaa bint Milhan bin Khalid bin Zayd bin Kiraam kutoka katika ukoo wa Khazraj. Alikuwa ni mwanamke mrembo, mwenye akili na rai mzuri, mkarimu na hodari. Kwa sifa hizi tukufu aliposwa na kuolewa na mtoto wa ami yake aliyekuwa akiitwa Malik bin nadhr na kuzaa mtoto Anas. Mwangaza wa Uislamu ulipoingia Madinah Umm Sulaym alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kusilimu. Hakujali kwa yatakayomfika. Wa mwanzo kuwa kikwazo kwake ni mumewe aliporudi safari, ambaye alimghadhibikia lakini yeye hakujali. Alimsilimisha mtoto wao mbele ya mumewe. Mumewe akawa anamwambia usimharibu mtoto wangu, lakini alijibu kuwa yeye anamfundisha adabu na nidhamu.

Mume alipoona kuwa mkewe ana azma ya nguvu kuliko mwamba alitoka nyumbani na huku amekasirika na hapo kukutwa na adui yake na kuuliwa. Baada ya hapo alimpeleka mtoto wake Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huku anaona haya na kumtaka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amchukue mtoto wake ili amtumikie. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimkubali na watu wakawa wanahadithia kuhusu Anas na mamake kwa ajabu. Abu Talhah aliposikia habari ya kufa kwa mumewe alienda ili kutaka kumposa kwa mali nyingi, lakini Umm Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) alikataa kwa kuwa yeye ni kafiri. Abu Talhah alikuja siku ya pili na kutaka kutoa mali zaidi. Lakini Daa‘iyah Umm Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) mbali na kuona mali mbele yake, jaha na ubarobaro alikataa kwa kusema: “Naapa kwa Allaah! Mfano wako ewe Abu Talhah hawarudishwi. Lakini wewe ni mtu kafiri na mimi ni mwanamke Muislamu. Haifai kwangu kuolewa na wewe, lakini unaposilimu tu hayo yatakuwa mahari yangu na wala sitakuuliza kitu chengine”.

Abu Talhah alishangazwa na maneno haya kwa kuona kuwa Ummu Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) si mwanamke wa kuchezewa. Yeye alikuwa ni mwanamke mwenye akili ambaye anakataa kuvutiwa na dunia. Hakujitambua ila ulimi wake unarudia shahadah. Umm Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) akamuangalia mtoto wake, Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) nae anasema kwa utukufu mkubwa kuwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) amemuongoza Abu Takhah kupitia kwa mkono wake. Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisimama hapo kumuoza Abu Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu) mamake. Kwa hayo alisema Thabit rawi wa Hadithi kutoka kwa Anas: “Sijasikia kabisa mwanamke aliyekuwa na mahari matukufu na ya ukarimu kuliko Ummu Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha). Mahari yake yalikuwa Uislamu”.

Aliishi Ummu Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) na Abu Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu) maisha ya ndoa yaliyosimama juu ya msimamo wa Kiislamu ambao umewapatia dhamana mume na mke maisha ya utulivu na mazuri. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Aliwapatia mtoto ambaye kuja kwake kulileta furaha na wakampatia jina Aba ‘Umayr. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Akawapatia mtihani kwa kumchukua mtoto mzuri waliompenda baada ya kuwa mgonjwa kwa muda. Wakati huo babake alikuwa amekwenda Msikitini. Mama huyu muumini alikubali matokeo haya kwa kusubiri na huku ameridhika kwa kusema: “Tunatoka kwa Allaah na Kwake tutarudi”. Aliwaambia watu wake, “Musimpashe Abu Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu) mpaka mimi mwenyewe ni muelezee habari hiyo ya kifo”.

Aliporudi Abu Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu), machozi ya rehema ya Umm Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) tayari yalikuwa yamekauka na alikuwa tayari kumpokea mumewe na kujibu maswali yake. Aliuliza, “Je, mtoto yu hali gani?” Akasema, “Yuko katyika hali bora kabisa”. Akadhania kwa utulivu na raha ya mkewe kuwa mtoto yu salama. Umm Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) alimletea mumewe chakula na kuvaa nguo mzuri kabisa, akajipamba na kujipaka manukato. Mumewe alipojitosheleza naye alimshukuru Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala). Ilipofika mwisho wa usiku alisema, “Ewe Abu Talhah! Waonaje ikiwa watu wamekukopesha kisha wakahitaji amana yao. Je, utawanyima?” akasema, “La!” Akasema tena, “Utasema nini watakapo gawa nusu na kutaka amana yao baada ya kufaidika nayo”. Akasema, “Hawakufanya haki”. Akasema, “Hakika mtoto wako ulikuwa ni mkopo kutoka kwa Allaah na Amemchukua”. Abu Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuweza kumiliki yaliyomsibu, hivyo kusema kwa hasira: “Umeniacha mpaka nilipoingiwa na doa ndipo uliponieleza kuhusu mtoto wangu”. Aliendelea kumkumbuka mpaka aliporudi Nyuma na kumshukuru Allaah na nafsi yake kutulia. Kulipopambazuka alikwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumhadithia yaliyotokea. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Allaah awabariki kwa usiku wenu”. Huo ndio usiku wa kushika mimba Umm Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha)  na kuzaliwa kwa ‘AbdAllaah bin Abi Talhah. Alipozaliwa alipatiwa Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) ampeleke kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitia tende mdomoni na ilipokuwa laini akamtilia mdomoni mwa mtoto. Akasema Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu), “Mpatie jina ewe Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”. Akasema, “Yeye ni ‘AbdAllaah”. Alisema ‘Ubabah mmoja wa watu katika isnadi, hakika nimewaona watoto wa huyu kijana wote wakiwa wamehifadhi Qur’ani.

Juu ya mama huyu mtukufu na mumewe muumini, Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) aliteremsha aya ambayo watu wataisoma mpaka Siku ya Mwisho. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, “Alikuwa mtu muhitaji na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa na chochote katika nyumba zake. Akasema: ‘Nani atakayemkirimu mgeni huyu Allaah atamrehemu’. Abu Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu)  akasema, ‘Mimi ewe Mjumbe wa Allaah’. Alipofika kwa mkewe (Umm Sulaym) alimuuliza, ‘Je, una chochote?’ Akasema, ‘La! Isipokuwa chakula cha watoto’. Akasema: ‘Wapumbaze na vitu mpaka walale. Atakapoingia mgeni wetu tumuonyeshe kama tunakula. Atakapoanza kula inuka ufanye kama unatengeneza taa kishe uizime’. Naye alifanya hivyo na mgeni akala mpaka akashiba na wao pamoja na watoto wakalala na njaa. Alipoamka alikwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alimwambia: ‘Hakika Allaah Ameona ajabu - au Allaah amefurahi na Fulani (mume) na Fulani (mke)”. Katika riwaya nyengine: “Allaah amestaajabu kwa kitendo chenu kwa mgeni wenu wa usiku. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Akateremsha aya inayosema:

…Na wanawapendelea kuliko nafsi zao ingawa wenyewe wana hali ndogo.

Ummu Sulaym (Radhiya Allaaha ‘anhu) alikuwa na daraja kubwa mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambaye hakuwa akienda nyumba nyengine yeyote isipokuwa yake. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimbashiria pepo aliposema: “Niliingia Peponi nikasikia sauti ya viatu. Nikasema nani huyu? Nikaambiwa, huyu ni Rumaisaa bint Milhan, mamake Anas bin Malik”.

Pongezi kwako ewe Umm Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) kwani unastahiki yote hayo. Ulikuwa mke mwema mwenye kutoa nasaha njema na Daa‘iyah mwenye hekima na mama mlezi mwenye muamko. Ulimuingiza mtoto wako katika Madrasa bora na kubwa zaidi iliyojulikana na ulimwengu, Madrasa ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye hajafika hata miaka kumi. Na kwa hivyo akawa mwananchuoni miongoni mwa wanavyuoni wa Uislamu.

7.3     SHAFAA’ BINT ABDALLAAH:

Ummu Sulayman Shafaa’ bint ‘AbdAllaah bin al-Harith, alikuwa Mqureshi katika ukoo wa ‘Adiy. Alisilimu kabla ya Hijrah na miongoni mwa watu wa mwanzo kuhama Madinah. Pia alikuwa miongoni mwa Waumini waliombai (kumuahidi) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) waliotajwa katika Qur’ani Tukufu. Alikuwa mwanamke mwenye akili na mbora wao na msomi miongoni mwa wasomi wa Kiislamu. Alikuwa na elimu nyingi na Imani.

Aliolewa na Abu Hathmah bin Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kutunukiwa mtoto aliyeitwa Sulayman. Shafaa’ (Radhiya Allaahu ‘anhu) alijifundisha kusoma na kuandika alipokuwa Makkah na kabla ya kusilimu. Aliposilimu aliwafundisha Waislamu wanawake akitarajia thawabu kutoka kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala). Kwa kazi hiyo akawa mwalimu wa kike wa kwanza wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Miongoni mwa wanafunzi wake ni Hafsah bint ‘Umar al-Khattab (Radhiya Allaahu ‘anhu), mke wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Inafahamika kuwa Shafaa’ alikuwa akifanya ruqyah wakati wa Ujahiliyyah. Aliposilimu alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu jambo hilo na kumuonyesha alivyokuwa akifanya. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimruhusu kuendelea na kumuambia amfundishe Hafsah.

Alijifunza Hadithi nyingi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuwa akiita watu katika Uislamu na kutoa nasaha kwa wote. Wamepokea kutoka kwake mtoto wake Sulayman, wajukuu zake AbuBakr na ‘Uthman bin Sulayman, Abu Salamah bin Abdur-Rahman, hafsah Ummul Mu’minina na mjakazi wake Abu Ishaaq. ‘Umar bin al-Khattab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akimtanguliza katika rai, akimtaka ushauri na kumheshimu. Pia alimtawalisha idara ya kuangalia mambo ya masoko. Naye alikuwa akimheshimu ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu). Alikuwa mkweli, kiigizo kizuri katika kusuluhisha, Uchaji Mwenyeezi Mungu na uadilifu. Siku moja aliwaona vijana wanatembea pole pole na wanazungumza kwa taratibu. Akasema: “Hii ni nini?” Wakasema: “Huu ni utawa”. Akasema: “Naapa kwa Allaah! Alikuwa ‘Umar anapozungumza anasikika na anapotembea anakwenda haraka na anapopiga anaumiza”.

Aliaga dunia mwaka wa 20 BH. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) amrehemu kwani aliutumikia Ummah huu katika mambo ya kheri. Anatakikana awe kielelezo chema kwa wasichana ili nao wasiwe mabakhili kwa kuitoa elimu waliyo nayo na kuwafundisha wengine katika njia ya Itikadi ya kumridhisha Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala).

7.4     MIFANO MENGINE:

Asmaa bint Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mtu wa kumi na saba kusilimu na kumbai Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akamuamini Imani ya nguvu. Mamake alikuwa akiitwa Qatilah bint ‘Abdul ‘Izzy. Alipokuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na babake wanahama, yeyepamoja na kuwa mja mzito alikuwa akiwapelekea chakula katika Pango la Thaur. Alipata adha mkononi mwa adui wa Allaah, Abu Jahl ambaye alikuja nyumbani na kuuliza: “Kenda wapi babako?” aliposema kuwa hajui, Abu Jahl alimzaba kofi la uso, hata vipuli vyake vikamdondoka na uso ukamwiva mwekundu. Hivi ndivyo wanavyofanya waoga kila zama, wakishindwa kuwapiga na kuwaua wanaume wanawapiga wanawake na watoto.

Ndiye muhaji wa kwanza wa kike kuzaa Madinah mtoto aliyeitwa ‘AbdAllaah. Mumewe alikuwa ni Zubayr bin Awwam (Radhiya Allaahu ‘anhu). Alikuwa shujaa asiyeogopa kitu katika njia ya Allaah. Wakati mtoto wake ‘AbdAllaah alipouliwa na Hajjaj bin Yusuf Makkah na mwili wake kusulubiwa, Hajjaj alikwenda kwa Asmaa na kumwambia: “Ewe mamangu! Hakika Amirul Mu’minin ameniusia juu yako. Je, una haja ya chochote?” Akasema: “Mimi si mama yako, lakini mama wa aliyesulubiwa. Nami sina haja, lakini ninakuhadithia kuwa nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ‘Atatoka kutoka Thaqeef mwongona mharabu’. Ama muongo tumemuona (akimaanisha Mukhtar na ama mharabu ni wewe”. Katika riwaya nyengine zinaeleza kuwa Hajjaj alipoingia kwa Asmaa (Radhiya Allaahu ‘anha) alimwambia: “Umeonaje jinsi nilivyomfanya mtoto wako, ewe Asmaa?” Akasema kwa utulivu: “Umeiharibu dunia yake, na yeye ameiharibu Akhera (mwisho) wako”.

Asmaa (Radhiya Allaahu ‘anha) alikufa siku chache baada ya kuuliwa mtoto wake ‘AbdAllaah (Radhiya Allaahu ‘anhu), Mfungo Nane (Jamadil Awwal) mwka 73 BH hapo Makkah. Alikufa akiwa mzee lakini hakutoa jino hata moja wala hakupoteza akili. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) amrehemu kwani alikuwa mfano mzuri wa ushujaa na subira.

Tunapata mfano wa Ummul Kulthum bint ‘Ali bin Abu Talib (Radhiya Allaahu ‘anhu), ambaye alikuwa mke wa Khalifa wa pili, ‘Umar bin al-Khattab (Radhiya Allaahu ‘anhu) walipokwenda usiku wa manane kuwahudumia mume na mkewe aliyekuwa na uchungu wa kuzaa.

Sumayyah bint Khayyat (Radhiya Allaahu ‘anha) ni mfano wa mwanamke aliyesilimu mikononi mwa mtoto wake ‘Ammar (Radhiya Allaahu ‘anhu). hapo ulianza mtihani kwa familia ya mama huyu ya kuteswa na kuadhibiwa lakini waote walisimama imara. Abu Jahl kuona uimara wa Sumayyah (Radhiya Allaahu ‘anha) alimuua kutumia mkuki na roho yake safi yenye Imani ikatoka. Hapo akawa shahidi wa kwanza katika Ummah huu wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hapa tunapata mfano mwema wa utukufu, ushujaa, istiqamah na Imani na kujitolea mhanga kwa kufa katika njia ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala).

Mfano mwengine ni Asmaa bint yazeed bin as-Sakan katika ukoo wa Aws. Alikuwa mzungumzaji mzuri, mujahidah mtukufu, mwenye akili na ufahamu wa dini na khatibah mpaka akaitwa khatibah wa wanawake. Kama wanawake wengi waliohitimu katika madrassah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hawakujua kujisalimisha katika maneno, wala kukubali udhalilifu wa kuzama kwa cheo bali walikuwa na ushujaa, uthabiti na uimara na juhudi walizowaletea mabanati jinsi yao mfano katika kila nyanja. Alikuwa akisikiliza Hadithi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hakuogopa wala kuona haya kuuliza maswali hata yakiwa nyeti namna gani katika mambo ya dini. Yeye ndiye aliyeuliza njia ya kujitahirisha kwa mwanamke na hedhi.

Asmaa (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa akiwakilisha wanawake katika kuzungumza na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mara moja alikuja na kusema: “Ewe Mtume wa Allaah! Mimi ni mjumbe Nyuma yangu kuna kundi la wanawake Waislamu wote wanasema ninayo yasema. Na wao wana mfano wa rai yangu … Hakika Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) amekutumiliza kwa wanaume na wanawake, tumekuamini na kukufuata. Na sisi kongamano la wanawake tuna upungufu, tunakaa majumbani mwetu na sehemu ya kuwatimizia matamanio wanaume zetu na kuwabebea watoto wao. Wanaume wana fadhila kwa kuhudhuria jamaa, kushuhudia janaza na jihadi. Wakitoka kueleke katika jihadi tunawahifadhia mali zao na tunawalea watoto wao. Je, tutashirikiana katika thawabu, ewe Mtume wa Allaah?” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwazungukia Masahaba zake na kusema: “Mumesikia maneno ya mwanamke. Je, kuna suali lililo bora zaidi katika dini yake kuliko hili?” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema tena: “Ewe Asmaa! Nenda uwaambie wanawake walio Nyuma yako ni bora mmoja wenu akae vizuri na mumewe katika Maisha ya ndoa na kutaka radhi yake na kufuata anayoyataka basi hayo yatakuwa sawa na mambo yote uliyoyataja ya wanaume”. Akaondoka Asmaa (Radhiya Allaahu ‘anha) na huku anatoa tahlil na takbir kutoa bishara njema kwa aliyo yasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Alishiriki katika vya vya Yarmuk na kuwaua Warumi tisa kwa kutumia kipande cha hema. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) amrehemu kwa juhudi zake kwa zile Hadithi alizozipokea na zile darasa muhimu tulizopata kutoka kwake kwa kutoona haya katika kuuliza masuala ya haki na ya dini. Alifariki mwaka 30 BH>

Umm Hiram bint Milhan (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa miongoni mwa Ansaar. Anasema Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu): “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anakwenda Quba alikuwa alikuwa akiingia kwa Umm Hiram ((Radhiya Allaahu ‘anha) na kula. Umm Hiram (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa mke wa Ubadah bin Saamit (Radhiya Allaahu ‘anhu). Siku moja alikwenda Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na baada ya kula akajinyosha na kulala. Baadae aliamka na huku anacheka. Umm Hiram (Radhiya Allaahu ‘anha) akasema, ‘Ni kipi kinacho kuchekesha ewe Mtume wa Allaah?’ Akasema, ‘Watu katika Ummah wangu wameonyeshwa kwangu wakipigana katika njia ya Allaah. Wamepanda meli kwenye bahari kubwa mfano wa wafalme juu ya mateka’. Akasema Umm Hiram (Radhiya Allaahu ‘anha), ‘Ewe Mtume wa Allaah! Niombee kwa Allaah niwe miongoni mwao”. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuombea kisha akalala tena, lakini akaamka tena na huku anacheka. Umm Hiram (Radhiya Allaahu ‘anha) akasema: “Ewe Mtume wa Allaah ni kipi kinacho kuchekesha?” Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Nimeonyeshwa watu katika Ummah wangu wakipigana katika njia ya Allaah mfano wa wafalme juu ya mateka’. Akasema: ‘Ewe Mtume wa Allaah! Niombee Allaah niwe pamoja nao’. Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Wewe uko pamoja na wale wa mwanzo’. Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema: Alitoka Umm Hirama pamoja na mumewe na walipofika baharini, meli ilipanda mnyama na kuvunjika naye akaaga dunia. Hivyo vilikuwa Vita vya Cyprus na akazikwa hapo. Amiri wa jeshi hilo alikuwa ni Mu‘awiyah bin Abi Sufyan (Radhiya Allaahu ‘anhu) katika Ukhalifa wa ‘Uthman (Radhiya Allaahu ‘anhu)”. Huo ulikuwa ni mwaka wa 27 BH. Umm Hiram (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa shahidi wa kwanza wa bahari.

Bila pia kuusahau mfano wa Tamadhir bint ‘Amr bin al-Harith (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye ni maarufu kwa jina Khansaa. Alikuwa mshairi mkubwa. Wakati wa Vita vya al-Qadisiyyah wakati wa Ukhalifa wa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwakusanya watoto wake wanne usiku ili kuwaelekeza na kuwahimiza wapigane kishujaa katika vita na wasirudi Nyuma. Aliwafanya wapende kufa mashahidi katika njia ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala). Hebu tupulikize wasiya wake mwema, alipowaambia: “Enyi watoto wangu! Nyinyi mumesilimu kwa kupenda kwenu na mulichagua kuhama. Naapa kwa Allaah, Ambaye hapana Mola ila Yeye kuwa nyinyi ni watoto wa mwanamke mmoja. Baba yenu hakufanya hiyana wala halati yenu hakuleta fedheha wala sikuchang’anya nasaba yenu wala sikubadilisha ukoo wenu. Nyinyi mnajua aliyowaandalia Allaah Waislamu kwa thawabu kubwa katika kupigana na makafiri. Na jueni kuwa nyumba yenye kubaki ni bora kuliko nyumba yenye kuondoka. Amesema Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala): ‘Enyi Mlioamini! Subirini na muwashinde makafiri (katika kusubiri), na kuweni imara (nyoyo zenu) na mcheni Allaah ili mpate kufuzu’. Mutakapo amka kesho InshaAllaah mukiwa salama jiandaeni kupigana na adui kwa uoni, hamasa na kwa hamu. Na Allaah Atawapatia nusra juu ya maadui. Mutakapoona vita vimeshamiri juu ya miguu na kuwaka moto wa kufululiza na moto kufinika njia za kupitia basi tieni nia ya kufanya bidii na mpigeni raisi wao kwa kuukata ushujaa wake, mutashinda kwa kupata ghanima (ngawira) na utukufu wa milele na cheo…” Siku ya vita vijana wote walipigana kwa ushujaa na wote wakafa mashahidi. Habari ilipomfikia mama Muumini mwenye kusubiri, hakubabika, hakuhuzunika wala hakulia juu yao bali alisema maneno yake mashuhuri ambayo historia yameyanukuu na kuyarudia. Haya maneno yatabaki kurudiwa mpaka atakapo penda Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala). Alisema: “Sifa zote njema anastahiki Allaah ambaye amenitukuza kwa kuwapatia Shahada. Naomba kwa Mola wangu anijumuishe nao katika makao ya rehema Yake”.

‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliutambua ubora wa Khansaa na watoto wake (Radhiya Allaahu ‘anha), hivyo kuendelea kumpatia sehemu ya chakula cha watoto wake mpaka alipofariki. Khansaa (Radhiya Allaahu ‘anha) alikufa jangwani mwaka 24 BH, mwanzo wa kipindi cha Ukhalifa wa ‘Uthman (Radhiya Allaahu ‘anhu). Huu ni mfano mwema wa subira na malezi mazuri kwa watoto na kutoa nasaha ambazo kila mwanamke anatakiwa aige. Naye alipatiwa jina la Umm Shuhadaa (mama wa mashahidi). 

 Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwabashiria wanawake ishirini Pepo kama alivyowabashiria wanaume kumi. Hawa wanawake walipata bishara hiyo kwa dauru kubwa waliocheza katika kuutetea na kuutumikia Uislamu. Nao ni Khadijah bint Khuwaylid, ‘Aishah bint AbuBakr, Hafsah bint ‘Umar, Zaynab bint Jahsh [hawa wanne walikuwa wake za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)], Fatimah bint Rasuul, al-Fari‘ah bint Malik, Ummu Mundhir bint Qays, Asmaa bint AbuBakr, Ummu Sulaym bint Milhan, Ummu Hiram bint Milhan, Ummu Waraqah bint ‘AbdAllaah al-Ansariyah, Asmaa bint Yazeed, Umm Hisham bint Haarithah, Fatimah bint Asad, Ummu ‘Ammarah Nusaybah bint Ka‘b, Ummu Ruuman Zaynab (au Da‘d) bint ‘Aamir, Barakah bint Tha‘labah, ar-Rabi‘ bint Mu‘awwadh, Sumayyah bint Khabbat na Kabshah bint Raafi‘.

Hii ni baadhii ya mifano ya wanawake watukufu waliotuachia kielelezo kizuri cha sisi kufuata. Wametuonyesha mwangaza katika giza la usiku na kutufundisha mengi lau tutayatilia maanani basi tutafaulu hapa duniani na kesho Akhera. Wametuachia mifano katika kutafuta elimu na kusomesha, katika biashara na kufanya kazi, katika nyanja zote za Jihadi na malezi ya watoto. Walicheza dauru yao muhimu na kuwaachia wanawake majukumu lau watayatekeleza basi tuhma zote dhidi ya mwanamke wa Kiislamu zitaondoka na maendeleo yatapatikana.

8.0    HITIMISHO

Hakika mwanamke Muislamu mwenye muamko, msomi na mwalimu, ni mtu anayejenga na mfanya kazi ni miongoni mwa wafanya kheri na anayeleta baraka kwa Ummah huu. Na huenda akasema msemaji kuwa bila shaka elimu leo, tunamshukuru Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) imeenea sana na kiwango cha wenye elimu ni kikubwa na ujinga ni mchache sana ikiwa haupo kabisa. Lakini mwenye kuangalia elimu iliyozagaa leo anaona elimu iliyo karibu kwa maana ya elimu ya kuandika na kusoma pekee. Laiti ingekuwa katika daraja ya juu ya kisomo na usahihi. Je, hiyo ndiyo elimu ambayo itajenga Ummah? Dkt. An-Nafeesy amesema katika kitabu chake ukurasa wa 17: “Napenda kusajili hapa kuwa masomo peke yake huenda yasiwe ni hatua ya kusonga mbele katika haki ya mwanafunzi. Mara nyingi haya hutegemea maumbile ya mfumo wa elimu na masomo na dhamana ya kijamii, kisiasa na kiitikadi”

Hivyo, ikiwa masomo yamejazwa na fikra za kimagharibi haitotumikia Uislamu hata ikiwa watamaliza mamia na maelfu kila mwaka na wala haimanishi kuwa hiyo ndiyo elimu inayohitajika na kuimbiwa. Elimu zote kwa ujumla zikiwa zinaleta kheri kwa wanadamu, sisi tutazipokea bila kujali nchi zinazotoka au kabila walizozitoa. Kizazi cha kwanza cha Ummah huu wamechukua elimu za mataifa mbali mbali zilizopita. Lakini wao walizibadilisha katika muelekeo wa Kiislamu na wakazihami na Itikadi, maadili na adabu tukufu. Kwa njia hiyo, ustaarabu huo wa Kiislamu ulitoa matunda ulioangaza mashariki na magharibi ya ardhi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza sana kuwa busara na elimu ni haki ya Muislamu pale aliposema: “Hekima ni kitu kilichompotea Muislamu, popote anapoipata ana haki zaidi (kuichukua)”.

Kwa hivyo ni wajibu wa dada Muislamu katika kutafuta elimu ajiepushe na athari za utamaduni wa kimagharibi au kujaalia kutokana na elimu kuwa ni njia ya kupata kazi katika hali zote. Leo tunaona kuwa elimu imechkuliwa kuwa njia ya kuandikwa kazi. Msichana anayepata Shahada (cheti) bila kupata kazi anahasirika katika masomo yake na umri wake ambao ameutumia bila ya kupata matunda. Muelekeo huu unawafanya watoto wetu (wavulana na wasichana) kuwa ni watu wa masikio ya kazi. Hawafikirii Misingi kwani elimu katika mipaka yao ni lengo wala sio njia. Kisha, bila shaka elimu katika zama hizi za sasa ni mtihani wa balaa wenye athari ya mbali na hatari kubwa. Hatari hii ni ya mchang’anyiko baina ya wasichana na wavulana na mambo haya ni wajibu tusifuate na tuwalinde vijana na hatari zake.

Sayyid Rahmatullah Hashemi amesema: “Hatuna shida (yaani serikali ya Taliban) yeyote na elimu ya wanawake. Tumesema tunataka elimu… kwani hiyo ni sehemu ya Itikadi yetu. Tumeamrishwa kufanya hivyo … Ni kweli kuwa tunapinga mchang’anyiko katika elimu lakini si kweli kuwa tunapinga elimu ya wanawake. Hivi karibuni tumefungua kitengo cha utabibu katika miji yote mikubwa ya Afghanistan na Kandahar. Wako wasichana wengi zaidi wanaosoma katika kitengo cha utabibu kuliko wavulana”.

Mwisho kabisa tunataka wasichana wa Kiislamu watie niya upya katika kutafuta elimu ili iwe hiyo niya kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) pekee. Lengo la kusoma liwe ni kuleta muamko na kujenga dola ya Kiislamu na kuleta faida katika kila nyanja na fani tofauti. Yote haya yatekelezwe kwa kutaka radhi za Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala), Aliyesema:

Sema: ‘Je, wanaweza kuwa wale wanaojua na wale wasiojua? Wanaotanabahi ni wale wenye akili tu.

Waingereza wana msemo unaosema: “When you teach a woman, you teach the family (Unapomfundisha mwanamke, umeifundisha familia)”. Na Mshairi mmoja wa Kiarabu amesema: “Mama ni Madrasa, ukimuandaa umeandaa jamii mzima.”