Majina Ya Manabii 25 Kama Walivyotajwa Katika Qur-aan Na Mpangilio Wao

 

Majina Ya Manabii 25 Kama Walivyotajwa Katika Qur-aan Na  Mpangilio Wao

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Kama nilivyo sema hapo juu mimi naomba majina ya Rusuli 25 walivyo kuja kwa utaratibu na unaweza kunichambuli vyema kama huyu ni baba wa huyu wabilahi tawfiq asalamaalaykum

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu kwa swali lako.

 

Pamoja na kwamba inasemwa kuwa idadi ya Manabii wanafika hadi 124,000 kutokana na baadhi ya mapokezi, lakini Hadiyth hizo zimedhoofishwa na hivyo hatuwezi kuzitegemea, ila kuna Hadiyth ambayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyosimuliwa na Abu Dhar ambayo alimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) idadi ya Manabii (‘Alayhim wa sallam) na akamjibu kuwa ni mia tatu na makumi kadhaa. Hadiyth hiyo imeelezwa usahihi wake na Imaam Al-Albaaniy kama ilivyo hapa chini:

 

عن أبي ذر ، قال : قلت : يا رسول الله ! أي الأنبياء كان أول ؟ ! قال : آدم ، قلت : يا رسول الله ! ونبي كان ؟ ! قال : نعم نبي مكلم ، قلت : يا رسول الله : كم المرسلون ؟ ! قال : ثلاث مئة وبضعة عشر ؛ جما غفيرا .
الراوي: أبو ذر الغفاري  -  خلاصة الدرجة: صحيح  -  المحدث: الألباني  -  المصدر: مشكاة المصابيح  -  الصفحة أو الرقم
: 5669

 

Kutoka kwa Abu Dhar ambaye amesema: Nilisema: Ee Rasuli wa Allaah, Nabiy yupi wa mwanzo? Akasema: ((Aadam)). Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah, alikuwa ni Nabiy? Akasema: ((Ndio Nabiy aliyesemeshwa)) Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah. Wapo Manabii wangapi? Akasema: ((Mia tatu na makumi kidogo)) [Mishkaat Al-Maswaabiyh ikiwa na daraja ya Swahiyh]

 

Hata hivyo idadi iliyotajwa katika Qur-aan ni Rusuli 25 pekee na dalili ni kauli ya (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

  وَرُسُلاً قَدْ قَصَصْنَاهُمْ عَلَيْكَ مِن قَبْلُ وَرُسُلاً لَّمْ نَقْصُصْهُمْ عَلَيْك 

Na Rusuli Tuliokwishakusimulia kabla; na Rusuli (wengine) Hatukukusimulia.[An-Nisaa: 164] 

 

Rusuli 18 wametajwa kwa pamoja katika Aayah 4 zifuatazo zinazofuatana:

 

وَتِلْكَ حُجَّتُنَا آتَيْنَاهَا إِبْرَاهِيمَ عَلَىٰ قَوْمِهِ ۚ نَرْفَعُ دَرَجَاتٍ مَّن نَّشَاءُ ۗ إِنَّ رَبَّكَ حَكِيمٌ عَلِيمٌ ﴿٨٣﴾ وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ ۚ كُلًّا هَدَيْنَا ۚ وَنُوحًا هَدَيْنَا مِن قَبْلُ ۖ وَمِن ذُرِّيَّتِهِ دَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ وَأَيُّوبَ وَيُوسُفَ وَمُوسَىٰ وَهَارُونَ ۚ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿٨٤﴾  وَزَكَرِيَّا وَيَحْيَىٰ وَعِيسَىٰ وَإِلْيَاسَ ۖ كُلٌّ مِّنَ الصَّالِحِينَ ﴿٨٥﴾ وَإِسْمَاعِيلَ وَالْيَسَعَ وَيُونُسَ وَلُوطًا ۚ وَكُلًّا فَضَّلْنَا عَلَى الْعَالَمِينَ ﴿٨٦﴾

Na hiyo ndio hoja Yetu Tuliyompa Ibraahiym juu ya watu wake.  Tunampandisha cheo Tumtakaye. Hakika Rabb wako ni Mwenye hikmah wa yote, Mjuzi wa yote. Na Tukamtunukia Is-haaq, na Ya’quwb. Wote Tukawahidi. Na Nuwh Tulimhidi kabla. Na katika dhuria wake Daawuwd, na Sulaymaan, na Ayyuwb, na Yuwsuf, na Muwsaa, na Haaruwn. Na hivyo ndivyo Tulipavyo wafanyao ihsaan.  Na Zakariyyaa, na Yahyaa, na ‘Iysaa, na Ilyaas. Wote ni miongoni mwa Swalihina. Na Ismaa’iyl, na Al-Yasa’a na Yuwnus, na Luutw. Na wote Tuliwafadhilisha juu ya walimwengu. [Al-An’aam:  83-86]

 

Manabii na Rusuli waliotajwa katika Qur-aan kwa mpangio wa ujio ni kama ifutavyo:

 

1.                 Aadam

2.                 Idriys

3.                 Nuwh

4.                 Huwd

5.                 Swaalih

6.                 Ibraahiym

7.                 Luutw

8.                 Ismaa'iyl bin Ibraahiym

9.                 Is-haaq bin Ibraahiym

10.               Ya'quwb bin Is-haaq bin Ibraahiym

11.               Yuwsuf bin Ya'quwb bin Is-haaq bin Ibraahiym

12.                Shu'ayb

13.                Ayyuwb

14.                Dhul Kifl

15.                Muwsaa

16.                Haaruwn nduguye Muwsaa

17.                Daawuwd

18.                Sulaymaan bin Daawuwd

19.                Ilyaas

20.                Alyasaa'

21.                Yuwnus

22.                Zakariyyaa

23.                Yahyaa bin Zakariyyaa

24.                'Iysaa bin Maryam

25.                Muhammad

(Swalla Allaahu 'alayhim wa sallam)

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share