Tashahhud: Kusema السَّلامُ على النَّبي Badala Ya Kusema السلام عليك أيّها النبي

SWALI:

Asalam Aleikum.

Baada ya kumshukuru Allah (s.w) na kumtakia rehma Mtume (s.a.w) ningeomba kuwashukuru ndungu zangu kwa website hii yenye faida kwa jamii.

Suali langu ni, kwenye Atahiyatu kwenye swala kwenye kumswalia Mtume unasema ASALAM ALAIKA AYUHA NABIYU au SWALU ALA NABIY. Kwani kuna ndugu amesema kua maswahaba walikua wakisema SWALU ALA NABIY baada Mtume (s.a.w) kufariki.

Shukran. Wabillah Tawfiq

  



JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu Tashahhud. Inaonekana kulingana na swali lako hukumuelewa vizuri huyo ndugu aliyekuambiwa hayo kwani katika Tashahhud hakuna kusema Swallu 'alan Nabiy. Hakuna riwaya hata ya kutungwa ambayo inatueleza hilo.

 

Hata hivyo, inaonyesha kuwa katika kuandika au kusikia ima ulisikia au uliandika makosa badala ya Assalaamu 'alan Nabiy ukasikia au ukaandika Swallu 'alan Nabiy. Hili tamko ambalo umeliandika mara nyingi hutumiwa na baadhi ya watu katika mihadhara na mawaidha wakitaka kuwarudisha watu katika kusikiliza mawaidha kwa kusema Swallu 'alan Nabiy, ingawa haya ni mambo yasiyothibiti na yasiyo na dalili. Kwa hiyo, tutajaribu kukuelezea kwa mujibu wa haya marekebisho ambayo tumeyafanya ili kuwe na faida kwa wasomi wa tovuti hii yenu. 

 

Uislamu kama ulivyo umewekewa vitu sahali na vyepesi kwa maslahi yetu sisi binadamu. Jambo hili humfanya kila mwanadamu anayefuata nidhamu hii kuweza kutekeleza maagizo bila kuchoka wala kuona shida. Kwa ajili hiyo ndio Allaah Aliyetukuka Akatuambia:

'Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini' (22: 78).

Na tena:

'Allaah Anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito' (2: 185).

 

Na kuhusu sifa kemkemu alizokuwa nazo Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam), Allaah Aliyetukuka Anasema: '… anawaamrisha mema na anawakataza yaliyo mabaya, na kuwahalalishia vizuri na kuwaharimishia vibaya, na kuwaondolea mizigo yao na minyonyoro iliyokuwa juu yao' (7: 157). Mizigo hii ni ile sheria ngumu waliokuwa Mayahudi wameamriwa kufuata.

 

Kwa minajili hiyo, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) akawa anawafundisha Maswahaba zake na hivyo kutufundisha sisi hasa katika duaa na adhkaar nyingi katika jambo moja ili iwe rahisi kwetu kufuata. Ikiwa Muislamu ameshindwa kuhifadhi du’aa moja ambayo ni ngumu au ndefu basi kwa jambo lile zipo sahali na fupi kwake kuweza kuhifadhi.

 

Tukija katika Tashahhud kama vile katika rukuu au sijdah utapata adhkaar nyingi kwa maslahi yake. Muislamu atachagua katika zile zilizo sahihi apendayo kuisoma ili atimize Ibaadah yake kwa njia iliyo nzuri yenye kuafikiana na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Hebu tuzitazame baadhi ya Tashahhud alizofundisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

a)   Tashahhud ya Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu): Amesema alinifundisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Tashahhud kama alivyonifundisha Surah katika Qur-aan: At-tahiyaatu Lillahi wasw-Swalawaatu watw-Twayyibaatu as-Salaamu 'alayka ayyuhan Nabiyy wa Rahmatu Llaahi wa Barakaatuhu … (hii ni alipokuwa kati yetu, pindi alipoaga dunia tulisema: As-Salaamu 'alan Nabiy) [al-Bukhaariy, Muslim, Ibn Abi Shaybah na Abu Ya'laa). Na kauli hii ya Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu): Tulisema, as-Salaamu 'alan Nabiy, hii ilikuwa kwa kukubaliwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nayo inatiliwa nguvu na Hadiyth ya mama wa waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) [Muhammad Naaswir ad-Diyn al-Albaaniy, Swifatusw Swalaatin Nabiyy, uk. 161]. Kauli ya Tashahhud aina hii pia imepokewa kwa 'Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu 'anhu) kama ilivyonukuliwa na Maalik na al-Bayhaqiy kwa Isnadi iliyo Sahihi na pia mama wa waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) kama ilivyonukuliwa na Ibn Abi Shaybah na al-Bayhaqiy mbali na kwamba ipo tofauti kidogo katika baadhi ya maneno yaliyomo ndani yake.

 

b)   Tashahhud ya Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma): Amesema alikuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) akitufundisha Tashahhud kama alivyokuwa akitufundisha Surah katika Qur-aan. Alikuwa akisema: At-tahiyaatu al-Mubaarakatu asw-Swalawaatu atw-Twayyibaatu Lillaahi as-Salaamu 'alayka ayyuhan Nabiyy wa Rahmatu Llaahi wa Barakaatuhu … (Muslim, Abu 'Awaanah, ash-Shaafi'iy na an-Nasaa'iy). Tashahhud kama hii imepokewa kutoka kwa Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhuma) kama ilivyo katika Abu Daawuud na ad-Daraqutwniy, naye akaisahihisha. Pia Abu Muusaa al-Ash'ariy (Radhiya Allaahu 'anhu) amepokea kama hivyo kama ilivyonukuliwa na Muslim, Abu 'Awaanah, Abu Daawuud na Ibn Maajah. Hata hivyo Tashahhud walizofundishwa na Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) zimetofautiana baadhi ya lafdhi.

 

Kwa muhtasari ni kuwa Tashahhud utakayoitumia katika hizo utakuwa umesibu kufuata Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), hivyo kuzidisha ujira wako na thawabu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share