005-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kauli Za Maimaam Wanne Kuhusu Kushikamana Na Sunnah Na Kuacha Kufuatwa Rai Zao

 

KAULI ZA MAIMAAM WANNE KUHUSU KUSHIKAMANA NA SUNNAH NA KUACHA KUFUATA RAI ZAO

 

Itakuwa ni manufaa makubwa ikiwa tutazieleza baadhi ya kauli zao hapa, kwani labda hii itamuonya mtu au itawakumbusha wale ambao wanafuata rai za Maimaam au madhehebu maalum, bali wanaofuata kwa upofu wale Waalimu au Mashaykh na wale walio chini ya daraja ya hao Maimaam wanne wakubwa[1] wakishikilia madhehebu yao au rai zao kama kwamba zimeteremeshwa kutoka mbinguni! Na hali Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

 ((اتَّبِعُواْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُمْ وَلاَ تَتَّبِعُواْ مِن دُونِهِ أَوْلِيَاء))

((Fuateni mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola Mlezi wenu, wala msifuate rafiki au walinzi wengine badala yake))[2]     

 

 

WASEMAVYO MAIMAAM

 

1) ABU HANIYFAH (رحمه الله)

Wa kwanza wao ni Abu Haniyfah Nu'maan bin Thaabit.

Wafuasi wake wamesimulia kauli zake mbali mbali pamoja na maonyo tofauti ambayo yote lengo lake ni moja, nalo ni: Wajibu wa kuikubali Hadiyth na kuachilia mbali kufuata rai za Maimaam ambazo zinakhitilafiana nayo.

  1. "Ikiwa Hadiyth imeonekana kuwa ni Swahiyh, basi hiyo ndiyo madhehebu yangu"[3]    
  2. "Hairuhusiwi[4]  kwa mtu yeyote kukubali rai zetu ikiwa hawatojua wamezipata kutoka wapi"[5]     

Katika usimulizi mwengine:"Imekatazwa[6]  mtu ambaye hajui dalili zangu kutoa hukmu[7]   kutokana na maneno yangu"

Usimulizi mwengine imeongezwa: "…Kwani sisi ni wanaadamu, tunasema jambo siku moja na kulirudisha (kulikataa) siku ya pili yake".

Na katika usimulizi mwengine: "Ole Ewe Ya'quub![8] Usiandike kila kitu unachosikia kutoka kwangu kwani huwa natoa rai moja leo na kesho huikataa. Au hutoa rai moja kesho na kuikataa keshokutwa".[9]    

  1. "Ninaposema jambo linalokhitilafiana na kitabu cha Allaah (سبحانه وتعالى) au yaliyosimuliwa na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), basi mpuuze kauli yangu".[10]         

 

 

2) MAALIK BIN ANAS (رحمه الله)

Imaam Maalik bin Anas yeye amesema:

  1. "Hakika mimi ni mwanaadamu: Ninafanya makosa (mara nyingine) na ninakuwa sahihi (mara nyingine). Kwa hiyo, tazameni rai zangu: zote ambazo zinakubaliana na Kitabu (Qur-aan) na Sunnah, zikubalini; na zote ambazo hazikubaliani na Kitabu (Qur-aan) na Sunnah, basi zipuuzeni". [11]

 

  1. "Kila mmoja baada ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), atakuwa na kauli yake itakayokubaliwa na kukataliwa, isipokuwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم)" [12]    

 

  1. Ibn Wahb amesema: "Nilimsikia Maalik akiulizwa kuhusu takhliyl ya vidole vya miguu (kuvichanganua vidole ili kupitisha maji) wakati wa wudhuu. Akasema: "Watu si lazima kufanya hivyo". Sikumkaribia hadi zogo la watu lilipopunguka. Nilipomwambia: "Tunajua kuwa ni Sunnah kuhusu jambo hilo". Akasema: "Jambo gani hilo? Nikasema: "Layth bin Sa'd, Ibn Lahiy'a na 'Amr bin Al-Haarith wamesimulia kwetu kutoka kwa Mustawrid bin Shaddaad Al-Quraishiy ambaye amesema: "Nilimuona Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akisugua baina ya vidole vyake vya miguu kwa kidole chake kidogo". Akasema: "Hadiyth hii ni Hasan (njema); sikuwahi kuisikia abadan ila leo". Kisha baadaye nikamsikia akiulizwa kuhusu jambo hili hili, naye akaamrisha kufanya takhliyl ya vidole vya miguu"[13]  

  

 

3) ASH-SHAAFI'IY (رحمه الله)

Ama kutoka kwa Imaam Ash-Shaafi'iy, kauli zake zilizonukuliwa ni nyingi na nzuri mno.[14] na wafuasi wake walikuwa ni bora kabisa katika kufuata.

 

  1. "Sunnah za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) zinamfikia na kumkwepa kila mmoja wetu. Kwa hiyo kila ninapotaja rai yangu au nikiunda sheria, na ikiwa ipo dalili kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), inayopinga rai yangu, basi rai iliyo sahihi ni aliyosema Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na hiyo ndio rai yangu"[15]    

 

  1. "Waislamu wamekubaliana pamoja kwamba ikiwa Sunnah ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) imebainishwa dhahiri kwa yeyote, hairuhusiwi[16]  kwake kuiacha kwa kufuata kauli ya mwengine yeyote[17]  

 

  1. "Ukiona katika maandishi yangu jambo ambalo ni tofauti na Sunnah ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), basi zungumza kwa kurejea Sunnah ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na acha niliyoyasema mimi". Katika usimulizi mwengine: "…basi ifuate (Sunnah) na usitazame tena pembeni kufuata kauli ya mwengine yeyote"[18]    

 

  1. Hadiyth ikipatikana kuwa ni Swahiyh, basi hiyo ndiyo madhehebu yangu"[19]    

 

  1. "Wewe (Imaam Ahmad)[20] ni mwenye elimu zaidi kuhusu Hadiyth kuliko mimi. Kwa hiyo Hadiyth ikiwa ni Swahiyh basi nijulishe, ikiwa ni kutoka Kufah, Basrah au Syria, ili nichukue rai ya Hadiyth madamu tu ni Swahiyh"[21]  

 

  1. "Katika kila jambo, ambako wenye kusimulia wakipata ripoti kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) ambayo ni kinyume na niliyoyasema, basi narudisha kauli yangu nyuma, ikiwa wakati wa maisha yangu au hata baada ya kufa kwangu"[22]    

 

  1. "Ukinisikia nasema kitu, na kinyume chake ni Hadityh Swahiyh kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), basi tambua kuwa akili yangu imetoweka"[23]    

 

  1. "Kwa kila ninalosema, ikiwa upo usimulizi ulio Swahiyh, basi Hadiyth ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) inakuja mwanzo, kwa hiyo usifuate rai yangu"[24]   

 

  1. "Kila kauli kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) ni rai yangu pia, japokuwa hujaisikia kutoka kwangu"[25]    

 

 

4) AHMAD BIN HANBAL (رحمه الله)

 

Imaam Ahmad alikuwa wa mbele miongoni mwa Maimaam kukusanya Sunnah na kuzishikilia sana hadi   alichukizwa kuona kinaandikwa kitabu kilichokusanya mambo yaliyogeuzwa na mambo yaliyotegemea rai zaidi[26]   kwa hilo akasema:   

 

  1. Msifuate rai yangu, wala msifuate rai ya Maalik, au Ash-Shaafi'iy au ya Awzaa’iy, wala Ath-Thawriy, lakini chukueni kutoka kule  walikotoa"[27]  

Katika usimulizi mmoja: "Msiige dini yenu kutoka kwa mtu yeyote katika hawa, bali chochote kilichotoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na Maswahaba zake, chukueni, kisha kwa At-Taabi'iyn (Waliofuata) ambako mtu ana khiari".

Mara moja kasema: "Kufuata[28] ina maana kwamba mtu anafuata yaliyokuja kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na Maswahaba zake, ama baada ya  At-Taabi'iyn (Waliofuata) anayo khiari" [29]   

  1. "Rai ya Awzaaiy, rai ya Maalik, rai ya Abu Haniyfah, zote ni rai, na ni sawa katika macho yangu. Lakini, dalili ni yale masimulizi kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na Maswahaba zake"[30]   

 

  1. "Yeyote atakayekanusha kauli ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) basi yumo katika ukingo wa kuangamia"[31]             

Hizi ndizo kauli za wazi kabisa za Maimaam, Allaah (سبحانه وتعالى) Awe radhi nao, kuhusu kushikamana na Hadiyth na kukataza kufuata rai zao bila ya kuwa na dalili iliyo dhahiri kabisa.

Kwa hiyo, yeyote aliyeshikamana na lolote la Sunnah ambayo imeshuhudiwa kuwa ni Swahiyh hata kama imepinga kauli ya baadhi ya Maimaam, hatokuwa anapingana na madhehebu yao, wala hatopotoka katika njia zao, bali mtu huyo atakuwa anawafuata wote na atakuwa amekamata kile kilichoaminiwa zaidi akishika mkono ambao hautavunjika. Lakini hii haitakuwa hali ya yule anayeziweka kando Sunnah Swahiyh kwa sababu tu zimepingana na rai za Maimaam, bali mtu huyo atakuwa sio mtiifu kwao na amepingia kauli zao hizo za juu. Na tunaona Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

((فَلاَ وَرَبِّكَ لاَ يُؤْمِنُونَ حَتَّىَ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لاَ يَجِدُواْ فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُواْ تَسْلِيمًا))

((La! Naapa kwa Mola! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayo khitalifiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utayo toa, na wanyenyekee kabisa.))[32]  

((فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ))

((Basi na watahadhari wanaokhalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu iumizayo))[33]

 

Haafidhw Ibn Rajab Al-Hanbali (رحمه الله) amesema: "Kwa hivyo ni wajibu kwa mtu yeyote anayesikia amri ya Mjumbe wa Allaah  (صلى الله عليه وآله وسلم) au kuijua, kuielezea kwa Ummah, kuwapa nasaha ya dhati na kuwaamrisha kufuata amri zake japo kama itakuwa ni kinyume na rai ya mtu mkubwa. Hii ni kwa sababu hukmu ya Mjumbe wa Allaah  (صلى الله عليه وآله وسلم) ina haki zaidi kuheshimiwa na kufuatwa kupita rai za mtu yeyote mkubwa aliyekwenda kinyume bila ya kujua na amri za Mtume katika jambo lolote. Ndio maana Maswahaba na waliofuatia walimpinga yeyote aliyekwenda kinyume na Sunnah Swahiyh, mara nyingine wakiwa wakali katika kuwapinga kwao[34], sio kutokana na kumchukia huyo mtu, bali alikuwa ni mpenzi wao na mwenye kuheshimiwa, lakini kwa sababu Mjumbe wa Allaah alikuwa mpenzi wao zaidi na amri zake zilikuwa juu ya amri za viumbe wengine. Hivyo inapokuwa amri ya Mtume na ya mtu mwengine zinapingana, amri ya Mtume huwa ndiyo ipasayo kutiliwa nguvu na kutekelezwa. Hakuna katika hili lingeliwazua wasimheshimu mtu waliyempinga kwa sababu wamejua kuwa atasamehewa[35] , bali aliyetajwa mwisho hatojali amri zake kupingwa itakapokuwa amri za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) zimeonyesha dhahiri kuwa ni kinyume chake [36]

Vipi wachukiwe hayo ikiwa wamewajibisha wafuasi wa kama ilivyo, na kama tulivyoona, kuwa wameamrisha waziache kando rai zao zinazokwenda kinyume na za Sunnah. Bali Imaam ash-Shaafi'iy (رحمه الله) aliwaambia Maswahaba zake kuzihusisha kwake Sunnah zilizo Swahiyh pia, japo kama hakuzitekeleza  au katekeleza zilizo kwenda kinyume nazo. Hivyo mhakiki Ibn Daqiyq alipokusanya pamoja katika mjalada mzito, mas-ala ambayo kila mmoja katika kauli za madhehebu ya Maimaam wanne kuwa yamekwenda kinyume na Hadiyth Swahiyh, kama alivyaondika mwanzoni mwake: "Imekatazwa kuhusisha majibu haya kwa Maimaam waliojitahidi na ni fardhi kwa wanasheria wanaofuata rai zao kujua hizi ili wasije kuzinukuu wakawazulia"[37]

 

Wafuasi Wa Maimaam Kuacha Rai Zao Ikiwa Zinapingana na Sunnah

 

 

Kutokana na yote tuliyotaja, wafuasi wa Maimaam,  ((Fungu kubwa katika wa mwanzo Na wachache katika wa mwisho))[38] hawakubali rai za Imaam wao, bali wanazipuuza nyingi wanapotambua kuwa zinakenda kinyume na za Sunnah. Hata Maimaam wawili Muhammad Ibn Al-Hasan na Bu Yuusuf (رحمها الله) walikhitilafiana na Shekhe wao Abu Haniyfah 'Fiy Nahw thuluth al-madhhab'[39] kama vitabu vya masaail vinavyothibitisha. Imesemwa hivyo hivyo kuhusu Imaam Al-Muzaniy[40] na wafuasi wengineo wa Ash-Shaafi'iy na Maimaam wengine. Tungelianza kutoa mifano majadiliano yangeliendelea kuwa marefu na tungelitoka nje ya makusudio katika mas-ala utangulizi huu, hivyo tutajiwekea mipaka kwa mifano miwili:

 

1.     Imaam Muhammad amesema katika Muwattwa yake[41] (Uk. 158). "Ama Abu Haniyfah hakuona kuwa kuna Swalah ya kuomba mvua, lakini kauli yetu ni kwamba Imaam anaswali Rakaa mbili na anaomba du'aa na anashika shuka yake…"

 

2.     Tunaye 'Iswaam bin Yuusuf Al-Balkhiy mmoja wa wafuasi wa Imaam Muhammad[42]  na mtumishi wa Imaam Abu Yuusuf[43]  ambaye akitoa hukmu kinyume na Imaam Abu Haniyfah kwa sababu hakujua ushahidi wake na ushahidi mwingine ulijitokeza kwake wenyewe hivyo alikuwa akiutolea hukmu:[44] . Hivyo alinyanyua mikono katika rukuu (kwenye Swalah) na anaponyanyuka[45] kama ilivyo mutawaatir Sunnah ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) bali Maimaam wake watatu (yaani Abu Haniyfah, Abu Yuusuf na Muhammad) wamesema vinginevyo na hawakumzuia kutekeleza Sunnah. Huu ni mfano ambao kila Muislamu inampasa kuwa nao kwani tumeshaona kutokana na ushahidi wa Maimaam wanne na wengineo huko juu.

 

 

 

 


 

[1]   Hii ni aina ya taqliyd (kufuata kwa upofu [kiujinga]) ambayo Imaam At-Twahaawiy alihusisha aliposema: "Hafuati rai ila ni mtu mkaidi au mjinga" (kufuata kama kipofu)

[2]   Al-A'raaf:3

[3]    Ibnul-'Aabidiyn katika al-Haashiyah (1/63) na katika inshaa yake   Rasm al-Mufti (1/4 kutoka Mkusanyiko wa Inshaa za Ibnul-'Aabidyin). Shaykh Swaalih Al-Fulaaniy katika al-Iyqaadhw al-Himaam (uk.62) na wengineo. Ibnul-'Aabidiyn amenukuu kutoka Sharh al-Hidaayah ya Ibn Al-Shahnah Al-Kabiyr, mwalimu wa Ibn Al-Himaam, kama ifuatavyo:

"Ikiwa Hadiyth iliyo kinyume na Madhehebu imeonekana kuwa ni Swahiyh basi mtu atende kwa kufuata hiyo Hadiyth na aifanye kuwa ni madhehebu yake. Kuifanyia kazi Hadiyth hakutombatilisha mtu kuwa sio mfuataji wa madhehebu ya Hanafi, kwani imeripotiwa kuwa Abu Haniyfah alisema: "Ikiwa Hadiyth imeonekana kuwa ni Swahiyh, basi hiyo ndiyo madhehebu yangu". Na hii imeelezewa na Imaam Ibn 'Abdil-Barr kutoka kwa Abu Haniyfah na kutoka kwa Maimaam wengine".

Hii ni sehemu ya ukamilifu wa elimu na uchaji Allaah wa Maimaam, kwani wameonyesha kwa kusema kwamba wao hawakuwa na maarifa (elimu) kamili ya Sunnah zote. Na Imaam Ash-Shaafi'iy amefafanua wazi wazi (tazama mbele). Hutokea wanapokwenda kinyume na Sunnah huwa ni kwa sababu hawakuitambua. Ndipo walipotuamrisha tushikilie Sunnah na tuizingatie kuwa ni sehemu ya madhehebu yao. Allaah Awashushie Rahma Yake kwao wote.

[4]    Sio halaal

[5]   Ibn 'Abdil-Barr katika Al-Intiqaa' fiy Fadhwaail Ath-Thalaathah Al-Aimmah Al-Fuqahaa (uk.145), Ibn Al-Qayyim katika 'I'laam Al-Muwaqi'iyn (2/ 309), Ibn 'Aabidiyn katika tanbihi zake kwenye Al-Bahr Ar-Raa'iq (6/ 293) na katika Rasm Al-Mufti (uk. 29, 32) na Sha'raaniy katika Al-Miyzaan (1/ 55) pamoja na usimulizi wa pili. Usimulizi wa mwisho ulikusanywa na 'Abbaas Ad-Dawriy katika At-Taariykh ya Ibn Ma'iyn (6/ 77/1) ikiwa na Isnaad Swahiyh kutoka kwa Zafar, mwanafunzi wa Imaam Abu Haniyfah. Usimulizi uliofanana upo kutoka kwa wafuasi wa Abu Haniyfah; Zafar, Abu Yuusuf na 'Aafiyah bin Yaziyd; taz. Al-Iyqaadhw (uk. 52). Ibn Al-Qayyim alithibitisha kwa nguvu usahihi wake kutoka kwa Abu Yuusuf katika I'laam Al-Muwaqi'yn (2/ 344). Nyongeza ya usimulizi wa pili unarejewa na mwandishi wa Al-Iyqaadhw (uk. 65) kwa Ibn 'Abdil-Barr, Ibn Al-Qayyim na wengineo.

     Ikiwa hivi ndivyo wanavyosema kwa mtu asiyejua dalili zao, jibu lao litakuwa nini kwa yule anayetambua kuwa dalili zinapingana na kauli yao, lakini bado anatoa hukumu iliyopinga dalili? Kwa hiyo, fuata usemi huu, kwani pekee unatosheleza kuvunja ufuataji rai kwa ujinga. Ndio maana nilipomlaumu mmoja wa Mashaykh (Muqallid) wa madhehebu katika kutoa fatwa (hukm) kwa kutumia maneno ya Abu Haniyfah bila ya kujua dalili, aligoma kuamini kuwa hiyo ni kauli ya Abu Haniyfah!

 

[6]    Haraam

[7]     Fatwa

[8]  Mwanafunzi mashuhuri wa Imaam Abu Haniyfah, Abu Yuusuf  (رحمه الله)

[9]  Hii ni kwa sababu Imaam kawaida hutoa rai yake kutokana na Qiyaas (analojia). Kisha tena hupata analojia iliyo na nguvu zaidi, au Hadiyth ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) humfikia. Kwa hiyo huikubali hiyo na kuipuuza rai yake ya nyuma. Maneno ya Sha'araaniy katika Al-Miyzaan (1/62) yamewekwa kwa mukhtasari kama ifuatavyo:

     "Imani yetu na ya kila mtafiti wa Imaam Abu Haniyfah (رحمه الله) ni kwamba, aliishi hadi iliporikodiwa Sharia. Na safari za wahifadhi wa Hadiyth katika miji mbali mbali na mipakani kwa ajili ya kukusanya na kuzipata. Angeliipokea na kupuuza analojia zote ambazo alizozitumia, idadi za Qiyaas katika madhehebu yake zingelikuwa kidogo kama zilivyo katika madhehebu mengine. Lakini kwa vile dalili za Sharia zimetapakaa kwa Waliotangulia na waliowatangulia, na haizikukusanywa wakati wa maisha yake, ilihitajika kuwepo Qiyaas nyingi katika madhehebu yake kulingana na Maimaam wengine. Maulamaa wa baada ya hapo, kisha wakafanya safari kutafuta na kukusanya Hadiyth kutoka nchi mbali mbali na miji na wakaziandika. Hivyo baadhi ya Hadiyth za Sharia zimeelezea nyingine. Hii ni sababu ya kuweko idadi kubwa ya qiyaas katika madhehebu yake wakati kwenye madhehebu mengine ilikuwa ni idadi ndogo"

     Abul-Hasanaat Al-Laknawiy amenukuu maneno yake kikamilifu katika An-Naafi' Al-Kabiyr (uk. 135) akiandika na kupanua tanbihi zake. Kwa hiyo yeyote anayependa kutafuta maelekezo yake afanye humo.

     Kwa vile hii ni uthibitishaji kuwa kwa nini Abu Haniyfah mara nyingine alikhitilafiana na Hadiyth zilizokuwa Swahiyh bila ya kukusudia na ni sababu barabara ya kukubaliwa, kwani Allaah Haikalfishi nafsi kwa yale isiyoweza kubeba. Hairuhusiwi kumtukana kwa sababu hiyo kama walivyofanya watu wajinga. Bali ni wajibu kumheshimu, kwani yeye ni mmoja wa Maimaam wa Waislamu ambao wameihifadhi hii dini hadi ikafikishwa kwetu kutoka katika kila matawi yake. Na kwa vile yeye analipwa (Na Allaah سبحانه وتعالى) kwa hali yoyote ile; ikiwa kapata au amekosea kwa kutokusudia. Wala hairuhusiwi kwa wafuasi wake wapenzi kuendelea kushikilia kauli zake ambazo zinakhitilafiana na Hadiyth zilizo Swahiyh kwani kauli hizo sio madhehebu yake kama kauli zake hapo juu zilivyosema. Kwa hiyo hii ni mipaka miwili; ukweli na uongo katika yake. ((Na waliokuja baada yao wanasema: Mola wetu Mlezi! Tughufirie sisi na ndugu zetu waliotutangulia kwa Imani, wala Usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kwa walioamini. Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu)) [Al-Hashr 59:10]

[10] Al-Fulaaniy katika Al-Iyqaadhw Al-Himaam (uk.50), ikifuatilia kwa Imaam Muhammad na kisha kusema: "Hii haimhusu Mujtahid, (mwenye kujitahidi kwa elimu yake na kutoa hukmu) kwa vile hakujifunga katika rai zao, bali inamhusu Muqallid (mwenye kufuata).

 

[11] Ibn 'Abdil-Barr katika Jaami'ul Bayaan Al-'Ilm (2/32), Ibn Hazm   akinukuu kutoka kwake katika Uswuul-Al-Ahkaam (6/149) na hali kadhaalika Al-Fulaaniy (uk. 72).

 

[12]  Hii inajulikana sana miongoni mwa Maulamaa wa baadaye kuwa ni kauli ya Maalik. Ibn 'Abdil-Haadiy alikiri kuwa ni Swahiyh katika Irshaad As-Saalik (227/1); Ibn 'Abdil-Barr katika Jaami'ul-Bayaan Al-'Ilm (2/91) na Ibn Hazm katika Uswuul Al-Ahkaam (6/145, 179) alisimulia kama ni kauli ya Al-Hakam bin 'Utaybah na Mujaahid; Taqiyud-Diyn As-Subki alisimulia  katika Al-Fataawa (1/148) kama ni kauli ya Ibn 'Abbaas akishangazwa kwa uzuri wake kisha akasema: "Haya maneno yameanzia kwa Ibn 'Abbaas na Mujaahid, na Maalik (رحمه الله) aliyachukua, na akawa mashuhuri kwayo". Inavyoelekea kwamba Imaam Ahmad kisha akachukua kauli hii kutoka kwao, kama Abu Daawuud alivyosema katika Masaail ya Imaam Ahmad (uk 276). "Nilimisikia Ahmad akisema: Kila mmoja anapokelewa na anakatiliwa katika rai zake, isipokuwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم)"

 

[13]  Kutoka kwa Utangulizi wa Al-Jarh wat-Ta'diyl ya Ibn Abi Haatim (uk. 31-32)

 

[14]    Ibn Hazm anasema katika Uswuul al-Ahkaam (6/118)

"Hakika, Mafuqahaa wote ambao rai zao zilikuwa zikifuatwa zilipingwa kwa taqliyd na waliwakataza wafuasi wao kufuata rai zao kijinga. Aliyekuwa mkali kabisa miongoni mwao ni Ash-Shaafi'iy (رحمه الله), kwani yeye alirudia kutilia mkazo zaidi kuliko yeyote mwengine kufuata usimulizi ulio Swahiyh na kukubali dalili yoyote iliyoamriwa. Vile vile alidhihirisha wazi na kujitenga kuwa hana hatia ikiwa atafuatwa yeye tu pekee na aliwatangazia hayo wale waliokuwa naye. Tunaomba hii imnufaishe mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) na thawabu zake ziwe za juu kabisa kwani alikuwa ni sababu ya mema mengi".

[15] Imesimuliwa na Al-Haakim ikiwa ina isnaad ya kuendelea hadi kwa Ash-Shaafi'iy kama ilivyo katika Taariykh Dimashq ya Ibn 'Asaakir (15/1/3), I'laam Al-Muwaqi'iyn (2/363,364) na Al-Iyqaadhw (uk. 100)

[16] Halaal

[17] Ibn al-Qayyim (2/361) na Al-Fulaaniy (uk. 68)

[18] Al-Haraawiy katika Dhamm Al-Kalaam (3/47/1) Al-Khatiyb katika Al-Ihtijaaj bi Ash-Shaafi'iy (8/2), Ibn 'Asaakir (15/9/10), An-Nawawiy katika Al-Majmuu' (1/ 63), Ibn al-Qayyim (2/ 361), na Fulaani (uk. 100) usimulizi wa pili ni kutoka Hilyah Al-Awliyaa ya Abu Nu'aym.

 

[19] An-Nawawiy katika Al-Majmuu' (1/ 63), Sha'raaniy (1/ 57), akitoa chanzo chake kama Al-Haakim na Al-Bayhaqiy na Al-Fulaaniy (uk. 107). Ash-Sha'raaniy kasema: "Ibn Hazm kasema: "Kwamba imeonekana ni Swahiyh naye au kwa Imaam mwengine". Kauli yake nyingine imethibitisha ufahamu huu.

     An-Nawawiy amesema: "Wafuasi wetu walitenda kutokana na hili katika mambo ya tathwiyb (mwito wa Swalah baada ya adhana), shuruti za kutoka katika ihraam kwa ajili ya ugonjwa, na mambo mengine yaliyojulikana vyema katika vitabu vya madhehebu. Miongoni wafuasi wetu ambao wameripotiwa kuwa walitoa hukumu kutokana na chanzo cha Hadiyth (yaani kuliko kuchukua kauli ya Ash-Shaafi'iy) ni Abu Ya'quub Al-Buwiity na Abul-Qaasim Ad-Daarikiy. Wafuasi wa Muhaddithiyn (Wakusanyao Hadiyth), Imaam Abu Bakr Al-Bayhaqiy na wengineo walitenda kwa kufuata kauli hii. Wafuasi wengi wetu wa zamani, walipokumbana na jambo ambalo ilikuweko Hadiyth na madhehebu ya Ash-Shaafi'iy yalikuwa ni kinyume nalo, basi walitenda  kwa kufuata Hadiyth na kutowa fatwa (hukmu) pia wakisema: "Madhehebu ya Ash-Shaafi'iy ni kila kinachokubaliana na Hadiyth". Shaykh Abu 'Amr (Ibn Asw-Swalaah) alisema: "Yeyote miongoni mwa Ash-Shaafi'iy akiona Hadiyth inayopinga madhehebu yake, alichukulia kama alitimiza shuruti za Ijtihaad kwa kawaida, au katika maudhui au jambo lile khaswa ambalo alikuwa huru kutenda kwa kufuata Hadiyth; kama sio. Lakini hata hivyo aliona vigumu kupingana na Hadiyth baada ya utafiti zaidi, hakuweza kupata uthibitishaji wa kukinaisha wa kupinga Hadiyth. Kwa hiyo, alibakia kutenda kwa kufuata Hadiyth ikiwa Imaam mwengine mwenye kujitegemea mbali na Ash-Shaafi'iy, basi alitenda kuifuata. Na hii huwa ni kithibitisho chake cha kuacha madhehebu ya Imaam wake katika jambo hilo". Alichosema (Abu 'Amr) ni Swahiyh na lililokubalika. Na Allaah Anajua zaidi.

     Kuna uwezekano mwingine ambao Ibn As-Swalaah alisahau kutaja: Afanyeje mtu ikiwa hakumpata mtu yeyote ambaye alitenda kwa kufuata Hadiyth? Hii imejibiwa na Taqiyud-Diyn As-Subkiy katika makala yake 'Maana Ya Kauli ya Ash-Shaafi'iy: Ikiwa Hadiyth ikipatikana kuwa ni Swahiyh, basi ndio madhehebu yangu' (uk. 102, Mjalada 3). "Kwangu, lililo bora kabisa ni kufuata Hadiyth. Mtu na awaze kwamba yuko mbele ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kama vile ameisikia kutoka kwake, je, atakwenda demani (kufuata mweleko wa upepo) acheleweshe kutenda kwa kuifuata? Hapana! WaLLaahi, na kila mmoja anabeba jukumu kutokana na ufahamu wake".

     Mjadala wake uliobakia umetolewa kuchambuliwa  katika I'laam Al-Muwaqi'iyn (2/ 303, 370)  na katika kitabu cha Al-Fulaaniy, (Kichwa cha habari kamili) Al-Iyqadhw Himam Uwl Al-Abswaar, Lil-iqtidaa Bisayyid Al-Muhaajiriyn Wal-Answaar, wa Tahdhiyrihim 'An Al-Ibitidaa' Ash-Shaai' fit-Quraa Wal-Amswaar, Min Taqlyid Al-Madhaahib Ma'a Al-Hamiyyat Wal-'Aswabiyyat Bayna Fuqahaa Al-A'swaar"

     Kitabu hicho ni cha pekee katika maduhui hii, ambacho kila mpenda haki akisome kwa ufahamu na kutafakari.

[20]  Akimwambia Imaam Ahmad bin Hanbal (رحمه الله)

[21] Imesimuliwa na Ibn Abi Haatim katika Aadaabu Ash-Shaafi'iy (uk. 94-5), Abu Nu'aym katika Hulya Al-Awliyaa (9/ 106), Al-Khatwiyb katika Al-Ihtijaaj Bish-Shaafi’iy (8/1) na kutoka kwake Ibn 'Asaakir (15/ 9/1), Ibn 'Abdil-Barr katika Al-Intiqaa' (uk. 75), Ibn Al-Jawziy katika Manaaqib Al-Imaam Ahmad (uk. 499) na Haraawiy (2/ 47/2) katika njia tatu kutoka kwa 'Abdullaah bin Ahmad bin Hanbal kutoka kwa baba yake kwamba Ash-Shaafi'iy alimhusisha nayo katika I'laam (2/325) kama alivyofanya Al-Fulaaniy katika Al-Iyqaadhw (uk. 152) na kisha akasema: "Al-Bayhaqiy amesema: "Hii ndio maana yeye, yaani Ash-Shaafi'iy alitumia Hadiyth sana, kwa sababu alikusanya elimu kutoka kwa watu wa Hijaaz, Syria, Yemen na Iraq. Kwa hiyo alikubali yote aliyoona kuwa ni Swahiyh bila ya kutegemea au kuangalia yale yaliyokuwa nje ya madhehebu ya watu wa nchi yake, wakati ukweli ulipodhihirika kwake kutoka sehemu nyingine. Wengineo kabla yake, walijiwekea mipaka kwa waliyoyakuta katika madhehebu ya watu wa nchi yao bila ya kujaribu kuhakikisha usahihi wa yale yaliyokuwa kinyume nayo. Allaah Atusamehe sote"   

[22] Abu Nu'aym (9/ 107), Harawiy (47/ 1), Ibn al-Qayyim katika I'laam Al-Muwaqqi'iyn (2/ 363) na Fulaani (uk. 104)

[23] Ibn Haatim katika Al-Adaab (Uk. 93), Abul-Qaasim Samarqandi katika Al-Amaal, kama katika uchaguzi kutoka kwa Abu Hafsw al-Mu'addab (234/ 1), Abu Nu'aym (9/ 106), na Ibn 'Asaakir (15/ 10/1) ikiwa ni sanad Swahiyh.

 

[24]    Ibn Abi Haatim, Abu Nu'aym na Ibn 'Asaakir (15/ 9/2)

[25]    Ibn Abi Haatim (uk. 93-4)

[26]    Ibn Al-Jawziy katika Al-Manaaqib (uk. 192)

[27]    Al-Fulaaniy (Uk. 113) na Ibn Al-Qayyim katika I'laam

[28]    Ittibaa'

[29]    Abu Daawuud katika Masaail ya Imam Ahmad (uk. 276-7)

[30]     Ibn 'Abdil-Barr katika Jaami' Bayaan Al-'Ilm

[31]     Ibn Al-Jawziy (uk. 182)

 

[32]    An-Nisaa:4:65

[33]    An-Nuur: 24:63

[34]    Japokuwa ni dhidi ya baba zao na walimu wao, kama Atw-Twahaawiy katika Sharh Ma'aaniy Al-Aathaar (1/ 372) na Abu Ya'laa katika Musnad yake (3/ 1317) wamesimulia, ikiwa na isnaad ya watu walioaminika kutoka kwa Saalim bin 'Abdillaah bin 'Umar (رحمه الله) ambaye amesema:

"Nilikuwa nimekaa na Ibn 'Umar (رضي الله عنه) msikitini siku moja, alikuja mtu kutoka Syria na akamuuliza kuhusu kuendeleza 'Umrah pamoja na Hajj (Inayojulikana kama ni Hajj At-Tamaattu'). Ibn 'Umar akajibu: 'Ni vizuri na jambo jema'. Kisha mtu akasema: 'Lakini baba yako (yaani 'Umar bIn Al-Khattwaab) alikuwa akikataza' Basi Akasema,' Ole wako! Ikiwa baba yangu alikuwa akikataza kitu ambacho Mjumbe wa Allaah  (صلى الله عليه وآله وسلم)alikuwa akifanya na kuamrisha, je, utakubali rai ya baba yangu au amri ya Mjumbe wa Allaah  (صلى الله عليه وآله وسلم)?' Akajibu: 'Amri ya Mjumbe wa Allaah  (صلى الله عليه وآله وسلم)' Akasema: 'Basi nenda zako mbali na mimi' Ahmad (Namba 57000) amesimulia kama hivyo kama alivyosimulia At-Tirmidhiy (2/ 82) na amekiri kuwa ni Swahiyh.

 

[35]   Bali atalipwa thawabu kwa sababu ya kauli ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Qaadhi akipitisha hukmu, akifanya juhudi (ijtihaad) na hukmu ikawa Swahiyh atapata thawabu mbili. Akifanya juhudi (ijtihaad) na akahukumu kimakosa, atapata thawabu moja)) [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]

[36]   Imenukuliwa katika tanbihi za 'Iyqaadhw al-Himam (Uk. 93)

[37]   Fulaaniy (Uk. 99)

[38]   Suratul Al-Waaqi'ah 56: 13-14

[39]   Ibn 'Aabidiyn Katika 'al-Haashiyah (1/ 62) na Al-Laknawiy kaipa chanzo chake kutoka katika An-Naafi' al-Kabiyr (Uk. 93) ya Al-Ghazaaliy.

[40]   Yeye mwenyewe amesema katika mwanzo wa 'Mukhtaswar Fiy Fiqhis-Shaafi'iy' (iliyochapishwa katika pembizo ya 'Al-Umm') "Kitabu hiki ni uchaguzi kutoka elimu ya Muhammad bin Idriys Ash-Shaafi'iy (رحمه الله) na kutokana na maana ya kauli zake kumsaidia yeyote anayekitaka akiwa anajua makatazo ya kufuata rai yake au ya yoyote mwengine ili mtu azingatie dini yake"

[41]   Ambako ameelezea kumpinga Imaam wake katika masaail ishirini (Namba 42, 44, 103, 120, 158, 169, 172, 173, 228, 230, 240, 244, 274, 275, 284, 314, 331, 338, 355, 356 kutoka Ta'liyq Al-Mummajjid 'alaa Muwattwa' Muhammad (Tanbihi muhimu ya Muwattwa ya Muhammad)

[42]   Ibn 'Aabidiyn amemtaja miongoni katika 'Al-Haashiyah' (1/ 74) na katika 'Rasm Al-Muftiy (1/17). Qurayshi amemtaja katika 'Al-Jawaahiyr Al-Madhwiyyah fiy Twabaqaat Al-Haniyfah' (uk. 347) na akasema: "Alikuwa ni msimulizi wa Hadiyth wa kutegemewa. Yeye na kaka yake Ibraahiym walikuwa Mashaykh wawili wa Al-Balakh katika zama zao".

[43]   Al-Fawaaid Al-Bahiyyah Fiy Taraajim Al-Hanafiyyah (uk. 116)

[44]   Al-Bahr Ar-Raaiq (6/ 93) na Rasm Al-Muftiy (1/ 28)

[45]   Al-Fawaaid … (uk. 116) kisha muandishi akaongeza tanbihi yenye faida:

"Kutokana na hii inawezekana kutambulika ubatilifu wa usimulizi wa Makhuul kutoka kwa Abu Haniyfah: 'Kwamba mwenye kunyanyua mikono yake katika Swalah, Swalah yake itakuwa batili' ambayo Amiyr mwandishi wa al-Itqaaniy alivyohadaiwa kama ilivyotajwa kaitka historia yake. 'Iswaam Ibn Yuusuf, mfuasi wa Abu Yuusuf alikuwa akinyanyua mikono yake.  

 

Share