Himma Na Umuhimu Wake - 1
Shams Elmi (Abu ‘Ilm)
NINI MAANA YA HIMMA
Hamna tafsiri sahihi ya Kiswahili inayoweza kuwakilisha neno Himma, lakini kwa maana nyepesi tunaweza kusema Himma ni Kupania, ni msukumo wa kufanya jambo.
Himma Chimbuko lake ni moyoni, moyo wenye himma utamsukuma mwenye moyo huo kupenda kufanya mambo mema yenye kuleta mabadilko chanya katika maisha yake na jamii yake.
HIMMA YA MUISLAMU HULIPWA KABLA YA MATENDO
Katika Uislamu,mtu kuwa na himma kubwa ya kufanya mambo na kupenda kuleta mabadiliko katika maisha yake na maisha ya jamii yake hulipwa na Allaah kama vile mtu aliefanya jema kamili; Anasema Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم):
( من همَّ بحسنة، فلم يعملها، كتبها الله عنده حسنة كاملة ) رواه البخاري
“Atakayepania kufanya jema, na asilifanye, Allaah Humuandikia kama vile amefanya jema kamili” Al-Bukhaariy
Na Akasema katika Hadiyth nyingine:
من سأل الله الشهادة بصدقٍ، بلَّغه الله منازل الشهداء، وإن مات على فراشه رواه مسلم وغيره
“Atakayemuomba Allaah kifo cha shahada kwa ukweli, basi Allaah Humfikisha katika hadhi za mashahidi hata (kama mtu huyo) atakufa katika kitanda chake” Muslim
Na Mtume ( صلى الله عليه وآله وسلم) ِAnatufundisha katika Hadiyth nyingine kuwa;
ما من امرئٍ تكون له صلاة بليل، فغلبه عليها نوم ، إلا كُتب له أجر صلاته، وكان نومه صدقةً عليه رواه النسائي
(Mtu yeyote atakayekuwa na Swalah ya usiku, usingizi ukamzidia (akapitiwa) ataandikiwa ujira wa Swalah yake, na usingizi wake utakuwa ni sadaka ya Swalah hiyo) An-Nasaaiy
SIFA ZA MWENYE HIMMA
Mwenye Himma ya juu ni yule ambaye yupo tayari kujitolea nafsi yake na kupambana na vikwazo na matatizo katika kufikia malengo yake, kwani anaelewa kuwa mambo mazuri na mema huzungukwa na vikwazo, utamuona mwenye himma ya juu hufanya mambo yake kwa kujiamini, na hana muda wa kupoteza – kwa kufanya mambo yasiyokuwa na maana – katika kufikia malengo yake ya juu. Na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiwaambia Maswahaba zake:
( إن الله تعالى يحب معالي الأمور ، ويكره سفاسفها )
“Hakika Allaah Hupenda mambo ya maana, na Huchukia mambo ya kipuuzi”
Mwenye Himma ya juu siku zote huona kuwa majukumu aliyonayo ni mengi kuliko muda alionao, na ndio maana utamuona siku zote ni mtu mwenye kujali sana wakati, ahadi, mazungumzo ya maana, na kushirikiana na watu wenye kupenda mafanikio, wenye mipangilio katika maisha yao na malengo yanayoeleweka. Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
إغتنم خمسا قبل خمس، حياتك قبل موتك، وصحتك قبل سقمك، وفراغـك قبل شغلك، وشبابك قبل هرمك، وغناك قبل فقرك
“Faidika na (mambo) matano kabla ya kufikiwa na matano; maisha yako kabla ya kifo chako, afya yako kabla ya maradhi yako, nafasi yako kabla ya kushughulishwa kwako, ujana wako kabla ya uzee wako, na utajiri wako kabla ya umasikini wako”
Mwenye Himma ya juu siku zote huishi kimalengo, huwa na malengo ya muda mfupi, na malengo ya muda mrefu, vilevile huwa na ratiba ya mambo ya kufanya kila siku kwa wakati, ratiba ambayo nyakati tano za Swalah huwa zinabaki palepale bila kuingiliwa siku zote.
Anasema Hasan Al-Baswriy:
ما من يوم ينشق فيه فجره إلا نادى، يا ابن آدم ، أنا خلق جديد وعلى عملك شـهيد، فتزود في بعمل صالح فإني لا أعود الى يوم القيامة
“Hakuna siku ichomozayo alfajiri yake isipokuwa huita; Ewe Mwanaadamu, mimi ni kiumbe kipya, na nitakuwa shahidi wa matendo yako, basi nitumie kwa kufanya matendo mema, kwani mimi sirudi sitarudi mpaka siku ya Qiyaamah.”
Itaendelea inshaAllaah…/
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


