Himma Na Umuhimu Wake - 2
Shams Elmi (Abu ‘Ilm)
Aidha ieleweke kuwa, ujana ni kipindi ambacho Allaah Anakipenda, na amali za mja zinapendeza zaidi kwa Allaah katika kipindi hiki kuliko kipindi kingine, kwani ni kipindi ambacho kinakuwa kimetawaliwa na matamanio, matumaini, kuipenda dunia, ubunifu, na nguvu za mwili na hisia, ni kipindi bora katika maisha ya mtu, na Allaah siku zote humpenda mtu anaetoa kwa ajili ya Allaah kilicho bora zaidi, Allaah Anasema katika Qur-aan:
((Hamtaweza kufikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda)) 3: 92
Na katika jumla ya mambo ambayo mtu anayependa ni ujana wake, hivyo amali njema ya Muislamu kijana inapendeza zaidi mbele ya Allaah kuliko amali hiyo hiyo atakapoifanya akiwa mzee, aidha Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) anatuambia:
(Hautanyanyuka unyayo wa binadamu siku ya Qiyaamah mpaka aulizwe juu ya mambo matano; umri wake aliumalizaje, na ujana wake aliutumiaje, na mali yake aliichumaje na aliitumiaje, na alitumiaje elimu aliyoipata). At-Tirmidhiy.
Katika mafundisho haya ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) tunaona kuwa mtu pamoja na kuulizwa umri wake aliumalizaje, lakini aidha ataaulizwa kuhusu ujana wake aliutumiaje, pamoja na ujana kuwa sehemu ya umri wa mtu, lakini kwa Allaah una nafasi maalumu, na ndio maana tukasema somo hili la Himma lina umuhimu mkubwa kwa vijana wa Kiislamu, ili kuwahi kupata fadhila za ujana wao kwa kupupia mambo ya kheri, na kujipinda katika kutafuta radhi za Allaah.
Mtu mwenye Himma ya juu, lengo lake kuu la kuishi ni kuitafuta pepo ya Allaah kwa kufanya yote yatakayomfanya apate radhi za Allaah na hatimaye aipate pepo, huwa siku zote yupo mstari wa mbele katika kuyashughulikia mambo ya jamii yake ya Kiislamu, hukerwa na kuguswa na hali ya Ummah na hutumia uwezo wake na nafasi yake kujaribu kutafuta njia, na fikra za kujaribu kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya jamii ya Kiislamu, na yote hayo huyafanya kwa ajili ya Akhera yake, Allaah Anasema katika Qur-aan:
(Na anayetaka akhera na akazifanyia jitahada amali zake, na hali ya kuwa ni Muislamu, basi hao jitahada yao hiyo itakuwa ni yenye kushukuriwa) 17:19
Himma ya mtu ni dalili ya akili yake na uwezo wa kufikiri, kwa yule mwenye Himma na mambo ya kipuuzi, anashughulishwa sana na mechi za mpira, asilimia themanini ya mazungumzo yake ni timu za mpira, ratiba ya mechi, mikataba ya wachezaji na kadhalika, basi huo ndio uwezo wake wa kufikiri, na ni mtu mwenye Himma ya chini sana.
Kuna mwingine yeye Himma yake ni kufuatilia mambo ya mitindo ya mavazi, ulimwende, ulimwengu wa nyimbo na mziki, basi huo ndio uwezo wake wa kufikiri, ni mtu mwenye Himma ya chini sana.
Anasema Ibnu Al-Jawziy:
“Katika alama za kukamilika kwa akili ya mtu ni kuwa mwenye Himma ya juu, na yule mwenye Himma za kipuuzi ni mpuuzi.”
Mafanikio yote ulimwenguni yamefanywa na watu wenye Himma za juu, watu ambao fikra zao zimevuka mipaka ya nafsi zao, watu ambao hawapotezi muda na juhudi katika mambo yasiyokuwa na faida kwa jamii, ukiangalia mifano ya Mitume wote wa Allaah walikuwa na Himma za hali ya juu sana.
SABABU ZA KUTOKUWA NA HIMMA:
1. KUIPENDA DUNIA NA KUCHUKIA KIFO
Aipandae dunia ni lazima atachukia kifo, huu ni msingi usiokubali mjadala, na kuipenda dunia ndio msingi wa maovu yote, na chanzo kikuu cha kuzama katika matamanio ya nafsi, mpenda dunia hayupo tayari kuipoteza dunia yake kwa sababu yoyote ile iwayo, hayuko tayari kupoteza cheo chake, mali yake, na starehe zake kwa ajili ya Akhera, na ndio maana anachukia kifo kwa sababu kifo ni kikata ladha, naye hana alichotanguliza Akhera, siku zote mwenye Himma ya chini huwa muoga wa kupoteza starehe za dunia, huwaogopa watu zaidi ya anavyomuogopa Allaah, yupo tayari kuuza Dini yake na misimamo yake kwa ajili ya kulinda na kuhifadhi dunia yake.
2. UVIVU NA UZEMBE
Mtu mwenye Himma ya chini siku zote huwa ni mvivu na mzembe, na hubuni mbinu nyingi za uvivu kwa kukwepa majukumu, mara nyingi utamkuta ni mtu mwenye kujiweka nyuma nyuma, huficha udhaifu wake kwa kupenda mzaha mzaha hata katika sehemu ambayo haihitaji mzaha, hushindwa kumwambia mtu ukweli, na badala yake humsengenya, na mara nyingi huwa hajiamini kabisa kwa kila analolifanya.
3. KUTAMANI NA KUTARAJIA
Mwenye Himma ya chini huwa ni mtu mwenye kutamani kupata ambacho hajakihangaikia, hupoteza muda wake katika kutarajia jambo ambalo halitatokea, huizuiya nafsi yake kufanya mambo ya kheri kwa kutaraji kuwa atakuja kuyafanya baadae, siku zote mambo ya kheri na yenye faida na Akhera yake yeye huyachelewesha ili ayafanye baadae, watu wa aina hii Allaah Amewataja ndani ya Qur-aan kwa kusema:
(Hata yatakapomfikia mmoja wao mauti, atasema; Mola wangu nirudishe ulimwenguni, ili nifanye mema sasa badala ya yale niliyoyaacha….) 23: 99-100
4. KUWAPENDA WASIO NA HIMMA
Mwenye Himma ya chini, siku zote huwapenda wasio na Himma kama yeye, na anapokaa nao hujisikia raha na huwaona wale ambao wana Himma ya juu kuwa wana majivuno na kiburi, na ni watu ambao huwezi kuishi nao na kufanya urafiki kwani wao muda wote, na mazungumzo yao ni mambo ya kazi, kuwajibika, kujadili, kupanga, kutekeleza, kutathmini, kufanya vikao, mikutano, na kadhalika, mambo ambayo kwa mwenye Himma ya chini anayaona kama adhabu. Hivyo mara nyingi utawakuta wenye Himma za chini wana muda mwingi kuliko majukumu, asilimia zaidi ya themanini ya mazungumzo yao ni porojo, mzaha, vichekesho, kusengenya, na kadhalika.
Itaendelea inshaAllaah…
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


