015-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Ulazima Wa Kusoma Suratul Faatihah Na Fadhila Zake

 

 

ULAZIMA (UFARADHI) WA AL-FAATIHA NA FADHILA ZAKE

 

Alikuwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akitilia mkazo na kusisitiza kuhusiana na (Alisisitiza mno) umuhimu wa Surah hii, alikuwa akisema: ((Hakuna Swalah kwa asiyesoma [ndani yake] Ufunguo wa Kitabu))[1]

 

Na Katika usemi mwengine: ((Swalah haitimii mtu asiposoma ndani yake Ufunguo wa Kitabu))[2]

 

Na wakati mengine anasema: ((Mwenye kuswali Swalah yoyote ile bila ya kusoma ndani yake Ufunguo wa Kitabu basi hiyo Swalah ni khiddaaj[3], ni khiddaaj, ni khiddaaj, haikukamilika))[4]

 

Na anasema (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Amesema: "Nimegawa Swalah[5] baina Yangu na mja Wangu (katika) sehemu mbili; nusu ya kwanza ni Yangu na nusu nyengine iliyobaki ni ya mja Wangu, na mja Wangu atapata alichokiomba" (Kisha) Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: Someni: Mja anasema: "Al-hamdu Llillaahi Rabbil ‘Alaamiyn”, Allaah (سبحانه وتعالى) Husema "Mja Wangu amenisifu" Mja akisema: "Ar-Rahmaanir Rahiym”, Allaah Husema: "Mja Wangu amenitukuza" Mja akisema: "Maalik/Malik”,Allaah Husema: Mja Wangu Ameniadhimisha" Mja akisema: "Iyyaaka na’budu wa iyyaaka nasta’iyn”, [Husema]: "Hii ni baina Yangu na Mja Wangu, na Mja wangu atapata atachoomba". Mja akisema: "Ih-dinaas swiraattal mustaqiym, swiraattal Laadhiyna An’amta ‘alayhim ghayril maghdhuubi ‘alayhim wala-dhwaaliyn”, [Husema] Yote haya ni ya Mja Wangu na Mja Wangu atapata aliyoyaomba"[6]

 

Alikuwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Allaah Aliyetukuka hakuteremsha katika Tawraat wala katika Injiyl chochote kile chenye kufanana na Ummul Qur-aan -Mama wa Qur-aan-, nayo Ni Aayah Saba zisomwazo mara kwa mara[7] [Na Qur-aan Tukufu niliyopewa])[8]

 

Alimuamrisha (صلى الله عليه وآله وسلم) "Mtu aliyeswali vibaya" aisome hiyo Faatihatul Kitaabu katika Swalah yake"[9](Lakini) na kwa yule asiyeweza kuihifadhi alimuambia (aliyeisahau): Sema:

 

Subhaana Llaah, Wal-Hamdu Lillaah, wala ilaaha illa Llaahu, wa Allaahu Akbar, wala Hawla wala Quwwata ila bi Llaah

 

Ametakasika Allaah  na sifa njema ni za Allaah  na hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Allaah, na Allaah  ni Mkubwa na Hakuna uwezo wala nguvu ila za Allaah[10]

 

 

Na (Pia) alimuambia "aliyeswali kimakosa": ((Ikiwa umehifadhi cho chote kile katika Qur-aan basi isome, vyenginevyo msifu Allaah, kiri Ukubwa Wake, na kiri kwamba hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye))[11]

 





 



[1] Al-Bukhaairy, Muslim, Abu 'Awaanah na Al-Bayhaqiy. Imetolewa katika Al-Irwaa (302)

[2] Ad-Daaraqutwniy, ambae amesema kuwa ni Swahiyh, na Ibn Hibbaan katika Swahiyh yake. Pia katika Al-Irwaa (302)

[3] Kwa maana kuwa ni kasoro, Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alifasiri kwa kusema: haikutimilia

[4] Muslim na Abu 'Awaanah.

[5] Ina maana kuwa ni Suratul Faatihah, ni katika mifano ya kutaja kitu chote lakini kinachokusudiwa ni baadhi tu ya kitu hicho, kwa kusisitiza umuhimu/utukufu wake.

[6] Muslim, Abu 'Awaanah na Maalik, na inayo yenye kuipa nguvu –shaahid- kutokana na Hadiyth ya Jaabir iliyothibiti kwa As-Sahmiy katika Taariykh Jurjaan (144)

[7] Al-Baajiy amesema: "Anakusudia maneno ya سبحانه وتعالى: ((Na tumekupa Aayah saba zinazosomwa mara kwa mara, na Qur-aan Tukufu)) [Al-Hijr: 15:87]. Imeitwa 'saba', kwa sababu ni Aayah saba, na al-Mathaaniy (inayosomwa mara kwa mara') kwa sababu inarudiwa katika kila rakaa, na sababu ya kuitwa (Imeitwa) 'Qur-aan Tukufu' kubainisha jina hili kwa ajili yake khaswa, japokuwa kila sehemu ya Qur-aan ni Tukufu. Kama inavyosemwa kuhusiana na Ka'abah kuwa ni 'Nyumba ya Allaah' japokuwa kuwa nyumba zote ni Zake Allaah, lakini hivi ni kwa njia ya kuibainisha umahsusi na utukufu wake"

[8]  An-Nassaiy na Al-Haakim ambae amesema kuwa ni Swahiyh na Adh-Dhahaabiy amekubaliana nayo.  

[9] Al-Bukhaariy katika makala yake 'Kusoma nyuma ya Imaam’ kwa isnaad Swahiyh.

[10] Abu Daawuud, Ibn Khuzaymah (1/80/2), Al-Haakim, At-Twabaraaniy na Ibn Hibbaan ambae pamoja na Al-Haakim, wamesema ni Swahiyh na Adh-Dhahabiy amekubaliana nayo. Imo katika Al-Irwaa (303)

[11] Abu Daawuud na At-Tirmidhiy ambae amesema ni nzuri; isnaad yake ni Swahiyh. (Swahiyh Abu Daawuud Namba. 807)

Share