Zingatio: Rudi Haraka

 

Zingatio: Rudi Haraka

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Dereva anakamata funguo za gari na kushtua engine ya gari, taratibu inaondoka na ipo barabarani tukiiona ikiwa kwenye mwendo. Rubani naye akamata usukani na kuirusha ndege hewani huku sisi ardhini tukiikodolea macho mithili ya udogo wa chembe ya mchanga hali ya kuwa ni yenye kusheheni mizigo au iliyojaa abiria walio wengi tu. Kama kweli twaamini ya kwamba ndani ya gari yupo dereva na ndani ya ndege yupo rubani, kwa nini tusikinaike kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaaa) ndiye Bwana wa Ulimwengu?

 

Na lau kama asingekuwepo dereva wa gari au rubani wa ndege, tusingeliona gari barabarani wala ndege angani. Na yareti kama asingekuwepo rubani, tusingeliona ndege ikiruka mji mmoja kwenda mji mwengine. Hali kadhalika, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ndiye Anayeliendesha jua, mwezi, nyota na sayari. Ndiye Anayegeuza usiku kwa mchana, na Yeye ndiye Aliyeumba kila kitu, basi hakuna shaka Muislamu kumuamini na kumkhofu Yeye tu kiitikadi na kivitendo. Na lau kama - astaghfiruLlaah – Ametakasika (Subhaanahu wa Ta’aalaa) – Angelikuwa hayupo, basi hakika jua, nyota, mwezi, sayari, usiku na mchana visingelikwenda na vingelisimama vyote. Hata utaratibu au nidhamu za vitu hivi visingekuwepo. Pia mimi na wewe wote tusingelikuwepo hapa duniani.

 

Mwenye kukanusha kuwepo kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) sio lazima atamke hadharani ya kwamba hamuamini Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ambaye Amechagua Uislamu kuwa ndio Diyn ya wanaadamu wote. Ni vitendo vyake ndio vitapambanua kwamba kweli anaamini au haamini kuwepo kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Uislamu unatutaka tunyenyekee kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Pekee bila ya kumshirikisha na tumche Yeye wakati wowote, mahali popote na hali yoyote[1]. Bila ya kusahau kwamba tunatakiwa mapenzi yetu yote tuyasalimishe kwa unyenyekevu mbele Yake, tunapohitaji msaada tuuombe Kwake moja kwa moja.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

Mjali Allaah naye Atakuhifadhi. Mjali Allaah utampata Yuko nawe. Ukimuomba muombe Allaah; ukitaka msaada taka msaada kwa Allaah...” [at-Tirmidhiy]

 

Katu binaadamu hakuja na chochote ndani ya Ulimwengu, vyote kavikuta na vyote ataviacha hapa duniani. Viumbe haviwezi kuwepo wenyewe bila ya sababu. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatoa kauli kali kabisa kwa wanaadamu kuasi kufuata maagizo Yake hali ya kuwa Yeye ndiye Aliyewaumba:

 

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ ﴿٣٥﴾أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ ﴿٣٦﴾

Au wameumbwa pasipo na kitu chochote au wao ndio waumbaji?Au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini. [At-twuwr: 35-36]

 

Elewa ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ndiye Bwana wa Ulimwengu na Yeye tu ndiye Anayeweka kumbukumbu kwa kila kitendo cha kila mwanaadamu. Tumche Yeye Pekee bila ya kumshirikisha na tutambue kwamba mapenzi Yake yapo karibu kuliko mapigo ya mioyo yetu, hivyo tunapotubia kwa ikhlaasw ya kweli basi Allaah kwa rahma Zake Atatupokea In sha Allaah. Nakuusia ndugu yangu Muislamu uzingatie Ukubwa wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ili upate kurudi haraka Kwake kabla ya kuchelewa.

 

[1] Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyopokelewa na At-Twaabraaniyy na iliyosimuliwa na Abu Dharr.

 

 

Share