021-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kunyanyua Sauti Na Kusoma Kimya Katika Swalah Tano Na Swalah Nyinginezo

 

KUNYANYUA SAUTI NA KUSOMA (KISOMO CHA) KIMYA KIMYA KATIKA SWALAH TANO NA NYINGINEZO

 

Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akitoa sauti katika Swalah ya Asubuhi na katika Rakaa mbili za mwanzo za Swalah ya Magharibi na 'Ishaa, na akisoma kimya kimya katika Swalah za Adhuhuri, Alasiri na Rakaa ya tatu ya Swalah ya Magharibi na Rakaa mbili za mwisho za Swalah ya 'Ishaa.([1])

 

Walikuwa wakiweza kuelewa kuwa anasoma kimya kimya kutokana na mtikisiko wa ndevu zake([2]) na kwa kuwasikilizisha Aayah mara nyingine([3]).

 

Pia alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akitoa sauti katika Swalah ya Ijumaa na Swalah za 'Iyd mbili([4]), na Swalah ya kuomba mvua([5]), na Swalah ya kupatwa([6]) jua au mwezi.

 

 

 

KUNYANYUA SAUTI NA KUSOMA KIMYA KATIKA SWALAH YA USIKU([7])

 

Ama katika Swalah ya usiku, mara nyingine alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma kimya kimya na mara nyingine kwa sauti([8]), na alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) anaposoma hali ya kuwa yuko nyumbani kwake, humsikia kisomo chake aliyeko barazani mwake([9]).

 

Huenda mara moja moja akapandisha sauti yake zaidi ya hivyo hadi akaisikia aliyelala([10]).  (Yaani nje ya baraza/uwa).

 

Na hivyo ndivyo alivyowaamrisha Abu Bakr na 'Umar (رضي الله عنهم) wakati alipokuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) ametoka nje usiku mmoja akatahamaki kumuona Abu Bakr (رضي الله عنه) anaswali huku akiishusha sauti yake chini. Na akampitia ‘Umar bin Al-Khatwtwaab (رضي الله عنه) aliyekuwa akiswali kwa kunyanyua sauti yake juu. (Baadaye,) walipokutana pamoja kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم). Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alisema: ((Ewe Abu Bakr! Nilikupitia na hali ukiwa unaswali kwa kushusha sauti yako)). Akasema: "Nimemsikilizisha niliyekuwa nanong’ona Naye ewe Mjumbe wa Allaah".  Akamwambia 'Umar: ((Nilikupitia na hali ukiwa unaswali kwa kupaza sauti yako)). Akasema: "Ewe Mjumbe wa Allaah! Nilikuwa naondosha usingizi na namkimbiza Shaytwaan". Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: ((Ewe Abu Bakr! Pandisha sauti yako kidogo. Na akasema kumwambia 'Umar: ((Ewe 'Umar! punguza sauti yako kidogo))([11]).

 

Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Mwenye kusoma Qur-aan kwa kunyanyua sauti, ni kama mfano wa mwenye kutoa sadaka kwa kuonekana na watu, na mwenye kusoma Qur-aan kimya kimya kwa kushusha sauti yake, ni kama mwenye kutoa sadaka kwa siri))([12]).

 





[1] Katika hili kuna Ijmaa ya Waislamu iliyopokewa na Khalaf kutoka kwa Salaf pamoja na Hadiyth Swahiyh ambazo zinathibitisha hayo kama alivyosema An-Nawawiy. Na zitafuatia baadhi yake. Tazama pia Al-Irwaa (345).  

[2] Al-Bukhaariy na Abu Daawuud.

[3] Al-Bukhaariy na Muslim.

[4] Tazama kisomo (sehemu ya TILAAWAH) chake (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Swalah ya Ijumaa na Swalah za 'Iyd mbili.

[5] Al-Bukhaariy na Abu Daawuud.

[6] Al-Bukhaariy na Muslim.

[7] 'Abdul-Haqq alisema katika Tahajjud (90/1):

"Ama Swalah za Sunnah za mchana, hakikusihi chochote Swahiyh kutoka kwake (صلى الله عليه وآله وسلم) chenye kuonyesha (kuhusu) kuswali kimya au kwa sauti katika Swalah hizo, Na kinachoelekea (inavyoelekea) zaidi ni kwamba alikuwa akisoma kimya kimya katika hizo Swalah. Imeripotiwa kutoka kwake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba mara moja (wakati wa mchana,) alimpitia 'Abdullaah Ibn Hudhaafa ambaye alikuwa akiswali mchana na kusoma kwa sauti, akamwambia: Ewe 'Abdullaah, Amesikia (mwache) Allaah (Asikie), na wala usitusikilizishe (sio) sisi)). Lakini Hadiyth hii haina nguvu"

[8]  Muslim na Al-Bukhaariy katika Af'aal Al-'Ibaad. 

[9] Abu Daawuud na At-Tirmidhiy katika Shamaail ikiwa na isnaad nzuri. Hadiyth ina maana kwamba yeye (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa yu katikati baina ya ukimya na kupaza sauti.   

[10] An-Nasaaiy na At-Tirmidhiy katika Shamaail na Al-Bayhaqiy katika Dalaail ikiwa na isnaad nzuri. 

[11] Abu Daawuud na Al-Haakim ambaye amesema kuwa ni Swahiyh na Adh-Dhahabiy amekubaliana naye.

[12] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.

Share