Nani Aliyepanga Surah, Aayah Na Nani Aliyetoa Majina ya Surah?

 

Nani Aliyepanga Suwrah, Aayah Na Nani Aliyetoa Majina ya Suwrah?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Swali La Kwanza: 

 

Asslaam aleykum,

Ni nani aliezipanga suwrah za Qur-an katika mpango tunaouona sasa. Ni kwa nini na kuna hikma gani. Ikiwa Suwrah Al-Baqarah imeteremshwa Madina kwa nini iwe ya pili katika msahafu na isiwe ya 86, kwani za mwanzo zilianza kuteremshwa Makkah?

 

Swali La Pili:

Shekh, naomba tafadhali maelezo nani aliyetoa majina ya sura za qurani?  Vipi zimepangwa aya ikiwa Qurani imeteremshwa kidogo kidogo kuanzia iqra hadi aya za mwisho kabla kufa Nabiy maana naona imeanza Alhamdu na kumalizikia Qul-audhu. 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Ni jambo linaloeleweka kuwa hakuna jambo lolote la Uislamu isipokuwa lina hekima kubwa ni sawa tunazijua hizo hekima au la.

 

Mpangilio wa Qur-aan na majina yake yamepangwa na Yeye Mwenyewe Allaah Mwenye hekima na busara kubwa. Tufahamu kuwa Qur-aan yote ilikuwa imehifadhiwa na Allaah Aliyetukuka katika sehemu inayoitwa Lawhul Mahfuudh na kisha kuteremshwa yote usiku wa al-Qadr katika mwezi wa Ramadhwaan hadi wingu wa duniani. Kutoka hapo Jibriyl ('Alayhis Salaam) akawa ni mwenye kupatiwa amri na Aliyetukuka kumteremshia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) kidogo kidogo kwa miaka 23 kulingana na mahitajio.

 

Kila ilipokuwa inateremshwa Surah au baadhi ya Aayah Jibriyl ('Alayhis Salaam) kwa maagizo kutoka kwa Allaah Aliyetukuka alikuwa akimuamuru Nabiy (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) aiweke mahali kadhaa na jina la Suwrah liwe kadhaa. Baada ya kuhama Madiynah, Jibriyl alikuwa akija kila Ramadhwaan kumsikiliza Nabiy (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) kisomo cha Qur-aan. Na ule mwaka aliokufa, Jibriyl alikuja mara mbili na mara ya mwisho Zayd bin Thaabit (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwepo.

 

Hivyo, alivyoaga dunia (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam), Swahaba (Radhwiya Allaahu 'anhum) waliandika Qur-aan kama walivyofundishwa na kuagiziwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam). Hata wale waandishi wa Nabiy (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wakipatiwa maagizo hayo.

 

Ama kuhusu Suwrah Al-Baqarah kuwa ni ya 86 si kweli na huenda kuwa ndugu yetu akawa amekosea katika ubinaadamu wake. Na hilo si la ajabu. Hakika ni kuwa Suwrah Al-Baqarah ni Suwrah ya 87 kuteremshwa na ya kwanza kuteremka Madiynah. Surwah ya mwisho kuteremshwa Makkah ilikuwa ni ya 86 nayo ni Suratul Mutwaffifiyn (83).

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share