Tunda Ambalo Alikula Nabiy Aadam Na Hawwaa

 

Tunda Ambalo Alikula Nabiy Aadam Na Hawwaa

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

As salaam aleikum, mimi naitwa mussa ni mkaazi wa unguja na ambae ni mfuatiliaji sana wa darsa za maalim othman, lakini hivi sasa nipo turkey, nilikuwa nauliza kwamba kunu tetesi kuwa lile tunda ambalo walokula nabiy adam na bi hawa ni kitendo cha kujaamiana, sasa ni kweli au pr

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Ninamshukuru ndugu yetu kwa swali lake hilo japokuwa sehemu ya mwisho haijafahamika Hakika zipo rai nyingi na tofauti kuhusu mti aliokatzwa Nabiy Aadam (‘Alayhis-salaam) kuukurubia. Tofauti hizi zipo baina ya Swahaba na watangu wema waliokuja baada yao. Na katika hilo mufassirina wametofautiana wapo ambao hawakutaja majina ya miti yenyewe na wapo wale ambao walijitahidi na kuitaja kama katika tafsiri ya Ibn Kathiyr, na Ash-Shawkaaniy na Al-Qurtubiy. Wao wametoa tofauti za wanazuoni na kusema kuwa mti huo ulikuwa ni wa mzabibu, na wengine wanasema wa shayiri, mtende, mtini na kadhalika. Lakini Ibn Kathiyr ameongeza kuwa hakuna aayah ya wazi inayotaja jina la mti huo wala Hadiyth Sahihi kuhusu jambo hilo.

 

Lililo muhimu ni kuwa kuujua mti aliokula Nabiy Aadam (‘Alayhis-salaam) na mkewe haitotufaidi sisi kwa chochote. Imani yetu haitazidi wa kupungua kwa kuujua au kutoujua. Na sisi kama Waislamu hatufai kupoteza muda mwingi sana katika jambo kama hilo kwani Muislamu hana wakati katika huu ulimwengu kuupoteza au kuukata kwa kuuua. Kila nukta inahesabiwa na tutakwenda kuulizwa kuhusu ujana wetu na umri wetu Siku ya Kiyama. Hivyo, tuachane na mijadala au tafiti kama hizo.

 

Fundisho tunalopata muhimu katika maisha yetu kuhusu kisa cha Aadam (‘Alayhis-salaam) na mkewe ni kuwa shetani ana njia nyingi za kumpoteza mwanadamu na anakuja kwa njia nzuri. Na hii njia tunaiona hapa pale Iblis alipowaambia:

 

وَقَاسَمَهُمَا إِنِّي لَكُمَا لَمِنَ النَّاصِحِينَ ﴿٢١﴾فَدَلَّاهُمَا بِغُرُورٍ ۚ فَلَمَّا ذَاقَا الشَّجَرَةَ بَدَتْ لَهُمَا سَوْآتُهُمَا وَطَفِقَا يَخْصِفَانِ عَلَيْهِمَا مِن وَرَقِ الْجَنَّةِ ۖ وَنَادَاهُمَا رَبُّهُمَا أَلَمْ أَنْهَكُمَا عَن تِلْكُمَا الشَّجَرَةِ وَأَقُل لَّكُمَا إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمَا عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿٢٢﴾

Naye akawaapia: Hakika mimi kwenu nyinyi wawili ni mwenye kukunasihini kidhati. Basi akawachota (wote wawili) kwa ghururi. Walipoonja mti ule zikawafichukia sehemu zao za siri; na wakaanza kujibandika majani ya Jannah. Na Rabb wao Akawaita: Je, kwani Mimi Sikukukatazeni mti huo na kukuambieni kwamba shaytwaan ni adui bayana kwenu?[Al-A'raaf: 21-22]

 

Na Allaah Anatueleza kwa uwazi kuhusu shaytwaan, Aliposema:

 

..وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿٢٠٨﴾

Na wala msifuate hatua za shaytwaan. Hakika yeye kwenu ni adui wa wazi. [Al-Baqarah: 208]

 

Hivyo, inafaa tujichunge sana tusije tukaingia katika mitego yake na hivyo kuhasirika hapa duniani na kesho Aakhirah.

 

Nukta ingine ni kusahihisha jina la mkewe Nabiy Aadam (‘Alayhis-salaam), ambalo kaka yetu kasema ni bi Hani na huu ni ubinadamu kukosea. Hakika ni kuwa jina la mkewe lilikuwa ni Bi Hawwaa. Natumai katika sentensi iliyopigwa msitari ndugu yetu atatufafanulia ili tuweze kumjibu kwa hilo pia.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi 

 

 

Share