Du’aa Ya Imaam Baada Swalah Inapasa Kunyanyua Mikono?

SWALI:

 

Pia alisema kuwa ikiwa imamu yuwatoa dua kwa jumla hatufai kuomba kwa matumbo ya mikono yetu twafaa tuitikie amin basi bila ya kunyanyua mikono, akasema kwa sababu ile huwa ni dua ya jumla na haipaswi kunyanyua mikono. Je hivi ni sawa.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu du'aa katika Swalah ya Ijumaa. Hata hiyo, swali lako haliko wazi na dhahiri kama inavyohitajika ili tuweze kukujibu kama inavyotakiwa. Hili huwa linatupatia usumbufu kwani inabidi tuanze kufikiria ulikuwa unataka kuuliza lini.

 

Tunawaomba waulizaji maswali waulize maswali yalio wazi ili kusiwe na usumbufu wa kuyarudisha kwa waulizaji kwa ajili ya kupata ufafanuzi. Inaonekana kama muulizaji anauliza kuhusu du'aa anayotoa Imaam wakati yuko juu ya mimbari. Inafaa tufahamu kuwa Imaam kutoa du'aa wakati huo ni Sunnah kwa sababu ya kufanya hivyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Sahl bin Sa'd (Radhiya Allaahu 'anhu) aliyesema: "Sikumuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akinyanyua mikono yake kabisa akiwa anaomba juu ya mimbar wala sehemu nyengine, lakini nilimuona akisema hivi, na akaashiria kwa kidogo chake cha shahada" (Abu Daawuud).

 

 Hivyo Imaam aweza kuomba du'aa ndani ya khutbah bila kunyoosha mikono yake na maamuma ni hivyo hivyo waweza kuitikia ndani ya nyoyo zao bila kunyoosha mikono yao.

 

Ama ikiwa ni baada ya Swalah basi Sunnah ni kuwa Imaam haleti du'aa na maamuma wakaitikia bali kila mmoja atasoma uradi uliofundishwa katika mafunzo sahihi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘layhi wa aalihi wa sallam) na kisha baada ya kuswali Swalah ya Sunnah mtu anaweza kumuomba Allaah Aliyetukuka kwa anachotaka. Na sehemu bora kabisa za kuomba du’aa tulishataja katika majibu mengine, nazo sehemu hizo ni katika wakati mtu anaposujudu ndani ya Swalah, au wakati anapomaliza tajiyaat na kabla hajatoa salaam.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share