Hizbut-Tahriyr Ni Nani, Wana Lengo Gani Na Je, Inafaa Kuwafuata?

 

Hizbut-Tahriyr Ni Nani, Wana Lengo Gani Na Je, Inafaa Kuwafuata?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Assalam Alaaikum  Sheh Naomba Kuuliza Kuhusu Suala Hili Lililoingia Sasa Yaha Ya Hawa Watu Wanojiita Hizbu Tahriri Vipi Naomba Maelezo Zaidi Kwa Sababu Naona Sijawaewa Hasa Wana Lengo Gani Katika Dini Jee Wanafaa Au Ni Wapotofu Katika Dini Plse Naomba Maelezo Kwa Ufafanuzi Zaidi Ili Niweze Kua Na Utulivu Ahsante.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Majibu ya swali hili ni marefu, lakini tutajaribu kukufahamisha kwa mukhtasari kwa faida yako na faida ya wasomaji wetu kuhusu Hizbut-Tahriyr.

 

Hizbut Tahriyr: Maana ya neno Hizbu ni Chama (umoja, walioungana), maana ya At-Tahriyr: kukifanya kitu kiwe huru, kukomboa.

 

Hizbut-Tahriyr ni chama cha kisiasa chenye mrengo wa Kiislamu, wanadai lengo lao kuu ni kurejesha mfumo wa Ukhalifa kwa kutegemea fikra na maono zaidi, katika kuleta mabadiliko hayo, tayari chama hicho kimeishatoa ijtihaadaat zake za kisharia ambazo nyingi miongoni mwa ijtihaadaat hizo zimepingwa vikali na Wanachuoni wa Kiislamu wanaotambulika.

 

Chama hiki kilianzishwa na Taqiyyud Diyn An-Nabahaaniy mwaka 1909 – 1979 huko Palestina, alizaliwa katika kijiji cha mji wa Hayfaa, na masomo yake ya juu aliyachukulia katika chuo kikuu cha Al-Azhar na Dar Al-‘Uluum nchini Misri, na kisha akarudi Palestina na kuwa mwalimu na hatimaye akateuliwa kuwa Qaadhi katika maeneo tofauti nchini Palestina.

 

Baada ya mwaka wa (nakbah) kushindwa kwa majeshi ya Kiarabu 1947-48 alihama yeye na familia yake katika mji wa Beirut, na hatimae kuteuliwa kuwa mjumbe katika Mahakama kuu ya Rufaa katika mji wa Quds, na kisha kuwa Mhadhiri katika Kitivo cha Uislamu Amman, Jordan.

 

Mwaka 1952 aliasisi chama chake na akawa Rais wa chama hicho, na shughuli zake kuu zikawa ni kuandika vitabu, makala, kusambaza vipeperushi kuandaa makongamano, warsha, mikutano ya kueneza sera na fikra ya chama hicho, na akawa ni mwenye kuhama hama baina ya Jordan, Syria na Lebanon, na hatimae alifariki na kuzikwa nchini Lebanon.

 

 

Fikra Na ‘Aqiydah Ya Hizbut-Tahriyr:

 

  • Fikra na ‘Aqiydah ya Hizbut-Tahriyr zinafanana na Khawaarij na wako mbali na misingi ya Ahlus Sunnah Wal-Jama’ah.

 

  • Lengo lao kuu ni kurejesha maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Dola ya Ukhalifa katika nchi za Kiarabu kwanza, kisha kusimamisha Ukhalifa katika nchi za Kiislamu, na mwisho kabisa kufanya Da’wah katika nchi zisizokuwa za Kiislamu.

 

  • Muasisi wa Hizbut-Tahriyr alikuwa ameathiriwa kwa kiwango kikubwa na imani ya utaifa (Qawmiyyah) kama alivyobainisha hayo katika kitabu chake ((رسالة العرب (Ujumbe kwa Waarabu) na ndio maana akagawa watu katika misingi ya Uarabu, Uislamu, na Ukafiri.

 

  • Muasisi wa chama hiki alikuwa na mahusiano ya karibu na Kundi la Ikhwaan Al-Muslimiyn (Muslim Brotherhood) la Jordan, lakini alitofautiana na kundi hilo katika muelekeo na vipaumbele (priorities) na kuamua kuanzisha chama chake.

 

  • Kigezo kikuu cha Hizbu katika kufikia malengo yake hayo, ni kutumia mfumo wa fikra na ustaarabu wa Kiislamu katika kumjenga Muislamu katika shakhsiyah yake na kisha kuujenga Ummah wa Kiislamu, chama hutia mkazo mkubwa kwa wanachama wake kuhakikisha kuwa inawajenga katika mfumo wa kimwili zaidi kuliko kiroho.

 

  • Malezi ya wanachama yanazingatia zaidi mwili na kupuuza mambo ya kiroho.

 

  • Wanapinga Hadiyth Al-Ahaad na kwa maana hiyo hawaamini juu ya adhabu ya kaburi.

 

  • Hawaamini kuwa kuna Masiyh Ad-Dajjaal.

 

  • Wana itikadi za kikafiri kama kuamini kuwa Nabiy 'Iysaa ('Alayhis-salaam) amekufa! Itikadi hii ni itikadi ya Makafiri Manaswara na wengine kama Qadiyaani (Ahmadiyyah).

 

  • Viongozi wa Hizbu wanaona kuwa suala la kuamrisha mema na kukataza maovu ni kikwazo cha kufikia malengo ya muda, na kazi hiyo ni jukumu la Dola ya Kiislamu na si watu binafsi.

 

  • Wana mashirikiano na makundi mengine potofu kama lao, kwa lengo la kukusanyana ili kufikia hiyo wanayodai ni Khilaafah.

 

  • Wana uadui mkubwa na Ahlus-Sunnah wal-Jamaa'ah (Salafi) na wako tayari kushirikiana na makundi mengine adui ili kupiga vita Da'watus-Salafiyyah.

 

  • Wanatukana Wanachuoni, na wanafikia kuwaita Wanaafiq na hata Makafiri. Hawana tofauti na Khawaarij.

 

  • Chama kina Katiba yake yenye vipengele 187 vya kusimamisha na kuendesha Dola ya Kiislamu.

 

Fiqh Na Shari’ah:

 

Katika vigezo vya kuzalisha hukmu za kishari'ah, hususan katika chimbuko la Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Wanachuoni wa Hizbu wamejiwekea vigezo vigumu ambavyo kwa mujibu wa vigezo hivyo hujikuta wakitoa fatwa zenye utata mkubwa, kama vile kutokubali Hadiyth za Aahaad (Hadiyth zilizokuja katika mapokezi mamoja na si katika mapokezi ya wengi ‘Mutawaatir’) katika masuala ya ‘Aqiydah.

 

Wanachuoni wa Chama hicho wametoa fatwa za ajabu kabisa katika mambo ya msingi kabisa katika Shari'ah za Kiislamu ambayo uharamu wake uko wazi, kama vile:

 

  • Kuruhusu kuangalia picha za uchi.

 

  • Kuruhusu kumbusu mwanamke asiyekuwa Mahram yako wakati wanaposalimiana, kama zile salaam za wasiokuwa Waislam wanapokutana.

 

  • Kujuzisha kwa Mwanamke kuvaa Wigi (Nywele za bandia) na Suruali.

 

  • Kujuzisha kuacha kuswali na kufunga kwa wakazi wa North Pole na South Pole.

 

  • Wanajuzisha watu wanaoishi Ulaya kuchukua misaada katika serikali na kutokufanya kazi, wakidai kwamba maadam hakuna Khaliyfah basi kunakuwa hakuna mkataba na Makafiri au nchi na hivyo kutokufuata sheria zao na kukiuka taratibu zilizowekwa.

 

  • Miaka ya 80 walikwenda viongozi wa Hizbu kumuona kiongozi wa Kishia wa Iran, Khomeini na kumpa bay’ah na kumuomba awakubali washirikiane nao katika kusimamisha Khilaafah, lakini Kiongozi huyo hakuwajibu chochote na mwisho waliachana naye na wakaifuta bay’ah yao kwake!

 

  • Kutukana na kuwakufurisha Wanachuoni na Waislamu wanaotofautiana nao ni jambo jepesi sana  kwao. Wameanzisha misamiati mbalimbali ya kuwatukana na kuwadhalilisha Wanachuoni wa Ahlus-Sunnah wal-Jamaa'ah kama kuwaita: 'Wanachuoni wa Sultani', 'Wanachuoni wa hedhi na nifasi', 'Vibaraka', 'Wanafiki' na hata kuwaita 'Makafiri'!

 

  • Wanashirikiana na kuunga makundi yote ya Takfiyriy (yenye kukufurisha Waislamu na kumwaga damu zao).

 

Masuala mengi kama haya wafuasi wadogo wadogo wa Hizbu ambao mara nyingi huwa ndio wenye hamasa na Jazba, hawayajui mengi katika haya, na hata wakitajiwa wanapinga kwa nguvu zote na kuhisi wanatuhumiwa. Inasikitisha wengi wao si wenye kutafuta elimu, wamegubikwa zaidi na hamasa na kufuatilizia tu mambo ya kisiasa na kupenda zaidi mjadala na malumbano na huwa mahodari sana wa kubishana na kila mmoja japo ataingia Hizbu siku chache na bila kuwa na elimu ya dini atasimama kwenye kiriri na kuhubiri na kupigania Khilaafah!

 

 

Hitimisho:

 

Waasisi wa Hizbut-Tahriyr, kama walivyokuwa waasisi wa makundi mengine ya Kiislamu kama Ikhwaan Al-Muslimiyn, waliasisi chama chao kutokana na uchungu waliokuwa nao juu ya hali ya Uislamu na Waislamu ulimwenguni.

 

Lakini katika kuweka misingi ya kuyaendea malengo yao, walitumia vigezo vya fikra na uzoefu wa kisiasa zaidi ya vigezo vya ufahamu sahihi wa Qur-aan na Sunnah.

 

Kama walivyokuwa Mu’utazilah katika kipindi cha nyuma, pamoja na juhudi kubwa waliyoifanya kupambana na falsafa na fikra za kizandiki, lakini waliingia katika kosa hili hili la kupima mambo kwa kutumia vigezo vya akili, mantiki, na falsafa, na kutafsiri mafunzo yote ambayo walikuwa wanayaona hayaendani na akili zao kwa mujibu wa ufahamu wao wa mazingira yao, jambo ambalo liliwaingiza katika uzandiki wa wazi kwa kukanusha mambo ambayo yana ushahidi sahihi wa Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Hizbut-Tahriyr ni chama cha kisiasa kimtazamo na kimuelekeo, na waasisi wa chama hiki wanakiri kupitia vitabu vyao kuwa ni chama cha kisiasa kabla ya kuwa chama cha Da’wah, hawaamini sana katika mihadhara na mawaidha kama inaweza kuleta mabadiliko, bali kwa juhudi za kisiasa na kubadili mifumo iliyopo.

 

Kwa mwanahizbu kuanza juhudi zake katika nchi zisizokuwa za Kiarabu ni kwenye kinyume na malengo makuu na sera za Waasisi, bali mabadiliko yanabidi yaanzie katika nchi za Kiarabu, Ukhalifa unapopatikana katika nchi hizo, nchi zingine za Kiislamu zitashinikizwa kuingia katika mfumo wa Ukhalifa, na Dola ndio itasimamia baada ya hapo kazi ya kuamrisha mema na kukataza maovu.

 

Kwa ujumla Hizbut-Tahriyr kama chama kina makosa mengi na ya msingi, na kwa mfumo wake ni vigumu kupata mafanikio chanya kwa ajili ya Ummah, bali madhara yake yanaweza kuwa makubwa kwa mustakbali mzima wa Uislamu.

 

Fikra yoyote inayopingana na mas-alah sahihi ya ‘Aqiydah yaliyothibiti, na kuachana na misingi ya mafunzo ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kutawaliwa na matamanio ya nafsi na hisia na hamasa bila chimbiko lenye mashiko, haziwezi kuwa fikra za kufuatwa japo ziletwe na yeyote awaye. Hivyo, mwamko huo na harakati hizo, si rahisi kufanikiwa hadi kwanza zirejeshe ufahamu sahihi wa Uislam kama ulivyoletwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Mfumo sahihi unaoweza kuleta faraja kwa Waislamu ni mfumo wa Ahlus Sunnah Wal-Jama’ah kwa ufahamu wa As-Salaf Asw-Swaalih, lakini kwa masikitiko, mfumo huu bado haujafahamika vizuri na Waislamu waliokuwa wengi.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share