026-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kisomo Chake (صلى الله عليه وآله وسلم) Katika Swalah Ya Usiku - Sifa Ya Swalah Ya Mtume

 

1.    SWALAH YA USIKU  

 

Alikuwa  (صلى الله عليه وآله وسلم)mara nyingine akifupisha ([1]) kisomo katika hiyo Swalah ya usiku, na mara nyingine hukirefusha, na wakati mwengine hukirefusha sana, mpaka ikampelekea 'Abdullaah bin Mas'uud kusema: "Usiku mmoja niliswali pamoja na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), basi aliendelea kusimama (kwa) muda mrefu sana mpaka nikawaza jambo baya. Pakaulizwa: "Uliwaza nini"? Akajibu: "Nilifikiria kukaa chini na kumuacha Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم)!([2]).    

 

Hudhayfah bin Al-Yamaan pia alisema:

"Usiku mmoja niliswali na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), basi alianza kusoma Suratul Al-Baqarah (2: 286). Nikasema (moyoni): "Atarukuu baada ya Aayah mia". Lakini aliendelea, nikawaza kuwa huenda ataimaliza Surah katika [rakaa mbili]. Lakini aliendelea na nikasema: "Atarukuu atakapoimaliza." Kisha akaanza kusoma Suratun-Nisaa (4: 176), akaisoma yote. Kisha akaanza kusoma Suratul-'Imraan (3: 200)([3]), akaisoma yote. Alikuwa akisoma polepole, anapopita kwenye Aayah zenye kumtukuza Allaah humtukuza, na anapopita kwenye Aayah zenye maombezi huomba, na anapopita kwenye Aayah za kujikinga hujikinga. Kisha akarukuu…" (Hadi mwisho wa) Hadiyth.([4])

 

Pia usiku mmoja alipokuwa akiumwa, alisoma Surah saba ndefu.([5])

 

Pia alikuwa akisoma moja ya Surah hizi saba ndefu katika kila rakaa.([6])

 

Haikupata kutokea kuwa yeye (صلى الله عليه وآله وسلم) alisoma Qur-aan nzima katika usiku mmoja [abadani]([7]), na wala hakumkubalia hivyo 'Abdullaah bin 'Amru (رضي الله عنه) wakati alipomwambia: ((Soma Qur-aan nzima kila mwezi)). Akasema: Nikamwambia: "Ninao uwezo wa kufanya zaidi ya hivyo". Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: ((Isome katika masiku ishirini)). Akasema: Nikamwambia: "Ninao uwezo wa kusoma zaidi". Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: ((Basi isome katika siku saba na wala usipunguze zaidi ya hapo)).([8])

 

Kisha Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alimruhusu kuisoma Qur-aan nzima katika siku tano.([9])

 

Kisha Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alimruhusu kuisoma Qur-aan nzima katika siku tatu.([10])

 

Kisha Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akamkataza kuisoma Qur-aan nzima chini ya hivyo([11]) na akatoa sababu kwayo kwa kumwambia: ((Yeyote atakayesoma Qur-aan nzima chini ya siku tatu, hatoweza kuifahamu))([12]). Na katika riwaaya nyingine: ((Hawezi kufahamu mwenye kuisoma Qur-aan nzima chini ya siku tatu)).([13])

 

Kisha alimwambia: ((Kwa hakika kila mwenye kuabudu huwa ana muda wa shirrah([14]),  na kila shauku ina kipindi cha kupunguka, aidha ielekee kwenye Sunnah au kwenye bid'ah. Hivyo basi mwenye kuwa upungufu wake umeelekea kwenye Sunnah, huyo basi amepata uongofu, na mwenye kuwa upungufu wake umeelekea kwenye kinyume cha hivyo, basi ameangamia))([15]).

 

Kwa sababu hii, akawa  (صلى الله عليه وآله وسلم) hasomi Qur-aan nzima chini ya siku tatu.([16])

 

Na alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Atakayeswali katika usiku na akasoma Aayah mia mbili, basi huandikwa miongoni mwa watiifu wenye kumtakasia Allaah )).([17]) 

 

Pia alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma Surat Bani Israaiyl (17: 111) na Surat Az-Zumar (49: 75) katika kila usiku([18]). Na alikuwa akisema: ((Atakayeswali katika usiku na akasoma Aayah mia, basi hatoandikwa miongoni mwa walioghafilika))([19]). Mara nyingine alikuwa akisoma katika kila Rakaa kiasi cha Aayah khamsiyn au zaidi([20]), na mara nyingine akisoma kiasi cha Suratul Al-Muzammil (73: 20).([21])

 

Na wala hakuwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akiswali usiku mzima([22]), isipokuwa kwa nadra, kwani mara moja ‘Abdullaah bin Khabbaab bin al-Arat - ambaye alishuhudia vita vya Badr pamoja na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) – alimpeleleza Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) usiku mzima, na katika riwaaya nyingine: katika usiku alioupitisha kwa kuswali usiku mzima hadi ikawa pamoja na Afajiri. Alipoimaliza Swalah yake, Khabbaab alimwambia: "Ewe Mjumbe wa Allaah! Kwa heshima zote za baba yangu, nakupa wewe na heshima zote za mama yangu!

 

"Usiku wa leo umeswali Swalah sikuwahi kukuona kuswali mfano wake".

 

Akasema   (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Ndio, ilikuwa Swalah ya shauku na khofu, (na mimi kwa hakika) nilimuomba Mola Wangu عزوجل  mambo matatu, Amenipa mawili, na Amenikatalia moja. Nilimuomba Mola wangu Asituangamize kwa kile Alichowaangamizia Ummah za kabla yetu [na katika riwaaya nyingine]: ((Asiuangamize Ummah wangu kwa njaa) Akanipa hilo, Nikamuomba Mola wangu عزوجل Asitusalitishe na adui asiye kuwa miongoni mwetu, Akanipa hilo, na nilimuomba Mola wangu Asituvurunge vurunge mpaka tukawa makundi yasiyopatana kwa mfarakano, (lakini) Amenikatalia hili)).([23]) 

 

Na usiku mmoja alisimama (صلى الله عليه وآله وسلم) (katika Swalah) akawa akikariri Aayah moja hadi alfajiri. Aayah yenyewe ni:

 

(( إِن تُعَذِّبْهُمْ فَإِنَّهُمْ عِبَادُكَ وَإِن تَغْفِرْ لَهُمْ فَإِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ))

 

((Ukiwaadhibu, basi hao ni waja Wako. Na Ukiwasamehe, basi Wewe Ndiye Mwenye nguvu na Mwenye hikmah)). [Al-Maaidah 5: 121]

 

[kwayo karukuu nayo, na kwayo kasujuduia na kwayo kaomba], [Kulipopambazuka, Abu Dharr (رضي الله عنه) alimwambia: "Ewe Mjume wa Allaah! Hukusita kuisoma Aayah hii hadi kumepambazuka, umerukuu nayo, umesujudu nayo] [na umeomba nayo] [hali ya kuwa Allaah Amekufundisha Qur-aan nzima], [lau (ingelikuwa) mmoja wetu amefanya hivi, tungelimkemea]. [Akasema: ((Hakika nimemuomba Mola wangu عزوجل kuwashufaia Ummah wangu, Akanipa hilo, na Uombezi huo utapatikana Allaah Akipenda kwa yeyote asiyemshirikisha Allaah na kitu cho chote kile)).([24])

 

Mtu alimwambia: "Ewe Mjumbe wa Allaah! Mimi ninaye jirani anayesimama kuswali usiku na hasomi isipokuwa:

 

((قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ))

((Sema: Yeye Allaah ni wa Pekee)) [Al-Ikhlaasw 112: 4],

(anaikariri) [haongezei nyingine] kama kwamba anaiona kuwa hadhi yake ni ndogo". Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: ((Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko Mikononi Mwake, hakika hiyo ni sawa na thuluthi ya Qur-aan)).([25])

 

 

[1]  An-Nasaaiy ikiwa na isnaad Swahiyh.

[2]  Al-Bukhaariy na Muslim.

[3] Hivi ndivyo ilivyopokelewa kutangulizwa Suratun-An-Nisaa (4) kabla ya Al-'Imraan (3), na hiyo ni dalili kwamba inaruhusiwa kusoma kwa kuacha kufuatilia mpangilio wa Msahafu wa 'Uthmaan katika kusoma. Umekwishapita mfano kama huu.

[4]   Muslim na An-Nasaaiy.

[5]  Abu Ya'laa na Al-Haakim ambae amesema kuwa ni Swahihy, na Adh-Dhahabiy amekubaliana naye. Ibn Al-Athiyr amesema: “….Surah saba ndefu ni: Al-Baqarah (2), Al-'Imraan (3), An-Nisaa (4), Al-Maaidah (5), Al-An'aam (6), Al-A'raaf (7) na At-Tawbah (9)".

[6]   Abu Daawuud na An-Nasaaiy kwa isnaad Swahiyh.

[7]   Muslim na Abu Daawuud.

[8]  Al-Bukhaariy na Muslim.

[9] An-Nasaaiy na At-Tirmidhiy ambaye amesema kuwa ni Swahiyh.

[10] Al-Bukhaariy na Ahmad.

[11] Ad-Daarimiy na Sa’iyd ibn Masnuur katika Sunan yake kwa isnaad Swahiyh.

[12] Ahmad kwa isnaad Swahiyh.

[13] Ad-Daarimiy na At-Tirmidhiy ambaye amesema kuwa ni Swahiyh.

[14] "Shirrah" ni msisimko, hamu, shauku, nguvu. Na Shirrah ya vijana mwanzo wake ni bidii, nguvu, hamasa na raghba. Imaam Atw-Twahaawiy amesema: "Ni bidii na hamasa katika vitendo ambavyo wanavitaka Waislamu kutokana na nafsi zao wenyewe katika ‘amali zao ambazo wanajikurubisha kwazo kwa Mola wao عزوجل. Na kwa hakika Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) anapenda zaidi kutoka kwao hivyo, na sio vile vitendo walivyovianza kutokana na shauku na hamasa ambayo hawana budi isipokuwa watakuwa na upungufu na kuachana navyo na kushikamana na kinyume chake. Kwa hiyo, aliwaamrisha waendelee kushikamana na vitendo vyema ambavyo wataweza kuviendeleza na kudumu navyo hadi watakapokutana na Mola waoعزوجل . Katika kulifafanua hili, imesimuliwa kutoka kwake  (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba amesema: ((Vitendo vipendezavyo kwa Allaah, ni vile vyenye kudumishwa japo kuwa ni vichache)).

Nasema: "Hadiyth hii ambayo ameitoa kwa njia ya kuonyesha kuwa  msimulizi wake hajulikani (Majhuul) kama linavyomaanisha neno "imesimuliwa", ni Swahiyh na ni waliyowafikiana kwayo Al-Bukhaariy na Muslim kutokana na Hadiyth ya Mama wa Waumini 'Aaishah (رضي الله عنها).

[15]  Ahmad na Ibn Hibbaan katika Swahiyh yake.

[16] Ibn Sa'ad (1/376) na Abu-Ash-Shaykh katika Akhlaaq An-Nabiyy (صلى الله عليه وآله وسلم) (281).

[17]   Ad-Daarimy na Al-Haakim ambaye amesema kuwa ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubaliana naye.

[18] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.

[19] Ahmad na Ibn Naswr kwa isnaad Swahiyh.

[20] Al-Bukhaariy na Abu Daawuud.

[21] Ahmad na Abu Daawuud kwa isnaad Swahiyh.

[22] Muslim na Abu Daawuud. Nimesema: "Kwa Hadiyth hii na nyingine, inaonyesha kuwa ni makruuh kukesha usiku mzima kila siku au aghlabu, kwani ni kinyume na mwenendo wake (صلى الله عليه وآله وسلم), na lau ingelikuwa kukesha usiku mzima ni bora, basi hilo lisingelimpita  Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم). Na uongofu bora kabisa ni uongofu wa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم). Na wala usidanganyike na yaliyosimuliwa kuhusu Abu Haniyfah kwamba yeye alikuwa akiswali Swalah ya al-Fajr kwa wudhuu wa 'Ishaa kwa miaka arubaini!! [Maelezo ya Mfasiri: Taz. Tabliygh An-Nisaab: Fadhila za Swalaah kilichoandikwa na Maulana Zakariyyah Kandhalvi kwa mifano ya dai kama hili]. Kwani usimulizi huu kutoka kwake, hauna msingi wo wote ule, bali 'Allaamah Al-Fairuuz ‘Abaadi amesema katika Ar-Radd 'alaa al-Mu'taridh (44/1): "Usimulizi huu ni miongoni mwa uongo uliowazi ambao haupaswi kuambatanishwa na Imaam, kwani hakuna fadhila yenye kutajwa katika kufanya hivyo. Na ilikuwa ni vyema kwa mfano wa Imaam kama huyu, kufanya yaliyo bora zaidi, na hakuna shaka yoyote ile kwamba kutawadha upya (Tajdiydul Wudhuu) kwa kila Swalah, ndilo linalopendeza zaidi, ndio ukamilifu na ndio bora zaidi. Hii kama itathibiti kuwa ilikuwa kweli kwamba yeye alikuwa akikesha usiku kwa miaka arubaini mfululizo! Jambo hili linaelekea kuwa kama jambo lisilowezekana, nalo ni katika simulizi za kale zilizozushwa na washabiki wajinga wavukao mipaka waliosema hivyo kuhusu Abu Haniyfah na wengineo, na yote ni uongo mtupu".

[23] An-Nasaaiy, Ahmad na Atw-Twabaraaniy (1/187/2). At-Tirmidhiy amesema ni Swahiyh.

[24] An-Nasaaiy, Ibn Khuzaymah (1/70/1), Ahmad, Ibn Naswr na Al-Haakim ambaye amesema ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubaliana naye.

[25] Ahmad na Al-Bukhaariy.

Share