Kumbikumbi Wanafaa Kuliwa?

 

SWALI:

 

assalam alaykum warahmatullah wabarakatuh, amma baada. kuna itilafu nyingi zijadiliwazo kuhusu ulaji wa KUMBIKUMBI, JE, inaswihi kula kumbikumbi kisheria?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kumbikumbi ni jamii ya wadudu warukao ambao hupatikana katika baadhi ya maeneo na katika baadhi ya misimu, na hujulikana kwa majina tofauti baina ya eneo na eneo.

 

Kwa kuwa jina la Kumbikumbi halipatikani katika lugha ya kiarabu imekuwa vigumu kueleweka hukmu ya kuliwa kwa mdudu huyo, na kwa msingi huo watu wamegawanyika katika makundi mawili wanaohalalisha na wanaoharamisha; wanaohalalisha kuliwa wanategemea vigezo vifuatavyo:

1.      Wanadai kuwa kumbikumbi ni jamii ya Nzige, kwa kuwa nzige amehalalishwa kuliwa, basi na kumbikumbi naye ni halali kuliwa na wakatoa dalili kuwa Mtume katika hadiyth iliyopokewa na Ibn 'Umar Amesema:

 

“Tumehalalishiwa maiti mbili, na damu mbili, Samaki na Nzige, na Ini na Bandama” An-Nawawiy

 

2.      Aidha wanatoa hoja nyingine kuwa Ibn 'Abbaas  Amesema:

 

Walikuwa watu wa Jaahilyyah wanakula baadhi ya vitu na kuacha baadhi ya vitu kwa kuona kinyaa, Allaah Akamtuma Mtume Wake na Akateremsha Kitabu chake, akahalalisha vya halali na kuharamisha vya haramu  alivyohalalisha ndio halaal, na alivyoharamisha ndio haraam, na alivyo vinyamazia ndio vilivyosamehewa ” Kisha akasoma maneno ya Allaah:

 

“Sema sioni katika yale niliyofuniliwa mimi (niliyoletewa wahyi, sioni) kitu kilichoharamishwa kwa mlaji kikila isipokuwa kiwe ni mzoga au damu inayomwagika au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu; au kile ambacho kwa kukhalifiwa amri ya Allaah kimechinjwa kwa jina la asiyekuwa Allaah…” 6:145

 

Kwa hoja hizo mbili kundi hili linaona kula kumbikumbi ni Halaal, kwani ni jamii ya Nzige ambao ni halali kuliwa kwa mujibu wa kauli ya Mtume, na maelezo ya Ibn 'Abbaas kuwa kilichonyamaziwa na Allaah ni ruhusa kuliwa.

 

Ama wale wanaoharamisha kuliwa kwa kumbikumbi wao wanasema:

 

Uislamu una sheria yake katika mas-ala ya chakula. Chakula cha Muislamu kina masharti na hawezi mmoja wetu kula anachotaka bila kurudi katika maandiko.

 

 

Uislamu umekataza kuliwa nyamafu, hata hivyo ukaruhusu kuliwa kwa samaki na nzige hata wakiwa wamepatikana wakiwa tayari wamekufa. Hayo yanaeleweka na kila mmoja wetu, hata yule Muislamu wa kawaida.

 

 

Shaykh al-Amiyn bin 'Aliy, katika kitabu chake Majina ya Nyama kwa Kiswahili na Kiarabu, ametupatia faida kwa nyama zilizo halali na haramu na akatupatia baadhi ya faida. Miongoni mwa faida ni yafuatayo:

"Nyama waliwawo hawawi halali ila baada ya kutindwa tindo (kuchinjwa chinjo) la sharia, ila nzige na waishio baharini, kama samaki, papa na wengineo, hawa hawaihitajii kutindwa (kuchinjwa)". 

 

Hitimisho 

Ni vema kwa Muislamu akajiepusha na mambo yasiokuwa na ushahidi ndani yake, au yenye shaka ili kubakia salam Kula kumbikumbi ni jambo ambalo halina kishiko ndani ya sheria za Kiislamu, ni vema kwa Muislamu kujiepusha na kuwala wadudu hao, hususan watu huwala kwa matamanio tu  na siyo kama chakula cha msingi. Na kujiepusha na mambo yaliyo na shaka ndivyo tulivyoamrishwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam):

 

Kutoka kwa  Abu 'Abdullaah An-Nu’uman bin Bashiyr (Radhiya Allaahu ‘anhu)  ambaye alisema: Nilimsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam)  akisema:  ((Halali iko wazi na haramu iko wazi, baina yao ni vitu vyenye shaka ambavyo watu wengi hawajui.  Kwa hivyo, yule anayeepuka vyenye shaka  anajisafisha nafsi yake kwenye dini yake na heshima yake, lakini yule anayetumbukia katika mambo yenye shaka, huanguka katika haramu, kama mchunga anayechunga pembezoni mwa mpaka, mara  huingia ndani (ya shamba la mtu).  Hakika kila mfalme ana mipaka yake, na mipaka ya Allaah ni makatazo Yake…)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kwa kumalizia, tukija katika suala hili la kumbikumbi tutakuta kuwa haikutajwa katika Qur-aan wala Sunnah kuwa ni halali. Kwa kutotajwa kuwa ni hivyo, wadudu hao wanakuwa ni haramu kwa kanuni tulizozitaja hapo juu. Na hasa kuwa mnyama mpaka achinjwe ndio awe halali isipokuwa waliotajwa kama samaki na nzige, na kumbikumbi hawamo katika hao. Hivyo, wanakuwa ni haramu kwetu kuwala. 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share