Kupandishwa Nabiy 'Iysaa (عَلَيْهِ السَّلام) Mbinguni Na Atarudi Duniani Kama Alama Kubwa Za Qiyaamah

SWALI:

MPAKA SASA SIJAPATA UKWELI KUHUSU KIFO CHAKE,KWANI NINACHOJUA MIMI KILA NAFSI ITAONJA UMAUTI.NINASHUKURU KWA MAJIBU MAZURI YA SWALI

LILILO PITA.Ahsanteni saana

 


 

JIBU:

AlhamduliLLaah - Sifa njema zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kupandishwa Nabii 'Iysaa ('alayhis-salaam) mbinguni ni jambo ambalo limewatia shaka watu wengi. Na wengi waliotia shaka hawakubaliani na mafunzo ya 'Aqiydah sahihi yanayopatikana dalili zake katika Qur-aan na Sunnah. Hivyo imewafikisha kukufuru kwani ni kama kukanusha maneno ya  Allaah سبحانه وتعالى .

 

Na sababu kubwa ya kuwafanya hadi wafikie katika hali hiyo ni kutokana na kupenda kujadiliana sana mambo ya Allaah سبحانه وتعالى  kwa kuyatilia shaka na kugeuza usemi huu na ule kutokana na fikra zao wakati tumeamrishwa kuwa tusiwe tunauliza sana mambo mengine ambayo Mwenyewe Allaah سبحانه وتعالى Ameyakidhia kwa Hikma Yake na ambayo Hayakuyaelezea zaidi bali tunatakiwa tuyapokee na kuyaamini kama yalivyotujia katika Qur-aan na Sunnah.

Anasema Allaah سبحانه وتعالى:

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ تَسْأَلُواْ عَنْ أَشْيَاء إِن تُبْدَ لَكُمْ تَسُؤْكُمْ وَإِن تَسْأَلُواْ عَنْهَا حِينَ يُنَزَّلُ الْقُرْآنُ تُبْدَ لَكُمْ عَفَا اللّهُ عَنْهَا وَاللّهُ غَفُورٌ حَلِيمٌ))     ((قَدْ سَأَلَهَا قَوْمٌ مِّن قَبْلِكُمْ ثُمَّ أَصْبَحُواْ بِهَا كَافِرِينَ))  

 

((Enyi mlioamini! Msiulize mambo ambayo mkidhihirishiwa yatakuchukizeni. Na mkiyauliza inapoteremshwa Qur-aan mtabainishiwa. Allaah Amesamehe hayo. Na Allaah ni Mwenye maghfira Mpole))  ((Waliyauliza hayo watu wa kabla yenu, kisha wakawa wenye kuyakataa)) [Al-Maaidah: 101-102]

 

Ukweli ni kuwa Nabii ‘Iysa ('alayhis-salaam) aliishi kwa muda katika hii ardhi, kisha akapandishwa mbinguni kisha atarudishwa na Allaah سبحانه وتعالى  katika mwisho wa zama ili kutekeleza mambo fulani kama Anavyotaka Muumba Mwenyewe. Baada ya umri wake kumalizika atakaporudi, atakufa na kufufuliwa kama watu wengine.

Na kufanya hivyo Allaah سبحانه وتعالى  Anatuonyesha tena uwezo na nguvu Zake ya kuwa Anaweza kufanya chochote Anapokiamrisha kiwe basi huwa.  Anafanya Anavyotaka wala Yeye Haulizwi. Na kuwa katika Itikadi yetu kama Waislamu ni kwamba Allaah سبحانه وتعالى  ni Muweza wa kufanya Alitakalo. Kuweko 'Iysaa ('alayhis-salaam) mbinguni ni kutuonyesha miujiza Yake na uwezo Wake na kwetu ni mtihani mkubwa sana kwani tusipoamini tutakuwa na hasara hapa ulimwenguni na Kesho Akhera.

 

DALILI KUTOKA KATIKA QUR-AAN  

((إِذْ قَالَ اللّهُ يَا عِيسَى إِنِّي مُتَوَفِّيكَ وَرَافِعُكَ إِلَيَّ وَمُطَهِّرُكَ مِنَ الَّذِينَ كَفَرُواْ وَجَاعِلُ الَّذِينَ اتَّبَعُوكَ فَوْقَ الَّذِينَ كَفَرُواْ إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأَحْكُمُ بَيْنَكُمْ فِيمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ))

((Pale Allaah Aliposema: Ewe 'Iysaa! Mimi Nitakufisha, na nitakunyanyua Kwangu, na Nitakutakasa na wale waliokufuru, na Nitawaweka wale waliokufuata juu ya wale waliokufuru, mpaka Siku ya Qiyaamah. Kisha marejeo yenu yatakuwa Kwangu, Nikuhukumuni katika yale mliyokuwa mkikhitalifiana)) [Al-'Imraan:55]

 

((وَقَوْلِهِمْ إِنَّا قَتَلْنَا الْمَسِيحَ عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ رَسُولَ اللّهِ وَمَا قَتَلُوهُ وَمَا صَلَبُوهُ وَلَكِن شُبِّهَ لَهُمْ وَإِنَّ الَّذِينَ اخْتَلَفُواْ فِيهِ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ مَا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ إِلاَّ اتِّبَاعَ الظَّنِّ وَمَا قَتَلُوهُ يَقِينًا))   ((بَل رَّفَعَهُ اللّهُ إِلَيْهِ وَكَانَ اللّهُ عَزِيزًا حَكِيمًا))   ((وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلاَّ لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا))  

((Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuua Masihi 'Iysaa, mwana wa Maryam, Mtume wa Allaah-nao hawakumuua wala hawakumsulubu, bali walifananishiwa tu. Na hakika waliokhitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana ujuzi nayo wowote, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuua kwa yakini)) ((Bali Allaah Alimtukuza kwake, na hakika Allaah ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima)) ((Na hawi katika Watu wa Kitabu ila hakika atamuamini yeye kabla ya kufa kwake. Naye Siku ya Qiyaamah atakuwa shahidi juu yao)) [An-Nisaa:157-159]

 

DALILI KUTOKA KATIKA SUNNAH

Hadiyth ya kwanza:

عن أبي هريرة  رضي الله عنه  قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((والذي نفسي بيده لَيُوشكَنّ أن ينزل فيكم ابن مريم حَكَمًا عدلا فيكسر الصليب، ويقتل الخنزير، ويضع الجزية، ويفيض المال حتى لا يقبله أحد، حتى تكون السجدة خيرا من الدنيا وما فيها))  ثم يقول أبو هريرة: اقرؤوا إن شئتم: (( وَإِنْ مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا))   ألبخاري

Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko Mikononi Mwake, hivi karibuni atateremka kwenu mwana wa Maryam ('Iysaa) akiwa ni kiongozi muadilifu na atavunja misalaba, na kuua nguruwe, na ataondosha Jizya (ushuru kutoka kwa wasio Waislamu ambao wamo katika himaya ya serikali ya Waislamu). Kisha kutakuwa na mali nyingi hadi itafikia kuwa hakuna mtu wa kupokea sadaka. Wakati huu sajda moja itakuwa ni bora kwao kuliko maisha haya na yote yaliyomo (katika dunia))), kisha akasema Abu Hurayrah "Someni mkipenda ((Na hawi katika Watu wa Kitabu ila hakika atamuamini yeye kabla ya kufa kwake. Naye Siku ya Qiyaamah atakuwa shahidi juu yao )) [Al-Bukhaariy]

 

Hadiyth ya pili:

عن أبي هريرة؛ أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: (( لَيُهِلَّن عيسى ابن مريم بفَجِّ الرَّوْحَاء بالحج أو العمرة أو ليثنينهما جميعًا))  أحمد

Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: (('Iysaa atasema Ihlaal [Talbiya – kusema kwa sauti anapoingia mtu katika Ihraam] kwa ajili ya Hajj au 'Umrah au kwa zote mbili,  kutoka mlima ulioko njia kuu ya Ar-Rawhaa [njia baina ya Makkah na Madiynah])) [Ahmad]

 

Hadiyth ya tatu:

عن أبي هريرة قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((ينزل عيسى ابن مريم فيقتل الخنزير، ويمحو الصليب، وتجمع له الصلاة، ويعطي المال حتى لا يقبل، ويضع الخراج، وينزل الروحاء فيحج منها أو يعتمر أو يجمعهما))  قال: وتلا أبو هريرة: (( وَإِنْ مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ   وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ شَهِيدً  ((أحمد

Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: (('Iysaa mwana wa Maryam atateremka na ataua nguruwe, atavunja misalaba, ataimamisha (ataswalisha) Swalah ya Jamaa na atatoa mali hadi sadaka haitapokelewa na mtu. Ataondosha Jizya na atakawenda Ar-Rahaa ambako atakwenda kufanya Hajj, 'Umrah au zote mbili)) Kisha Abu Harayrah akasoma ((Na hawi katika Watu wa Kitabu ila hakika atamuamini yeye kabla ya kufa kwake. Naye Siku ya Qiyaamah atakuwa shahidi juu yao) [Ahmad]

 

Hadiyth ya nne

 عن أبي هريرة قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: (("كيف أنتم إذا نزل فيكم المسيح ابن مريم، وإمامكم منكم؟)) البخاري

Imetoka kwa Abu Hurayra  رضي الله عنه Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Mtakuaje atakapoteremka Al-Masiyh, mwana wa Maryam na atakapokuwa ni Imaam miongoni mwenu?)) [Al-Bukhaariy]  

 

Hadiyth ya tano

  عن أبي هريرة؛ أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((الأنبياء إخوة لِعَلات أمهاتهم شتى ودينهم واحد، وإني أولى الناس بعيسى ابن مريم؛ لأنه لم يكن بيني وبينه نبي، وإنه نازل، فإذا رأيتموه فاعرفوه: رجل مربوع إلى الحمرة والبياض، عليه ثوبان مُمَصّرَان، كأن رأسه يقطر وإن لم يصبه بَلَل، فيدق الصليب، ويقتل الخنزير، ويضع الجزية، ويدعو الناس إلى الإسلام، ويهلك الله في زمانه الملل كلها إلا الإسلام،  ويهلك الله في زمانه المسيح الدجال، ثم تقع الأمنة على الأرض، حتى ترتع الأسود مع الإبل، والنّمار مع البقر، والذئاب مع الغنم، ويلعب الصبيان بالحيات لا تضرهم، فيمكث أربعين سنة، ثم يُتَوَفى ويصلي عليه المسلمون))    أحمد أبو داود

Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Mitume ni ndugu katika sehemu, mama zao ni tofauti lakini dini yao ni moja. Mimi nina haki zaidi kwa 'Iysaa  mwana wa Maryam kuliko mtu yeyote kwa sababu hakukuwa na Mtume baina yake na yangu. Atateremka, na mtakapomuona mtamtambua: Ni mwenye mwili uliojengeka, (rangi ya ngozi yake) ni baina ya nyekundu ya nyeupe. Atateremka akiwa amevaa nguo mbili ndefu za rangi ya manjano khafifu. Kichwa chake kitakuwa kinachuruzika maji, japokuwa hakikuguswa na umande. Atavunja misalaba, ataua nguruwe na ataondosha Jizya na atawaita watu katika Uislamu. Katika muda atakaokuwepo, Allaah Ataziangamiza dini zote isipokuwa Uislamu. Na Allaah Atamuangamiza Masiyhid-Dajjaal (Masihi Muongo). Usalama utajaa ardhini hadi kwamba simba watachanganyika pamoja na ngamia, chui na ng'ombe na mbwa mwitu na kondoo. Watoto watacheza na nyoka bila ya kuwadhuru. 'Iysaa atabakia miaka arubaini kisha atakufa, na Waislamu watamswalia Swalah ya Janaazah)) [Ahmad na Abu Daawuud] .

 

Hadiyth ya sita:

عن أبي هريرة؛ أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((لا تقوم الساعة حتى ينزل الروم بالأعماق -أو بدابق-فيخرج إليهم جيش من المدينة من خيار أهل الأرض يومئذ، فإذا تصافّوا قال الروم: خلوا بيننا وبين الذين سَبَوا منا نقاتلهم. فيقول المسلمون: لا والله لا نخلي بينكم وبين إخواننا. فيقاتلونهم، فينهزم ثلث لا يتوب الله عليهم أبدًا، ويُقْتَلُ ثلثه أفضل الشهداء عند الله  عز وجل  ويفتح الثلث لا يفتنون أبدا فيفتتحون قسطنطينية، فبينما هم يقسمون الغنائم قد عَلَّقوا سيوفهم بالزيتون، إذْ صاح فيهم الشيطان: إن المسيح قد خلفكم في أهليكم. فيخرجون، وذلك باطل. فإذا جاؤوا الشام خرج، فبينما هم يُعدّون للقتال: يسوون الصفوف، إذ أقيمت الصلاة، فينزل عيسى ابن مريم فأمَّهم فإذا رآه عدوّ الله ذاب كما يذوب الملح في الماء، فلو تركه لانذاب حتى يهلك ولكن يقتله الله بيده، فيريهم دمه في حَرْبته))   مسلم

Kutoka kwa Abu Hurayrah  رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Qiyaamah hakitasimama hadi Warumi watakapomiliki Al-A'maaq au  Daabiq. Jeshi kutoka Madiynah litakuwa lenye watu bora kabisa katika ardhi. Watakapokutana uso kwa uso, Warumi watasema: "Tupigane na wale waliotuteka baadhi yetu". Waislamu watasema: "Hapana! Wa-Allaahi hatutawaachilia nyinyi muwateke ndugu zetu". Watapigana nao. Thuluthi ya jeshi la Waislamu litakimbia kwa sababu ya kushindwa, nao ni ambao Allaah Hatawasamehe. Thuluthi nyingine watauliwa, nao ni mashahidi bora kabisa. Thuluthi ya mwisho watakuwa ni washindi na hawa ndio hawatofitinika abadan na wataiteka Constantinople (Istanbul). Watakapokuwa wanagawa ngawira baada ya kutundika mapanga yao juu ya miti ya zaituni, shaytwaan  atapiga kelele baina yao na atasema: 'Al-Masihid-Dajjal yuko pembeni ya watu wenu". Wataondoka kukutana na Ad-Dajjal Shaam. Huu utakuwa ni wito wa udangayifu na watakapofika Shaam Ad-Dajjaal atatokea. Waislamu watakapokuwa wanasawazisha safu zao za vita na Swalah itakapoadhiniwa, 'Iysaa mtoto wa Maryam atateremka na kuwaimamisha Swalah. Adui wa Allaah atakapomuona, (Masihi muongo) atayeyuka kama chumvi inavyoyayuka katika maji na ikiwa bado atabakia ataendelea kuyeyuka mpaka atakufa. Allaah Atamuua kwa mkono wa 'Iysaa na atawaonyesha Waislamu damu yake katika mshale wake)) [Muslim]

 

Hadiyth ya saba (mji atakaoteremka)

حديث النواس بن سمعان : (( فَيَنْزِلُ عِنْدَ الْمَنَارَةِ الْبَيْضَاءِ شَرْقِيَّ دِمَشْقَ بَيْنَ مَهْرُودَتَيْنِ وَاضِعًا كَفَّيْهِ عَلَى أَجْنِحَةِ مَلَكَيْنِ، إِذَا طَأْطَأَ رَأْسَهُ قَطَرَ، وَإِذَا رَفَعهُ تَحَدَّرَ مِنْهُ مِثْلُ جُمَانِ اللُّؤْلُؤ، لَا يَحِلُّ لِكَافِرٍ يَجِدُ رِيحَ نَفَسِهِ إِلَّا مَاتَ، وَنَفَسُهُ يَنْتَهِي حَيْثُ يَنْتَهِي طَرَفُه))  مسلم

Hadiyth kutoka kwa An-Nawaas bin Sam'aan ((Atateremka karibu ya mnara mweupe Mashariki ya Damscus. Atavaa nguo mbili zenye rangi ya zaafarani (manjano) khafifu, mikono yake ikiwa katika mbawa mbili za Malaika wawili. Kila atakapoinamisha kichwa chake, matone ya maji yatamdondoka. Kila atakapoinua kichwa chake, mapambo ya thamani yatamuanguka. Hakuna kafiri atakayesalimika na pumzi za 'Iysaa, na pumzi zake zitafika umbali wa upeo wa macho yake)) [Muslim]

 

Maelezo kuhusu kupandishwa kwake:

Ibn Haatim amesimulia kwamba  Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما  amesema: "Kabla ya Allaah Kumpandisha 'Iysaa mbinguni, 'Iysaa alikwenda kwa Maswahaba zake kumi na mbili katika nyumba. Alipofika, nywele zake zilikuwa zikichuruzika maji akasema:"Kuna miongoni mwenu ambao watanikufuru mara kumi na mbili baada ya kuniamini". Kisha atasema: "Nani atakayejitolea abadilishwe umbo lake liwe kama langu ili auliwe badala yangu na atakuwa pamoja na mimi Peponi?" Mmoja wao aliye mdogo kuliko wote alijitolea lakini 'Iysaa akamuambia akae chini. Kisha 'Iysaa akauliza tena atakayejitolea na kila mara ilikuwa ni huyo huyo kijana mdogo aliyejitolea lakini 'Iysaa akamuambia akae chini. Kisha tena kijana huyo akajitolea tena na mwisho 'Iysaa akasema : "wewe utakuwa ni huyo mtu". Akafananishwa na 'Iysaa na 'Iysaa akapandishwa mbinguni akipaa juu katika uwazi  (uliofunuka juu ya sakafu ya nyumba). Mayahudi walipokuja kumtafuta 'Iysaa wakamuona huyo kijana (wakidhani kuwa ni 'Iysaa) wakamuua (kwa kumsulubu) Baadhi ya maswahaba wakamkufuru mara kumi na mbili baada ya kumuamini. Kisha wakajigawa katika makundi matatu. Kundi la mwanzo Al-Ya'aqubiyyah (Jacobites) wamesema: "Allah Amebakia na sisi Alivyojaalia kisha akapanda juu". Kundi la pili An-Nasturiyyah (Nestorians) wamesema: 'Mtoto wa Mungu alikuwa na sisi alivyojaaliwa kisha Allaah Akampandisha mbinguni. Kundi la tatu Waislamu wakasema: "Mja na Mjumbe wa Allaah amebakia na sisi Alivyomjaalia Allaah, kisha Allaah Akamchukua Kwake". Makundi mawili yaliyokufuru wakaungana dhidi ya Waislamu na wakawua. Tokea ilivyotokea hivyo, Uislamu ukafunikwa, hadi Allaah Alipomleta Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم " [Usimulizi huu una isnaad sahihi inayofikia hadi kwa 'Ibn 'Abbas na An-Nasaiy amesimulia kutoka kwa Abu Kurayb ambaye amepokea kutoka kwa Abu Mu'aawiya – Ibnu Kathiyr: 3-28-29]    

Baada ya kupata maelezo yote hayo, Muislamu inampasa ayaamini maneno ya Allaah سبحانه وتعالى na Mtume Wake صلى الله عليه وآله وسلم kuhusu kupandishwa Nabii 'Iysaa ('alayhis-salaam) na ajitoe na shaka yoyote nyingine ili aokoke na upotofu uliowapoteza wengi.

Na kama inawashangaza wengi kupandishwa kwake na baadhi yao wenye kutumia akili zao juu ya dini badala ya kufuata Qur-aan na Sunnah, wanapaswa wakumbuke kuwa kwa Allaah سبحانه وتعالى hilo si kubwa, kama Alivyomleta duniani kwa kuzaliwa na mama yake bila kuingiliwa na mwanamume,

((إِذْ قَالَتِ الْمَلآئِكَةُ يَا مَرْيَمُ إِنَّ اللّهَ يُبَشِّرُكِ بِكَلِمَةٍ مِّنْهُ اسْمُهُ الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ وَجِيهًا فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ وَمِنَ الْمُقَرَّبِينَ))    )) وَيُكَلِّمُ النَّاسَ فِي الْمَهْدِ وَكَهْلاً وَمِنَ الصَّالِحِينَ))   (( قَالَتْ رَبِّ أَنَّى يَكُونُ لِي وَلَدٌ وَلَمْ يَمْسَسْنِي بَشَرٌ قَالَ كَذَلِكِ اللّهُ يَخْلُقُ مَا يَشَاء إِذَا قَضَى أَمْرًا فَإِنَّمَا يَقُولُ لَهُ كُن فَيَكُونُ((  

 

((Na pale Malaika walipo sema: Ewe Maryam! Hakika Allaah Anakubashiria (mwana) kwa neno litokalo kwake. Jina lake Masihi 'Iysaa mwana wa Maryam, mwenye hishima katika dunia na Akhera, na miongoni mwa waliokaribishwa (kwa Allaah)))  ((Naye atazungumza na watu katika utoto wake na katika utuuzima wake, na atakuwa katika watu wema))   ((Maryam akasema: Mola wangu Mlezi! Vipi nitampata mwana na hali hajanigusa mwanaadamu? Allaah Akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Allaah Huumba Apendacho. Anapohukumu jambo, Huliambia: Kuwa! Likaw)) ni[Al-'Imraan: 45-47] 

 

Na pia kupewa uwezo mbali mbali wa kufanya mambo ya ajabu  kama Anavyoyaelezea Allaah سبحانه وتعالى katika Aayah ifuatayo:

((وَرَسُولاً إِلَى بَنِي إِسْرَائِيلَ أَنِّي قَدْ جِئْتُكُم بِآيَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ أَنِّي أَخْلُقُ لَكُم مِّنَ الطِّينِ كَهَيْئَةِ الطَّيْرِ فَأَنفُخُ فِيهِ فَيَكُونُ طَيْرًا بِإِذْنِ اللّهِ وَأُبْرِىءُ الأكْمَهَ والأَبْرَصَ وَأُحْيِي الْمَوْتَى بِإِذْنِ اللّهِ وَأُنَبِّئُكُم بِمَا تَأْكُلُونَ وَمَا تَدَّخِرُونَ فِي بُيُوتِكُمْ إِنَّ فِي ذَلِكَ لآيَةً لَّكُمْ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ))

 

((Na ni Mtume kwa Wana wa Israili kuwaambia: Mimi nimekujieni na Ishara kutoka kwa Mola Mlezi wenu, ya kwamba nakuundieni kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Allaah. Na ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti kwa idhini ya Allaah, na ninakwambieni mnacho kila na mnacho weka akiba katika nyumba zenu. Hakika katika haya ipo Ishara kwenu ikiwi nyinyi ni wenye kuamini) [Al-'Imraan: 49]

Kwa hiyo vile vile kufanya asife na kupaishwa juu hilo pia kwa Allaah سبحانه وتعالى sio kubwa! 

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share