Daku: Nilikuwa Na Maji Kinywani Nikashtukizia Adhaana Ya Pili Ya Alfajiri Nikayameza Nini Hukmu?

SWALI : 

Asalaam alaykum.

Napenda kuuliza suala langu kuhusu Ramadhan "Nimeamka usiku na kula daku mapema, lakini nikaamka usiku na kuendelea na ibada, nilipokuwa nikiendelea na ibada, mara kiu ikanishika na nikanywa maji, lakini kwa bahati nikasikia adhana ya pili ya sala ya alfajiri, wakati huu, yale maji nusu yamekwenda na nusu yamo mdomoni, nikaendelea kuyanywa yale yaliyo mdomoni wakati huu adhana hiyo ya pili inaendelea kusomwa. JEE HUKUMU YANGU NINI KUHUSU USAHIHI WA FUNGA YANGU 

 


 JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“…Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku...” Al-Baqarah: 187

Ni waajib kwa mwenye kufunga ajizuie kula au kunywa pale panapoingia Alfajiri ya kweli, kwa hali ya leo hii wengi wanajua alfajiri ya kweli kwa sauti ya Adhaan ya pili japo hiyo inaweza isiwe ni kipimo sahihi mia kwa mia kwani Misikiti mingi huadhiniwa kwa kutazamwa saa na si kwa kutazamwa weupe wa alfajiri ya kweli kama ushadhihirika au la.

Swawm yako inaweza kuwa ni sahihi kutokana na kutokujua kwako hukumu ya jambo hilo.

Hadiyth ifuatayo inatuonyesha kuwa mtu anaruhusiwa kumaliza tonge au chakula chake alichoonza kula wakati Adhaan inapoadhiniwa:

Imesimuliwa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Atakaposikia mmoja wenu Adhaan na hali ana chombo cha chakula mkononi mwake, asikishushe chini hadi amalize kilichomo” [Ahmad, Abu Daawuud, na Shaykh Al-Albaaniy kaitaja katika Swahiyh ya Abu Daawuud].

Hata hivyo, Hadiyth hii isichukuliwe moja kwa moja kuwa mtu anaweza kuendelea kula na hali ishaingia Alfajiri ya kweli. Kwani kuna makatazo ya wazi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

“Msisimamishe daku yenu mnaposikia Adhaan ya Bilaal, kwani yeye anaadhini usiku, kwa hiyo kuleni na kunyweni mpaka Ibn Umm Maktuum aadhini.” Al-Bukhaariy

Kwa hali yako muulizaji, ni bora uwe makini kutokula tena baada ya Adhaan ya pili ambayo huwa ndio kipimo cha Alfajiri ya kweli, na kwa sababu ulikuwa hujui hukumu hapo mwanzo, basi tunataraji Swawm yako itakuwa sahihi inshaAllaah.

Lakini ni vizuri Muislamu kuchukua tahadhari ya kujua muda gani khaswa Adhaan ya kwanza na muda gani ni Adhaan ya pili ili asalimike na matukio kama haya. Hakika ni dakika chache tu mtu unaweza kujiweka katika usalama wa kula daku

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Daku Baada Ya Kusikia Adhaan

Wakati Wa Mwisho Wa Kula Daku

Ufafanuzi Wa Wakati Wa Mwisho Wa Kula Daku

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

Share