Jimai: Ameota Yuko Na Mke Wake Akatokwa Na Madhii Katika Ramadhwaan Nini Hukmu Yake?

SWALI:

 

asalam alaikum

swali langu ni kwamba mimi nilivo kuwa kitandani usubuhi nikawa namfikiria

demu wangu mpaka nikatokwa na manii aina ya maji ila mazito ila sio manii

ya kawaida nai yale ya kutamani je nimefungua na hukmu yake ninini na timeile nilikuwa macho.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunashukuru kwa swali lako hilo la kusikitisha.


Tunakunasihi utumie Lugha nzuri ya heshima unapouliza maswali, hii ni tovuti ya dini na si kijiwe cha kupiga soga za kidunia na mambo machafu.


 
Ama kuhusu swali lako, inadhihirika kwanza wazi kuwa una rafiki wa kike (Girl Friend) na hiyo ni hatari kubwa kwa Muislam. Uislam umeharamisha mahusiano yoyote yasiyo ya kisheria baina ya jinsia mbili hadi watu watakapooana. Unayofanya ni mambo ya haraam na unapaswa uyaache haraka sana ikiwa wewe ni Muislam na unamuogopa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na siku ya mwisho.
 
Allaah (Subhanaahu wa T'ala) Amekataza japo kuikaribia zinaa, Aliposema:
 

 

(( وَلاَ تَقْرَبُواْ الزِّنَى إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاء سَبِيلاً))

((Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya)) [Israa : 3]

 


Na vile vile tambua kuwa mahusiano hayo hayaruhusiwi si mwezi wa Ramadhaan tu, bali hata miezi mingine yote iliyobaki. Na adhabu ya mzinifu ni kali sana hapa duniani na huko Akhera ikiwa hajafanya Tawbah ya kweli.

Adhabu za Zinaa katika sheria ya Kiislamu ni kali mno na lau kama zingelifuatwa basi kusingelikuweko na maasi haya. Adhabu ni kama zifuatavyo:

 

Mzinzi ambaye hajaoa au kuolewa anafaa apigwe mijeledi mia moja hadharani kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

((الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا مِئَةَ جَلْدَةٍ وَلَا تَأْخُذْكُم بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّهِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَلْيَشْهَدْ عَذَابَهُمَا طَائِفَةٌ مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ))

((Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Allaah, ikiwa nyinyi mnamuamini Allaah na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini)) [An-Nuur: 2]

 

Na ikiwa ameoa au ameolewa basi wapigwe mawe hadi kufa kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:

فِي الصَّحِيحَيْنِ مِنْ رِوَايَة الزُّهْرِيّ عَنْ عُبَيْد اللَّه بْن عَبْد اللَّه بْن عُتْبَة بْن مَسْعُود عَنْ أَبِي هُرَيْرَة وَزَيْد بْن خَالِد الْجُهَنِيّ فِي الْأَعْرَابِيَّيْنِ اللَّذَيْنِ أَتَيَا رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ أَحَدهمَا : يَا رَسُول اللَّه إِنَّ اِبْنِي هَذَا كَانَ عَسِيفًا - يَعْنِي أَجِيرًا - عَلَى هَذَا فَزَنَى بِامْرَأَتِهِ فَافْتَدَيْت اِبْنِي مِنْهُ بِمِائَةِ شَاة وَوَلِيدَة فَسَأَلْت أَهْل الْعِلْم فَأَخْبَرُونِي أَنَّ عَلَى اِبْنِي جَلْد مِائَة وَتَغْرِيب عَام وَأَنَّ عَلَى اِمْرَأَة هَذَا : الرَّجْم فَقَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ :  ((وَاَلَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَأَقْضِيَنَّ بَيْنكُمَا بِكِتَابِ اللَّه تَعَالَى الْوَلِيدَة وَالْغَنَم رَدّ عَلَيْك وَعَلَى اِبْنك مِائَة جَلْدَة وَتَغْرِيب عَام . وَاغْدُ يَا أُنَيْس - لِرَجُلٍ مِنْ أَسْلَم - إِلَى اِمْرَأَة هَذَا فَإِنْ اِعْتَرَفَتْ فَارْجُمْهَا))  فَغَدَا عَلَيْهَا فَاعْتَرَفَتْ فَرَجَمَهَا     البخاري و مسلم

 Katika Swahiyhayn kutoka kwa Abu Hurayrah na Zayd bin Khaalid Al-Juhaniy (Radhiya Allaahu 'anhum) katika kisa cha Mabedui wawili waliokuja kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Mmoja alisema: "Ewe Mjume wa Allaah, mwanangu (wa kiume) aliajiriwa na bwana huyu kisha akafanya zinaa na mke wake. Nimemlipa fidia kwa ajili ya mwanangu kwa kumpa kondoo mia moja na mtumwa mwanamke. Lakini nilipowauliza watu wenye elimu, wamesema kwamba mwanangu apigwe mijeledi mia na ahamishwe mji kwa muda wa mwaka na mke wa huyu bwana apigwe mawe hadi afariki".  Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, nitahukumu baina yenu wawili kutokana na Kitabu cha Allaah. Rudisha mtumwa mwanamke na kondoo  na mwanao apigwe bakora mia kisha mwanao ahamishwe mbali kwa muda wa mwaka. Nenda Ewe Unays!)) Alimwambia mtu katika kabila la Aslam, ((Nenda kwa mke wa huyu bwana na akikiri makosa yake, basi mpige mawe hadi mauti [yamfike])) Unays akamuendea na akakiri makosa yake, kwa hiyo akampiga mawe hadi mauti. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Pia tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo kuhusu Madhara ya Zinaa na Adhabu Zake

 

Nini Hukumu Ya Mwenye Kuzini Kwa Siri?

Kufanya Mapenzi Bila Ya Kitendo Cha Ndoa Kwa Ambaye Hajaolewa?

 

Kuwa kwako na mahusiano ya haraam kumekupelekea hadi kumuota huyo mwanamke kwenye ndoto zako katika mwezi huu mtukufu. Tunamuomba Allaah Akusamehe na Akuongoze, na fanya toba ya kikweli kweli. Tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho upate makala za Tawbah.

 
Tawbah


Ikiwa ushaacha mahusiano hayo ya haraam. Na ikiwa bado hujaacha mahusiano hayo ya haraam, basi hii ni fursa kubwa katika mwezi huu kuacha na kurudi kwa Mola wako Aliyekuumba na Akakupa pumzi na uhai na rizki na afya njema ambayo wewe hivi sasa unaitumia katika kumuudhi na kumuasi huyo Aliyekuruzuku vitu hivyo.


 
Ama kuhusu swali lako, ikiwa hayo yaliyotoka si manii halisi kama ulivyosema, basi yatakuwa ni Madhii ambayo ni majimaji mazito yanayotangulia kutoka na ambayo yanasababishwa na matamanio ya kimwili. Hukmu yake ni kuwa Swawm yako ni sahihi lakini unapaswa ukajioshe sehemu hiyo na ukaoshe sehemu iliyoingia Madhii hayo ili upate kuwa Twahara kwa ajili ya Swalah 


 
Na haifai kukaa kujiwazisha na kujifikirisha mambo machafu na maovu kama hayo ambayo msingi wake ni Haraam. Na hali hiyo inaharibu ujira wa Swawm yako na kujipotezea thawaab nyingi japo Swawm yako itakuwa ni sahihi.
 
Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share