Skip navigation.
Home kabah

Zingatio La Wiki - Kwa Wenye Akili

 

‘Abdun-Naaswir Hikmany

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amemuumba mwanaadamu ni mwenye matamanio na akili. Tofauti na Malaika ambao wamepewa akili bila ya matamanio au wanyama waliopewa matamanio bila ya akili. Na ndio maana Qur-aan haikuteremshwa kwa Malaika wala wanyama. Imeteremshwa kwa wanaadamu ambao wanazo akili za kufahamu ili kutekeleza matamanio yao kwenye njia sahihi.

Kwa hakika inakuwa ni vigumu kuelewa ya kwamba mwanasayansi anashindwa kuingia kwenye Uislamu kidhati kabisa. Kwani Qur-aan imejaa sayansi aina wa aina za kumuacha mdomo wazi huyo mwanasayansi. Na wala Hakukosea Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kuumba Moto kwa nafsi zisizotaka kutanabahi ukweli uliomo ndani ya Qur-aan ulio wazi kabisa.

Ni wajibu wa kila mwanaadamu kuutafuta ukweli wa kuumbwa kwake na lengo la kuwepo kwake hapa ulimwenguni. Hata Nabii Ibraahiym (‘Alayhi Swalaatu was-Salaam) aliangalia mwezi na jua akijaribu kuvuta fikra kwamba huwenda vitu hivi vikawa ni miungu yake, lakini hakufikia huko akamalizia kwa qawl ya:

{{Mimi nimuelekeza uso wangu kwa Yule Aliyeziumba mbingu na ardhi. Hali ya kuwa nimewacha dini za upotevu. Mimi (ni Muislamu) wala si miongoni mwa washirikina.}} [6:79]

Mara kadha wa kadhaa Aayah za Qur-aan zinamalizia na qawl za 'wenye akili', 'wenye kutanabahi', 'uongofu kwa wamchao' na kadhalika. Haingii akilini kuona kwamba Muislamu anayedai kuisadiki Qur-aan akimshirikisha Mola Mlezi. Na anapoambiwa hukaidi akiona kuwa ni haki yake kufanya mambo ya ushirikina.

{{Katika kuumbwa mbingu na ardhi na mfuatano wa usiku na mchana, ziko hoja kwa wenye akili. Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa na wakilala. Na huzingatia umbo la mbingu na ardhi (Wakasema:) "Mola wetu! Hukuviumba hivi bure. Utukufu ni Wako. Basi Tuepushe na adhabu ya Moto.}} [3:190-191]

Aayah namna hizo ziliposhushwa kwa kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) uso wake ulipiga wekundu na machozi yakaanza kumbubujika hadi ndevu zake zikaroana. Hiyo sio hali inayozikuta nafsi zetu kwa Mola wetu, nafsi ambazo zinazidi kurudi hatua nyuma badala ya kwenda mbele. Tunaenziwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na tukafunzwa na Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lakini bado hatuhitaji kutanabahi. Eeh nafsi… Wataka niambia kwamba moto ndio utakaokwenda kuwa ni gereza lako?

Basi elewa ewe nafsi kwamba wamekwenda kombo waliorukwa na akili mfano wa kuku, wakadonoa ulimwenguni vingi vizuri na mabaya wakazidi kuyatafuna, dunia kwao ilivamiwa kwa anasa za kila aina uijuayo na dhambi za fitna, wakapumbazika na kilevi hichi kibaya wasielewe usiku wala mchana,
kwao halali na haramu zilikuwa ni kauli za ajabu wakazidi kukana,
sasa wameshatangulia kaburini na waovu wengine wamepangana,
malipo ya utovu wa akili zao Ayajua Jalaali Rabbana.

Basi tunatamka na tunakuomba kama ulivyotufunza:

{{Mola wetu! Wale ambao Utawaingiza Motoni, basi itakuwa Umewadhalilisha na hawatakuwapo wasaidizi kwa ajili ya madhalimu.

Mola Wetu! Tumesikia mwitaji anayeita kwendea Uislamu kwamba: "Mwamini Mola wetu." Tukaamini.

Mola wetu! Tusamehe madhambi yetu na Utufutie makosa yetu na Utufishe pamoja na watu wema.

Mola wetu! Na Utupe uliyotuahidi kwa (ndimi za) Mitume Yako, wala Usitufedheheshe siku ya Kiama, bila shaka Wewe huvunji miadi.}} [3: 192-195]