Zingatio: Sio Kila Kitu Kinaonekana

 

Zingatio: Sio Kila Kitu Kinaonekana

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Dunia ni tamu na kawaida ya mwanaadamu kupenda mazuri mno. Hujitahidi kadiri ya juhudi zake kukusanya yale ayaonayo kuwa ni yenye kufurahisha nafsi yake. Hutafuta yale yenye laghai na anasa - 'material world'.

 

Hilo halina shaka na hata Qur-aan na Sunnah yatuthibitishia kwamba dunia imeumbwa kuunganishwa na matamanio ya mwanaadamu. Lakini sio yote ambayo Muislamu anatakiwa kuyatilia mkazo kwa kuyavamia. Ndio lengo la kuwepo halali na haramu ndani ya Uislamu ili kumtofautisha mwanaadamu na Muislamu.

 

Waislamu walio wengi kabisa wanatamka shahaadah ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni Mmoja na Ndiye Apaswaye kuabudiwa pamoja na kutiiwa Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kikomo cha wengi kinamalizia hapa kwenye kauli tu. Matendo yao yanakuwa kinyume na kauli hii. Hivyo, hufanya ibada kwa kudanganya macho ya waumini, kwani wanatenda mbele ya kadamnasi, wanapokuwa peke yao huingia kwenye hiyo 'material world' kwa mapana na marefu. Hiyo sio iymaan inayopigiwa mfano na Rabb Mlezi: 

الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُم بِالْغَيْبِ وَهُم مِّنَ السَّاعَةِ مُشْفِقُونَ ﴿٤٩﴾

Wale wanaomkhofu Rabb wao kwa ghayb nao wanaikhofu Saa. [Al-Anbiyaa: 49]

 

Taariykh yatufunza kwamba Waislamu hapo kale walilelewa kwenye Tawhiyd ya kumuamini Allaah pamoja na Malaika, Rusuli, Vitabu, Siku ya Mwisho, Qadar kheri na shari. Kwa wakati wa sasa ni Kitabu cha Qur-aan pekee ndicho kilicho mbele ya macho yetu. Vilivyobaki vyote vinabaki kuwa nyuma ya pazia 'ghayb'.

 

Imesimuliwa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘Anhu): amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba:

 

 

"Iymaan ni kumuamini Allaah, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake, na Kukutana Kwake (Siku ya Qiyaamah), na Rusuli Wake na kuamini ufufuo wa Siku ya Mwisho." [Imepokewa na Shaykhaan]

 

Kukosa kuamini moja ya nguzo za iymaan, kunapelekea kutoamini ghayb. Hivyo, kuanguka kwa iymaan ya ghayb kutasababisha kuondoka iymaan ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Yupo.

 

Ni ghayb hii inayomfanya mwanaadamu na hata Muislamu kutotilia mkazo kuutafuta ukweli halisi wa Uislamu, ghayb ndiko kunakomfanya Muislamu kutotenda mema kwa lengo la kupata ridhaa ya Allaah. Thawabu wala dhambi hazioni mtu, Malaika wanaoandika mema na maovu nani anayewaona? Haya yote yapo kwenye ghayb. Muislamu anatakiwa kuamini hii ghayb bila ya mjadala. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatuambia: 

 

وَقُلِ اعْمَلُوا فَسَيَرَى اللَّـهُ عَمَلَكُمْ وَرَسُولُهُ وَالْمُؤْمِنُونَ ۖ وَسَتُرَدُّونَ إِلَىٰ عَالِمِ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ﴿١٠٥﴾

Na sema: Fanyeni (mtakavyo). Allaah Ataona ‘amali zenu na Rasuli Wake na Waumini (pia wataona). Na mtarudishwa kwa Mjuzi wa ghayb na dhahiri; kisha Atakujulisheni kwa yale mliyokuwa mkiyatenda. [At-Tawbah: 105]

 

Apambanue Muislamu juu ya kukosa kwake iymaan ya ghayb na kuirudisha nyuma akili kabla ya kuwepo kwake; yeye alikuwa ni nani? Nani aliyemhifadhi ndani ya tumbo la mama kwa miezi tisa? Hivyo, ghayb ni wajibu kuiamini na kwamba yapo mambo nyuma ya macho yetu yanatokea au yapo tayari kutokea.

 

Kukosekana kwa iymaan ya ghayb ndani ya nafsi ya Muislamu ndio kwamfanya awache himma ya kutenda mema. Ni sababu hii inayowafanya vijana walio wengi kujishughulisha mno na ratiba za mipira inayokula muda wa Waislamu. Nao kina dada kutilia mkazo urembo, mikusanyiko ya haramu na kutembea kwao utupu kunatokana na kukosa kwao kuamini ghayb.

 

Basi na aangalie Muislamu alivyoumbwa, chakula chake kinavyoyayushwa na kugaiwa sehemu mbali mbali. Vitamini, damu, madini, sukari, chumvi, mafuta na vyengineo; vyote vinapelekwa na kuhifadhiwa sehemu zake maalum. Atupe jicho lakekwa kuangalia linapotoka na kuzama jua, tofauti ya usiku na mchana, hali ya uzima na ugonjwa, maisha na mauti na mengineyo:

 

وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ ۖ وَيَوْمَ يَقُولُ كُن فَيَكُونُ ۚ قَوْلُهُ الْحَقُّ ۚ وَلَهُ الْمُلْكُ يَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ ۚ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ ﴿٧٣﴾

Naye Ndiye Ambaye Ameumba mbingu na ardhi kwa haki. Na Siku Atakaposema: Kun! basi (jambo) huwa! Kauli Yake ni haki.  Naye Atakuwa na ufalme Siku itakapopulizwa baragumu. Mjuzi wa ghayb na dhahiri. Naye ni Mwenye hikmah wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [ Al-An’aam: 73]

 

Basi ni mengi yaliyopo Mkononi Mwako yaa Allaah! Namna tutakavyojifunza katu hatutafikia chembe ya 'ilmu Yako. Hivyo, tunatamka kama ambavyo Umetufunza:

 

وَإِذْ قَالَ اللَّـهُ يَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ أَأَنتَ قُلْتَ لِلنَّاسِ اتَّخِذُونِي وَأُمِّيَ إِلَـٰهَيْنِ مِن دُونِ اللَّـهِ ۖ قَالَ سُبْحَانَكَ مَا يَكُونُ لِي أَنْ أَقُولَ مَا لَيْسَ لِي بِحَقٍّ ۚ إِن كُنتُ قُلْتُهُ فَقَدْ عَلِمْتَهُ ۚ تَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِي وَلَا أَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِكَ ۚ إِنَّكَ أَنتَ عَلَّامُ الْغُيُوبِ ﴿١١٦﴾

Na pindi Allaah Atakaposema: Ee ‘Iysaa mwana wa Maryam!  Je, wewe uliwaambia watu: ‘Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni waabudiwa wawili badala ya Allaah? (‘Iysaa) Atasema: Utakasifu ni Wako hainipasi mimi kusema yasiyo kuwa haki kwangu; ikiwa nimesema hayo basi kwa yakini Ungeliyajua; Unayajua yale yote yaliyomo katika nafsi yangu; na wala mimi sijui yale yaliyomo katika Nafsi Yako; hakika Wewe ni Mjuzi wa ghayb. [Al-Maaidah: 116]

 

 

 

Share