Mume Hataki Nizae Kwa Vile Ana Watoto Wa Mke Wa Mwanzo Je Inafaa Nizuie Kuzaa?

SWALI:

Assalamu alaykum warahmatullah,

Kabla ya kuanza sina budi kumshukuru Muumba wa yote kwa kutujaalia uzima na afya na kukumbushana mambo tofauti yenye kheir nasi namuomba Allah Subhanaahu Wattaala akulipeni jaza njema.

Pia nimejaribu kutafuta sana hili suala kama mnavyotuarifu lakini nimepata tu baadhi ya majibu lakini lile hasa ninalolitaka bado sijalipata kwa hivyo inshaallah natarajia majibu mema.

Mume ana watoto wengi alozaa kwa mke mwengine lakini mimi ninae mmoja ambae sijazaa na yeye lakini kwa sasa hataki tena kuongeza watoto je ninaruhusiwa kuishi nae kwa kutumia njia za kuzuia kizazi mpaka itakapofikia khatima au nifanyeje?

Naomba majibu yenu inshaallah.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuzuia kizazi. Tufahamu kuwa lengo kubwa la ndoa miongoni mwa malengo mengine ni kupata kizazi. Uislamu umepiga marufuku kabisa kwa Waislamu kufunga kizazi kabisa kabisa ila kwa sababu za dharura kubwa inayokubalika kisheria na si hiyo uliyoitaja. Sababu kubwa inaweza kuwa ni kupata shida kwa mama wakati wa uzazi katika hali ya kuwa yuko baina ya uhai na mauti.

Haifai kwa Muislamu kufunga kizazi kwa ajili eti ana watoto wengi na hana njia ya kuwalisha au kuwavisha. Hata hivyo Uislamu umeruhusu kupanga uzazi na sio kufunga kabisa kama tulivyoelezea. Kupanga ni kwa njia za kisheria zinazokubalika na ambazo hazitamtia mwanamke katika madhara na maafa. Njia nyingi zinazotumika za kutumia kemikali zinakuwa na madhara hivyo Waislamu wanatakiwa wajiepushe nazo. Ikiwa ipo sababu ya kutaka kupanga kwa kuhofia afya ya mama kwa kuzaa kila mwaka inawezekana mume na mke wakazungumza kwa kushauriana na kuafikiana njia bora. Njia ambayo haina madhara kwa mama lau mume ataafiki ni kufanya ‘azl (kumwaga nje) kama walivyokuwa wakifanya Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum).

Haifai nyinyi kuzuia kizazi kwa sababu hiyo mpaka mtakapofikia khatima yake. Inabidi mkae chini na mumeo mlizungumzie jambo hilo kwa kina na kwa muono wa Kiislamu. Hata hivyo, inaonyesha makosa yametokea kwa wewe kutozungumza na mumeo alipokuja kukuposa. Ilikuwa kabla ya Nikaah mzungumze kuhusu mambo yenu na kuafikiana katika mambo mengi hasa ya kuwa ulijua kuwa yeye alikuwa tayari ana wake wengine. Na ikiwa hakukutajia dhamira yake hiyo toka mwanzo, hilo ni kosa upandse wake na kama hana sababu za msingi za kukataa kuzaa nawe ila hiyo tu, basi atakuwa mkosa mbele ya Allaah kwa hilo.

Kwa kila hali jambo hilo bado lipo mikononi mwenu kama wanandoa ambao mnaweza kujadili na kushauriana kwa maslahi yenu wawili na familia yenu kwa ujumla. Hata hivyo, usifanye haraka kutaka talaka kutoka kwa mumeo kwani hilo ni jambo ambalo mnaweza kuzungumza na hata kama atakataa sasa huenda akakubali baadaye. Na ikiwa ameshikilia msimamo wake huo, basi uamuzi uko kwako; kuvumilia kuishi katika hali hiyo huku ukiwa katika stara ya mume, au kuomba talaka na huku ukiwa huna uhakika wa atakayekuja kukuoa na ikiwa naye huyo atakayekuja kukuoa naye atakuwa na tatizo kubwa zaidi ya hilo au la! Ni wajibu wako kuswali Swalah ya Istikhaarah na kumtaka Allaah ushauri kwani hakika suala lako ni gumu na si rahisi kukupa ushauri wa kukata moja kwa moja. Hata hivyo, usikubali kufunga kizadi moja kwa moja kwani hilo si lengo la ndoa na si katika yale Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ametutaka tuoe wanawake wenye mapenzi wenye kuzaa ili kuuongeza Ummah wake huu na siku ya Qiyaamah ajifakharishe kwa Ummah wake kwa wingi wa idadi yake.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share