Maana Ya Kauli Ya Allaah (عزَّ وجلَّ): وَأَمَّا بِنِعْمَةِ رَبِّكَ فَحَدِّثْ

 

Maana Ya Kauli Ya Allaah 'Azza wa Jaal: (وَأَمَّا بِنِعْمَةِ رَبِّكَ فَحَدِّثْ)

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalaam Alykum Warahmatullaah Wabarakaatuh! Shukrani zote anastahiki Allaah (mwingi wa rehma na mwenye kurehemu) na pia awazidishie kila la khayr katika jihad hii, mie nilikuwa nahitaji fasiri na sherehe ya aayah ya mwisho katika suwrah Adhw-Dhwuhaa (muulizaji aliandika Aayah kimakosa kwa kilatini)

 

  وَأَمَّا بِنِعْمَةِ رَبِّكَ فَحَدِّثْ

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Tafsiri ya Aayah hiyo ni kama ifuatavyo:

وَأَمَّا بِنِعْمَةِ رَبِّكَ فَحَدِّثْ ﴿١١﴾

Na neema ya Rabb wako ihadithie. [Adhw-Dhwuhaa: 11]

 

Kwanza hivyo ulivyoandika sivyo, na huwa ni makosa katika kuiandika na kuisoma Qur-aan kwa hali hiyo kwani hubadilisha maana ya kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Inavyotakiwa kuanzwa Aayah hiyo ni kwa neno 'Wa' na si 'Fa' kama ulivyoandika. 

 

Labda huenda tukauliza je, maana ya kuisimulia ni vipi? Jawabu ni kuwa kuisimulia hapa inamaanisha kumshukuru Allaah Aliyetukuka kwa kukupa neema hiyo kwa kufanya amali njema; si kwa njia ya kujisifu. Hakika ni kuwa majisifu kawaida yanampeleka mtu katika kujionyesha (Riyaa), na Riyaa inampeleka mtu kuingia katika Moto wa Jahannam.

 

Na wengine wamefasiri neema hapa kuwa Qur-aan, hivyo akaamrishwa aisome na kuihadithia kwa kuisambaza na kuwafundisha wengine. Nasi pia tunatakiwa tuisome na kuwahadithia mafundisho yake wengine.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share