Imaam Awasubiri Wanaofanya Uvivu Kuunga Safu Au Aanze Kuswalisha?

SWALI:

 

Assallam Alaikum Warahmatullah Wabarakatu, La mwanzo ninamshukuru ALLAAH SUBHANA HU WA TAALA kwa kukujaalieni ndugu zetu wa ALHIDAAYA kwa kutuelimisha kupitia kwenye mtandao INSHAALLAAH ALLAAH akulipeni mema mengi duniani na kesho akhera nyinyi na sisi kwa waislam sote.

 

Suala langu lipo katika swala la mwanzo panapokimiwa tunakuta wenzetu wanakuwa wavivu katika kuinuka utakuta mpaka imamu anafikia kukaa karibu dakika tatu mpaka nne kwa kiwasuwabiri kujiunga safu suala langu lipo je huyu imamu anatakiwa awasubiri kama anavyofanya huyu wetu au inatakiwa tufunge swala sisi ambao tumekwisha kujipanga kwa ajili ya swala? Suala langu la pili…


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuzembea katika Swalah na kujiunga katika safu kwa haraka.

Tufahamu kuwa Swalah kama ‘Ibaadah iliyofaradhishwa na Allaah Aliyetukuka imewekewa masharti yake. Na ni muhimu kuwa haya masharti yakamilike ili Swalah yenyewe iwe ni nzuri na yenye kumpatia thawabu nyingi mwenye kuitekeleza.

 

Ni katika Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alikuwa hafungi Swalah mpaka safu ziwe zimenyooka na kuwa barabara. Na wakati mmoja alikuwa ameingia kuswalisha na akawa karibu kupiga takbira ya kufungia Swalah mara akamuona Swahaba mmoja tumbo lake limetoka nje na hapo akawahimiza wawe ni wenye kuweka safu sawa.

 

Inaonekana Imaam wenu kufanya hivyo kwa kuwangojea ni kuwa lau atafunga Swalah basi safu hazitalingana naye kama Imaam ndiye atakayebeba mzigo wa kosa hilo. Kwa hivyo analofanya ni sawa.

 

Hata hivyo, inaonekana kuwa maamuma bado hawajaelewa mas-ala ya kuiendea Swalah kwa wepesi na kuwahi safu za mbele na takbira ya kufungia Swalah. Hivyo, tunaona ni vyema wewe uzungumze na Imaam aweke darsa ya kuwafahamisha maamuma wake kuhusu vipengele vifuatavyo:

 

1.     Sifa ya Swalah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

2.     Daraja na umuhimu wa Swalah.

3.     Umuhimu wa safu ya mbele na kutengeneza safu sawa sawa.

4.     Umuhimu wa kuiwahi Takbiyratul Ihraam (Takbira ya kufungulia Swalah) na Imaam.

 

Twatumai likifanyika hilo basi mambo huenda yakawa mazuri na matatizo hayo yanayosababishwa na ujinga wa kutoifahamu Swalah vizuri yataondoka inshaAllaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share