Du’aa Gani Asome Ili Apate Mume Wa Kheri?

SWALI:

 

Assalam Aleikum,

 

Kwanza nawapongeza sana kwa website yenu, ni nzuri sana na inatusaidia sana kwa sisi vijana tuliokuwa mda mwingi kazini. Inanipa faraja sana kujua kuwa kila nnapotaka kusoma dua yoyote au kusikiliza naweza kuingia humu.

 

Lakini naomba niwaulize swali moja linalonisumbua siku nyingi sana. Sasa najiuliza, hivi kuna dua yoyote kubwa inayopaswa kuisoma kama mwanamke anaetafuta mume ambae ni wa kheri kwake?

 

Asante sana


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Molai wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Du’aa ya kupata mume.

 

Hakika ni kuwa hatujapata kuona wala kusikia Du’aa kama hiyo. Hata hivyo, kukosekana Du’aa ya moja kwa moja haimanishi kuwa ndio basi, bali zipo njia nyingi za kufanikisha hilo.

 

Tufahamu kuwa Allaah Aliyetukuka Hakutuachia kitu chochote isipokuwa Ametuelezea kama Alivyosema katika Qur-aan:

Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote. Kisha kwa Mola wao i watakusanywa” (6: 38).

 

Swali linaweza kuja kwa nini basi hakuna Du’aa ya kupata mume wa kheri? Jibu kwa swali hili ni kuwa Allaah Aliyetukuka Ametuambia:

Niombenei Nami nitawaitikia”.

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye ametuelezea nyakati ambayo Du’aa inakuwa ni yenye kukubaliwa kwa urahisi kabisa. Hivyo, inabidi ujitume ili kufikia hilo kwa kumuomba Allaah Aliyetukuka Akufanikishie hilo. Katika baadhi ya nyakati ambamo Du’aa zinakubaliwa ni:

 

1.     Baina ya Adhaana na Iqaamah.

2.     Thuluthi ya mwisho ya usiku ambamo utainuka uswali Tahajjud, na humo uombe.

3.     Ukiwa katika sijdah ndani ya Swalah.

4.     Siku ya Ijumaa baina ya Khutbah mbili.

5.     Baada ya Alasiri siku ya Ijumaa na kabla kuchwa jua.

6.     Uwe ni mwenye kula, kunywa, kuvaa vya halali na uwe ni mwenye kumridhisha Allaah Aliyetukuka.

7.     Wakati unapokuwa safarini.

8.     Wakati unapokuwa umefunga, funga ya Faradhi (Ramadhaan) au ya Sunnah. Hivyo, jaribu kujikurubisha kwa Allaah kwa kufunga Jumatatu na Alkhamiys na ndani yake nyenyekea kwa Allaah.

9.     Kabla hujatoa Salaam ndani ya Swalah.

 

Fanya bidii umuombe Allaah, naye Atakupa mwenye kheri na mswalihina InshaAllaah wala usife moyo katika hilo. Twamuomba Allaah Aliyetukuka Akupe mume mwenye kheri na mcha Mungu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share