Mashairi: Mafuriko Na Magonjwa

                     Abdallah Bin Eifan

                 (Jeddah, Saudi Arabia)

Salaam ziwafikie, popote pale mlipo,

Ibada tuzingatie, mavuno yake ni pepo,

Baya tusikaribie, madhambi yasikuwepo,

Mafuriko na Magonjwa, sababu ni dhambi zetu.

Majumba kuporomoka, na miti inaanguka,

madaraja kuvunjika, na magari kutoweka,

na watu kuhangaika, ona wanavyotoroka,

Mafuriko na Magonjwa, sababu ni dhambi zetu.

Mavuno kuadimika, vyakula kuharibika,

Na umeme kuzimika, na watu kulalamika,

Adhabu imetufika, ni ghadhabu ya Rabbuka,

Mafuriko na Magonjwa, sababu ni dhambi zetu.

Radi inapopasuka, mvua kumiminika,

inapovuka mipaka, ni onyo hilo kumbuka,

hapo tuombe haraka, Mungu Apate ridhika,

Mafuriko na Magonjwa, sababu ni dhambi zetu.

Mvua ikisimama, na watu kusalimika,

kina baba kina mama, wote wanafurahika,

wanasahau ya nyuma, zote zile hekaheka,

Mafuriko na Magonjwa, sababu ni dhambi zetu.

Mara ardhi hukauka, mvua hakuna tena,

twaanza kulalamika, mbona hivi Subhana,

ukame unatufika, na shida za kila aina,

Mafuriko na Magonjwa, sababu ni dhambi zetu.

Kila pembe ufisadi, utaona umezidi,

umezidi uhasidi, fitina na ukaidi,

dua zetu zinarudi, kuomba twajitahidi,

Mafuriko na Magonjwa, sababu  ni dhambi zetu.

Epukana na uzinzi, huo ndugu si mapenzi,

mwisho wake ni majonzi, na majuto na machozi,

epukana na uizi, Anakuona Mwenyezi,

Mafuriko na Magonjwa, sababu ni dhambi zetu.

Danguro na vilabuni, na disco kila makani,

matapeli na wahuni, wametanda mitaani,

hao ndio mashetani, adui wa Waumini,

Mafuriko na Magonjwa, sababu ni dhambi zetu.

Tushike kamba ya Mungu, nawaomba ndugu zangu,

Muumba ardhi na mbingu, ni Mungu sio Mzungu,

Nafunga shairi langu, nawaaga walimwengu,

Mafuriko na Magonjwa, sababu ni dhambi zetu.

Share