Alisilimu Kwa Ajili Ya Mume Akaritadi Alipopewa Talaka, Sasa Anataka Kurudi Uislamu Anafaa Kuolewa?

SWALI:

 

 

Ndugu yangu alioa mke aliyemsilimisha. Wakaachana na mke akarudi dini yake ya ukristo. Baadaye yule ndugu yangu alipomuuliza akasema atarudi uislamu kama atamrudia na amerudi ukristo kwa sababu ya hasira ya kuachwa. Sasa ndugu yangu mke amrudie au la? Na wana mtoto mmoja.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuritadi kwa mwanamke aliyeolewa kisha akaachwa. Hakika mas-ala ya mwanamke na mwanamume kuritadi imekuwa ni jambo la kawaida. Hili hasa limetokea kwa sababu ya kusilimishwa bila ya kupata mafunzo au mmoja kati ya jinsia moja kuoa au kuolewa kwa sababu ya kupendana tu au kwa maslahi fulani mengine ya kidunia.

 

Inatakiwa anayesilimu awe ni mwenye kupatiwa mafunzo kuhusu Uislamu. Hakika si sawa kabisa kwa mwanaume kupatiwa mke baada ya tu kusilimu na mwanamke asiolewe tu baada ya kusilimu kwani hilo limeleta matatizo makubwa katika jamii yetu. Inatakiwa kabla ya kupatiwa mke au mume wawe ni wenye kupatiwa muda waweze kuulewa Uislamu. Ikiwa hatutaweza kufanya hivyo ndio hupata matatizo makubwa na hata watu kuritadi kwa sababu hawakusilimu kwa ajili ya Uislamu bali kwa sababu ya mke au mume au mambo mengineyo.

 

Hivyo kuhusu swali lako haitakuwa busara wala hekima kwenu kumsilimisha tena huyo mwanamke ili apate kuolewa. Na lau mtafanya hivyo basi huenda mkapatikana na maafa makubwa sana kwani huenda akasilimu kwa ajili ya mume lakini pindi anapoolewa kubadilika tena au kuwalea watoto watakaopata kwa njia mbaya au kuwaingiza katika Ukristo. Nasaha yetu ni kuwa twaomba mumfanyie Da'wah na kumkinaisha kuwa Kusilimu ni maslahi yake. Ikiwa atakubali kusilimu kwa njia hiyo, mumpatie mafunzo kwa muda kabla ya kufanya harusi. Lau atataka kuingia kwa atakavyo yeye ni bora asiolewe na aachwe aendeshe maisha atakavyo yeye mwenyewe.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share