Mashia Wanaodai Kuwa Unabii Ulipaswa Umfikie 'Aliy Nini Hukmu Yao Na Kitabu Gani Chao Kimetaja?

 

Mashia Wanaodai Kuwa Unabii Ulipaswa Umfikie

'Aliy Nini Hukmu Yao Na Kitabu Gani Chao Kimetaja?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

Assalamu aleikumwarahmatullahi wabarakaatuhu, napenda kuuliza kuwa niliwahi kusikia kwamba mashia wanasema kuwa utume uliomjia Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ulistahiki kwenda kwa Imamu Aliy ('Alayhis-salaam), naomba munitajie kitabu ambacho mashia wenyewe wamethibitisha madai haya, naomba tafadhali munisaidie

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Kwanza tunapenda kukutanabahisha ndugu yetu kuandika kwa kirefu hizo sifa tulizopigia mistari hapo juu badala ya kutosheka kuzifupisha hivyo. 

 

Asli katika Unabii ni Wahy na Wahy umetufunulia kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndie Nabiy wa mwisho hakuna Nabiy baada yake kama inavyotuhakikishia na kututhibitishia Qur-aan.

 

Pia ni vyema ieleweka kuwa Unabii si jambo la mtu kujitangazia au la kujiamulia yeye mwenyewe kuwatangazia watu au kutangaziwa na washabiki wake au na kila wenye kusingizia kuwa wanampenda kwa sababu moja au nyengine, bali ni uteuzi wake al-Waahidul Ahad Asiyezaa wala kuzaliwa, Qur-aan ilimtaka Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwatangazia watu hivi:

 

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ ۖ فَآمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ النَّبِيِّ الْأُمِّيِّ الَّذِي يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَكَلِمَاتِهِ وَاتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ ﴿١٥٨﴾

 

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hakika mimi ni Rasuli wa Allaah kwenu nyinyi nyote. (Allaah) Ambaye Pekee Anao ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Anahuisha na Anafisha. Basi mwaminini Allaah na Rasuli Wake; Nabiy asiyejua kusoma wala kuandika ambaye anamwamini Allaah na maneno Yake, na mfuateni ili mpate kuongoka. [Al-A’raaf: 158]

.

Hivyo basi ni kuwa hakuna atakayekuja au kujitokeza na kudai Unabii na kisha wale wenye kuamini Allaah na Siku ya Mwisho wakamkubali madai yake, bila shaka huyo ni muongo na hafai kusikilizwa wachilia mbali kuulizia kuhusu habari zake baada ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) .

 

Hii ina maana kuwa si katika imani thabiti na itikadi sahihi ya Kiislamu juu ya Allaah na Siku ya Mwisho kumsikiliza au kumdadisi ataedai unabii kwa kisingizio chochote kile kwani Muislamu anaelewa kuwa hakuna Unabii baada ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mwenye kukubali kuwepo unabii ni katika wenye kukanusha kauli ya Allaah na kusema kivitendo (kwa kumsikiliza anayedai unabii) kuwa Allaah si mkweli (Nastaghfiru Allaah!) aliposema kuwa:

 

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴿٤٠﴾

Hakuwa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Rasuli wa Allaah na ni mwisho wa Manabii. Na Allaah daima ni Mjuzi wa kila kitu. [Al-Ahzaab: 40]

 

Hivyo basi si jambo la kawaida kujitokeza miongoni mwa wenye kuamini Allaah na Siku ya Mwisho kuwa na suala kama ‘napenda kuuliza kuwa niliwahi kusikia kwamba mashia wanasema kuwa utume uliomjia Nabiy Muhammad’ (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ulistahiki kwenda kwa Imamu ‘Aliy’.

 

Hili si katika suali la kuweko kwa wenye kuamini Allaah na Siku ya Mwisho wachilia mbali kulitangaza na kulipeleka huku na kule kwa kisingizio cha kutaka kuelewa ukweli.

 

Hatari ya suala kama hili ni kuwa mwenye kuuliza au hata kulisikiliza uzushi kama huu bila ya kumsawazisha na kumueleza msemaji/ mtangazaji wa fitna kama hii kuwa ni muongo na hafai kusikilizwa bali anastahiki kupigwa marufuku katika jamii huwa kwa uhakika anasema kuwa Jibriyl ambaye anaeleweka kama ni Amiynul Wahy si muaminifu kwani alifanya khiyana au aliasi kwa kubadilisha alichoamrishwa na Allaah na kujiamulia kufanya akitakacho kwa kuacha kufikisha ujumbe kwa aliyetumwa amfikishie na kumpekekea Ujumbe asiyestahiki wala asiyeamrishwa kumpelekea (hii ni kufr); la pili ni kuwa huwa kwa uhakika anasema kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye kwa imani yake kuwa Jibriyl amekosea, si Nabiy kweli kwani aliyekuwa akistahiki kupewa na aliyechaguliwa na Allaah ni mtu mwengine hivyo Qur-aan na Hadiyth zilizopokelewa kutoka kwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zote hazifai kwani hakuwa Nabiy (hii ni kufr pia na mtu huwa ameshatoka katika mila akiwa na imani kama hii); la mwisho ni kuwa huwa unasema kuwa aliyoyasema Allaah kuhusu Malaika kuwa wanafanya waliyoamrishwa na hawamuasi Allaah si kweli kama ilivyothibitisha Qur-aan kwani Jibriyl ni katika Malaika na hakutekeleza Alichoamrishwa, yaani alitakiwa aufikishe Unabii kwa mtu mwengine na kwa akili yake aliupeleka kwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hivyo Aayah yenye kusema kuwa Malaika hawaasi ina mushkil (Nastaghfiru Allaah!):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ﴿٦﴾

Enyi walioamini! Jikingeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe; juu yake wako Malaika washupavu hawana huruma, shadidi, hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa. [At-Tahriym: 6]

 

Muislamu kusikia au kusikiliza suala kama hili na bila ya kulizuia hapo hapo ni sawa na mtu aliyekubaliana na msemaji, la sivyo ikiwa ulikuwa kama kweli umelisikia uliulize hapo hapo kama unaamini Allaah na Siku ya Mwisho sio uliweke na kulisambaza kwa Waislamu kwani ni sumu inayoweza kuwatoa wengi katika duara la imani, na kubwa kuliko hayo ni kuwa kwenda kwako katika sehemu zenye kuelezwa mambo kama hayo ni katika makosa na wewe utaulizwa kwa kila ulichokisikia, basi kama umesikia na hukuchukuwa hatua zitakiwazo jiandae na jawabu mbele ya As-Samiy’u Al-‘Aliym.

 

Ndugu muulizaji katika tovuti hii tunajaribu kadiri ya uwezo wetu na kwa tawfiki yake Allaah kusaidia kuweza kuwaongoza wenzetu na kuwafunua macho na kuwaelekeza kila tunaloamini na kuitakidi kuwa litaweza kuwapelekea kwa uwezo wake Allaah kuongoka na kuwa wenye imani yenye kukubalika mbele ya Allaah, hii ina maana kuwa si katika tunayotarajia kuyafanya ni kumpotosha Muislamu kwa kumpoteza kwa kumuelekeza au kumtajia kila tunachoamini kuwa ndani yake ni kufr na upotofu, na hivyo hatuwezi kukuongoza kwenye vitabu vya Kishia vilivyojaa kufru, upotofu na ushirikina, kama ulivyotaka kwa maneno yako haya: ‘naomba munitajie kitabu ambacho mashia wenyewe wamethibitisha madai haya, naomba tafadhali munisaidie.’

 

Kukutajia kitabu chochote kile cha Kishia si kukusaidia bali ni kukupoteza na kukuongoza kwenye upotofu na hilo si katika mamrisho ya Allaah kwani tunatakiwa tuamrishane mema na tuakatazane mabaya na tushirikiane katika mema na Taqwa na si vinginevyo; na yaliyomo katika vitabu vya Shia kwa ujumla si ya kumuelekeza mtu kwenda kuyaona ikiwa mtu mwenyewe hajapikika kiimani kwani wengi wanaouliza ni wanafunzi wa kiwango cha chini katika Uislam hivyo tutakuwa hatushikamani na muongozo wa ufundishaji tukiwatilia kitu sio katika kiwango chao kwani watachanganyikiwa maana kuna baadhi ambao hawakuwa wanaujua Uislam wao, walihadaiwa na maandiko yao na wemepotoka kama walivyopotoka Mashia wenyewe.

 

Ushauri ni kuwa hakuna msaada wa kukupoteza bali tunapenda na tunamuomba Ar-Rahmaan Atujaalie katika wenye kutoa maelekezo na  misaada ya kukuongoza katika yale aliyokuwa akiyafundisha na kuyasisitiza Rasuli wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo ni kushikamana na Qur-aan na Sunnah zake na Sunnah za Swahaba zake waongofu ambao ni Makhalifa zake wanne na kuachana na kila uzushi kama uzushi wa kusema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwateua Imamu na hao Imamu ni Ma’suum (wamelindwa na madhambi/ hawakosei) haya si katika mafundisho ya Uislamu bali ni katika uzushi na upotofu ulio wazi na katika Uislamu, kwani aliyekuwa Ma’suum ni mwenyewe Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Mwisho ni kuwa muulizaji ni katika wenye kupigia mfano kama huu wa Kiiarabu unaosema:

 

Wa’in-da Juhaynat al-Khabarul Yaqiyn

 

Kwa maana kuwa muulizaji ima awe katika washabiki wa shia au mpinzani wao, basi kwa hakika anaelewa ukweli bali ana yakini katika anayoyauliza.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share