Kumnyoa Mtoto Nywele Staili Za Kihuni Na Kumchora Michoro Mwilini

Kumnyoa Mtoto Nywele Staili Za Kihuni Na Kumchora Michoro Mwilini

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Asalam Alaqum Warahmat llah wabarakat. Swali langu ni hili je inafaa kumnyoa mtoto nywele za mtindo wa pank au kuchorwa michoro mbali mbali kama vile nike na vinginevyo. Naomba ushahidi wa aya na hadithi. Asalam allaiqum.

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. 

 

Kumnyoa mtoto mitindo ya kihuni au kumchora michoro mbali mbali kwenye kichwa. Kuhusu nukta ya kwanza ambayo ni mtindo wa panki ambao Kiislamu unaitwa Qaza‘, nao ni kunyoa baadhi ya nywele na kuacha nyingine. Hii imekatazwa na sharia kwa Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) aliyesema: “Amekataza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kukata baadhi ya nywele za kichwa na kuacha nyingine” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na amesema tena (Radhiya Allaahu ‘anhuma): Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  aliwaona watoto ambao wamenyolewa baadhi ya nywele na kuachwa nyingine, akawakataza kufanya hilo. Akasema: “Nyoeni zote, au ziacheni zote” [Abu Daawuwd na an-Nasaa’iy].

 

Ama kuchora michoro mbali mbali pia imekatazwa na kuharamishwa katika Dini yetu. Huko ni kubadilisha umbile la Allaah Aliyetukuka Alilomuumba nalo Allaah na kufanya hivyo ni kumfuata shaytwaan (4: 119). Kisha kufanya hivyo ni kujifananisha na makafiri ambako Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza. Pia Abdullaah Bin Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) amewalaani wenye kuchanja – kutia chale (tattoo) na mwenye kuchanjwa, mwenye kuchonga meno na mwenye kuchongwa kama ilivyotajwa na katika Hadiyth ifutayo:

 

عَنْ عَلْقَمَةَ، عَنْ عَبْدِ اللَّهِ، لَعَنَ اللَّهُ الْوَاشِمَاتِ، وَالْمُسْتَوْشِمَاتِ، وَالْمُتَنَمِّصَاتِ وَالْمُتَفَلِّجَاتِ لِلْحُسْنِ، الْمُغَيِّرَاتِ خَلْقَ اللَّهِ تَعَالَى، مَالِي لاَ أَلْعَنُ مَنْ لَعَنَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم وَهْوَ فِي كِتَابِ اللَّهِ وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ‏ ‏‏.‏

Amesimulia ‘Alqamah (رضي الله عنه): Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه) amesema: Allaah Amewalaani wenye kuchanja, na wenye kuchanjwa, na wenye kunyoa nyusi, na wenye kuchonga meno kwa urembo, na wenye kubadilisha umbile la Allaah (سبحانه وتعالى). Kwa nini nisimlaani yule aliyelaaniwa na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na aliyelaaniwa katika Kitabu cha Allaah?:

 

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٧﴾

“Na lolote analokupeni Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) basi lichukueni, na analokukatazeni, basi jiepusheni.” [Al-Hashr (59:7) Hadiyth amepokea Imaam Al-Bukhaariy Kitabu Cha Mavazi (77)]

 

Na huku kuchanja kunaumbua na kuharibu uso na mikono kwa chale zitiwazo na nakshi mbaya ichorwayo, na wengine wamepindukia kwa kuchora mwili mzima. Pia yapo maumivu na adhabu inayosababishwa katika kuchorwa na sindano na hata kama hakuna maumivu mwilini ni jambo lililokatazwa.

 

 

Ama kuchora kichwani mchoro wa ‘nike’ au hata kuvaa mavazi ya nembo hiyo ya ‘nike’, kwanza kabla Muislam hajavaa nguo za mitindo au kutumia majina na nembo mbalimbali, ni muhimu sana kwanza ajue jina au nembo hiyo inawakilisha nini? Nembo na jina la ‘nike’, linamaanisha ‘mungu wa kike wa ushindi’ katika miungu ya kigiriki ambao wao walikuwa na miungu ya kila kitu!

 

Kwa maana tu ya jina hilo, basi haifai kabisa Muislam kuvaa majina kama hayo au kutumia nembo zake kwani kwa njia moja au nyingine ni kukubaliana na ushirikina huo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share