Vipi Mtu Anapata Husda Kwa Ajili Ya Kusoma Qur-aan Na Hali Qur-aan Ni Kinga?

 

Vipi Mtu Anapata Husda Kwa Ajili Ya Kusoma Qur-aan Na Hali Qur-aan Ni Kinga?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Assalamu Aleykum warahmatullahi wabarakatu, kuna kiswa au viswa flani ambavo nimewahi kuviskia kuhusu mtu kuhusudiwa kwa namna anavosoma Qur-aan au kwa Qira'a -chake kizuri sasa huwa vipi mtu akapata husda na hali yakuwa yeye asoma Qur-aan? Natujuwavo Qur-aan ni kinga ya kila kitu mbona isiwakinge watu kama hao waliopatwa na Hasad na hali yakuwa wao wanasoma Qur-aan? Maana nimewahi kusikia yakuwa Kassim radhi allahu waanhum mtoto wa Nabiy Muhammad sallaallahu waaleyhi wassallam amedhurika kwa Hasad wakati alipokuwa akisoma Qur-aan, sasa mimi swali langu ni kuwa naomba munifahamishe/Shukran wa Ramadwaan Kareem. 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu kupata husda na ilhali unasoma Qur-aan.

 

Mwanzo kabla ya kuingia katika suala lenyewe kama kichwa cha habari kinavyosema ni kujaribu kuweka sawa kuhusu hasad kwa mtoto wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Qaasim kuwa alikuwa akisoma Qur-aan na akadhurika. Huu ni uongo kwani Qaasim alizaliwa kabla ya babake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kupatiwa Utume na aliaga dunia akiwa mtoto mdogo sana wa kutoweza kusoma. Hiyo ndio historia yake kwa ufupi, kwa hivyo kisa hicho ni cha uongo bila ya shaka ya aina yoyote.

 

 

Kila kitu katika Uislamu kina sifa zake na mambo yake ambayo kwayo kunapatikana faida kwa kila mwanaadamu. Qur-aan bila shaka ni kinga ya hasad na pia na Moto kwa mwenye kuisoma inavyotakiwa, kwa nia nzuri na ikhlaswi. Bila ya hivyo inakuwa haimsaidii mwenye kuisoma. Kuna Hadiyth Qudsiy ambayo inatufahamisha, “Na mtu ambaye amepatiwa elimu na kuifundisha na kuisoma Qur-aan. Ataletwa na Allaah Atamjulisha neema Aliyompa, naye atazitambua. (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atasema: ‘Je, uliifanyia nini?’ Atasema: ‘Nilisoma elimu ya Dini na kuisomesha na niliisoma Qur-aan kwa ajili Yako’. Allaah Atasema: ‘Umesema uongo, lakini ulisoma elimu ya Dini ili uambiwe, mwanachuoni na umesoma Qur-aan ili uambiwe kuwa wewe ni Qaarii (msomaji). Na hakika umeambiwa’. Kisha ataamuriwa kuburuzwa juu ya uso wake na kuingizwa Motoni” [Muslim, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy].

 

Hivyo hivyo, kama alivyoingizwa Motoni huyo mwenye kusoma Qur-aan kwa ajili ya kujionyesha ndivyo anakavyopatwa na hasad mwenye kuisoma kwa sababu nyingine yoyote isiyokuwa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Hivyo, tunatakiwa tuisome Qur-aan inavyotakiwa ili tuepukane na Moto wa Jahanamu na hasad.

 

Na tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atuepushe na Hasad na Moto.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share