001-Hakimu Wa Kiislamu: Dibaji

 

DIBAJI

 

Sifa zote ni Zake Allaahu Bwana wa viumbe vyote. Na rahma na amani ziwe juu ya Nabii Wake msema kweli mwaminifu, na juu ya Maswahaba wake na wale waliowafuata kwa wema hadi siku ya Qiyaamah.

Waba'adu...

Kwanza kabisa napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa ndugu yetu Naaswir Haamid kwa kujitolea kwake kuifanikisha shughuli hii pevu na ngumu. Bila shaka ni kazi ambayo inahitaji umakinifu na subira ya hali ya juu kabisa kutokana na ugumu wake. Nina matumaini makubwa kwamba kazi yake hii ya kukusanya mwenendo wa kesi baina ya Shari'ah na Sheria, itakuwa na manufaa makubwa kabisa kwa Waislamu wote Waswahili kwa vizazi vya sasa na vijavyo mpaka siku ya Qiyaamah. Tunamwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Azijaalie thawabu za kazi yake hii ziwe katika mizani ya mema yake katika siku hiyo ambayo mali wala watoto hawatafaa kwa chochote ila kwa mtu aliyemjia Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa moyo usio na doa.

Mimi kwa upande wangu nikiwa kama mpitiaji, nahisi jukumu ni kubwa sana la kuhakikisha kuwa kila kitu ni madhubuti na barabara na hakuna dosari wala kasoro yoyote. Nahisi jukumu hili ni zito mno kwanza kabisa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na kisha kwa wasomaji. Lakini nimekuwa nikijipa moyo kuwa kwa hali yoyote ile, bin Aadam ni bin Aadam tu, hakosi kasoro wala makosa. Wakati wote nimekuwa nikilikumbuka neno Lake Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Aayah ya 286 ya Suratul-Baqarah:

{{Mola wetu! Usituchukulie tukisahau au tukikosea}}

Upitiaji wa kazi hii ni mgumu kwa sababu ya kuzichunguza pokezi za Hadiyth zilizotumika. Kwani kama tujuavyo kwamba, kuna Hadiyth nyingi za uongo ambazo amezushiwa Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na hapo ndipo ugumu wenyewe ulipojikita.

Narudia tena nikisema kuwa bin Aadam hakosi kasoro au upungufu. Bila shaka msomaji kwa hali yoyote, anaweza kukuta dosari kadhaa katika kazi hii pale ambapo pengine tumepitikiliwa au tumeghafilika. Tutashukuru sana kama atachangia kwa kututanabahisha na kutuelezea maoni yake, kwani hilo litazingatiwa kuwa ni mchango wake yeye pia katika kazi hii itakayowanufaisha wengi kwa miaka na miaka.

 

Abu 'Abdillaah

01 Muharram 1430

01/01/2009

 

Share