Amekhasimikiana Na Ndugu, Naye Anakhofu Hatari Zake Na Kupata Madhara Yake Na Kukosa Fadhila Za Kupatana

 

SWALI:

 

ASSALAMA ALAEKUM WA RAHMATU LLAHI WA BARAKATU SHEKH TUNASHUKURU SANA KWA JUHUDI ZENU MNAZO ZICHUKUA KATKA KUTUELIMISHA DINI YETU YA ISLAM MADDA MULIO ITOA HIVI KARIBUNI YA KUSULUHISHA WALIO GOMBANA MIMI BINAFSI YANGU YAMENIPATA HAYA BAADA YA KUDAI HAKI YANGU BAADA YA BABA YETU MUNGU AMREHEMU WALINIFUKUZA KWA MUDA MREFU SASA NIMEPATA KHOFU BAADA YA KUSOMA MAKALA HII YA WALIOGOMBANA NIMEFIKIRIA KWENDA KWA SHEKH AHMED AL KHALILI ILI AWAITE NA

KUWAPA MAWAIDHA NAOMBA USHAURI WENU

 

 



 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukurani kwa kujua kwamba unafaidika na mafunzo ya Alhidaaya na unafuata nasaha zetu. Hii ni neema kwako kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Kutaka Kukuongoza na Kukuepusha na shari hii, inapasa umshukuru kwa Hidaaya Yake.

 

Kutokana na umuhimu wake jambo hili na hatari zake, tumefanya juhudi haraka mno kukujibu kabla ya wengine ambao maswali yao yameingia zamani sana kabla yako. Hii kwa sababu tunamkhofia kila Muislamu mwenye kukhasimikiana na nduguye, ikiwa undugu wa Kiislamu au undugu wa uhusiano wa damu, kupoteza ‘amali zake na kupata madhara yake kama zilivyotajwa katika makala ya 'Nasiha Ya Ijumaa' na humu kwenye jibu hili.

 

Bila shaka ikiwa umekhasimikiana na ndugu zako, jambo ambalo linachukiza sana kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), bali Analaani wenye kukata uhusiano wa damu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

((فَهَلْ عَسَيْتُمْ إِن تَوَلَّيْتُمْ أَن تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ وَتُقَطِّعُوا أَرْحَامَكُمْ ))  (( أُوْلَئِكَ الَّذِينَ لَعَنَهُمُ اللَّهُ فَأَصَمَّهُمْ وَأَعْمَى أَبْصَارَهُمْ))  

 

((Basi yanayotarajiwa kwenu mkitawala ndio mfisidi katika nchi na muwatupe jamaa zenu)) ((Hao ndio Allaah Aliowalaani, na Akawatia uziwi, na Akawapofoa macho yao)) [Muhammad: 22-23]

 

 

Pia Anasema:

 

 ((الَّذِينَ يَنقُضُونَ عَهْدَ اللَّهِ مِن بَعْدِ مِيثَاقِهِ وَيَقْطَعُونَ مَا أَمَرَ اللَّهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيُفْسِدُونَ فِي الأَرْضِ أُولَئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ))

((Wanaovunja ahadi ya Allaah baada ya kwishaifunga, na wakayakata Aliyoamrisha Allaah kuungwa, na wakafanya uharibifu katika nchi; hao ndio wenye khasara)) [Al-Baqarah: 27]

Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameonya kwamba mwenye kukata uhusiano wa damu hatoingia Peponi! Hali kadhaalika mwenye kukata uhusiano wa ndugu Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Hukmata, na ni sababu mojawapo wa kupunguziwa rizki, umri na mali. Maonyo mbali mbali kama haya tunapata katika kauli za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zifuatazo:

 

Hadiyth ya kwanza:

 قال رسول الله صلى الله عليه وسلم:  (( لا يدخل الجنة قاطع رحم)) رواه الترمذي.

Amesema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Haingii Peponi mwenye kukata udugu)) [At-Trimidhiy]

 

 

Hadiyth ya pili:

عن عائشة رضي الله عنه قالت: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم :  ((الرحم معلقة بالعرش تقول: من وصلني وصله الله ومن قطعني قطعه الله))  رواه البخاري ومسلم

Kutoka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Uteresi [Fuko la uzazi] limetundikwa na 'Arsh [Kiti cha Enzi cha Allaah] linasema: Atakayeniunga, Allaah Atamuunga, na atakayenikata, Atakatwa na Allaah)) [Al-Bukhaariy na Muslimu]

 

Hadiyth ya tatu:

 

 ((إن الله خلق الخلق حتى إذا فرغ من خلقه قالت الرحم: : هذا مقام العائذ بك من القطيعة.  قال:  نعم.  أما ترضين أن أصل من وصلك واقطع من قطعك؟  قالت:  بلى يا رب قال فهو لك )) رواه البخاري ومسلم.

 

((Hakika Allaah Ameumba viumbe mpaka Alipomaliza likasema uteresi [fuko la uzazi) Huyu amesimama anajikinga Kwako na anayemkata, Akasema ndio hivi huridhii Nikimuunga anayekuunga na Ninamkata anayekukata? Akasema sawa. Akasema hilo lako [umekubaliwa ombi lako])) [Al-Bukhaariy]

 

Hadiyth ya nne:

 

فعن أنس بن مالك رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال:  ((من أحب أن يبسط له في رزقه وينسأ له في أثره فليصل رحمه)) رواه البخاري ومسلم.

Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kupenda kutanuliwa rizki yake, na azidishiwe baraka katika umri wake, basi aunge undugu wake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth ya tano:

عن أبي أيوب الأنصاري رضي الله عنه أن رجلا قال: يا رسول الله: أخبرني بعمل يدخلني الجنة   . فقال رسول الله صلى الله عليه وسلم:   ((تعبد الله لا تشرك به شيئا وتقيم الصلاة وتؤتي الزكاة وتصل الرحم)) رواه البخاري ومسلم.

    

Kutoka kwa Abu Ayyuub Al-Answaariyy (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba mtu alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Ewe Mtume wa Allaah, nifahamishe tendo litakaloniingiza Peponi na litakaloniepusha na moto.  Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): ((Umuabudu Allaah wala Usimshirikishe na chochote, usimamishe Swalaah utoe Zakaah na uunge undugu)) [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Kwa hiyo nasaha zetu za dhati kama ulivyotaka kwetu, ni kwamba fanya haraka kabisa upatane na ndugu zako kwa ili ubakie salama na ‘amali zako, na upate fadhila na kujepusha na madhara yaliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah, na upate Radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).

 

Pia tambua kwamba mwenye kuanza kupatana na nduguye ni bora mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwani daraja yake hupandishwa kwa kunyenyekea kwake na kuwa yeye wa kwanza kumlaani Shaytwaan ambaye anawashawishi watu  wakhasimikiane.  Na pindi ukifanya  juhudi ya kuwasiliana na ndugu zako kwa kutaka kupatana nao, kisha wao wawe wakaidi, basi wewe utakuwa huru na umeshajitoa hatiani katika kupata madhara ya kukata uhusiano wa ndugu; watabaki wao kubeba dhambi. Lakini tunaomba kuwa isiwe hivyo bali wote warudie kwa Mola wao kuunga undugu inshaAllaah.

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi kuhusu maudhui hii muhimu mno kwa kila Muislamu:

 

Kukata Undugu

 

Amezuiliwa Kuonana Na Mama Yake Afanyeje?

 

Baba Ametukataza Tusiwasiliane Na Dada Yetu – Je Tumtii?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share