Mariyah Alikuwa Ni Miongoni Mwa Wakeze Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Je Alikuwa Mtumwa?

SWALI:

 

Assalaam alaykum

 

Watukufu waislam wenzangu nina jambo linaniumisha kichwa na nitafurahi kulipatia ufumbuzi hapa kwa waislam wenzangu.

Tunaambiwa na masheikh wetu Mtume {S.A.W.} alipata kuoa wake 12 na aliwahi kuletewa zawadi ya wajakazi na mmoja akamfanya suria na suria huyo aliwahi kumzalia mtoto wa kiume jina lake IBRAHIIM.

 

Swali

je huyu suria ni katika wale wakeze 12?

je alimbakisha na kumtumia kama suria mda wote?

na kama alimuoa vipi ilikua ndoa yake? Natumai kupata majibu yenye marejeo {rifrence} ili niweze kujiamini.


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu  (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah,  (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu wakeze Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na suriya wake. Mwanzo ni kurekebisha kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na wake 11 na sio 12 kama ulivyo andika na pia alikuwa na suriya wawili. Ama wakeze walikuwa ni kama wafuatao:

 

  1. Khadiyjah bint Khuwaylid (Radhiya Allaahu ‘anha).

  2. Sawdah bint Zam‘ah (Radhiya Allaahu ‘anha).

  3. ‘Aa’ishah bint Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anha).

  4. Hafswah bint ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anha).

  5. Zaynab bint Khuzaymah (Radhiya Allaahu ‘anha).

  6. Ummu Salamah Hind bint Abi Umayyah (Radhiya Allaahu ‘anha).

  7. Zaynab bint Jahsh (Radhiya Allaahu ‘anha).

  8. Juwayriyah bint al-Haarith (Radhiya Allaahu ‘anha).

  9. Ummu Habiybah Ramlah bint Abi Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘anha).

  10. Swafiyah bint Huyayy bin Akhtwab (Radhiya Allaahu ‘anha).

  11. Maymuunah bint al-Haarith (Radhiya Allaahu ‘anha).

 

Wakeze tisa walimkalia eda kwani alikufa kabla yao ilhali wawili (Khadiyjah na Zaynab bint Khuzaymah (Radhiya Allaahu ‘anhuma) walikufa kabla yake.

 

Ama masuriya wake wawili alikaa nao katika hali ya usuriya, nao ni Mariyah Mqibti na Rayhaanah bint Zayd an-Nadhwariyah. Ilhali wanachuoni wengine kama Abu ‘Ubaydah anasema kuwa masuriya wake walikuwa ni wanne (4).

 

Haya unaweza kuyapata katika vitabu vya Siyrah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mfano ar-Rahiyq al-Makhtuum cha Swafiyur-Rahman al-Mubaarakfuuriy. Kitabu hicho kimefasiriwa kwa Lugha ya Kiswahili na pia Kiingerza.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share