001-Talbiys Ibliys - Ufunikaji (Uhadaifu) Wa Ibilisi: Upambaji Wa Ibilisi - Wasiwasi Katika Swalah: Wudhuu

 

Muhammad Faraj Saalim As-Sa’y

 

 

Talbiys Ibliys

 

Katika kitabu chake kiitwacho ‘Talbiys Ibliys’ (Upambaji wa Ibilisi), mwanachuoni maarufu Shaykhul Islaam Ibn Taymiyah anasema:

 

“Jua ya kwamba mlango mkubwa anaopitia Ibilisi katika kuwaharibia Waislam ibada zao ni mlango wa ‘ujinga katika dini’. Ibilisi huwaingilia watu kwa kupenya kupitia mlango huo kwa raha zake huku akiwapambia na kuziona kuwa ni njema. Kwani Ibilisi keshawaharibia wengi miongoni mwa wafanyao ibada kwa ajili ya kutokujuwa kwao namna ya kumuabudu Mola wao kama anavyotaka kuabudiwa. Ama wale wenye kufahamu, Ibilisi huwaingilia kwa kuibia ibia tu.”

 

Mmoja katika Maulamaa wakubwa aitwae Matraf bin ‘Abdillaah amesema:

“Fadhila ya elimu ni kubwa kupita fadhila ya ibada”.

 

Na hii ni kwa sababu elimu ni nuru inayomuongoza mja kuijua njia sahihi ya kumuabudu Mola wake bila kupunguza wala kuvuka mipaka. Na Allaah Amekwishatuelimisha kupitia kwa Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), namna gani anatutaka tumuabudu.

Allaah Anasema:

 

ثُمَّ جَعَلْنَاكَ عَلَى شَرِيعَةٍ مِّنَ الامْرِ فَاتَّبِعْهَا وَلا تَتَّبِعْ أَهْوَاء الَّذِينَ لا يَعْلَمُونَ

 

“Kisha tumekuweka juu ya Sharia ya amri yetu, basi ifuate, wala usifuate matamanio ya wale wasiojua (kitu).” Al-Jaathiyah: 18

 

 

Siku ile alipofukuzwa Peponi na kutolewa katika rehma ya Allaah, Ibilisi aliapa kuwa atazifisidi ibada za wanaadamu na kuwakalia juu ya kila  njia iliyonyoka.

Allaah Anasema:

 

قَالَ فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ

 

“Akasema (Ibilisi); ‘Kwa kuwa umenihukumia upotofu (upotevu) basi nitawakalia (waja Wako) katika njia Yako iliyonyoka (ili niwapoteze).” Al-A’araaf: 16

 

Ibilisi hawaandami wale waliokwishapotoka, lakini moyo wake unaungulika kila anapowaona walio juu ya njia iliyonyoka wakiswali na kufanya ibada zao kama walivyoamrishwa.

 

Ili kuzifisidi ibada zao, Ibilisi hutumia hila nyingi zikiwemo:

1.     Kuwatia wasi wasi.

2.     Kuwafanya wahisi tabu au dhiki wanapoanza kufanya ibada.

3.     Kuwapambia ibada za uzushi na kuwafanya waongeze au wapunguze.

 

Ibilisi humfisidia mtu kwa kumtia wasi wasi akiwa ndani ya ibada na kumfanya ahisi kama kwamba hajaifanya vizuri, hakuikamilisha, ina kasoro, Wudhuu wake haukutimia nk. Na kutokana na hayo humfanya aongeze katika Swala au katika Wudhuu, akidhani kuwa hiyo ndiyo sahihi inayomridhisha Mola wake, bila kuelewa kuwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mafundisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Waliokula Hasara Katika Vitendo Vyao

 

Ibada yoyote isiyokuwa na amri ya Allaah au ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haifai na haina uzito wowote juu ya mezani.

Allaah Anasema:

 

قُلْ هَلْ نُنَبِّئُكُمْ بِالأخْسَرِينَ أَعْمَالا. الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا.

 

“Sema; ‘Je! Tukujulisheni wenye hasara katika vitendo (vyao)?. Hao ambao bidii zao (hapa duniani) zimepotea bure katika maisha ya dunia, nao wanafikiri kwamba wanafanya ‘amali njema!” Al-Kahf: 103-104

 

Katika kuzifasiri aya hizi, anasema Ibn Kathiyr kuwa; ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

“Aya hii inamsibu kila mwenye kumuabudu Allaah kinyume na mafundisho ya Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na huyo anakuwa mbali na njia inayomridhisha Allaah, akidhani kuwa ‘amali yake hiyo inakubaliwa, wakati ukweli ni kuwa anafanya makosa, na ‘amali zake hizo zinapotea bure.”

 

Allaah pia Anasema:

 

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَاللّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

 

“Sema; ‘Ikiwa nyinyi mnampenda Allaah, basi nifuateni; (hapo) Allaah atakupendeni na atakughufirieni madhambi yenu. Na Allaah ni Mwenye maghufira (na) Mwenye rehema”.

Aali-‘Imraan: 31

 

 

Kuvuka Mipaka

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

 

يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لاَ تَغْلُواْ فِي دِينِكُمْ وَلاَ تَقُولُواْ عَلَى اللّهِ إِلاَّ الْحَقِّ

 

“Enyi watu wa kitabu msipindukie mipaka katika dini yenu wala msiseme juu ya Allaah ila yaliyo kweli”. An-Nisaa: 171

 

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametukataza kuvuka mipaka katika ibada na kuifanya iwe nzito, kwani yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameletwa ili kutuwepesishia na si kuyafanyia mambo yakawa magumu.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Mumeletwa ili muwepesishe na hamkuletwa kuyafanya mambo yakawa magumu” Al-Bukhaariy, At-Tirmidhiy, Al-Bayhaqiy, An-Nasaaiy na Imaam Ahmad

 

Na katika Hadiyth iliyopokelewa na Imaam Ahmad na An-Nasaaiy, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Msipindukie mipaka katika dini kwani kilichowaangamiza waliokuja kabla yenu ni kupindukia mipaka katika dini”.

 

Dalili juu ya ubaya wa kuzusha au kupindukia mipaka katika ibada, tunaipata katika Hadiyth iliyopokelewa na Al-Bukhaariy na Muslim na kusimuliwa na Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) inayosema:

 

“Watu watatu walikwenda katika kila nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwauliza wakeze vipi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya ibada zake, na baada ya kujulishwa, mmoja wao akasema:

“Sisi wapi na Mtume wapi. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekwishasamehewa madhambi yake yote yaliyotangulia na yanayokuja. Ama mimi nitakuwa nikiswali usiku kucha wala sitolala”.

Mwengine akasema:

“Ama mimi nitafunga siku zote na wala sitokula mchana tena”.

Wa tatu akasema:

“Ama mimi sitofunga ndoa kabisa (ili niweze kufanya ibada zangu vizuri).”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliporudi na kuhadithiwa, alipanda juu ya minbari akasema:

“Nimesikia kuwa watu wanasema hivi na vile. Ama yule anayemjua Allaah zaidi na kumuogopa zaidi kuliko wote ni mimi. Lakini mimi ninafunga na ninakula. ninaamka usiku kuswali na (pia) ninalala, na ninaoa wanawake. Kwa hivyo yeyote atakayekwenda kinyume na mafundisho yangu basi huyo hayuko pamoja nami”.

 

Hadiyth hii inatufundisha umuhimu wa kufuata na ubaya wa kuzusha. Umuhimu wa kusahilisha na ubaya wa kuchupa mipaka katika ibada kwa kisingizio cha kujikurubisha zaidi kwa Allaah, hata kama Niyah ni njema. Niyah pekee haitoshi ikiwa ndani yake hapana muongozo wa mafundisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa sababu Allaah Haridhiki na ibada yoyote isipokuwa ile tu aliyoitolea amri Yake.

 

 

Wasiwasi Katika Wudhuu

 

Baadhi ya watu hawaridhiki wanapotawadha kwa kuosha viungo vyao mara tatu kama tulivyofundishwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ibilisi anawatia wasiwasi na utawaona wakizidisha idadi ya kuosha kwa kisingizio cha kuondoa wasiwasi, wakati ukweli ni kuwa huko kuongeza kwao ndio wasiwasi wenyewe.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuyafanyia israfu maji.

 

Siku moja alipomuona mmoja katika Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhu) akitawadha, alimuuliza:

“Kwa nini unafanya israfu katika maji?”

Swahaba (Radhiya Allaahu ‘anhu) akauliza:

“Kwani hata katika maji pana israfu?”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia:

“Ndiyo. Hata kama unatawadha penye mto wa maji yanayokwenda.”

Imaam Ahmad

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kutawadha kwa kuosha viungo vyake mara moja moja, aliwahi pia kutawadha kwa kuviosha mara mbili mbili na mara tatu tatu. Kwenda kinyume na hayo ni kupindukia mipaka katika mafundisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Mtu mmoja alimuuliza Imaam Ahmad bin Hanbal:

“Ninaweza kuongeza zaidi ya mara tatu katika Wudhuu?”

Imaam akamjibu:

“La, huwezi. Hafanyi hivyo isipokuwa mwenye maradhi (ya wasi wasi).”

 

Imepokelea kutoka kwa Abu Daawuud kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Kutakuwa na watu katika umati wangu wanaopindukia mipaka katika kujitwahirisha na katika kuomba du’aa”

 

Na akasema:

 

“Hakika katika kutia Wudhuu, pana Shaytwaan (mwenye kuwatia watu wasiwasi) anayeitwa Al-Walahan, kwa hivyo jiepusheni na wasiwasi wa Wudhuu”. At-Tirmidhiy

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

 

إِنَّهُ لاَ يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ

 

“Yeye (Allaah) hawapendi wapitao mipaka.” Al-A’araaf: 55

 

Kwa vile kuzidisha katika Wudhuu wa mwenye wasiwasi ni katika uchupaji wa mipaka, basi huo unaingia katika zile ibada asizozipenda Allaah.

 

Anasema Ibn Qudaamah, katika kitabu chake kiitwacho “Dhamm Al-lMuwaswasiyn”:

 

“Ukimuuliza mwenye wasi wasi kwa nini unatawadha zaidi ya mara tatu?

Atakujibu: 'Akiba ya maneno, pengine nimekosea au nimepunguza idadi ya kuosha viungo vyangu.'

“Mtu anaweza kuipa sababu anayoitaka,” anaendelea kusema mwanachuoni huyo. “Lakini suali linakuja; “Je, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wakifanya hivyo?"

Bila shaka jawabu itakuwa ;’La. Hawakuwa wakifanya hivyo’. Kwa sababu kusema kuwa walikuwa wakifanya hivyo, ni kuwazulia uongo."

 

Iwapo tutakiri kuwa hawakuwa wakifanya hivyo, basi itatulazimu na sisi kuacha mwenendo huo, kwani kuuendeleza ni kwenda kinyume na mafundisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”.

 

 

Kuvunjika Kwa Wudhuu

 

Katika wasiwasi ni pale mtu anapokuwa ndani ya Swalah akasikia mingurumo tumboni mwake, akadhani kuwa upepo umekwishamtoka, akaamua kuvunja Swalah na kwenda kutawadha kwa dhana tu.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametukataza kufanya hivyo aliposema:

 

“Mmoja wenu anaposikia sauti tumboni mwake akatia shaka, je, kimetoka kitu (upepo) au hakijatoka? Basi asivunje Swalah isipokuwa kama (ana hakika kuwa) amesikia sauti (ikitoka) au harufu”. Muslim

 

Imepokelewa pia kuwa mtu mmoja alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa; huwa anahisi kila anaposwali kama kwamba upepo unamtoka. Akajibiwa kuwa asivunje Swalah mpaka asikie sauti au harufu. Al-Bukhaariy na Muslim

 

Katika Musnad ya Imaam Ahmad na Sunan za Abu Daawuud, Imeelezwa na Abu Sa’iyd Al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Shaytwaan humjia mtu katika Swalah yake na kumfanya ahisi kama kwamba ametoa upepo, basi mtu asiivunje Swalah yake mpaka asikie sauti au harufu”.

 

Na katika Sunan ya Abu Daawuud, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Shaytwaan anapomjia mtu na kumwambia kuwa Wudhuu wako umevunjika”. Basi naye asema (moyoni pake); “Muongo wewe”, isipokuwa pale anaposikia harufu kwa pua yake au sauti kwa sikio lake”.

 

Katika kitabu chake kiitwacho; “Dhamm Al-Muwaswasiyn”, anasema Ibn Qudaamah:

 

“Kwa ajili ya kuyapiga vita maradhi ya wasi wasi, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuamrisha kumkadhibisha Shaytwaan, juu ya kuwa kitendo hicho (cha kutoka upepo) kinaweza kuwa kimetokea kweli. Vipi basi mtu anakubali kumfuata Shaytwaan pale uongo wake unapokuwa dhahiri, pale anapoambiwa na Shaytwaan kuwa; “Hukutawadha vizuri au hukutia Niyah sawa n.k., wakati anajua kuwa huo ni wasi wasi wa Shaytwaan tu, na kwamba anajaribu kumchezea”.

 

 

Share