006-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Lawama Nyingi Hukausha Nyoyo

 

LAWAMA NYINGI HUKAUSHA NYOYO

 

Lawama zako zisiwe katika dogo na kubwa, jifunze namna bora ya kusamehe na kukubali mambo mengine bila ya kushindana, kwa hakika maisha ya ndoa huhitajia sana wanandoa kusameheana kuliko jambo lolote lingine.

 

‘Abdullaah bin Ja’afar bin Abi Twaalib alimuusia mwanawe wa kike alipokuwa anaolewa kwa kumwambia,

“Jihadhari na wivu kwani ni ufunguo wa talaka, na jihadhari na lawama nyingi kwani hurithisha maudhi, jilazimishe na kupaka wanja kwa kuwa ni bora na jambo lililo bora zaidi ya manukato ni maji”

 

Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) naye kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema,

“Je, niwaambieni kuhusu wake zenu peponi? Tukajibu: Ndio ewe Mtume wa Allaah, akasema, Ni wenye upendo na wenye kizazi, atakapoghadhibika au kukosewa, au atakapokasirika mume wake, atasema, “Mkono wangu huu uko juu ya mkono wako, sipaki wanja ukiwa na hasira na macho yangu hayatoona usingizi hadi uridhike”[1]

 

Acha kiburi ewe mke Muumini, na uende kwa mumeo atakapoghadhibika na umridhishe kwani atakupa hadhi na atanyanyua shani yako katika moyo wake na lililo muhimu sana katika yote ni kuwa baada ya hayo utakuwa umepata radhi za Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) kwani radhi za mume ni katika radhi za Allaah (Subhaanahu wa Taala), katika Hadiyth tunasoma, “Mwanamke atakayekufa na mumewe akiwa radhi nae ataingia peponi”

 

Katika Wasia wa Asmaa bint Khaarijah Kwa Mwanae Wakati wa Ndoa Yake:

“Kuwa kwake mume wako ni ardhi, naye atakuwa kwako mbingu, na uwe kwake tandiko atakuwa kwako nguzo, wala using’ang’anie kitu akakuchukia na usiwe mbali nae akakusahau, na akikusogelea msogelee zaidi”

 



[1] At-Twabaraaniy

Share