008-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Kumtii Mume Huchuma Moyo Wa Mume Na Huondoa Ghadhabu Ya Allaah

 

KUMTII MUME HUCHUMA MOYO WA MUME NA HUONDOA GHADHABU YA ALLAAH (SUBHAANAHU WA TA’ALA)

 

Mwanamke mmoja alikwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema,

“Mimi ni mwanamke niliyekuja kwako, Jihaad ni faradhi waliyoandikiwa wanaume, wakijeruhiwa hupata thawabu na wakifa huwa hai kwa Mola wao wakiruzukiwa. Ama sisi wanawake ndio wasaidizi wao, je, hatuna ujira kama wanavyopata? Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “Waambie wanawake wenzako utakaokutana nao kuwa utiifu kwa mume na kujua haki zake ni sawa sawa na Jihaad, ni wachache miongoni mwenu mfanyayo hayo”[1]

 

Kwa hakika kumti mume hulingana na Jihaad katika njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), ujira wa anayemtii mume wake na akajua haki zake ni kama ujira wa mwenye kupigana (Mujaahid) katika njia ya Allaah, lakini wanawake wengi hawajui, na utii wa mume humpelekea mkewe peponi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Pindi mwanamke atakaposwali Swalah zake tano (za faradhi), na akafunga (mwezi wake wa Ramadhaani) na akahifadhi tupu yake, na akamtii mume wake ataingia peponi”[2]

 

Mwanamke mmoja alifika kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume akamuuliza,

“Je una mume? Mwanamke yule akajibu, Ndio ninaye, uko vipi naye? Mwanamke akajibu, “Ninamhudumia kadiri ya uwezo wangu ila lile ambalo sina uwezo nalo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia, “vipi wewe kwake? Mume wako ndio pepo yako na moto wako”[3]

 

Fahamu ewe dada wa Kiislamu kuwa mume wako ndiye pepo na moto wako, kwa mume wako ndio utaingia peponi pindi unapomtii, na kwake ndio utaingia motoni (Mwenyezi Mungu Atukinge na hayo) pindi utakapomuasi.

 

Mtume aliulizwa ni mwanamke gani bora? Mtume akasema,

“Ni yule ambaye akimuangalia anapendeza, na atakapotii pindi atakapoamrishwa, wala asikhalifiane naye katika nafsi yake na mali yake, kwa lile litakalomchukiza”[4]

 

Tukiangalia matatizo mengi yanayokabili familia nyingi utaona kuwa matatizo mengi yanatokana na sababu ya mke kumuasi mume wake, kutokuwa na utii kwa mumewe na kumkhalifu kwa lile lenye kuchukiza, haya yote yanatokana na sababu ya ujinga wa mwanamke na kujua haki za mumewe juu yake au inawezekana kutokana na kiburi alichonacho, wasiwasi wa Shaytwaan na kushawishiwa vibaya ili awafarikishe baina ya mume na mkewe. Yapasa mwanamke kufahamu ya kuwa haki ya mumewe kwake na fadhila zake juu yake ni kubwa mno, kwa dalili ya Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam),

“Lau ingefaa kwa mwanaadamu kumsujudia mwanaadamu mwenzake basi ningeliamrisha kwa mwanamke kumsujudia mumewe kwa ukubwa wa haki yake kwake”[5]

 



[1] Hadiyth hii imepokewa na Al-Bazaar na At-Twabaraniy

[2] Imepokewa na Ahmad na wengineo.

[3] Ahmad na wengineo

[4] Ahmad na wengineo.

[5] Ahmad, An-Nasaaiy na Ibn Maajah

Share