Yuko Kwenye Dhiki Na Mateso Ya Mume - Amemtisha Kuwa Akiolewa Na Mwengine Atamuua

 

SWALI:

Assalamu alaykum Maalim.

Napenda kumshukuru Allaah kwa kuniwezesha na kunipa nguvu ya kuandika na kuulizia masuala haya yafuatayo. Maalim ningependa nitowe masikitiko yangu na ndani yake kuna masuala ambayo yananisumbua roho yangu kila siku ya Allaah inapopita. Mimi nimeolewa na Bwana ambaye ni Muislamu kam\ a mimi, ameniowa takribani miaka 6-7 sasa na tumejaaliwa na Allaah kupata watoto watatu. Alhamdulilah.

Tulianza maisha yetu vizuri mimi na mume wangu tukiwa tunasikilizana na kupanga mipango ya maisha ya baaadae kwa mategemeo ya mafanikio kama familia nyengine. Maisha yetu na mawasiliano yetu yalianza kuharibika baada ya mimi kuzaa mtoto wa pili. Mume wangu akaanza kunipiga, kunitukana, kunisumbulia kwa maneno haya na yale, kanipiga mpaka kufikishana polisi sio mara moja wala tatu na yeye kufungwa kwa muda wa siku tatu mpaka nne.

Amenitamkia sio mara moja wala mbili kwamba mimi hanitaki na nitafute pahala niende sababu amechoka kuishi na mwanamke asiosoma, mjinga, mvivu, na hali ya kuwa anajua kwamba mimi aliniowa nikiwa na miaka 18 kutoka kwetu na sikumaliza masomo sababu ya hii ndoa yetu, na niyeye alionifikisha hapa nilipo leo.

Vile vile ameshawahi kunipiga mpaka akanitia kovu usoni na kuniharibu sura kwa alama za mapigo kwa kutumia vitu mbali mbali kunipiga na hata kunipiga kichwa usoni kama vile vile anapigana na mwanamume mwenzake.

Na ameniahidi kwamba ataendelea kunipiga mpaka anitie kilema nisisahau maisha yangu yote na kunipa vitisho mbali mbali kwamba ikiwa nitatengana naye ataniuwa na au kunifanyia lolote lile katika maisha yangu.

Vile vile amenitamkia kwa kauli yake kamba ikiwa nitajiachisha serikalini basi mtu yoyote yule atakaye niowa atampiga na hata kumuua.Nimejaribu kuwaeleza wazazi wangu walioko mbali na mimi, wamenipa ushauri wa kuachana naye kwa kumuomba Talaka. Baada ya kumuomba talaka yangu amekataa kwa kuhofia kwamba atapoteza fedha nyingi kunilipa mimi na watoto tuliozaa nao, vile vile anapokwenda safari ya mbali hunifungia ndani kwa kunambia kwamba mimi sina haki na ruhusa ya kutembea nje na kuwaona jamaa na marafiki.

Amenikataza nisitumie kitu chochote cha mawasiliano ya ndani kama simu, computer,etc kwa kuwasiliana na watu wa nje.Amenipiga marufuku kufanya contact na watu ambao hunipa mawazo na fikra za mimi kubadlisha maisha yetu mimi na mume wangu, mfano watu wa social serikalini.

Huyu bwana wangu alishawahi kuowa wake wanne na wote walimtoroka na kukimbia katika kipindi cha mwaka mmoja kabla yangu mimi ni mke wa 5.  Nilikuwa ninasoma kwa ajili ya kuomba uraia amenikataza nisome na masomo nimeacha na amenitamkia sio mara moja au mbili kwamba haniombei mimi kupata uraia na kufanikiwa katika maisha yangu. Kwa fikra zangu na mawazo yangu ni kuwa huyu mumewangu ameniweka na kuniowa kama mtumishi wa kumlindia nyumba na kupata nafasi ya yeye kuomba mikopo na mali serikali.

Tangu aliponiowa mwaka wa 6/7 sasa sijatembelea wazazi wangu Africa na nikimuuliza vipi lini tutakwenda kuwatembelea wazazi Africa ananambia kwamba yeye hana pesa za safari na hali ya kuwa Alhamdullilah kipato chake kinamruhusu kwa sisi kufika huko.

Inasikitisha yeye anapenda kualika watu kuja nyumbani kufanya sherehe mara kwa mara na gharama zote za sherehe kujitolea yeye mwenyewe, kila baada ya miezi 3/4 hufanya sherehe kukumbuka familia yake na ndugu zake.

Kwa hakika niko kwenye maisha ya ziki na kusumbuliwa kila wakati,kupigwa,kutukanwa, kunyimwa hata nafasi ya kuwasiliana na ndugu zangu.

Nilishauriwa na mwanasheria baada ya kunipiga usoni hata nikavimba uso mzima na kupasuka kwamba anifanyia talaka yangu lakini nikaogopa kwamba huyu Bwana atakuja kuniuwa kama alivyoniahidi. Nikakataa talaka kutoka serikalini.

Pia mume wangu anapenda kujionyesha kwa watu kwamba yeye ni muislam mkarimu na mpenda watu lakini hapa nyumbani ananifanyia mateso mbali mbali hata wanapokuja wageni hunifungia chumbani nisiwaone au kusalimiana nao

Kuna pesa ambazo mimi ninastahili kupata kutoka serikalini kila mwezi amechukua mpaka card ya bank kwamba mimi sina haki ya kuwa nayo sababu ni mjinga sijui jinsi ya kuitumia hiyo card.

Ninaomba ushauri kutoka kwako maalim nini nifanye na jee dini itaniruhusu. Kuomba talaka kwa kupitia mahakama ya kadhi kule nyumbani Africa au hata hapa nilipo kiserikali. Haya ndio masikitiko yangu na masuala na ushauri ninahitaji kutoka kwako kama kuna makosa niliandika naomba msamaha.

Maasalamu


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tunashukuru kwa swali lako zito lenye maelezo ya kusikitisha sana.

Pendekezo muhimu sana kwako na kwa wengine watakaopenda kutuma maswali yao ni kuwa vyema kuleta suala badala ya kuleta historia yako au maisha yako na matatizo yake, muhimu linalohitajika ni swali au utata kwa ufupi ukiwa umegusa lengo muhimu la swali lako; hivyo basi mara nyingine ukijaaliwa kutaka kuuliza suala au masuala leta masuala kwa ufupi na kwa uwazi ili upate kujibiwa kwa haraka na kwa ufanisi insha Allaah.

Na kwa sababu swali lako ni refu sana na lina maeleo mengi muhimu, hivyo yanahitajika kujibiwa kipengele kwa kipengele, na hivyo majibu yetu tayakuwa marefu sana na hivyo tunaomba uwe mvumilivu kuyasoma yote.

Mwanzo umeeleza kuwa mlipooana mlikuwa na malengo ya ‘kupanga mipango ya maisha ya baaadae kwa mategemeo ya mafanikio’. Muislamu hutarajiwa awe na yakini kuwa Allaah Ameshamuandikia kila kitu na hatokipata chochote isipokuwa kilekile alichokadiriwa akipate na Allaah; na hatokikosa isipokuwa asichokadiriwa; hivyo basi kupanga maisha kwa mategemeo ya mafanikio si katika mambo anayotarajiwa yamuumize kichwa Muislamu kwani kama tutakuwa na Iymaan thabiti na kutekeleza Anayotutaka Allaah tuyatekelze kama Alivyoagiza; basi Yeye Mola Kachukuwa jukumu la kusimamia mambo yetu yote ya baadaye ikiwemo watoto wetu na kuwa mafanikio ni lazima kwa kila Muislamu awe na Iymaan na itikadi isiyo kuwa na chembe ya shaka kuwa mafanikio hutoka kwa Allaah na si vyenginevyo na wala hakuna katika tuliyonayo iwe mali au kazi nzuri yanayoweza kuleta mafanikio kama Allaah hataki; hivyo basi mafanikio yetu na maisha ya baadae ni mipango inayotakiwa ipangwe kwa kila mmoja wetu kutekeleza aliyoagiza Allaah na Yeye Allaah Atasimamia kila letu; Qur-aan inasema:

Na ama ukuta, huo ulikuwa ni wa vijana wawili mayatima kule mjini. Na chini yake ilikuwako khazina yao; na baba yao alikuwa ni mtu mwema. Basi Mola wako Mlezi alitaka wafikie utu uzima na wajitolee khazina yao wenyewe, kuwa ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Wala mimi sikutenda hayo kwa amri yangu. Hiyo ndiyo tafsiri ya hayo ambayo wewe hukuweza kuyasubiria.” Al-Kahf: 82. 

 

Hivyo basi kama utakuwa mwema basi hali ndio kama hiyo hapo; na hakuna wema kama mtu kutekeleza yote Aliyoamrisha Allaah kadiri ya uwezo wake na kujikataza na makatazo Yake mara moja; na kama hutokuwa mwema kuwa na mipango yote waliyonayo watu wa dunia hutoweza kupata mafanikio hata yenye uzito wa mdudu chungu.

Ukaendelea kusema, ‘Mume wangu akaanza kunipiga, kunitukana, kunisumbulia kwa maneno haya na yale’, katika mafundisho ya Uislamu ni kuwa mke hapigwi; na mbora wetu ni yule aliye mbora kwa ahli zake na hakuna katika umma huu wote aliyekuwa mbora kwa ahli zake kuliko alivyokuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na yeye hakuwahi hata mara moja kumpiga mkewe wala kumtukana wala kumsimbulia wala kuwaambia wake zake maneno haya wala yale.

Ukasema, ‘Amenitamkia sio mara moja wala mbili kwamba mimi hanitaki na nitafute pahala niende,’ tunasema, kama uko mkweli katika maneno yako na kama huyo mumeo ni mkweli basi kwanini asikupe talaka yako?! Katika Uislamu mtu yeyote kama hawezi kuishi na mwenzake kwa sababu yoyote ile basi hakuna haja ya kumkejeli wala kumdhuru wala wala; kama humtaki au hakutaki yawezekana na hii ni hakika kuna wangapi wanakutaka; kama amechukia tabia fulani kwako basi akumbuke kuwa kuna nyengine anazipenda au alizipenda na kama hayo hayapo basi ushauri ni kutengana kwa ihsaan na akupe talaka yako kwa wema na ihsaan.  Si haki yako kutoka katika nyumba yake bila kukupa talaka yako na bila ya kukamilisha eda yako ama akikutoa kwa ujahili wake na kiburi chake basi atakuwa ni katika wenye kwenda kinyume na amri ya Allaah na huna haja ya kutafuta pahala pa kwenda wewe hapo ndio pako na yeye kama anataka utafute pahala pa kwenda basi akupe talaka yako na sio wewe umkere kwa hilo, na kisha umalize eda yako hapo na utafute pahala pa kwenda kwa wema na ihsaan.

Ukaendelea kusema, ‘kunipa vitisho mbali mbali kwamba ikiwa nitatengana naye ataniuwa,’ kama maneno yako haya ni sahihi basi mbona kuna kugongana mgongano mkubwa? Maana kwengine umesema: ‘Amenitamkia sio mara moja wala mbili kwamba mimi hanitaki na nitafute pahala niende’ sasa itakuwaje asiye kutaka kwa kuthibitisha kila aina ya viroja na mara unasema kuwa anakupa vitisho na ukitengana naye atakuua, kisha hapo hapo amekwambia utafute pahala pa kwenda?! Au labda huyo mume hajui anachokisema?

Nasaha zetu kwako na kwa kila Muislamu ni kumuogopa Allaah na kukumbuka Siku ya kufa kwake na Siku ya kufufuliwa na kusimamishwa mbele ya Allaah, na kutokuwa tayari kuamini au kuitakidi kuwa huyo mumeo ana uwezo wa kukufanya jambo lolote lile na kuwa kama atakuua basi huna hasara. Akifanya hivyo atakuwa amekuharibia dunia yako ambayo haina thamani mbele ya Akhera na atakuwa kwa kukuua amekutengenezea Akhera yako ambayo ndio kusudio na lengo la kila mwenye Iymaan thabiti; na kwa upande wake ataona kuwa amejitengenezea dunia yake ambayo haina muda mrefu ataiondoka na kujiharibia Akhera yake ambayo ni ya milele.

Hivyo basi, nyote wawili mnahitaji nasaha za kuelewa kuwa Allaah Ndiye muhusika katika kuchukuwa roho za waja na atakayejaribu kuichukua kazi hiyo basi ametafuta hatari kubwa kwani ghadhabu na adhabu za Allaah zitakuwa ndio malipo yake; kwani atakuwa amekuua kwa makusudi na kumuua Muislamu kwa makusudi hakuna isipokuwa hili:

“Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannamu humo atadumu, na Allaah Amemkasirikia, na Amemlaani, na Amemuandalia adhabu kubwa.” An-Nisaa: 93.

Ukaeleza hivi, ‘Vile vile amenitamkia kwa kauli yake kamba ikiwa nitajiachisha serikalini basi mtu yoyote yule atakaye niowa atampiga na hata kumuua.’ Kwanini ujiachishe nah ali umeeleza kuwa ‘Amenitamkia sio mara moja wala mbili kwamba mimi hanitaki’ Ndugu yetu kinachojitokeza hapa ni kuwa nyote wawili mnatakana kwani kama ingekuwa kinyume chake basi wewe ungekuwa ushaachwa na sio kujiachisha; na yeye asingempiga huyo atekayekuoa kama utaachwa wala asingemuua yeyote si wewe wala si huyo atakayekuoa kama utaachwa.

Nyinyi bado mnatakana na mnahitaji mtu wa kuwaweka kitako kuwafunua macho na kuwaeleza kwa uwazi kuwa kila mmoja wenu hajijui kwa mwenzake na hivyo kila mmoja aweke akili yake vizuri na aache kuchezea wakati wa watu kwani hakuna mnachokitaka.

Ukaendelea kusema, ‘Nimejaribu kuwaeleza wazazi wangu walioko mbali na mimi, wamenipa ushauri wa kuachana naye kwa kumuomba Talaka.’ Na ukasema, ‘Amenitamkia sio mara moja wala mbili kwamba mimi hanitaki’ tunachotaka ufahamu ni kuwa kuomba talaka ni katika makosa makubwa hutopata harufu ya pepo kama utaomba talaka bila ya kuwa na sababu ya msingi sababu inayokubalika kuwa unayo. Tunasema haya kwa sababu maelezo uliyotupa sehemu zingine yanagongana. Na ikiwa ulivyosema kuwa, ‘Amenitamkia sio mara moja wala mbili kwamba mimi hanitaki na nitafute pahala niende,’ basi unahitaji mtu kukaa na nyinyi wawili na kumueleza huyo mumeo kuwa kama hakutaki basi akupe talaka yako kwa wema na ihsaan na huu ndio ushauri wa dini yenu.

Ukaeleza, ‘Baada ya kumuomba talaka yangu amekataa kwa kuhofia kwamba atapoteza fedha nyingi kunilipa mimi na watoto tuliozaa nao,’ kama utakuwa unacheza mchezo wa watu wasio kuwa Waislamu kuwa ulipwe kwa talaka ikiwemo kugawanya mali nusu nusu na mumeo basi hilo si katika Uislamu. Watoto wana haki kwa baba yao ya kumthiri kulingana na Mirathi Aliyoiweka Allaah na wewe kwa kuwa hutakuwa mkewe wakati huo akifariki hutokuwa na haki ya kumrithi kwani hutokuwa miongoni mwa warithi wako ama watoto ni warithi wake hata kama atakuwa na mke mwengine na watoto wengine. Hivyo Kiislamu huna cha kulipwa kama ataamua kukupa talaka si wewe wala si watoto wenu ila kama mlikuwa mnashirikiana kama mapesa yenu na kuchanga kwa pamoja basi hilo ni jengine lakini huna haki ya kulipwa kwa sababu amekupa talaka; haki yako ni talaka tu au akipenda anaweza kukupa chochote cha kukusaidia mbeleni kwa khiyari yake na si kwa kulazimishwa na serikali za kikafiri na sheria zao.

Umeendelea kueleza: ‘Amenipiga marufuku kufanya contact na watu ambao hunipa mawazo na fikra za mimi kubadlisha maisha yetu mimi na mume wangu,’ kama kuna wa kuweza kukusaidia na kukupa mawazo na fikira za kuishi basi hawa unaowataja ‘mfano watu wa social serikalini’ watachoweza kukusaidia ni kukupotosha na dini yako na mafundisho ya dini yako kwani hawana ushauri wala fikra zenye kutaka kukupelekea wewe au mwngine ye yote aliye Muislamu isipokuwa kuhakikisha kuwa wanakwenda kinyume na mafundisho ya dini yao kwa kufuata mafundisho ya kimagharibi; hivyo basi hata kama huyo mumeo ana makosa basi tafuta Waislamu wenye elimu na upeo wakusaidie kutatua tatizo lako na usiwe na tamaa ya kutaka kupata pound kwa kutaka kupewa talaka basi tafuta radhi za Mola wako kutosheka na mafundisho ya dini yako na mafundisho yake yanakutaka uchukue ushauri wenye kwenda sambamba na dini yako.

Umesema: ‘Huyu bwana wangu alishawahi kuowa wake wanne na wote walimtoroka’ kama hilo lilikuwa tatizo basi wewe bila shaka yoyote ile ulikuwa unalielewa kabla ya kuolewa na yeye na ukachagua kuolewa juu ya kuelewa hayo; ahtujui ni sababu gani haswa iliyokupelekea kukubali? Kama ilikuwa ni sababu yuko Ulaya, au mali au lolote lile la kidunia, basi utakuwa hujaifahamu Qur-aan ambayo tayari imeshatueleza kuwa matatizo na misukosuko yoyote inayotusibu na kuyachukia ni kwa sababu ya maasi yetu; Qur-aan inasema:

“Na misiba inayokusibuni ni kwa sababu ya vitendo vya mikono yenu. Naye Anasamehe mengi.” Ash-Shuuraa: 30.

Ukaendelea kueleza hivi: ‘nilikuwa ninasoma kwa ajili ya kuomba uraia amenikataza nisome na masomo nimeacha na amenitamkia sio mara moja au mbili kwamba haniombei mimi kupata uraia na kufanikiwa katika maisha yangu.’ Jambo la kufanikiwa katika maisha ni lazima iwe katika iymaan yako na itikadi yako kuwa hilo haliko katika mikono ya kiumbe yeyote yule awe atavyokuwa ni katika yenye kumuhusu Mola; hivyo basi kama atakuombea du’aa yoyote ile huwa haina maana hasa kama utakuwa unatekeleza amri za Mola kadiri ya uwezo wako na kujikataza na makatazo yake mara moja; nasaha zetu ni kuwa tunatakiwa tuamini na tuitakidi kuwa hapa duniani hakuna kitu kinachoitwa mafanikio kwa maana ya mafanikio ambayo hayatokuwa na mabadiliko wala hayahitajii mtu kuwa na wasiwasi kwani ni mambo ya daima na milele; bali yote tuyapatayo ambayo tunayaona kuwa ni mafanikio, kwa kweli na huu ndio uhakika huwa ni mitihani kutoka kwa Mola; na mafanikio ya kweli kweli na ndio hasa ya kuyatafuta asubuhi na jioni ambayo sisi na wewe na wengine wote wenye kuamini Siku ya Mwisho tunatakiwa tuelewe hivyo ni vipi tutaweza kuepushwa na Moto na kutiwa Peponi?!

“Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kaamili Siku ya Kiyama. Na atakayeepushwa na Moto na akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu” Al-‘Imraan:185

Ukaendelea: ‘Tangu aliponiowa mwaka wa 6/7 sasa sijatembelea wazazi wangu Africa na nikimuuliza vipi lini tutakwenda kuwatembelea wazazi Africa ananambia kwamba yeye hana pesa za safari na hali ya kuwa Alhamdullilah kipato chake kinamruhusu kwa sisi kufika huko.’ Safari ni majaaliwa; omba du’aa Allaah awape umri mrefu na akupe wewe subira ya kuweza kuvumilia na kuweza kumkumbuka Mola kila wakati kila siku. Kama mumeo hali ndio kama hiyo uliyokuwa unaitangaza mwanzo wapi atakupa tiketi ya kwenda kuwatembelea watu wako?! Unachohitaji kwa sasa sio kuwatembelea wazazi bali kuwataka wakuombee du’aa uweze kwa uwezo wa Mola kutatua matatizo yako na mume wako ambaye kama tulivyosema kuwa kuna kila kinachothibitisha kuwa bado kila mmoja hajijui kwa mwenzake. Kwani kama ingekuwa hali kinyume ambayo ndio maelezo yako ni tangu ulipozaa mtoto wa pili ambapo inaonyesha labda ni miaka kwa uchache mitano au minne si muda mdogo au haya matatizo ndio yameanza jana na juzi?! Kama ni ya jana na juzi basi yanaweza kupatikana kwa ufumbuzi ama kama ni ya miaka yote hiyo na huku watoto kupatikana basi kuna mambo yanajificha katika maisha yako ambayo unayaelewa wewe na Mola wako ukweli wake.

Umesema: ‘Inasikitisha yeye anapenda kualika watu kuja nyumbani kufanya sherehe mara kwa mara na gharama zote za sherehe kujitolea yeye mwenyewe, kila baada ya miezi 3/4 hufanya sherehe kukumbuka familia yake na ndugu zake. Je, anapata wapi cha kuwakirimu hao wageni wake?! Bila shaka yoyote ile huwa anaagiza kutoka hoteli moja au nyengine; vyenginevyo wewe ndio huwa mtayarishaji na mpikaji wa hayo maakulati na mashurubaat; kama kuna ugomvi baina yako na wewe kama unavyodai basi hatudhani kama utakuwa na haja ya kushughulikia wageni wa mtu unayedai kuwa hakutaki wala wewe humtaki, achilia mbali kupika na kupakuwa. Ndugu yetu Allaah Atakutatulia matatizo yako kama yapo na kama hayapo atakupa utulivu katika ndoa yako na Iymaan yako.

Katika Uislamu kinachitakiwa kufanya kwa kuwakumbuka waliotangulia ni kuwaombea du’aa na kuwatolea Sadaqah na Sadaqah hiyo wapewe wanaostahiki kama uko UK waswahili karibu wote wanaoishi hapo hawastahiki kupewa Sadaqah kwani karibu wote ni wenye kujiweza; hivyo basi cha kumshauri huyo mumeo na Waislamu wanaoishi huko ni kuwa kama tutafikwa na misiba au kama tutataka kuwakumbuka wazee kwa kutoa Sadaqah lililo bora na zuri mbele ya Allaah ambalo liko mbali na kujionyesha ni kupeleka fedha vyuoni au Misikitini na kuwaomba walipie malipo ya umeme, maji, na mengineyo muhimu.

Ukasema: ‘Kwa hakika niko kwenye maisha ya ziki na kusumbuliwa kila wakati, kupigwa, kutukanwa, kunyimwa hata nafasi ya kuwasiliana na ndugu zangu.’ Kwa mujibu wa maelezo yako basi utakuwa hauko katika maisha ya dhiki bali hilo ni katika mitihani Alikyokupa Allaah ima kwa sababu ya mikono yako mwenyewe kama Aayah iliyotangulia inavyotueleza, au umeyachuma hayo au kwa sababu nyengine na yote ni kutakiwa kurudi kwa Mola na kumuomba tawbah na Maghfirah na rehma Zake.

Ukaeleza: ‘Pia mume wangu anapenda kujionyesha kwa watu kwamba yeye ni muislam mkarimu na mpenda watu’ fahamu kuwa katika mafundisho ya Uislamu ni kuwa mbora wetu ni yule aliyembora kwa ahli zake na hakuna katika umma huu wote aliyekuwa mbora kwa ahli zake kuliko alivyokuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); hivyo Uislamu wake ukarimu wake hauwezi ukashinda ukarimu na Uislamu wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na yeye hakuwa akijionyesha kwa lolote lile; kwani katika mafundisho yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hiyo ndio Iymaan na itikadi anayotakiwa awe nayo kila mmoja wetu ni kuwa ‘amali yoyote ya mja ikiwa ndani yake kuna kujionyesha iwe kwa ‘amali za kawaida au hata maalumu kama Swalah, kusoma Qur-aan na kadhalika hueleweka kama ni riyaa, mtu kutaka kusifiwa, mtu kutaka kutajwa na wengine, mtu kumkusudua mtu kwa hiyo ‘amali, mtu kufanya kwa sababu tu watu wasije wakaona kuwa hajafanya kwani ni katika mila zao, mtu kufanya ili apate kitu kwa wengine, mtu kufanya kwa ajili ya aonekane kuwa anafanya hili au lile kwa lengo la kushindana na mwengine na kadhalika; basi huwa haina thamani mbele ya Allaah; hivyo watu watakula wali na baada ya kumaliza kula wewe au huyo mumeo huondokea matupu mbele ya Allaah.

Na huenda akapata ujira wa kujionyesha ambao unaweza kufikia kuwa ni shirk kubwa kwani asili ya kujionyesha ni shirk ndogo; hivyo unachotakiwa ni kumshitua ili asifikie kuingia Motoni kama ni ndugu yako katika dini achilia mbali huyo ni habibi wako wa roho usiyeweza kumkosa wala kuachana naye.

Ukasema: ‘hata wanapokuja wageni hunifungia chumbani nisiwaone au kusalimiana nao’ ndio akawa anakuchunga usije ukatekwa kama alivyokuteka yeye; na kama wao ni watu wazuri ambao ni wachache katika dunia ya leo basi wangelikuwa wakitoa salaam zao kwako bila hata ya kutaka kukuona au kuwaona; na wewe usiwe na haja ya kuwaona kwani ni mke wa mtu. Hivyo tosheka na kumuona mumeo kwani kama yeye ni mwenye sura tofauti na wengine unaweza kuingia katika fitina kama hii uliyonayo na kutaka muachane; na kinyumne chake pia yawezekana kwa kuwa ‘anapenda kujionyesha kwa watu’ yawezekana mumeo amewahi kuwaona wake za hao waalikwa akawatamani na hivyo anaogopa wewe kuonekana na wengine ukaja kutamaniwa, kwa sababu inaonyesha yeye na hao waalikwa si watu wenye kujua dini yao na kuchunga mipaka ya sheria.

Umeeleza: ‘kuna pesa ambazo mimi ninastahili kupata kutoka serikalini kila mwezi amechukua mpaka card ya bank kwamba mimi sina haki ya kuwa nayo sababu ni mjinga sijui jinsi ya kuitumia hiyo card.’ Hili linathibitisha kuwa mapenzi yenu hayana wa kuweza kuyaelewa; kwani kama madai haya ni ya kweli na uko katika nchi za kitwaaghuut ambazo wanawake ni wenye haki kupita kiasi basi unaelewa fika unayosema na unaelewa fika cha kufanya; na madai yako ndugu yetu kama ndio hivyo, basi kwanini usitafute watu wenye Iymaan zao wapate kukusaidia matatizo yako na huyo mpenzi wako wa maisha.

Ukaendelea: ‘jee dini itaniruhusu. Kuomba talaka kwa kupitia mahakama ya kadhi kule nyumbani Africa au hata hapa nilipo kiserikali.’ Madai yako yanahitaji pia kusikilizwa upande wa pili; kwani kama tulivyokueleza kuwa kama maelezo yako yote ndivyo haswa hivyo yalivyo ‘Amenitamkia sio mara moja wala mbili kwamba mimi hanitaki basi anatakiwa akupe talaka wala huna haja ya kwenda pahala popote ni haki yako kwani wewe si mtumwa wake wala si kitu chake anachokimili kama hakutaki kama unavyodai basi akuache kwa wema na ihsaan.  Ama kwenda kuchukuwa talaka katika serikali au nyumbani kwa ma-Qaadhi hili lina mushkeli wake kwani Qaadhi ataweza kuitoa talaka bila ya kusikia upande wa pili haswa haswa siku hizi ambako kila kitu hupatikana kwa kutoa fedha na hilo pekee linaonyesha kuwa talaka nyingi za serikalini huwa hazina uzito mbele ya dini  kwa kuwa kama mume yuko na ni Muislamu mwenye kuelewa mafundisho ya dini yake na hata kama haelewi pia kama anaelewa kuwa kuna kutakiwa na kukataliwa na hii ndio hali halisi na ya ukweli wa dunia kuna kupata na kukosa basi alikuwa kama ana akili kidogo tu akupe talaka yako kama anahisi kuwa hakutaki au hana haja na wewe tena baada ya muda huu mliokaa na kuzaa.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share