Nakuwa Na Hasira Sana Bila Ya Sababu, Nini Tiba Yake?

SWALI:

 

Asalaam Alaykum,

 

natumai inshallah kwa iwezo wa Allah hamjambo na Azidi kuwahifadhi na kuwapa maendeleo kwani maendeleo yenu ndio ya umma wote.inshallah amen. Mie swali langu ni kwamba kuna wakati nakuwa na hasira saaaaana hata pengine sababu sioni, na hasira inakuwa inakaa pengine hata siku 3. nakuwa nasikia roho inauma saana na kifua kinabana. na sababu inakuwa sio ya kunifanya niwe vile. siipendi hali hiyo kwani hasira ni tabia za shaitaan. najaribu saana kusoma dua za huzuni, za balaa, sura za Qur'an. nakuwa napata nafuu lakini tena inarudi. je ni nini? na nini tiba yake?


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuwa na hasira ya kupita kiasi.

 

 

Hakika ni kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia:

 

 

Mwenye nguvu si yule mwenye kupiga watu mieleka bali ni yule anayemiliki nafsi yake anapo ghadhibika”.

 

 

Sasa kama Waislamu inabidi tufanye juhudi za hali ya juu kuweza kudhibiti hali ya kuimiliki nafsi wakati mtu anapokasirika. Bila kufanya hivyo tutahasirika hapa duniani na Kesho Akhera.

 

Uislamu umetupatia sisi mafunzo mazuri ya kuweza kudhibiti ghadhabu. Bila shaka umetaja baadhi yake na jinsi gani njia hizo zimekusaidia kwa kiasi fulani. Njia nyingine ni kama zifuatazo kama alivyotufundisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

1.      Kubadilisha mkao au sehemu aliokuwa nayo aliyeghadhibika: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Anapokasirika mmoja wenu naye amesimama basi akae; ikiondoka sawa na lau itabaki basi alale kwa ubavu (ajinyoshe)” (Ahmad).

 

2.      Kuchukua wudhuu wakati wa hasira: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ghadhabu zinatokana na Shaytwaan, na Shaytwaan ameumbwa na moto; na moto unazimwa na maji. Hivyo, anapokasirika mmoja wenu na achukue wudhuu” (Abu Daawuud).

 

3.     Kunyamaza wakati wa hasira: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Anapokasirika mmoja wenu basi anyamaze” (Ahmad).

 

4.      Kujilinda kwa Allaah kutokana na Shaytwaan aliyelaaniwa: Imenukuliwa katika Swahiyh mbili kuwa walitukanana watu wawili mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na mmoja wao akawa anamtusi mwenziwe na huku amekasirika hata uso wake kuwa mwekundu. Hapo akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakika mimi najua neno lau atalisema basi yote anayohisi (ghadhabu) yatamuondokea … lau atasema: A‘udhu BiLlaahi Minash Shaytwaanir Rajiym”.

 

Huu ni wasiya muhimu sana ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupatia katika kutuliza ghadhabu na kupunguza makali yake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share