Kupenda Futboli Ni Vibaya? Hukmu Ya Wanaoacha Swalaah Kwa Ajili ya Kutazama Mpira Wa Miguu?

 

SWALI:

 

Assalamu Aleykum Warrahmatullahi Wabarakatu.

 

Naomba kuuliza swali. Swali langu ni kama ifuatavyo; jee ni haramu kucheza, kuangaliya ama kuwa shabiki mkuu wa football? Sababu ya kuuliza swali hili ni kutaka kupata uhakika kuhusu swali hili. Kuna baadhi ya watu ambao wanapoteza wakati wao wote wakiwa wanaangaliya mpira na huku umewadiya wakati wa swala lakini hawaendi kuswali kwa sababu hawataki kupitwa na mchezo huwo.

Tafadhali nijibuni swala hili ili niweze kujadiliyana nao, shukran. Wa jazakummullahul kheir.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kupenda mpira au mchezo mwengine wowote ule.

Hakuna uharamu wowote kwa mtu kucheza mchezo wowote ule ambao unakwenda sambamba na shari’ah, kuangaliya au kuwa shabiki kwa mipaka ya Uislamu.

 

Tufahamu kuwa Uislamu ni Dini ya vitendo wala sio ya mawazo matupu. Inawachukulia wanaadamu kama wanaadamu. Kwa ajili hiyo, Uislamu ni Dini na dunia. Kuna namna nyingi ya michezo waliowekewa Waislamu na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili kujifurahisha na kujipumzisha, nayo kwa wakati huo yanaitayarisha nafsi zao kuweza kufanya ‘Ibaadah zao na wajibu wao kwa nashati kubwa zaidi na hima kubwa zaidi. Nyingi katika hizo ni Riyadha zinazowazoweza kupambana na mazito, na kuwatayarisha kwa vita vya Jihaad na kupigana kwa ajili ya Allaah Aliyetukuka. Katika michezo iliyo halali ni kama ifuatayo:

 

1.     Mbio, naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anashindana na mkewe ‘Aa’ishah (Radhiya Allaahu ‘anha).

2.     Miereka, naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alishindana na Rukaana na kumshinda (Abu Daawuud na Ahmad).

3.     Kurusha mishale. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwapita Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wakishindana kurusha mishale, naye akawahimiza kwa kuwaambia: “Rusheni nami ni pamoja nanyi” (al-Bukhaariy).

4.     Kucheza na mikuki.

5.     Kupanda farasi.

6.     Kuogelea pia kumehimizwa sana.

7.     Kuwinda kwa kutumia ala kama mishale, mikuki na kwa sasa bunduki.

 

Uislamu pia umeweka kanuni za kijumla ya kuufanya mchezo wowote ule kuwa halali au haramu. Kanuni hizo ni kama zifuatazo:

 

1.     Uhalali unategemea manufaa au hasara inayopatikana. Ikiwa manufaa ni makubwa zaidi mchezo utakuwa halali na lau itakuwa kinyume chake basi utakuwa ni haramu.

2.     Mchezo wowote wenye kamari unakuwa ni haramu.

3.     Isicheleweshwe Swalah kutoka kwa wakati wake kwa ajili ya mchezo wowote ule. Hatari hiyo inakuwa kubwa kwa kupoteza wakati na kujishughulisha watu kukosa kutekeleza wajibu wao.

4.     Mchezaji ahifadhi ulimi wake wakati wa kucheza, asitukane na kutokwa na maneno machafu.

5.     Mchezo kama wa ngumi ni mchezo uliokuwa haufai kwani kuna kudhuriuana uso ambako kumekatazwa na Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuleta madhara ya ubongo na mifano ni mingi.

6.     Mavazi yalingane na stara ya iliyowekwa kishari’ah. Haifai kuvaa vikaptula vinavyonyesha mapaja ya mwanaume kama ilivyo kwenye mpira wa miguu na mbio na pia nguo za kubana zenye kuonyesha maungo ya ndani kama kwenye michezo ya kukimbia, kuogelea, michezo ya viungo kama jimnastiki (sarakasi) n.k.

7.     Wanawake hawakatazwi kucheza maadam wako wenyewe, na wawe wamevaa stara za kishari’ah. Hata hivyo wanawake haiwapendezei kucheza michezo ya nguvu iliyo kinyume na maumbile yao kama mieleka, mpira wa miguu na mingine ambao wanawake wa siku hizi wameanza kuiga.

 

Ikiwa moja katika masharti yaliyo juu haikutimizwa, basi mchezo huo utakuwa ni haramu. Hivyo, uhalali na uharamu wa kushabikia mchezo wa mpira itagemea na vigezo vilivyo juu. Na hapo umeuliza kwa uwazi kabisa kuwa watu wanaoshabikia mchezo huo huwa wanakosa Swalah, hivyo, kwa hali hiyo kunafanya kucheza kwa wakati huo na kutazama au kushabikia kuwa haramu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share